Benki ya NIC Tanzania yatoa huduma kwa wafanyabiashara Zanzibar


Benki ya NIC Tanzania yatoa huduma kwa wafanyabiashara Zanzibar

Takwimu zinaonyesha Zanzibar imeendelea kujenga uchumi imara na endelevu, ufanisi katika mfumo wa fedha ni moja ya mahitaji ya muhimu na ya msingi katika ukuaji wa uchumi na maendeleo kwa ujumla. Tukiwa na hili akilini benki ya NIC Tanzania iliona umuhimu wa kuwekeza hapa Zanzibar ili kuendeleza ukuaji wa uchumi.

Benki ya NIC Tanzania ilizindua rasmi tawi lake jipya huko Zanzibar Februari 21, mwaka 2019. Tawi hilo linapatikana katika Jengo la Muzammil Centre, mtaa wa Mlandege.

Tukio hilo kubwa la kihistoria liliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Margaret Karume na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mwenyekiti wa bodi ya NIC, Sharmapal Aggarwal, Wakurugenzi wa bodi hiyo na wateja wa benki hiyo ambao ni wakazi wa Zanzibar. 

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Dkt.Khalid Salum Mohamed akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein.

Uzinduzi huo uliongeza idadi ya matawi kutoka matano na kufikia sita kwa bara na tawi moja pekee kwa upande wa visiwani.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Margaret Karume, alielezea historia fupi ya benki, “Benki ya NIC Tanzania ni benki ya kibiashara ambayo mnamo mwaka 2010, Benki mama ya NIC (NIC Bank Group) ilinunua hisa katika benki ya Savings and Finance (S&F) Commercial Bank na kuibadilisha kwa mafanikio makubwa kuwa benki ya NIC Tanzania. NIC Bank Group ndio benki mama ya benki ya NIC Kenya, ambayo ina mafanikio makubwa sana Kenya ambapo ni benki ya 7 kwa ukubwa wa wanahisa naya 9 kwa ukubwa wa rasilimali.

Hapo awali tulikuwa na matawi matano (5) nchini Tanzania, matawi mawili (2) yakiwemo Arusha na Mwanza, na matatu (3) Dar es Salaam- Ohio, Samora na Kariakoo, Benki ya NIC Tanzania Ltd iko chini ya Kundi la NIC PLC ambayo ni benki inayotoa huduma zote za kibenki ikiwa na matawi arubaini na nne(44) nchini Kenya, Tano(5) nchini Tanzania, na tatu(3) nchini Uganda na imeshashinda tuzo nyingi za kidijitali katika huduma za benki katika Kanda.”

Karume alielezea, “Takwimu zinaonyesha Zanzibar imeendelea kujenga uchumi imara na endelevu, ufanisi katika mfumo wa fedha ni moja ya mahitaji ya muhimu na ya msingi katika ukuaji wa uchumi na maendeleo kwa ujumla. Tukiwa na hili akilini benki ya NIC Tanzania iliona umuhimu wa kuwekeza hapa Zanzibar ili kuendeleza ukuaji wa uchumi. Benki ya NIC Tanzania imetengeneza huduma katika muundo bora ambao ni rahisi kutumia na utakao mfaa kila moja wetu kwa mahitaji yake hii ni katika kurahishisha utunzaji wa fedha, utoaji wa mikopo na hata uwekezaji. 

Katika kufungua tawi hili jipya hapa Zanzibar Benki ya NIC Tanzania imekuja na huduma zilizotengenezwa rasmi kufikia na kutimiza mahitaji ya wateja wetu.Baadhi ya huduma hizo ni huduma za Uwakala, Mawakala wakubwa wa TigoPesa, EzyPesa pia wanaweza kuweka fedha katika tawi hili. Pia tumeingia ubia na Zantel kwa ajili ya wateja wao kuweza kutoa fedha kutoka katika akaunti zao za benki na kuweka katika simu zao za mkononi. 

Tutawapa wateja wetu kadi ya MOVE Visa, ambayo mteja ataweza kutoa fedha katika ATM yoyote iliyo na chapa ya VISA, na pia ataweza kununua bidhaa katika eneo lolote la mauzo hapa mjini Zanzibar na katika nchi yoyote, hii itapunguza adha ya kubeba fedha taslim wakati unasafiri.

Kuhusiana na fedha za kigeni, tunafanya biashara ya kubadili fedha mbalimbali kwa kutumia bei za kiushindani na fedha hizi ni dola ya Kimarekani, Paundi ya Uingereza, Euro, KES, ZAR na UGX. n.k,” anaeleza Karume.

Kwa upande wa Mgeni Rasmi, Dkt. Khalid Salum, alisema kuwa, “Tumepokea kwa mikono miwili ufunguzi huu wa tawi jipya Zanzibar, na natumaini ni hatua nzuri kuelekea kukuza uchumi wa Zanzibar, na sasa tunataka kuupa changamoto uongozi wa benki hii kuona namna wanaweza kusaidia kuboresha ustawi wa jamii katika upande wa afya au elimu.”

Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NIC Tanzania, Sharmapal Aggarwal naye alikuwa na haya ya kunena, “Hili ni eneo ambalo lina biashara zinazokuwa kwa kasi kwa pamoja ambapo zinaweza kukuza utalii. Kwa sasa tunalenga kutafuta idadi kubwa ya wateja maeneo ya visiwani na kupata fursa ya kutanua mtandao wa kikanda katika miaka ijayo.”

Mwishoni mwa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo Margaret Karume alimshukuru Mgeni Rasmi, Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Dk.Khalid Salum Mohamed kwa kukubali kujumuika nao lakini pia aliwapongeza wafanyakazi wenzake na Bodi kwa kujitoa kwao. Mkurugenzi huyo alitumia fursa hiyo kumtambulisha Meneja wa Tawi la Benki ya NIC Tanzania, Zanzibar, Bwana Majid Mohamed.