Miaka 55 ya Muungano: Yajue majukumu ya NEMC katika kuhifadhi na kusimamia mazingira nchini


Miaka 55 ya Muungano: Yajue majukumu ya NEMC katika kuhifadhi na kusimamia mazingira nchini

Kumekuwepo na kukua kwa uelewa wa wajibu wa kila mmoja wa kutunza mazingira, kushiriki kikamilifu katika michakato na maamuzi yanayohusu mazingira.

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilianzishwa na sheria ya Bunge namba 19 ya mwaka 1983 kutoa ushauri kwa Serikali juu ya masuala yote yanayohusu usimamizi wa mazingira. 

Sheria ya Mazingira Na. 20 ya 2004 ikaendeleza uwepo wa Baraza lenye wajibu wa kutekeleza baadhi ya majukumu ya usimamizi wa mazingira chini ya Sheria ya Mazingira. Katika makala hii inayoenda sambamba na maadhimisho ya miaka 55 ya Muungano.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Mhandisi Dk. Samuel G. Mafwenga anaeleza zaidi kuhusu majukumu ya Baraza, Tafsiri ya Mazingira na Uchafuzi wa Mazingira, hali ya utunzaji wa mazingira nchini, changamoto na mambo yanayochangia uharibifu wa mazingira, sheria zinazoongoza usimamizi na utunzaji wa mazingira na jitihada zinazofanywa na NEMC kutoa elimu kwa jamii namna ya kuhimili uharibifu wa mazingira na jinsi inavyoshirikiana na wadau wengine wa mazingira.

Majukumu ya Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)

Kulingana na Sheria ya Mazingira Na. 20 ya Mwaka 2004, majukumu ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ni pamoja na:

 1. Ukaguzi wa mazingira;
 2. Kufanya mapitio ya taarifa ambazo zitasaidia katika hifadhi na usimamizi wa ubora wa mazingira;
 3. Kufanya na kuratibu utafiti na uchunguzi kwenye  mazingira ili  kukusanya na kusambaza taarifa kuhusu matokeo ya utafiti na uchunguzi huo;
 4. Kupitia na kutoa mapendekezo juu ya kupitisha taarifa za tathimini ya athari ya mazingira;
 5. Kuainisha aina ya miradi ambayo itahitaji Tathmini ya athari kwa mazingira na ufuatiliaji;
 6. Kusimamia utekelezaji wa viwango vya usafi wa mazingira na kuhakikisha kuwa viwango hivyo vinafuatwa;
 7. Kuandaa mbinu na kuweka mikakati ya uzuiaji wa ajali ambazo zinaweza kusababisha uharibifu wa mazingira;
 8. Kushirikiana na Wizara na wadau wengine kuandaa mipango yenye lengo la kutoa elimu ya mazingira na kuongeza uelewa kwa umma juu ya umuhimu wa kuwepo kwa usimamizi bora wa mazingira
 9. Kutoa na kusambaza machapisho na vitabu vya miongozo kuhusu usimamizi wa mazingira na uzuiaji au upunguzaji wa uharibifu wa mazingira;
 10. Pale inapowezekana, kutoa ushauri na msaada wa kiufundi kwa taasisi mbalimbali zinazojihusisha na usimamizi wa maliasili na mazingira ili kuziwezesha kutekeleza wajibu wao ipasavyo; na
 11. Kufanya shughuli nyingine yoyote ambayo Waziri ataagiza katika utekelezaji wa Sheria hii.

 

NEMC inatafsiri vipi neno “Mazingira” na “Uchafuzi wa Mazingira?

Sheria ya Mazingira Na. 20 ya Mwaka 2004 inatoa tafsiri ya Neno Mazingira na Uchafuzi wa Mazigira kama ifuatavyo:

Neno “Mazingira” linahusisha maumbile halisi yawazungukao binadamu ikiwa ni pamoja na hewa, ardhi, maji, tabianchi, sauti, mwanga, harufu, ladha, vijiumbe, hali za kibaolojia za wanyama na mimea, rasilimali za kitamaduni na masuala ya uchumi jamii na inahusisha mazingira asilia na yaliyoundwa na binadamu na jinsi yanavyoingiliana;

“Uchafuzi wa Mazingira” ni mabadiliko ya moja kwa moja au yasiyo ya moja kwa moja, ya rasilimali za kimaumbile, hali ya joto, kikemikali, kibiolojia, au sifa nururishi, ambazo kwazo ni sehemu ya mazingira kwa kumwaga, kuachia, au kuweka taka; hivyo kuleta madhara kwa matumizi yenye manufaa, kusababisha hali ambayo ni hatari kwa jamii kiafya, kiusalama au ustawi wa binadamu, au kwa wanyama, ndege, wanyamapori, samaki au viumbe wa majini, au kwa mimea au  kusababisha kukiukwa kwa sharti lolote, kikomo, au kizuio chochote kwa mujibu wa leseni chini ya Sheria hii;

Ni vitu gani vinavyochangia kutokea kwa uharibifu wa mazingira?

 • Kuongezeka sana kwa matumizi ya mifuko ya plastiki nchini inayotumika kubebea bidhaa mbalimbali madukani, sokoni na maeneo mengine. Ongezeko la mahitaji na matumizi ya mifuko ya plastiki limechangia kuongezeka kwa taka za plastiki zinazozalishwa ambazo huchangia kuziba miundombinu ya maji ya mvua na majitaka na kusababisha mafuriko na kuenea kwa magonjwa (kipindupindu na magonjwa ya kuhara).

 

 • Utiririshaji katika mazingira maji yenye kemikali kutoka viwandani

 

 • Baadhi ya viwanda (kutokuwa miundombinu sahihi ya mazingira) kuweka angani hewa ukaa kutokana na matumizi ya nishati ya mafuta.
 • Utupaji ovyo wa taka unaopelekea uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji.

 

 • Kilimo kwenye miinuko, kingo za mito, misitu na aradhioevu kunapelekea uchafuzi na kupungua ubora wa maji au vyanzo vya maji.

 

 • Uharibifu wa misitu unaotokana na kukata miti ovyo kwa ajili ya shughuli za kilimo, ujenzi na mahitaji makubwa ya nishati ya mkaa/kuni.

 

 • Mabadiliko ya tabianchi yanayohusisha kubadilika kwa majira kwa mfano mvua kutonyesha kwa wakati, ongezeko la joto, mafuriko, ukame ongezeko la kina cha bahari, kupungua vya vina mito na maziwa, n.k

 

 • Ukosefu wa mpangilio mzuri wa uanzishaji na ukuaji wa miji nchini katika maeneo yetu mengi yanayokua kwa kasi, hivyo kusababisha matatizo makubwa ya kimazingira na kiafya. Usimamizi bora wa mazingira mijini unaweza kusaidia kuepusha athari hasi nyingi za kimazingira.

 

 • Kutokea kwa majanga kama vile mafuriko, matetemeko ya ardhi na sunami ni mojawapo ya vyanzo vya uharibifu wa mazingira.

 

Sheria zinazoongoza usimamizi na utunzaji wa mazingira

Sheria ya mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 inatambua kuwepo kwa sheria nyingine za kisekta zinazohimiza hifadhi na Usimamizi wa mazingira. Baadhi ya Sheria hizo ni:-

 1. Sheria ya Ardhi Na 4 ya mwaka 1999
 2. Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na 5 ya mwaka 1999
 3. Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002
 4. Sheria ya Huduma ya Maji na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2009
 5. Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji ya mwaka 2009
 6. Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na marekebisho ya 2017
 7. Sheria za Mamlaka za Serikali za Mitaa na 7 na 8 za mwaka 1982
 8. Sheria ya Hifadhi ya Wanyama pori ya mwaka 1974, n.k.

 

Sheria zinasisitiza uvunaji na matumizi ya rasilimali kwa njia endelevu zinazozingatia utunzaji wa mazingira.

Jitihada za Baraza katika kutoa elimu kwa jamii juu ya kuzuia athari za uharibifu wa mazingira

Katika jitihada za kutoa elimu kwa jamii juu ya kuzuia athari za uharibifu wa mazingira, Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) linafanya mambo yafuatayo;

 • Kuandaa na kutekeleza programu (kupitia radio, televisheni na magazeti) za kukuza weledi kwa umma kuhusu masuala ya mazingira na kuzuia athari za uharibifu wa mazingira.

 

 • Kuandaa machapisho na vitabu vinavyotoa elimu ya mazingira kwa umma.

 

 • Kuendelea kuchapisha na kusambaza vitabu vya miongozo, kanuni za kisheria au miongozo kuhusu usimamizi wa mazingira na kuzuia au kupunguza uharibifu wa mazingira.

 

 • Kuingiza elimu ya mazingira katika mitaala ya shule.

 

 • Kupitia Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) kuendelea kuhamasisha ushirikishwaji wa wananchi katika kuelewa athari mbalimbali zitokanazo na miradi ya maendeleo na namna ya utekelezaji wa usimamizi wa mazingira.

 

 • Kuendelea kufanya uchunguzi na utafiti utakaosaidia kuzuia athari za uharibifu wa mazingira.

 

 • Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuendelea kufanya na kuratibu utafiti na uchunguzi kwenye mazingira ili kukusanya na kusambaza taarifa kuhusu matokeo ya utafiti na uchunguzi huo.

 

Hali ya utunzaji wa mazingira ilivyo kwa sasa hapa nchini

Ni takribani miaka 15 ya utekelezaji wa Sheria ya Mazingira Na.20 ya mwaka 2004. Usimamizi wa utunzaji wa mazingira kwa kipindi chote hiki kimeongeza uelewa wa elimu na utunzaji wa mazingira kwa vitendo.

Wadau mbalimbali wa mazingira wameongeza ufahamu wa hatari zilizopo na zinazoweza kujitokeza katika mazingira ikiwa ni pamoja na kuzuia uchafuzi katika maji, hewa au ardhi, utupaji na umwagaji na utunzaji wa takamadhara.

Kumekuwepo na kukua kwa uelewa wa wajibu wa kila mmoja wa kutunza mazingira, kushiriki kikamilifu katika michakato na maamuzi yanayohusu mazingira.

Pamoja na uelewa na utunzaji wa mazingira kuongezeka miongoni mwa jamii hali ya utunzaji wa mazingira imeendelea kukumbwa na changamoto kubwa za kimazingira katika sekta mbalimbali. Changamoto hizi zinahusisha mrundikano wa taka katika miji; uchafuzi wa mito, maziwa na bahari; uvuvi haramu, uchafuzi kutoka viwandani na shughuli za kilimo; uharibifu na ukataji ovyo wa misitu.

Kulingana na changamoto zilizopo za mazingira na zinazoendelea kukua hususani kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na mahitaji yao kunakopelekea uhitaji mkubwa wa matumizi ya rasilimali. Kuliko wakati mwingine wowote ule, ni muhimu sana utunzaji wa mazingira kuwekwa kuwa kiini cha kila uamuzi unaofanywa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Ushirikiano wa Baraza na wadau wa mazingira katika kuhakikisha kuwa athari za kimazingira zinapungua kama si kuisha kabisa

Sheria ya Mazingira ilipitishwa na Bunge mwaka 2004 na kuanza kutumika rasmi mwaka 2005. Tangu kuanza kutumika kwa sheria ya Mazingira, Baraza limekuwa likifanya yafuatayo kama juhudi za kuzuia uharibifu wa mazingira:

 • Kutoa elimu ya mazingira kwa wananchi na wadau mbalimbali wa mazingira kuhakikisha wanakuwa na ufahamu mzuri kuhusiana na Sheria ya Mazingira na Kanuni mbalimbali za mazingira,

 

 • Kwa kuvishirikisha vyombo mbalimbali vya habari (televisheni, radio, magazeti n.k) katika kufikisha elimu na taarifa mbalimbali za mazingira katika umma na jamii. Habari ama taarifa nyingi za mazingira huifikia jamii kupitia waandishi wa habari. Aidha taarifa muhimu za mazingira zenye ubora mkubwa pia hupatikana katika magazeti na majarida.

 

 • Kuwasisitizia wawekezaji kujali na kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu zilizowekwa na Serikali katika kuendesha miradi yao,

 

 • Kuwakumbusha kwa kutoa adhabu wale wote ambao wanavunja Sheria ya mazingira na kanuni zake.

 

 • Kuipongeza miradi ya maendeleo iliyofanya vizuri katika utunzaji wa mazingira kuzidisha juhudi katika utunzaji wa mazingira.

 

NEMC ilivyojipanga katika kukabiliana na changamoto za kimazingira zitokanazo na shughuli za viwandani katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea kwenye uchumi wa viwanda

Baraza limejipanga kuongeza ueledi wa utunzaji wa mazingira miongoni mwa umma na wamiliki wa viwanda na msisitizo wa utekelezaji wa Sheria ya Mazingira na kanuni zake katika kuendeleza rasilimali za nchi yetu kwa kuzielekeza kwenye programu sahihi za utunzaji wa mazingira.

Kuendelea kujenga uwezo wa watumishi wa Baraza katika kusimamia shughuli za utunzaji wa mazingira.

Kuandaa Kanzidata ya viwanda vyote nchini ili kuwezesha shughuli za uperembaji wa shughuli za utunzaji wa mazingira katika viwanda.

Kuimarisha timu za uperembaji na ukaguzi wa mazingira (environmental compliance monitoring and audit).

Kuimarisha utendaji kazi wa ofisi za NEMC (katika kanda) wa kusimamia utunzaji wa mazingira na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika maeneo hayo. Maafisa mazingira katika ngazi mbalimbali ni watendaji wakuu wanaosimamia mazingira na ni tegemeo la Serikali na wananchi kwa ujumla katika kuitekeleza Sheria ya Mazingira. 

Kuhamasisha matumizi ya sayansi na teknolojia katika kutatua matatizo ya mazingira na kuimarisha udhibiti wa taka hatarishi (hazardous waste).

Kuhakikisha viwanda vinakuwa na miundombinu sahihi ya mazingira inayohakikisha maji yenye kemikali viwandani yanatibiwa kabla ya kuachiwa kuingia katika mazingira. Kufanya tafiti za mazingira ili kutatua changamoto mbalimbali za mazingira na kusaidia maamuzi ya kupitisha miradi ya maendeleo.

Mikakati ya Baraza katika maadhimisho ya miaka 55 ya Muungano

Katika maadhimisho haya ya miaka 55 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Baraza limedhamiria kutambua mchango wa umma na kutia moyo bidii zinazofanywa na vyombo vingine kwa lengo kuendeleza elimu ya mazingira na elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa usimamizi mwafaka wa mazingira.

Kuwapa wananchi ufahamu mkubwa zaidi katika maana halisi ya umuhimu wa kutunza mazingira na jinsi mifumo ikolojia inavyotegemeana, uharibifu wa ikolojia mojawapo huleta athari kwa mfumo mzima wa ikolojia.

Wito wa NEMC kwa Watanzania katika kipindi hiki cha maadhimisho ya sherehe za Muungano

Kila mwananchi ni mdau wa mazingira hivyo tunapaswa kuyatunza mazingira yetu na kutumia rasilimali zilizomo kwa njia endelevu kwa kuzingatia uwepo wake na wa vizazi vijavyo.

Kila mmoja wetu kwa nafasi yake anatakiwa ashiriki kikamilifu katika hifadhi ya mazingira kulingana na Sheria ya mazingira inavyoelekeza.

Kuwataka wale wote ambao miradi yao ina sifa ya kufanyiwa TAM lakini haijafanyiwa TAM kuisajili mara moja miradi hiyo katika Baraza na kupata maelekezo zaidi.