Bunge, BWL sehemu ya kero za Muungano


Bunge, BWL sehemu ya kero za Muungano

Miaka ya 55 imetimia tangu kuasisiwa kwa Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuzaliwa kwa Tanzania kukawa kifo cha Tanganyika. Upande wa pili, Zanzibar imebaki hai lakini kwa manung'uniko. Kuna Serikali ya Mapinduzi, vilevile kuna Baraza la Wawakilishi, yaani Bunge la Zanzibar.

Miaka ya 55 imetimia tangu kuasisiwa kwa Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuzaliwa kwa Tanzania kukawa kifo cha Tanganyika. Upande wa pili, Zanzibar imebaki hai lakini kwa manung'uniko. Kuna Serikali ya Mapinduzi, vilevile kuna Baraza la Wawakilishi, yaani Bunge la Zanzibar.

Tanganyika hakuna Bunge wala Serikali. Vuguvugu la wabunge wa Tanzania Bara (Tanganyika), maarufu kama G55, kudai Serikali ya Tanganyika na Bunge lake, nje ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano miaka ya 1990, lilizimwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Hali ya Tanganyika kukosa Bunge na Serikali, husababisha wabunge wa Tanzania wadhani Bunge la Tanzania ni Bunge la Tanganyika. Hili lilisababisha kauli zilizowaudhi mno wabunge wa Zanzibar mwaka jana.

Mbunge wa Nkasi (CCM), Ally Kessy alisema bungeni kuwa wabunge wa Zanzibar wasiwe wanahudhuria Bunge kipindi cha kujadili hoja ambazo si za Muungano. Alijielekeza zaidi kwenye bajeti za wizara, kwamba wasichangie zisizowahusu.

"Muda wa kujadili wizara ambazo siyo za Muungano mwende nje, mtupishe tubaki wenyewe. Tukimaliza tutawaita. Mnajadili Wizara ya Kilimo inawahusu? Wizara ya Maji inawahusu?" alisema Kessy akishangiliwa na wabunge wengi ambao ni wa CCM upande wa Tanzania Bara.

Mbunge anayewakilisha Baraza la Wawakilishi, Jaku Hashim Ayoub (CCM), alimworodhesha Kessy katika kero za Muungano. Mbunge wa Welezo (CCM), Saada Mkuya alisema kuna kauli zilizotolewa na bungeni, zinafanya wabunge wa Zanzibar wajione ni daraja la pili, wakati wabunge wote ni sawa.

Kulikuwa na hoja ya sukari ya Zanzibar kuruhusiwa kuuzwa Tanzania Bara. Serikali ilisema sukari ya Zanzibar haitoshelezi mahitaji ya Wazanzibari, kwa hiyo haiwezekani kuuzwa Bara. Baadhi ya wabunge wa Zanzibar walisema takwimu za uzalishaji sukari visiwani humo zinakosewa, kwamba kiasi kinachozalishwa ni kikubwa kuliko mahitaji.

Kessy katika hoja yake kuhusu sakata la sukari ya Zanzibar alisema sukari inayozalishwa Zanzibar ni kidogo na haiwatoshi Wazanzibari, alisema:

"Sukari mnalima tani 8,000 kwa mwaka, matumizi yenu ni tani 17,000. Au hamnywi chai. Kama hamna pesa ya kunywa chai semeni tuwasaidieni."

Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, badala ya kumjibu Kessy kwa hoja yake, wengine walifikia hatua ya kuishambulia Tanzania Bara. Yupo mjumbe alisema na yupo kwenye kumbukumbu kwamba Watanzania Bara ndiyo wana njaa, kwani wengi ni maskini.

Hivi karibuni, mbunge wa Temeke (CCM), Abdallah Mtolea alisema Tanzania Bara ndiyo inayopaswa kuumizwa na Muungano kwa sababu inaibeba Zanzibar. Akasema anayebebwa hawezi kuchoka. Zipo kauli nyingi hutolewa kwa namna ya "sisi na wao" ndani ya Bunge na Baraza la Wawakilishi. Ni hatari sana.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, alionya Aprili 2016 bungeni kuhusu kauli zenye kuukosea heshima Muungano. Alimtaja Kessy kwa jina, kwamba japo ni mbunge wa CCM lakini kauli zake ni zenye kukosa utambuzi kuwa Tanzania ni Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Pamoja na onyo hilo la Makamba, bado kauli za kibaguzi zinaendelea kushamiri bungeni. Unakuta mbunge anatoa kauli ya namna hii: "Kazi yenu kupitisha magendo mnaleta huku kwetu." Kauli ya hivyo ni kutoa hukumu kwamba Wazanzibari Bara siyo kwao, na wanaitumia kujinufaisha kwa biashara ya magendo. Je, Wazanzibari wote wanafanya magendo?

Mtu wa Tanzania Bara akienda kuweka makazi Zanzibar, halafu akapata kashfa ya ubakaji, hapo itamkwe Watanganyika kazi yao ni kwenda Zanzibar kubaka wanawake? Kwa nini na wahalifu wa Zanzibar wanaoingiza magendo kwa majahazi, wasichukuliwe ni wahalifu wachache kuliko kuchukuliwa ndiyo sifa ya Wazanzibari?

Kimsingi Bunge na Baraza la Wawakilishi, vimekuwa vyombo vyenye kukuza kero za Muungano kuliko kuzitatua. Wabunge na wawakilishi wenye kutoa kauli mbaya hawaonywi wala kuadhibiwa ndiyo maana wanaendelea.

Kama Muungano ni wa nchi mbili, kauli yenye kusema Zanzibar ina watu asilimia nne, kwa hiyo lazima wapate hivyohivyo si sawa. Kauli hiyo inazungumzwa ndani ya Bunge ambacho ni chombo alama ya Muungano. Uongozi wa Bunge kuwa kimya kwa kauli hizo au uongozi wa CCM kutomwonya mbunge wa chama chao mwenye kusema hayo ni nyongeza ya kero za Muungano.

Njia ni Serikali ya Kibunge

Nimezungumza hoja hii mara nyingi, kwamba usalama wa Muungano kwa namna ulivyo ni kuwa na Serikali ya Kibunge, yaani Parliamentary Democracy na kuachana na hii ya sasa ya nusu urais, kwa maana ya Semi Presidential.

Muundo wa Semi Presidential unamfanya Rais anakuwa kiongozi wa Serikali, vilevile ndiye Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu. Katika Parliamentary Democracy, Mkuu wa Nchi hawi kiongozi wa Serikali wala sehemu ya Serikali.

Tukishakubaliana kuhusu Parliamentary System, jukumu linabaki moja tu, kuunda Serikali mbili zisizoingiliana. Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar, kila moja inaongozwa na Waziri Mkuu.

Serikali ya Tanganyika ifanye kazi ya kuhudumia Watanganyika, na Serikali ya Zanzibar iwahudumie Wazanzibari, kusiwe na mwingiliano katika masuala ya Serikali hizo mbili. Kila moja itimize wajibu wake kwa uhuru.

Halafu awepo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye hatakuwa na Serikali, isipokuwa Mkuu wa Nchi, vilevile Amiri Jeshi Mkuu. Rais ndiye anakuwa nembo ya Muungano, maana cheo chake ni mwavuli utakaofunika pande zote mbili za Muungano.

Mkuu wa nchi hatakuwa na mamlaka ya kuingilia Serikali yoyote, kwa hiyo itapunguza malalamiko ya Muungano kwa sehemu kubwa, kwamba Wazanzibari watajiendesha wenyewe na Serikali yao, kama Watanganyika na Serikali yao, halafu tutabaki nchi moja kupitia mwavuli wa Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Rais.