Mei Mosi 2019 itumike kutatua changamoto za wafanyakazi nchini


Mei Mosi 2019 itumike kutatua changamoto za wafanyakazi nchini

Tarehe 1 Mei kila mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani. Hii ni siku muafaka ya kutafakari na kutathmini kazi iliyofanyika kwa kipindi cha mwaka mzima, ili kujiwekea tena sera na mikakati ya kuboresha mafanikio yaliyofikiwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

“Kazi ni uhai”. Huu ni msemo maarufu uliojaa ukweli mtupu. Ustawi wa mtu au jamii yoyote (likiwemo Taifa la Tanzania), hutegemea sana ni kwa kiasi gani watu wake wanajituma kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kuweza kujikimu na maisha na pia kupata ziada ya akiba na uwekezaji katika maendeleo.

Lakini pia, sehemu yoyote yenye kazi lazima iwe na wafanyakazi. Wafanyakazi ndio nguzo ya eneo lolote la kazi. Wafanyakazi wana umuhimu mkubwa katika ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla, hivyo kutokana na umuhimu wao Shirika la Kazi Duniani (ILO) liliamua kutenga siku maalum kwa ajili ya kutafakari umuhimu na mchango wa wafanyakazi katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Tarehe 1 Mei kila mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani. Hii ni siku muafaka ya kutafakari na kutathmini kazi iliyofanyika kwa kipindi cha mwaka mzima, ili kujiwekea tena sera na mikakati ya kuboresha mafanikio yaliyofikiwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kadhalika kila ifikapo siku hii Watanzania huungana na wenzao duniani kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani maarufu kama Mei Mosi. Kihistoria siku hii ilitokana na maandamano ya wafanyakazi huko Marekani waliokuwa wakishinikiza azimio la muda wa kazi uwe ni saa nane kwa siku, litambuliwe kisheria.

Azimio hilo lililopitishwa na Shirikisho la Wafanyakazi nchini humo mwaka 1884, likitaka utekelezaji wake uanze Mei 1, 1886 lilisababisha kuibuka kwa maandamano makubwa ya amani yaliyohusisha maelfu ya wafanyakazi wakishinikiza waajiri na Serikali kukubaliana nalo.

Kufanyika kwa maandamano hayo kulisababisha viongozi wa wafanyakazi kukamatwa, kufungwa, kuteswa na baadhi yao kuuawa. Hatimaye wafanyakazi walipata ushindi kwani mwaka 1886 ilikubalika nchini Marekani kuwa saa za kazi ziwe nane kwa siku.

Ushindi huo ndio ulioibua Siku ya Wafanyakazi Duniani baada ya mkutano mkuu wa pili wa kimataifa wa Jumuiya ya wafanyakazi mwaka 1890 jijini Paris nchini Ufaransa kupitisha azimio kuwa tarehe moja ya Mei ya kila mwaka iadhimishwe siku ya wafanyakazi duniani kote.

Mbali na maadhimisho ya siku hii kufanyika kwa mafanikio hapa nchini, bado wafanyakazi katika sekta mbalimbali wamekuwa wakikutana na changamoto katika maeneo yao ya kazi. Changamoto hizo zimekuwa zikisababisha migomo, vurugu na wakati mwingine kwenda mbali zaidi ya baadhi ya watu kufikishana mahakamani.

Katika Makala hii tutaangalia baadhi ya changamoto ambazo wafanyakazi wa Kitanzania wamekuwa wakikutana nazo na njia za kufanya ili kuweza kuzitatua changamoto hizo.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Dk Yahya Msigwa anasema kwanza wafanyakazi wamegawanyika katika makundi mawili ambayo ni wafanyakazi wa sekta ya umma na wafanyakazi wa sekta binafsi na changamoto zao zinatofautiana.

Wafanyakazi wa umma kwa sasa wana nafuu kidogo kwa upnade wa changamoto, shida kubwa ipo kwa upande wa wafanyakazi wa sekta binafsi.  “Wafanyakazi wa sekta binafsi viwango vyao vya mishahara ni vidogo sana, wafanyakazi wa sekta binafsi wengi hawana mikataba ya ajira, wafanyakazi wengi wa sekta binafsi hawashirikishwi katika masuala yanayohusu shughuli za sehemu zao za kazi,” anasema Dk Msigwa.

Anaendelea kuwa, “Wafanyakazi wa sekta binafsi pia wanakabiliwa na changamoto ya afya na usalama mahali pa kazi kwa sababu sehemu nyingi mfano viwanda mazingira ya kazi siyo rafiki kwa afya za wafanyakazi. Changamoto nyingine inayowakabili wafanyakazi wengi wa sekta binafsi ni kupata huduma za mifuko ya hifadhi ya jamii.”

Anasema kuwa, Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambalo mwaka huu linatamiza miaka 100 toka kuanzishwa kwake kauli mbiu yao ya mwaka huu ni “Kazi Nadhifu” na moja kati ya sifa za kazi nadhifu ni kulipwa kipato kinachoweza kukutosheleza kuishi wewe na familia yako ambacho kitakuwezesha kupata huduma zote za muhimu pamoja na huduma za mifuko ya hifadhi ya jamii lakini wafanyakazi wengi wa sekta binafsi hawapati huduma hizi.”

Changamoto nyingine ambayo inawaumiza wafanyakazi wa sekta zote mbili ni kodi. Kiwango cha kodi kinachotozwa ni kikubwa sana kwa wafanyakazi hapa nchini, mfano; kwa wafanyakazi wa kipato cha kati na cha juu, kodi yao inafikia mpaka asilimia 30 ya mishahara yao. Hivyo kama Shirikisho la vyama vya wafanyakazi tumeshauriana na Serikali na mambo yanakwenda vizuri ya namna ya kupunguza viwango vya kodi na changamoto nyingine zinazowakabili wafanyakazi.

Afisa Uhusiano wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Eleuter Mbilinyi anasema changamoto zipo nyingi, lakini kwa upande wangu mimi naona kuna changamoto kubwa tatu.

“Changamoto ya kwanza ni kipato cha mfanyakazi. Vipato vingi vya wafanyakazi haviendi sambamba na mabadiliko ya gharama za maisha, utakuta mtu ameajiriwa miaka mitano iliyopita kwa kiwango fulani cha mshahara lakini miaka mitano baadae yupo kwenye kiwango kile kile na ukiangalia uhalisia wa maisha unakuta gharama za maisha zimepanda,”

“Changamoto nyingine ni za mazingira ya kazi kuwa mabovu kwa baadhi ya maeneo ya kazi. Baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya mazingira mabovu ya kazi kutokana na baadhi ya waajiri ambao pengine hawaoni umuhimu sana wa kuboresha mazingira ya kazi,”

Mbilinyi anasema, Changamoto nyingine ni vitendea kazi. Kuna baadhi ya sehemu za kazi hazina vitendea kazi ambavyo vinawawezesha wafanyakazi kutimiza majukumu yao kwa asilimia mia moja, hii inasababisha wafanyakazi hao kufanya kazi katika mazingira magumu.

Mbilinyi anatoa wito kuwa, “Ili tuweze kuziondoa changamoto hizi ni lazima waajiri kuangalia mabadiliko ya gharama za maisha ili kuainisha na vipato wanavyowalipa wafanyakazi wao, pia wanatakiwa kuboresha mazingira ya kazi ikiwemo kuhakikisha kunakuwa na vitendea kazi vya kutosha.”

Anaongeza kuwa, “Tutumie maadhimisho ya siku hii ya wafanyakazi kwa baadhi ya waajiri kujitafakari na kuwahamasisha waajiri kuboresha mazingira ya kazi ili kuhakikisha kwamba changamoto hizi zinaisha.”

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Mwalimu Ezekiel Olouch anasema, “Changamoto zipo lakini mimi nitazungumzia sana kwa upande wetu sisi walimu.”

“Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kutoa waraka wa upandishaji vyeo, lakini moja ya changamoto ambayo walimu wanakutana nayo ni pamoja na mrundikano wa wanafunzi madarasani, upungufu wa walimu ambapo kwa sasa kuna upungufu wa walimu 69,000 jambo linalofanya mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi wengi zaidi.”

“Changamoto nyingine ni upungufu wa vyumba vya madarasa na nyumba za walimu, nyingine ni viwango vya mishahara haviendani na hali ya maisha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo  mfumuko wa bei za bidhaa na huduma,” anasema Mwalimu Olouch.

Mwalimu Olouch anasema, “Ili kutatua changamoto hizi, kwanza idadi ya walimu wanaoajiriwa inabidi iongezeke ili kufidia upungufu uliopo, na hapa niishukuru Serikali kwa sababu imeanza kuajiri walimu kwa kasi kubwa, hii ni hatua kubwa katika kupunguza changamoto hii. Kuhusu nyumba, wadau wanatakiwa wakae kwa pamoja ili kuona namna gani wanaweza kusaidia katika ujenzi wa nyumba za walimu kwa sababu safari ya mafanikio huanza na mwalimu.”