Wizara ya fedha kukusanya Sh4.9 trilioni mwaka 2024/25
Unguja. Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar inakadiria kukusanya Sh4.9 trilioni mwaka wa fedha 2024/25 sawa na ongezeko la asilimia 77 ikilinganishwa na makadirio ya kukusanya Sh2.76 trilioni yaliyopangwa kukusanywa mwaka wa fedha 2023/24.
Hayo yamebainishwa Juni 10, 2024 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo katika Baraza la Wawakilishi, huku akitaja vipaumbele 14 vya wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya kukusanya kodi.
“Fedha hizi ni kupitia mamlaka ambazo zinasimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango, katika kuimarisha mwelekeo wa uchumi wetu,” amesema.
Dk Saada amesema katika bajeti hiyo wizara imepangiwa kutumia Sh1,133 trilioni.
Akitaja vipaumbele hivyo Dk Saada amesema wanajiandaa kufanya upembuzi yakinifu kuhusu uanzishaji wa soko la hisa (ZSE) pamoja na Benki ya Uwekezaji Zanzibar (ZIB).
Kipaumbele kingine ni kuandaa kanzidata ya vipaumbele vya ujuzi vya Taifa (NSD) ambayo itatoa fani walizonazo katika soko la ajira na zinazohitajika pamoja na mfumo wa kuwatambua wahitimu wa elimu ya juu Zanzibar.
“Wizara itasimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali, kutekeleza bajeti yenye kuzingatia jinsia. Kuanza maandalizi ya kuanzisha Chuo cha Usimamizi wa Fedha Chwaka,” amesema.
Amekitaja kipaumbele kingine kuwa ni kuimarisha utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara wadogowadogo, ukusanyaji wa mapato katika masoko mapya, kufanya na kuratibu tafiti nne na maandiko mafupi ya sera 10 za kimkakati kulingana na vipaumbele vya tafiti vya Taifa.
Waziri Saada amesema wameshirikiana na Wizara ya Fedha ya bara katika upatikanaji wa rasilimali fedha za mikopo na misaada kwa ajili ya miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa uwanja wa ndege wa Pemba, mradi wa afya ya mama na mtoto na ujenzi wa barabara.
Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali kupitia bajeti ya kazi za maendeleo inaendelea na utekelezaji wa mpango kabambe wa uimarishaji takwimu awamu ya pili (TSMP II) ambao umelenga kuimarisha shughuli za utoaji wa takwimu za kawaida.
Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA)
Katika mwaka wa fedha 2024/25 ZRA imepangiwa kukusanya Sh845.9 bilioni sawa na asilimia 25 ya ongezeko la makadirio ya Sh675.6 bilioni ya mwaka wa fedha 2023/24 huku Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) unatarajia kukusanya Sh323.3 bilioni kutoka vyanzo vikuu viwili ambavyo ni michango ya wanachama na uwekezaji.
Michango ya wawakilishi
Mwakilishi wa Dimani, Mwanaasha Khamis Juma amesema pamoja na mafanikio yaliyofikiwa na wizara hiyo lakini kuna changamoto hususani ukosefu wa fedha hivyo inatakiwa kulitazama jambo hilo kuhakikisha zinapatikana kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Mwakilishi wa Mfenesini, Machano Othman Said amesema ofisi ya Mtakwimu Mkuu inatakiwa kufanya tafiti zaidi zikiwamo kuu mbili, kwanza kujua changamoto ya matukio ya moto ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara wakishirikiana na kikosi cha zimamoto.
Pia unaohusu suluhisho la ongezeko la ajali barabarani na mauaji kwani havileti tija katika kisiwa hicho, huku akiishauri Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kufungua matawi katika miji ya Mbeya, Mwanza na Arusha.
“ZSSF na ZRA wafanye kazi vizuri lakini waongeze kasi zaidi kwa kuwa na miradi ya kimaendeleo kwa upendeleo na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato.”
Naye mwakilishi wa kuteuliwa Juma Ali Khatib (Ada Tadea), amesema ZRA inastahili kupongezwa kwani malalamiko ya wafanyabiashara yamepungua kwa kiasi kikubwa.
“Mfumo wao wa kupokea simu ni mzuri sana kwa hiyo tuwapongeze sana kwa mwendo wanaokwenda nao hakika mapato yataongezeka zaidi,”amesema.
Hata hivyo, amesema zipo baadhi ya taasisi zinapangiwa makusanyo makubwa wakati hazina uwezo wa kukusanya kiwango hicho, “naishauri wizara kuangalia upya jambo hilo bila kuzipa mzigo mzito taasisi hizo (bila kuzitaja).”
Mwakilishi wa Mtoni, Hussein Ibrahim Makungu ameshauri kuimarisha zaidi mifumo ili kurahisisha ulipaji kodi kwani bado kuna usumbufu.
Amesema hata wao (wawakilishi) wanapaswa kupata semina kuhusu kodi ili wawe mabalozi wazuri kwa wananchi wanaowawakilisha kwenye majimbo yao.
Pia ametaka kuimarisha bandari na uwanja wa ndege kwani hiyo ndio milango mikuu ya kuingiza mapato Zanzibar.
Pia ameshauri, ZRA, uhamiaji na Kamisheni ya utalii wawe na mfumo wa pamoja, ili wanapoingia watalii kila mmoja ajue, jambo litakalosaidia kuongeza mapato na kuziba mianya ya wizi.