Wasemavyo wafanyakazi kuhusu Siku ya Mei Mosi


Wasemavyo wafanyakazi kuhusu Siku ya Mei Mosi

Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani yanalenga kuwakutanisha wafanyakazi wote na kuangalia matatizo wanayokumbana nayo mahala pa kazi. Kwa hapa nchini tangu tuanze kuadhimisha siku hii baadhi ya changamoto za muda mrefu za wafanyakazi zimeweza kutatuliwa kwa kiasi chake kama vile muda wa kazi kuwa masaa nane, nyongeza za mishahara kwa baadhi ya Ofisi n.k.

Ulimwengu unatarajia kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi duniani  inapofika Tarehe 1 Mei ya kila mwaka. Mei Mosi (May Day) ni jina la sikukuu tofauti tofauti ambazo huadhimishwa kila tarehe moja ya mwezi wa tano.

Lakini kubwa na iliyo maarufu zaidi ni Siku ya Kimataifa ya Wafanyakazi ambayo ni ukumbusho wa mafanikio ya kijamii na kiuchumi yakiwa ni matokeo yaliyoletwa na vuguvugu la wafanyakazi.

Tarehe moja ya mwezi Mei hutumika kwa sababu mwaka 1884 Shirikisho la muungano wa Wafanyabiashara na Wafanyakazi, lililoanzishwa na wafanyakazi mwaka 1872 huko Canada, lilipigania kuwepo kwa masaa nane tu ya kufanya kazi kwa siku wakiwa wamevutiwa na hatua waliyoichukua wenzao wa Canada Wafanyakazi wa Marekani nao wakadai kuwepo na muda kama huo wa kufanya kazi nchini mwao ifikapo Mei mosi mwaka 1886.

Hali hii ilisababisha hali ya vurugu na kuyumba kwa soko la Marekani na hii ilikuwa mwaka 1886, pia huu ndiyo ukawa mwanzo rasmi wa utaratibu wa kufanya kazi kwa masaa nane tu kwa siku nchini Marekani.

Zipo changamoto nyingine kama vile mazingira magumu ya kufanyia kazi, mshahara kidogo n.k. ambazo jamii ya wafanyakazi walikuwa wanakabiliana nazo kipindi cha nyuma huko Marekani.  

Matatizo haya ya wafanyakazi huwa yanafanana karibu katika kila sekta na ndiyo maana maadhimisho ya siku hii yamekuwa yakienda sambamba na utafutaji suluhu wa matatizo haya kwa kushirikisha Serikali za nchi husika na Vyama vya Waajiri.

Ofisi nyingi ambazo kwa sasa zimeajiri vijana na katika namna moja ama nyingine zimekumbana na changamoto kadha wa kadha katika utekelezaji wa majukumu yao katika kipindi kifupi walichokuwepo kazini.

Kundi kubwa la wafanyakazi ambao ndiyo vijana wanaweza wasiwe na namna ya kueleza matatizo yao endapo hawatakuwa na uelewa wa kutosha wa Maadhimisho haya na melngo ya kuadhimishwa kwake ulimwenguni.

Hivyo kwa kulitambua hilo, Gazeti la hili limefanya mazungumzo na baadhi ya wafanyakazi wa taasisi mbalimbali juu ya uelewa wao wa Siku hii ya Wafanyakazi duniani.

Mkufunzi wa Masomo ya Uandishi wa Habari, Chuo cha Utalii cha Musoma kilichopo Tabora, Ndugu Juma Mudimi anaeleza namna anavyoifahamu siku hii, “Mei Mosi naifahamu kama Siku ya Wafanyakazi duniani hapa tunagusa “Tabaka la Wafanyakazi” kwa maana ya kwamba Siku hii ni maalumu kwa wafanyakazi wote wa umma na wale kutoka taasisi binafsi wanaungana kwa pamoja ulimwenguni kote.

Kwa Tanzania, Siku hii kwa miaka ya nyuma ilionekana kuwa na tija kubwa sana ukilinganisha na miaka ya hivi karibuni, ambapo kwa nyakati zile, Serikali ilikuwa inataja kima kipya cha mshahara kwa wafanyakazi kwa mwaka. Pia, siku hii wafanyakazi walikuwa wanakutana kwa minajili ya kuwasilisha matatizo yao. Maadhimisho kwa hapa nchini yamekuwa yakifanyika katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimkoa kwa baadhi ya mikoa.

Daktari kutoka Zahanati ya Kilolo, mkoani Iringa, Abdularhman Mwegio naye hakusita kueleza ufahamu wake kuhusu siku hii, “Kwa ufahamu wangu mdogo, Mei Mosi ni Siku ya Wafanyakazi duniani ambapo wafanyakazi huandamana kwa kubeba mabango kuonyesha changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika maeneo yao ya kazi na wanataka Serikali na wadau husika kuzifanyia kazi kabla ya kufika kwa maadhimisho mengine.”

Alipoulizwa kuhusu kuwahi kuhudhuria maadhimisho hayo, Dk Mwegio alisema, “Sikuwahi kuhudhuria hata mara moja katika Maadhimisho hayo kwa sababu ya changamoto ya eneo langu la kazi kwa maana ninafanya kazi vijijini hivyo nakuwa nimezungukwa na wagonjwa wengi muda wote lakini natamani siku moja nihudhurie.”

Mhandisi kutoka Kampuni ya Nyanza Road Works Ltd iliyopo Jijini Mwanza, Hussein Nganyagwa naye hakusita kutoa maoni yake kuhusiana na maadhimisho ya Siku hiyo, “Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi duniani yanalenga kuwakutanisha wafanyakazi wote na kuangalia matatizo wanayokumbana nayo mahala pa kazi. Kwa hapa nchini tangu tuanze kuadhimisha siku hii baadhi ya changamoto za muda mrefu za wafanyakazi zimeweza kutatuliwa kwa kiasi chake kama vile muda wa kazi kuwa masaa nane, nyongeza za mishahara kwa baadhi ya Ofisi n.k.

Siku hii ni muhimu sana kwa kila mfanyakazi ambapo anapata fursa ya kukutana na wenzake na kuweza kubadilishana uzoefu wa mahala pao pa kazi. Na mimi nadhani bado ipo haja ya kuendelea kuadhimisha siku hii ili watu wengi waweze kuelewa adha wanazokumbana nazo wafanyakazi kila uchwao na kutafuta namna ya kuzitatua na kuboresha ustawi wao kwa kukutana na wadau wote kwa pamoja,” anahitimisha Nganyangwa.

Licha ya baadhi ya wafanyakazi kufahamu msingi wa siku hii lakini bado elimu inahitajika kuendelea kuufahamisha umma kuhusu maslahi ya wafanyakazi. Vyama vya wafanyakazi vina wajibu wa kuwaelimisha viongozi wake na wanachama kwa ujumla kuhusu masuala mbalimbali ya vyama vya wafanyakazi ili kuwapa uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli zote za chama cha wafanyakazi.

Elimu hii pia itawasaidia wanachama wa kawaida kutekeleza majukumu yao ya kazi katika sehemu zao za kazi kwa ueledi. Aidha ni jukumu la chama kuelimisha wanachama kwa kutoa habari na mafunzo kwa njia ya machapisho; mfano vipeperushi, makala, vijarida, magazeti, na machapisho mengine.