Maoni ya HakiElimu kuhusu Bajeti ya Sekta ya Elimu kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020


Maoni ya HakiElimu kuhusu Bajeti ya Sekta ya Elimu kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Uwiano kati ya bajeti ya sekta ya elimu na bajeti kuu ya Serikali umeshuka na kupungua chini ya viwango vinavyokubalika kikanda na kimataifa, vikiwamo viwango vilivyowekwa na Tamko la Incheon (2015) ambalo linazitaka nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara kutenga 20% ya bajeti ya Serikali kwenda sekta ya elimu.

Utangulizi

Mwaka wa Fedha 2018/2019 unakamilisha kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli. Miradi mikubwa ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii imeanzishwa na inaendelezwa katika awamu hii.

Ukiitazama sekta ya elimu ongezeko la udahili wa wanafunzi katika ngazi zote za elimu ni mojawapo ya mafanikio makubwa yaliyochagizwa na Serikali ya Rais John Pombe Magufuli. 

Udahili  wa watoto katika shule za msingi umeongezeka kwa 17% kutoka wanafunzi 8,639,202 mwaka 2016 hadi wanafunzi 10,111,255 mwaka 2018. Vivyo hivyo, kumekuwa na ongezeko la 12.6% ya wanafunzi katika shule za sekondari kutoka wanafunzi 1,908,857 mwaka 2017 hadi 2,148,466 mwaka 2018.

Udahili katika shule za msingi umefikia karibu na kiwango kilichowekwa kimataifa kwa asilimia 96.9% (kwa watoto wote walioandikishwa bila kuzingatia umri) na asilimia 84% (kwa watoto walioandikishwa wakiwa na umri sahihi wa kuanza shule). Zaidi ya 70% ya wanafunzi wote wanaomaliza darasa la saba wanaendelea na elimu ya sekondari. Mafanikio haya tunayaona yamechangiwa na uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuondoa ada katika elimu msingi.

Lakini pamoja na mafanikio haya mazuri, bado kuna changamoto kadhaa ambazo zinaikabili sekta ya elimu. Changamoto hizi hasa ni zile   zinazosababishwa na upungufu wa fedha zinazotengwa na zinazopelekwa katika sekta hii.

Kwa mfano, wakati udahili wa wanafunzi umeongezeka kwa wastani wa 17% kama ilivyoelezwa hapo juu, idadi ya shule imeongezeka kwa 1% tu kwa shule zote za Msingi na Sekondari tangu mwaka 2016.

Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2016/17, inaonesha upungufu wa 85% ya madarasa kwa shule za Msingi, 83%, wa mashimo ya choo, 66%, wa nyumba za walimu  na 14% wa madawati.

Aidha, shule za Sekondari zina upungufu wa 52% ya madarasa 84%, ya maabara 86%, ya madawati 85% ya nyumba za walimu na vilevile 88% ya mabweni na 53% ya mashimo ya choo. Jambo hili linashtua sana.

HakiElimu tukiwa mojawapo ya wadau muhimu katika sekta ya elimu, tunalo jukumu la kuishauri Serikali pamoja na bunge na kupendekeza njia sahihi za kufikia malengo ya mipango ambayo Serikali imeweka ili kufanikisha elimu bora kwa wote.

Wakati huu ambapo wabunge na Wizara zinakaa kwa ajili ya kupanga bajeti kwa mwaka wa fedha 2019/20, HakiElimu inatumia fursa hii kutoa mapendekezo ya maeneo ambayo tunadhani ni muhimu kuzingatiwa kama ifuatavyo:

•     Kuongeza bajeti ya sekta ya elimu: 

Katika vipindi vitatu vya miaka ya fedha iliyopita, bajeti ya elimu imekuwa ikishuka kwa takribani asilimia moja kila mwaka.  Mathalani mwaka 2016/17 bajeti ilikuwa  Tsh bilioni 4,770 lakini ikashuka hadi kufikia Tshs bilioni 4,706 katika mwaka wa fedha 2017/18 na mwaka 2018/19 bajeti iliyoidhinishwa ilishuka zaidi  hadi kufikia Tshs bilioni 4,628.   Katika hali ya kawaida tungetegemea bajeti ya sekta ya elimu ingepanda ili kukidhi mahitaji ya ongezeko la wanafunzi wanaodahiliwa na utekelezaji wa elimu msingi bila ada.

Uwiano kati ya bajeti ya sekta ya elimu na bajeti kuu ya Serikali umeshuka na kupungua chini ya viwango vinavyokubalika kikanda na kimataifa, vikiwamo viwango vilivyowekwa na Tamko la Incheon (2015) ambalo linazitaka nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara kutenga 20% ya bajeti ya Serikali kwenda sekta ya elimu.

Uwiano wa bajeti ya elimu kwenye bajeti ya Serikali (ukijumuisha deni la taifa) umepungua kutoka 16.1% kwa mwaka 2016/17 hadi 15% kwa mwaka 2017/18 na kushuka zaidi hadi kufikia 14% kwa mwaka 2018/19.  Kwa kuzingatia ongezeko la bajeti ya taifa katika miaka mitatu na kama Serikali ingetenga walau 20% kwa sekta ya elimu, bajeti ya sekta ya hii   ingeongezeka kwa jumla ya Tshs bilioni 4,666.

Kama kiwango hiki kingepangwa na kutolewa kingepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto za miundombinu tulizozitaja awali.

HakiElimu inaishauri Serikali, wizara husika na wabunge kuchagiza ongezeko la bajeti na uwiano wa bajeti ya sekta ya elimu na ule wa bajeti ya Serikali kufikia 20%.

•     Bajeti kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika elimu msingi. Ajira kwa ajili ya walimu wa shule za msingi. Pamoja na mambo mengine, ubora wa kujifunza unategemea na upatikanaji wa walimu wenye uwezo. Kulingana na Wizara ya Elimu (Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, 2018/19) shule za msingi nchini zina upungufu wa walimu 85,916 hadi kufikia mwezi Aprili, 2018. Tarehe 2 Mei, 2018 Serikali kupitia Naibu-Waziri wa TAMISEMI, Joseph Kakunda, waliliambia Bunge kuwa hadi kufikia tarehe 30 Juni 2018, Serikali itakuwa imeajiri jumla wa walimu 10,140 wa shule za msingi ili kukabiliana na upungufu wa walimu katika shule za msingi. Hata hivyo, hadi kufikia mwezi Julai 2018, ni walimu 4,840 ambao walikuwa wamepangiwa shule za msingi na sekondari. Mwezi Februari 2019, Serikali ilitangaza kuajiri takribani walimu 4,549 tu katika ngazi mbalimbali za elimu. Hivyo kwa idadi hii ni dhahiri kuwa Serikali imeshindwa kufikia lengo la kuajiri walimu 10,140 wa shule za msingi.

Ni muhimu kufahamu kuwa, kama lengo la kuajiri walimu 10,140 wa shule za msingi kama ilivyotangazwa kwa mwaka 2018 likitekelezwa kila mwaka, itatuchukua miaka minane kuondoa upungufu wa walimu katika shule zetu za msingi. Hivyo basi kama azma ya kuajiri walimu hadi   kufikia walimu 20,000 itatekelezwa itachukua miaka minne kuondoa upungufu wa walimu wa msingi uliopo kwa sasa. 

 Utekelezaji wa mipango na bajeti

Pamoja na umuhimu wa upangaji wa bajeti suala la utekezaji wa bajeti inayoidhinishwa ni muhimu zaidi.  Kwa miaka kadhaa tumeshuhudia tofauti kati ya bajeti iliyoidhinishwa na kiasi halisi kilichotolewa katika ketekeleza mipango mbalimbali. Kwa mfano katika mwaka wa fedha wa 2018/19 bajeti iliyoidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo ya Wizara Elimu ilikuwa bilioni 929, lakini hadi kufikia mwezi Machi 2019 ni Tshs bilioni 529 (57%) tu ndiyo ilikuwa imetolewa kwa ajili ya utekelezaji.   Vile vile mtakumbuka mwezi Juni mwaka 2018 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Selemeni Jafo, alitoa ahadi ya kupeleka kiasi cha Tsh 29 bilioni kwa ajili ya miundombinu katika shule za kidato cha tano na sita. Fedha hizo zililenga kujenga madarasa 478 na mabweni 269 kwa ajili ya wanafunzi 21,808 waliokuwa wanatarajia kujiunga na kidato cha tano lakini hawakuweza kufanya hivyo kwa sababu ya upungufu wa madarasa. Mhe. Jafo, alitoa miezi miwili kwa Serikali za mitaa kukamilisha ujenzi wa miundombinu hiyo. Je, fedha hizo zilipelekwa? Na kama jibu ni ndiyo, je madarasa yaliyotegemewa yalijengwa? Na, je wanafunzi walianza shule katika kipindi stahiki? Majibu haya yatawasaidia wabunge na jamii kushauri ipasavyo.

•     Utekelezaji wa tamko la kufuta kodi ya ongezeko la thamani katika taulo za kike. HakiElimu inatambua na inaipongeza Serikali kwa uamuzi wa kufuta kodi ya ongezeko la thamani (VAT) katika taulo za kike, uamuzi uliofanyika katika bajeti ya mwaka 2018/19. Uamuzi huu ulichukuliwa kwa ajili ya kutatua changamoto ya muda mrefu ya wanafunzi wa kike kushindwa kuhudhuria shule kwa siku 2 hadi 3 kila  mwezi kwa sababu tu wanashindwa kukabiliana ipasavyo na namna ya kujihifadhi wakati wa siku za hedhi kwa kutokuwa na uwezo wa kununua taulo za kike. Kuondoa kodi kulitegemewa kungepunguza bei ya taulo za kike na kuzifanya ziweze kununuliwa kiurahisi na watoto wanaotoka katika familia duni. Hata hivyo, utafiti mdogo uliofanywa na HakiElimu katika soko la bidhaa na kwa wanafunzi wa kike unaonesha kuwa kuna muitikio mdogo na sehemu zingine hakuna utekelezwaji kabisa wa tamko hili la Serikali. Katika maduka mengi bei ya wastani ya taulo za kike ni ile ile ya shilingi 2,000/- ambayo familia duni nyingi haziwezi kuimudu. Jambo hili linakatisha tamaa sana siyo tu kwa wanafunzi wa kike bali hata kwa Serikali. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, aliwasilisha masikitiko yake tarehe 15 Februari 2019 baada ya kugundua kuwa taulo za kike zinauzwa katika bei ambazo walio na maisha duni hawawezi kuzimudu. Alisema kuwa ameandika barua kwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Viwanda na Biashara kuwasilisha masikitiko yake. Ni matumaini yetu kuwa wizara itafuatilia suala hili.  Pamoja na hatua hii HakiElimu tunapendekeza Serikali iangalie uwezekano wa kufanikisha upatikanaji wa taulo za kike moja kwa moja mashuleni kama ambavyo inafanyika kwenye baadhi ya nchi jirani.

•     Kuongeza bajeti ya maendeleo ya elimu msingi.  Ili kuhakikisha kuwa mazingira ya kujifunzia na kufundishia yanaboreshwa na njia zinazopendekezwa zinafanikiwa; Serikali inapaswa iwe makini katika kuweka dhamira ya kuongeza, kutenga na kuitekeleza bajeti ya maendeleo ya sekta ya elimu. Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Serikali ilitenga kiasi kidogo kwenye bajeti ya maendeleo ya sekta ya elimu ukilinganisha na bajeti iliyotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Kwa wastani, ni 7% tu ya bajeti yote ya TAMISEMI ndiyo iliyotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Kwa mfano, katika mwaka 2016/17 wakati bajeti ya matumizi ya kawaida ilikuwa Tsh bilioni 2,872 (93.6%), bajeti ya maendeleo ilikuwa Tsh. bilioni 198 (6.4%) na katika mwaka 2017/18 wakati bajeti ya matumizi ya kawaida ilikuwa Tsh. bilioni 3,025 (93.7%) bajeti ya maendeleo ilikuwaTsh.  bilioni 202 tu (sawa na 6.3%).

Ikumbukwe kuwa TAMISEMI ni mtekelezaji mkuu wa elimu msingi na wizara hiyo ina jukumu la kuweka na kuendeleza miundombinu ya kujifunzia na kufundishia. Hivyo basi, HakiElimu inashauri kuwa bajeti ya maendeleo ya elimu msingi iongezwe kufikia 30% ya bajeti inayotengwa kwa ajili ya TAMISEMI. Kuimarisha utengaji wa bajeti kutaimarisha utekelezaji wa bajeti na mwisho kuwezesha utatuzi wa changamoto zilizoainishwa hapo awali.

•     Kuongeza uwazi wa upangaji wa bajeti ya sekta ya Elimu (classification of the education sector budget).

Kwa kawaida bajeti ya sekta ya elimu hupagwa kupitia wizara zaidi ya moja (TAMISEMI, Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jisia, Wazee na Watoto). Upangaji huu umekuwa ukichangia kutokufahamika vizuri fedha zinazopangwa kwenye sekta ya elimu. Hivyo, ili kukuza uwazi, uwajibikaji na utekelezaji wa bajeti, tunaikumbusha Serikali kuweka pamoja mpango na utekelezaji wa bajeti ya sekta ya elimu.  Hivyo, tunaishauri Serikali kufikiria kuwasilisha bajeti moja ambayo inajumuisha fedha zote zinazotengwa kwa ajili ya sekta yote ya elimu.

Ni matumaini yetu kuwa ushauri na maoni yetu pamoja na wadau wengine utazingatiwa ili kuinua ubora  elimu nchini  na hivyo kuchangia  katika kufikia malengo ya Taifa ya kuwa na uchumi wa  kati ifikapo mwaka 2025.

Dkt. John Kalage

Mkurugenzi Mtendaji, HakiElimu