OSHA: Hivi ndivyo tunavyoadhimisha siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi Duniani


 OSHA: Hivi ndivyo tunavyoadhimisha siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi Duniani

Jukumu kubwa la OSHA ni kusimamia Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi na ili kukamilisha jukumu hilo kikamilifu, Wakala uliunda Kurugenzi yake ya Usalama na Afya mahali pa kazi ambayo imegawanyika katika sehemu mbili; Usalama na Afya. 

Aprili 28 ya kila mwaka, Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi. Siku hii huadhimishwa kama kampeni ya kidunia yenye lengo la kubainisha changamoto za kiusalama na afya zilizopo na kutazama namna kujenga na kuhamasisha utamaduni wa kujikinga na madhara yaliyopo katika sehemu za kazi kunavyoweza kupunguza matukio ya vifo, ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani chimbuko lake ni iliyokuwa siku ya Kimataifa ya kuwakumbuka walioumia, waliopata magonjwa ama kupoteza maisha wakiwa kazini. Siku hiyo ya kuwakumbuka waathirika hao ilianza kuadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1996. Maadhimisho hayo yalikuwa yakifanywa na Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Duniani kwa ufadhili wa kamisheni ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa.

Ilipofika mwaka 2003, Shirika la Kazi Dunia lilianza kujihusisha na maadhimisho ya siku hii baada ya kupata mwaliko kutoka kwa shirikisho hilo la vyama vya wafanyakazi duniani. Tangu mwaka huo, ILO imekuwa ikiizingatia siku hii kwa kuweka mkazo katika utamaduni wa ushirikiano na majadiliano ya kijamii katika kushughulikia masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi.

Aidha, tangu Shirika la Kazi lilipoanza kujihusisha na maadhimisho haya, Aprili 28 imekuwa ikitazamwa kama siku kukuza uelewa kimataifa kuhusu Usalama na Afya miongoni mwa vyama vya wafanyakazi, waajiri na serikali.

ILO inatambua uwajibikaji wa pamoja miongoni mwa wadau wote muhimu na kuwasisitiza kuhamasisha utamaduni wa kujikinga dhidi ya vihatarishi vya kiusalama na afya ili kutimiza wajibu wao wa kuzuia ajali, magonjwa na vifo vinavyokutokea katika sehemu za kazi na hivyo kuwapa wafanyakazi fursa ya kurejea majumbani kwao wakiwa salama.

Hapa kwetu Tanzania siku hii ilianza kuadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2004. Tangu wakati huo tumekuwa tukiadhimisha siku hiyo kila mwaka na kwa mwaka huu tunaadhimisha kwa mara ya 16.

Maadhimisho haya yamekuwa yakifanyika katika mikoa mbali mbali nchini yakiwa na kauli mbiu tofauti kila mwaka. Ifuatayo ni orodha ya mikoa yalikofanyika maadhimisho tangu mwaka 2004 pamoja na miaka husika katika mabano;

Dar es Salaam (2004, 2005, 2012, 2013 na 2014), Arusha (2006), Mwanza (2007), Mbeya (2008 na 2019), Dodoma (2009, 2015 na 2016), Morogoro (2010), Ruvuma (2011), Kilimanjaro (2017), Iringa (2018).

Aidha, Shirika la Kazi Duniani hutoa kauli mbiu inayoongoza shughuli za maadhimisho kwa mwaka husika. Kwa mwaka huu ujumbe wa maadhimisho ni: “Usalama na Afya na mustakabali wa kazi” (Safety and Health and the future of work).

Hata hivyo, ili kuleta uwiano kati ya kauli mbiu ya maadhimisho kidunia na uhalisia wa mazingira na sera za nchi yetu kwasasa ambapo msisitizo wake ni kujenga uchumi wa viwanda, kauli mbiu hiyo imeboreshwa na kuwa “Usalama na Afya na mustakabali wa kazi kuelekea uchumi wa viwanda.”

Kauli mbiu hii inaendana na kipindi hiki ambacho ILO inatimiza miaka 100 ya kushiriki katika kuimarisha Usalama na Afya katika sehemu za kazi duniani kote.

Aidha shirika hili linaleta changamoto kwa wadau katika kutazama namna ya kuendeleza jitahada hizi katika kipindi kijacho kupitia teknolojia pamoja na mambo mengine ikiwemo maendeleo endelevu na mabadiliko ya tabia nchi.

Kitaifa maadhimisho haya huratibiwa na serikali kupitia Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa kazi (OSHA). Kila mwaka, serikali imekuwa ikishirikiana na wadau wa utatu yaani Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) pamoja na Chama cha Waajiri (ATE) katika kuandaa na kuratibu maadhimisho hayo kwa kutekeleza shughuli mbalimbali zikiwemo; Kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari kwa lengo la kuongeza ufahamu kuhusu usalama na afya miongoni mwa wadau na kufanya makongamano ya wafanyakazi, waajiri na wananchi wote kwa ujumla.

Shughuli nyinginezo ni kutoa mafunzo ya Usalama na Afya kwa wajasiriamali wadogo ambao mara nyingi wamekuwa wakiachwa nyuma katika mfumo ulio rasmi, kufanya maonesho ya Usalama na Afya kazini pamoja na kutoa tuzo kwa wadau wanaofanya vizuri katika kuboresha Usalama na Afya kwenye sehemu zao za kazi.

Taarifa iliyotolewa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, inafafanua jinsi taasisi yake ilivyojipanga kuadhimisha siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi Duniani kwa mwaka huu.

Maadhimisho ya mwaka huu kitaifa yatafanyika mkoani Mbeya yakiongozwa na kauli mbiu isemayo “Usalama na Afya na mustakabali wa kazi kuelekea uchumi wa viwanda” (Safety and Health and the future of work towards industrial economy).

Katika maadhimisho haya mwaka huu, Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa kazi imejiandaa kufanya shughuli mbalimbali kuelekea siku ya kilele kama yafuatayo;

Shindano la tuzo za Usalama na Afya mahali pa kazi.

Wakala wa Usalama na Afya mahali pa kazi, umeandaa shindano la tuzo kwa maeneo ya kazi ambayo yanatekeleza vyema Sheria Na.5 ya Afya na Usalama mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

Taarifa kuhusu shindano husika pamoja na utaratibu wake wa kushiriki ulitangazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari na kuwekwa katika tovuti za OSHA na wadau wake. Maeneo mbali mbali ya kazi ambayo yalipenda kushiriki na yenye vigezo yaliwasilisha maombi ya kushiriki shindano hilo. Maeneo ya kazi takribani 30 walijitokeza kushiriki katika shindano husika.

Tuzo za shindano hili zinatarajiwa kukabidhiwa kwa washindi katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Usalama na Afya mahali pa kazi Duniani ambayo ni tarehe 28 Aprili 2018 na Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu), Mh. Jenista Mhagama.

Maonesho ya Afya na Usalama mahali pa kazi

Katika maadhimisho ya siku ya Afya na Usalama mahali pa kazi mwaka huu, OSHA imeandaa maonesho ya Usalama na Afya mahali pa kazi yenye lengo la kuwaleta pamoja wadau wetu kuja kuonesha mifumo mbalimbali ya kiusalama ambayo wanaitumia katika maeneo yao ya kazi inayosaidia kulinda Afya na Usalama wa wafanyakazi. Takribani washiriki 40 wamethibitisha kushiriki katika maonesho hayo.

Maonesho haya yanayofanyika katika viwanja vya Bustani ya Jiji la Mbeya karibu na uwanja wa Sokoine, yatawasaidia wadau na waajiri mbalimbali kubadilishana uzoefu wa namna bora zaidi za kulinda Afya na Usalama wa wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi.

Mafunzo ya Afya na Usalama mahali pa kazi kwa wajasiriamali wadogo

Mafunzo haya ni mwendelezo wa taasisi katika kutoa mafunzo ya Afya na Usalama mahali pa kazi kwa watanzania. Mwaka huu mafunzo haya yamejikita katika maeneo mbali mbali ya Nyanda za Juu Kusini katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, Songwe na Katavi.

Mafunzo haya yatahusisha makundi mbalimbali wakiwemo wachimbaji wadogo, wakulima, watu wanaofanya shughuli za misitu na mbao pia kutakuwa na kundi kubwa la mafundi katika Nyanja mbali mbali ambao watapewa mafunzo ya namna ya kujikinga wakiwa kazini pamoja na vifaa mbalimbali vya kujikinga dhidi ya vihatarishi kulingana na shughuli zao.

Kongamano la Afya na Usalama mahali pa kazi

Kitu kingine ambacho OSHA wanatarajia kukifanya katika maadhimisho ya siku hii muhimu kwa mwaka huu ni kuendesha Kongamano la Afya na Usalama mahali pa kazi.

Kongamano hili linawahusu waajiri au wamiliki wa sehemu za kazi kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini. Lengo la kongamano hili ni kuwaleta kwa pamoja waajiri ama wamiliki wa sehemu za kazi ili kufanya nao majadiliano kuhusu kuboresha Afya na Usalama mahali pa kazi.

Kongamano hili kwa mwaka huu litakwenda sambamba na uzinduzi wa kampeni ya kuzuia ajali na magonjwa katika sehemu za kazi ijulikanayo kama Vision Zero yenye lengo la kuhamasisha wamiliki wa maeneo ya kazi kuwa na mfumo wa kujisimamia wenyewe katika kuboresha mifumo ya Afya na Usalama mahali pa kazi. Waajiri wapatao 100 wanatarajiwa kushiriki katika kongamano hilo.

Mafanikio ya Maadhimisho

Kupitia maadhimisho hayo, serikali imekuwa ikiwakumbusha waajiri, wafanyakazi na umma kwaujumla kuhusu umuhimu pamoja namna bora zaidi za kuboresha mazingira ya kazi. Serikali pia imekuwa ikitoa motisha kwa kwa waajiri wanaozingatia vyema Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 kwa kuwapa tuzo maalum. Tuzo hizo hutolewa kama sehemu ya kutambua mchango wao katika utekelezaji wa sheria na kuleta hamasa kwa maeneo mengine ya kazi yaweze kufanya vizuri pia.

Aidha, serikali imekuwa ikitumia maadhimisho kukuza uelewa wa masuala ya Afya na Usalama miongoni mwa wananchi wake kupitia kampeni zinazofanywa katika vyombo vya habari, makongamano na mafunzo ambayo hutolewa kwa makundi mbali mbali ya wajasiriamali wadogo.

Hatua hizo zimefanya sehemu nyingi za kazi kuweka mifumo bora, sera, mikakati pamoja na programu za kulinda Afya na Usalama wa wafanyakazi. Jambo ambalo limesaidia sana katika kupunguza ajali na magonjwa katika maeneo ya kazi.

Kutokana na hamasa hiyo inayotolewa katika maadhimisho hayo, sehemu nyingi za kazi zimeweka huduma za msingi za Usalama na Afya kwa wafanyakazi wao mfano upimaji wa afya za wafanyakazi, kutathmini vihatarishi sehemu za kazi na mafunzo ya Afya na Usalama kwa wafanyakazi.

OSHA inavyosimamia Usalama na Afya kazini

OSHA ni kifupi cha maneno ya kiingereza (Occupational Safety and Health Authority) ambapo katika lugha ya Kiswahili inajulikana kama ‘Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi’, hii ni taasisi ya serikali ambayo ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu iliyoanzishwa tarehe 31 Agosti, 2001 chini ya Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 ya mwaka 1997 kama sehemu ya maboresho katika utoaji huduma kwenye sekta ya umma.

Taasisi hii ina dhamana ya kusimamia utekelezaji Sheria Na.5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003.

Kabla ya Wakala huu kuanzishwa, usimamizi wa Usalama na Afya mahali pa Kazi ulikuwa sehemu chini ya Idara ya Kazi iliyojulikana kama Kitengo cha Ukaguzi wa Viwanda (Factory Inspectorate Unit); ambacho kutokana na uwigo wake mdogo kisheria hakikuweza kukidhi mahitaji ya usimamizi wa huduma za Usalama na Afya nchini. Kitengo hiki kilikuwa kinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Ukaguzi wa Viwanda ya mwaka 1950 (Factory Ordinance, 1950), ambayo ilijikita zaidi katika masuala ya Usalama huku masuala ya Afya yakiwa si sehemu yake.

Kimsingi usimamizi huo haukukidhi vigezo vilivyowekwa na Shirika la Kazi Duniani inayozitaka nchi wanachama kuwa na chombo cha kitaifa cha kusimamia Usalama na Afya Mahali pa Kazi.

Kusudi ya kuanzishwa kwa Wakala huu ilikuwa ni kupata chombo cha Serikali chenye jukumu la kuboresha na kusimamia Usalama na Afya mahali pa kazi Tanzania Bara, ambayo katika usimamizi huo utaongeza tija na uzalishaji mali hivyo kukuza pato la taifa.

Kwa mujibu wa maelezo ya Afisa Uhusiano wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Eleuter Mbilinyi, Wakala huo unatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria Na.5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake.

Majukumu ya OSHA

Jukumu kubwa la OSHA ni kusimamia Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi na ili kukamilisha jukumu hilo kikamilifu, Wakala uliunda Kurugenzi yake ya Usalama na Afya mahali pa kazi ambayo imegawanyika katika sehemu mbili; Usalama na Afya.  

Kazi zinazofanywa na sehemu hizi mbili zote kwa pamoja zinalenga kuboresha mazingira ya kazi kwa wafanyakazi hususani katika kutoa huduma za ukaguzi wa usalama mahali pa kazi na pia kutoa huduma za upimaji wa afya za wafanyakazi.

Huduma za Usalama Mahali pa Kazi

Huduma hii inahusika na usimamizi wa mifumo yote inayowekwa katika sehemu za kazi kwa ajili ya kuwakinga wafanyakazi dhidi ya ajali na magonjwa yatokanayo na kazi. Mifumo inayoelezwa hapa inatazamwa kama viwango vya kitaifa vinavyozingatia viwango vya Shirika la Kazi Dunuani (WHO-OSH 2001).

Aidha, Sheria Na.5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 inasisitiza wajibu wa mwajiri na mfanyakazi kuhakikisha kuwa eneo la kazi ni salama kwa maana ya kuwa na mifumo inayozuia ajali ama magonjwa yatokanayo na kazi.

Aina ya kaguzi katika sehemu za kazi

Aina ya kaguzi katika sehemu za kazi ambazo zinafanywa na Wakala wa Usalama na Afya mahali pa kazi ni pamoja na; Ukaguzi wa Jumla, Ukaguzi wa mitambo, Ukaguzi wa usalama wa umeme, Ukaguzi wa viwango vya mazingira ya kazi na Ukaguzi wa Egonomia.

Kwakuhitimisha, OSHA inapenda kuwaalika wadau wake na Watanzania wote kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya mwaka huu yanayofanyika kitaifa mkoani Mbeya. Aidha inawaalika kuitafakari kauli mbiu ambayo inatoa wito wa kufanya tathmini ya hali ya Usalama na Afya kwasasa huku tukijaribu kujenga taswira ya hali itakavyokuwa katika kipindi kijacho kwakuzingatia mabadiliko makubwa ya kiteknolojia ambayo dunia inayapitia.