Njia bora ya kudumisha Muungano ni kufufua mchakato wa Katiba Mpya


Njia bora ya kudumisha Muungano ni kufufua mchakato wa Katiba Mpya

Mimi nafikiri kwamba kama kweli kuna mtu ana nia ya dhati ya kutatua kero za muungano na kuudumisha muungano wetu basi atakuwa na ujasiri wa kuilazimisha serikali iirejeshe mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya.

Naweza kusema mimi nipo katika kizazi cha Watanzania ambao wamezaliwa ndani ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao sherehe zake zinafanyika leo.  

Takribani miongo mitatu tangu kuundwa kwake, mimi ndiyo kwanza nilikuwa nazaliwa. Kwa hiyo mimi ni zao la muungano na najivunia kwa hilo haijalishi upatikanaji wake kutokana na nadharia kadhaa zilizopo, ambazo hapa si mahala pake.  

Itoshe tu kusema kwamba binafsi, kama ilivyo kwa maelfu ya vijana wengine wa Zanzibar, nimenufaika na muungano.

Nasema hivyo kwa kumaanisha kabisa kwani najiona kama moja kati ya ushahidi unaoishi wa kwa nini tunahitaji kuendelea kuungana.

Kwa kiasi kikubwa sana, elimu yangu ya shahada ya kwanza niliweza kuikamilisha kutokana na mkopo niliopata kutoka kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Tanzania (Heslb).

Punde tu baada ya kuhitimu kidato cha sita, niliomba mkopo kutoka Heslb na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar.

Hizi ni mamlaka mbili tofauti zenye kufanya kazi moja kwa walengwa tofauti. Wanafunzi wa Zanzibar wanaweza kuomba mikopo kutoka kwenye mamlaka zote mbili, fursa ambayo wenzao wa Bara hawana kwani hawawezi kuomba kwenye bodi ile ya Zanzibar.  Lakini kwa Zanzibar nilikosa mkopo wake.

Nakumbuka jinsi mimi na wenzangu tulivyokuwa tunaomba Mungu tupate mkopo wa Heslb kwani tulikuwa tunapenda muundo wake na uwezo wake wa kumsaidia mwanafunzi kukabiliana na gharama za maisha ya chuo.

Siwezi sema kwamba kama isingekuwa mkopo huo ndiyo ndoto yangu ya kupata elimu ya juu isingetimia, lakini pia sitasema uongo kwamba haukunisaidia, ulisaidia sana kwani ulibeba majukumu ambayo ingewapasa wazazi wangu kuyabeba.

Hii ni moja tu kati ya sababu nyingi ambazo zinanifanya niamini kwa nini tunauhitaji muungano.

Nyingine ni kama vile uhuru wa kutembea bila vikwazo kati ya sehemu zote mbili za muungano, suala la ulinzi na usalama na kwa umuhimu zaidi, udugu ambao tayari umeshajengeka kati yetu kama wananchi. 

Lakini huu ni upande mmoja tu wa shilingi na ni kutokana na nia hiyohiyo ya kudumisha muungano, ndiyo tunapaswa kuangalia pia upande wake wa pili ambao, kwa maoni yangu, una sura mbaya zaidi inayotishia uwepo wake. 

Moja kati ya mambo ambayo yanaufanya upande huu kuwa mbaya ni kile ambacho mimi nadhani kinahusu uwezo wa Wazanzibari kama watu kuamua mambo yao ndani bila ya kuingiliwa na serikali ya muungano, hususani katika eneo la siasa ambalo linahusisha uchaguzi wa serikali ya kuongoza visiwani humo.

Ninachokiona mimi na ambacho nadhani hakileti picha nzuri ya muungano ni uingiliaji wa wazi wa shughuli za kisiasa ndani ya Zanzibar.  

Lakini pia kuna hali ya watu kushindwa kupaza sauti zao dhidi ya wanayofanyiwa kwa kuhofia kuitwa magaidi. Ukienda Zanzibar leo, ni ngumu sana kuona aina yoyote ya harakati za kisiasa si tu dhidi ya kero za muungano bali hata ukinzani wa sera na hatua za serikali iliyopo madarakani.  

Aina yoyote ya harakati visiwani humo inamweka mtu hatarini ya kutafsiriwa kama gaidi, kitu ambacho kinawafanya vijana wengi kujiepusha nazo.

Pengine hakuna sheria ambayo inajulikana zaidi miongoni mwa vijana wengi wa Zanzibar kama Sheria ya Ugaidi ya mwaka 2002. Hii ndiyo sheria iliyopelekea kukamatwa kwa masheikh wa Uamsho Oktoba 2012 kwa tuhuma za ugaidi ambao kesi yao inaendelea mahakamani na kujenga hofu iliyopo.

Takribani miaka sita sasa tangu kukamatwa kwao, masheikh hawa ambao walikuwa mstari wa mbele kupaza sauti dhidi ya kinachoitwa kero za muungano, bado wapo mahabusu huku serikali ikiendelea kuchunguza mashtaka yao.  

Haya ni baadhi tu ya masuala mazito ambayo mimi nadhani yanatufanya wengi tunaotoka Zanzibar tuuangalie muungano kwa jicho la wasiwasi. Hii haimaniishi kwamba wenzetu Bara hawana kero zao za msingi. La hasha! Lazima watakuwa nazo lakini, kama nilivyosema awali, mimi natokea Zanzibar, na hivyo nazungumza kutika muktadha huo.

Kwa maoni yangu, kama kweli tumedhamiria kudumisha muungano, basi nadhani ni muhimu kuwashirikisha wananchi wenyewe katika zoezi hilo kwa kuwawezesha kutoa maoni na mapendekezo kwa uhuru jinsi ya kuuboresha.

Ni kwa bahati nzuri sana sehemu ya zoezi hili imeshafanyika na kilichobaki ni kutekelezwa kwa yale mapendekezo ambayo Watanzania, kwa umoja wao, waliyatoa kwa Tume Maalumu ya Mabadiliko ya Katiba au maarufu kama Tume ya Warioba. 

Ikifanya shughuli zake chini ya uenyekiti wa waziri mkuu mstaafu Joseph Warioba, tume hiyo iliyoundwa Aprili 2012 ilizunguka nchi nzima kukusanya maoni ya wananchi kuhusu uundwaji wa Katiba mpya.

Wakati wa zoezi hilo, moja kati ya masuala ambayo yalijadiliwa kwa kina ni lile la muungano ambapo wananchi wa Bara na Zanzibar, walitoa maoni yao kuhusu mambo mbalimbali ya muungano na nini kifanyike ili kuuboresha.

Ingawaje wananchi wengi hawakupendekeza waziwazi wazo la muungano wa serikali tatu, yaani ile ya Zanzibar, Tanganyika na Muungano, tume ilifikiri isingewezekana kuyatekeleza mapendekezo yao chini ya muundo uliopo wa serikali mbili, yaani ya Zanzibar na Muungano. Hii ndiyo sababu ya kuja na pendekezo la serikali tatu. 

Kwa bahati mbaya, rasimu ya katiba ambayo ilichukua pendekezo hili ilikataliwa na Bunge Maalum la Katiba lililokuwa limetawaliwa na wajumbe kutoka chama tawala ambao waliamua kuja na katiba tofauti kabisa inayoubakisha muundo wa serikali mbili. 

Mimi nafikiri kwamba kama kweli kuna mtu ana nia ya dhati ya kutatua kero za muungano na kuudumisha muungano wetu basi atakuwa na ujasiri wa kuilazimisha serikali iirejeshe mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya.

Serikali inaweza kufanya hivyo kwa kuanzia na rasimu ya katiba inayopendekezwa, au Rasimu ya Warioba kama inavyoitwa mara nyingi, ambayo Bunge Maalumu la Katiba liliibadilisha ili iweze kujadiliwa tena na kupelekwa kwenye kura ya maoni.

Ni kwa kufanya hivyo ndiyo tunaweza kusema mtu anataka kudumisha muungano na kwa kweli anaweza kuwa kwenye upande sahihi wa historia.

 Khalifa Said ni mwandishi wa habari za siasa katika magazeti ya The Citizen na Mwananchi. Twitter: @ThatBoyKhalifax