Tume kuandika wapigakura wapya 14,878 Z’bar, ACT-Wazalendo watoa neno
Muktasari:
- Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imepanga kutumia siku saba kuanzia Oktoba 7-13, 2024 kuandikisha wapigakura wapya 14,878 visiwani Zanzibar ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Unguja. Wakati maboresho ya daftari la mpigakura yakitarajia kuanza Oktoba 7 hadi 13, 2024, wapiga kura wapya 14,878 wanatarajiwa kuandikishwa kisiwani humo ambao watakuwa na fursa ya kupiga kura moja tu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kutokana na shughuli hiyo, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetumia siku tatu kuanzia Septemba 29 hadi leo Jumatano, Oktoba 2, 2024 kutoa mafunzo kwa wadau wa uchaguzi na watendaji ngazi ya mkoa namna bora ya shughuli hiyo itakavyoendeshwa.
Katika mafunzo hayo, Mjumbe wa INEC, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Asina Omari amewataka wasimamizi hao kuzingatia taratibu na miongozo kuhakikisha kila anayestahili kupata fursa hiyo haikosi huku akisema wanatarajia upata ushirikiano kutoka kwa wadau.
“Twende tukasimamie sheria taratibu na miongozo ili kila anayestahili kuandikishwa asikose huduma hii,” amesema.
Mkurugenzi wa INEC, Ramadhan Kailima amesema kwa kipindi cha siku hizo wanatarajia kuandikisha wapigakura 14,878 ikiwa ni ongezeko la asilimia 18 ya wapiga kura 83,197 waliopo kwenye daftari la wapigakura.
“Inatarajiwa baada ya uandikishaji itakuwa na wapiga kura 98,075 watakaopiga kura moja tu ya kumpigia Rais wa Jamhuri wa Mungano wa Tanzania,” amesema.
Nao baadhi wadau wa vyama vya siasa wamesema ni kama wameshtukizwa katika hatua hiyo kwani walitakiwa kupewa taarifa muda mrefu kwa ajili ya kuwaandaa wananchi na wafuasi wao.
Ofisa Uchaguzi wa ACT Wazalendo, Muhene Rashid amesema taarifa hizo zimekuja kwa muda mfupi hivyo inaweza kuathiri wananchi wasipate taarifa mapema.
"Hili jambo lilikuwa limepangwa mapema, ila muda umeshakwenda tunatakiwa tujipange na tuhamasishe wananchi lakini kwakuwa muda umeisha inaweza kuathiri na watu wasihamasike zaidi," amesema.
Hata hivyo, Kailima amesema ni vyema wakatumia muda uliopangwa kupitia majukwaa halali kuhamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi badala ya kuona kama muda hautoshi.
Ofisa mwandikishaji Unguja, Amina Saleh amesema:“Tumepata miongozo na sisi tutahakikisha tunasimamia na kuendesha shughuli hii kama ilivyopangwa na malengo ya serikali yafikiwe.”