Friday August 15 2014

 

Dar es Salaam. Patrick Phiri, kocha mpya wa Simba amewasili katika ardhi ya Tanzania akionekana mpole vile vile kama alivyokuwa miaka mitatu iliyopita.


Alikuwa yule yule, ambaye alionekana mwenye aibu kiasi, mpole na anayezungumza taratibu na kwa makini.

Wakati kocha wa Croatia, Zdravko Logarusic akiwa ameondoka nchini takribani saa 48 zilizopita huku akishutumiwa kwa hulka ya ukali uliopitiliza iliyosababisha asielewane na mastaa wa timu hiyo, Phiri mwenye hulka tofauti na hiyo amewahi kushutumiwa kwa kuwa mpole zaidi na kuwaruhusu mastaa kufanya wanachotaka.Mastaa kama Juma Kaseja, Mussa Hassan Mgosi, Kelvin Yondani na wengineo walishutumiwa kwa kumuweka kiganjani kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya zamani hali iliyosababisha viongozi wasimuongezee mkataba wake miaka mitatu iliyopita ikiwa ni sababu tofauti ya iliyomfukuzisha Logarusic kuwa ni mkali sana.

Baada ya kutua jana, Phiri (58) alitarajiwa kumwaga wino wa kuinoa Simba kwa miaka miwili na aliahidi kurudisha furaha katika klabu hiyo kwani anaamini ilikuwa imepotea kutokana na matokeo iliyokuwa inayapata.

Phiri anayependelea kuvaa suti nyeusi alitua saa saba na nusu mchana na kupokelewa na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Idd Kajuna, Collin Frinch na Said Tully ambao walimpeleka Mikocheni kukutana na matajiri wa klabu hiyo ya Msimbazi.

Akizungumza na waandishi mara baada ya kutua nchini, Phiri alisema,”Namshukuru rais wa Simba, Evans Aveva, pia Tanzania ni kama nyumbani kwangu kwa pili, nimekuwa nikija mara kwa mara na kuondoka, nimefanya kazi na viongozi wa Simba siku za nyuma nikaondoka, sasa nimerudi tena kurejesha heshima ya Simba.