Wadaiwa kulawitiana kwenye mahabusu ya Polisi

Kamanda wa Jeshi la Polisi  Mkoa wa Mjini Magharibi, Richard Thadei Mchomvu akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake Madema Zanzibar. Picha na Zuleikha Fatawi

Muktasari:

  • Taarifa za tukio hilo zimetolewa na baadhi ya mahabusu waliodai wenzao walichomoka pembeni na kufanya kitendo hicho cha jinai.

Unguja. Watuhumiwa wenye makosa mawili tofauti, wamedaiwa kulawitiana wakiwa katika mahabusu ya Kituo cha Polisi Madema, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.

Mtuhumiwa mmoja ni miongoni mwa vijana 13 waliokamatwa na Jeshi la Polisi hivi karibuni wakituhumiwa kujihusisha na vitendo vya kulawiti na kulawitiwa kisiwani humo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Richard Mchonvu amesema hayo leo Alhamisi Novemba 30, 2023 wakati akizungumzia hali ya uhalifu mkoani humo akibainisha kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 22, 2023.

"Taarifa hizi tunazichunguza, ikibainika tutawapeleka mahakamani, tulipata taarifa hizo kutoka kwa wenzao waliokuwemo mahabusu, walichukuana wakaenda kando kidogo na kulawitiana,” amesema Mchomvu.

Kamanda Mchomvu amesema wameshafungua jalada la upelelezi wa kesi hiyo kufuatia tukio hilo lililofanyika ndani ya mahabusu.

“Ninachokisema ikiwa mtu kakaguliwa ndani ya saa moja na akafanya jambo hilo, sasa jamii pamoja na wazazi tuone uzito wa hili pindi watoto utakapowaacha kwa saa mbili bila ya kuwa na taarifa nao,” amesema Mchomvu.

Kuhusu matukio mengine, Kamanda Mchonvu amesema ndani ya mwezi huu, wamekamatwa watuhumiwa 139 wakiwemo 84 wenye makosa ya wiz, ubakaji (10), shambulio (27), ulawiti (11), unyang'anyi manne na udanganyifu matatu.

Kwa mujibu wa Mchomvu, kati ya makosa hayo vijana watatu wanatuhumiwa kumbaka kwa mkupuo msichana mwenye umri wa miaka 17.

Utapeli wakithiri

Aidha, Kamanda Mchomvu amesema wapo vijana wanaotumia njia za udanganyifu kujipatia fedha ambapo vijana wawili wametapeli watu kutoka Pemba na Unguja wakiwalaghi kuwapatia ajira katika Mahakama ya Ardhi.

"Naomba jamii iwe makini, wapo watu wanaotatumia njia za udanganyifu kujipatia fedha, suala la ajira si rahisi lina michakato yake, matapeli hao wamefanikiwa kupata Sh1.6 milioni kutoka kwa wananchi,” amesema Mchomvu.