Kombe la Mapinduzi lilete tija Yanga, Azam, Simba

Monday January 4 2016

Inawezekana kuhoji mashindano haya ya Kombe la Mapinduzi yaliyoanza jana kisiwani Zanzibar na kushirikisha timu mbalimbali, zikiwamo za Ligi Kuu ya Bara, yana manufaa gani kwa maendeleo ya soka?

Lakini, mashindano yanayoshirikisha timu za Yanga na Azam, wawakilishi wetu kwenye mashindano ya klabu ya Afrika baadaye mwaka huu, yanaweza kuwa yenye manufaa.

Hata hivyo, ni iwapo tu yatatumiwa vizuri na makocha wa klabu hizo mbili katika kutengeneza vikosi kwa ajili ya mashindano hayo.

Ushauri wetu kwa makocha wa klabu hizo mbili zitakazoshiriki mashindano ya kimataiofa ya klabu mwaka huu ni kuyatumia vizuri kuwajenga vizuri wachezaji wao ambao watashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Pia, ni wakati mzuri wa kupata nafasi ya kusahihisha makosa ambayo timu hizo zimekuwa zikiyafanya kwenye ligi na mashindano ya Afrika kila mara zinaposhiriki.

Hivyo tunapenda kuwashauri makocha hao na wasaidizi wao wa ufundi kutumia mashindano hayo kufanya maandalizi ya mwisho kabla ya kuingia kwenye mechi hizo za Afrika mwezi ujao.

Ni lazima makocha watambue kuwa timu za Tanzania zimekuwa hazifanyi vizuri kwenye mechi za Afrika, hivyo mwaka huu zinatakiwa zifanye vizuri kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa mashabiki kuwa timu zetu haziwezi kuvuka raundi za mwanzo za mashindano ya kimataifa.

Tunawashauri wachezaji wa Yanga na Azam watambue kuwa wanakabiliwa na kibarua kikubwa. Hata kama wamepangiwa na timu dhaifu za raundi za awali, wanapaswa wazingatie maandalizi kwa kuwa watakutana na timu ngumu kutoka Afrika Magharibi na Kaskazini kwenye hatua za baadaye.

Itakuwa ajabu kwa makocha hao kuendelea kuwachezesha wachezaji ambao wamekuwa wakipata nafasi kwenye ligi, badala ya kuwapa nafasi hiyo wachezaji wote waliosajiliwa kucheza kwenye mashindano ya Zanzibar ili kujua uwezo wao.

Hali kadhalika, tunawashauri wachezaji wetu kuzingatia mafunzo wanayopewa na nidhamu ya mchezo ili waweze kufanya vizuri dhidi ya timu wanazopangiwa nazo. Mara nyingi makocha wanakuwa wanatimuliwa baada ya timu kufanya vibaya, lakini wakati mwingine makosa ya wachezaji ndio huchangia timu kufanya vibaya. Wito wetu ni kwa wachezaji pia kuzingatia wajibu wao na kujituma mazoezini, kwenye mechi za majaribio, za mashindano ya ndani na ya kimataifa.

Mbali na Azam na Yanga, klabu za Zanzibar zitakazoshiriki mashindano hayo hazina budi kutia nia zaidi, hasa ikizingatiwa kuwa Ligi Kuu ya visiwani imekuwa ikikumbwa na matatizo yaliyosababisha isimame kwa muda mrefu.

Maana yake ni kwamba wachezaji wa timu hizo hawajapata mechi za kutosha kuwawezesha kuwa tayari kimashindano. Kwa hiyo Kombe la Mapinduzi linazipa nafasi ya kupambana na timu kubwa ambazo zitasaidia kuwapa matayarisho mazuri kwa ajili ya ushiriki wao kwenye michuano ya Afrika mwaka huu.

Zaidi ya yote, tunazitakia kila la heri timu zote zinazoshiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu, tukizitaka ziache kuyachukuliwa kuwa ya kawaida na kushiriki kwa mazoea.

Uwapo wa timu kutoka nje ya nchi kunayapa mashindano hayo hadhi ya kimataifa na kwa maana nyingine kunazipa timu zote nafasi ya kuongeza uzoefu wa mashindano ya kimataifa.

Bila ya kuona umuhimu huo, timu zetu zitaendelea kushiriki kwa mazoea na kuondoa umuhimu wa mashindano hayo ya kila mwaka ya Kombe la Mapinduzi.