NBC Insurance Agency inakupa huduma, elimu na ushauri kuhusu masuala ya bima


NBC Insurance Agency inakupa huduma, elimu na ushauri kuhusu masuala ya bima

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ilianza kutoa huduma za bima ikiwa kama wakala mdogo wa Kampuni ya Bima ya Taifa (NIC) kwa zaidi ya miaka 20.  NBC baada ya kufunguliwa kwa soko la Bima Huria ilianza kufanya kazi na Kampuni ya African Risk & Insurance Services (ARIS) ambayo zamani ilikuwa inafahamika kama Alexander Forbes ikiwa kama wakala mdogo.

Bima ni makubaliano ya malipo ya fidia inayotolewa na kampuni ya bima kwa wateja wake dhidi ya hasara na majanga wanayoweza kuyapata muda wowote kwa malipo ya ada au mchango kwa muda maalum.

Mteja anachangia kiasi kidogo cha fedha ndani ya muda maalum na kampuni inatoa ahadi ya kumfidia mteja huyo kwa aina ya hasara atakayopata kwa mujibu wa makubaliano.

Bima ipo kwa ajili ya kulinda mali za watu, makampuni na jamii endapo majanga yatatokea.

Bima zipo za aina nyingi na nyingine ni lazima kwa mujibu wa sheria za nchi. Kwa mfano Tanzania ni lazima ukate bima ya gari aina ya Third party kwa mujibu wa sheria.

Bima ni muhimu sana kwa jamii. Wananchi wengi hawana fikra ya mipango ya bima katika shughuli zao, wengi wanachukulia bima kama ni aina fulani ya kodi au gharama ya bure ama hudhani ni gharama kubwa hawawezi kuilipa.

Kutokana na changamoto hizo za mitazamo hasi kuhusu bima kwa baadhi ya wananchi, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) iliamua kuingia kwenye sekta ya bima ili kuhakikisha kwamba inakuja na mwarobaini wa kuondoa changamoto za upatikanaji wa huduma za bima kwa kuanzisha uwakala wa bima kupitia makampuni kadhaa ya bima hapa nchini.

Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Bima wa NBC, Benjamin Nkaka anaeleza historia ya NBC Insurance Agency pamoja na mafanikio yake tangu walipoingia kwenye soko la bima.

Tueleze historia ya NBC Insurance Agency

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ilianza kutoa huduma za bima ikiwa kama wakala mdogo wa Kampuni ya Bima ya Taifa (NIC) kwa zaidi ya miaka 20.  NBC baada ya kufunguliwa kwa soko la Bima Huria ilianza kufanya kazi na Kampuni ya African Risk & Insurance Services (ARIS) ambayo zamani ilikuwa inafahamika kama Alexander Forbes ikiwa kama wakala mdogo.

Baada ya kupata uzoefu wa kufanya kazi za uwakala wa bima pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA) kuruhusu mabenki kutoa huduma za uwakala wa bima, mwaka 2013 benki ya NBC ilisimama yenyewe katika kutoa huduma za bima na ikawa wakala kamili chini ya makampuni makubwa ya bima hapa nchini.

Kwa nini benki ya NBC iliamua kuanzisha utoaji wa huduma za bima?

Sababu zipo nyingi, lakini kubwa benki ilitaka kuhakikisha kwamba wateja wa benki yetu wanapata huduma zote za masuala ya kifedha wakiwa ndani ya benki, ili kuwahakikishia huduma nyingi kwa wakati mmoja.

Sababu ya pili ni kuhakikisha kwamba tunawapa wateja wetu bidhaa za bima kwa ajili ya kuweza kukinga mali pamoja na fedha zao dhidi ya majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza.

Sababu ya tatu ni kwamba tulitaka kuhakikisha kwamba Watanzania walioko maeneo yote hapa nchini wanapata huduma na rahisi na sahihi za bima kupitia matawi yetu ya benki kwa sababu kuna maeneo ambayo watu walikuwa wanakosa fursa za kupata huduma za bima kutokana na kampuni za bima au mawakala wa makampuni ya Bima kushindwa kufika kwenye maeneo hayo.

Ni bidhaa gani za bima ambazo zinatolewa na NBC Insurance Agency?

Bima zimegawanyika katika makundi makuu matatu ambayo ni: bima za maisha, bima za afya na bima za mali, ajali na amana.

Bima za maisha

Hizi ni bima za maisha kwa ajili ya kujiwekea akiba na pia ni kinga kwa familia endapo mkata bima atafariki. Bima za maisha pia zinamsadia mkata bima kufidiwa endapo atapa ulemavu wa maisha utakaomsababisha kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kumuingizia kipato. Zaidi ya hayo mwanachama huweza kujipatia faida kupitia akiba aliyojiwekea. Bima hizi za maisha zinapatikana NBC Insurance Agency kupitia kampuni washirika wetu.

Mfano kwenye bima hizi tuna bidhaa inaitwa Educare. Huu ni mpango maalum wa kumsaidia mzazi au mlezi kutimiza malengo ya mtoto wake kwenda shule, aidha mzazi huyo akiwa hai, akiwa amepata ulemavu wa kuduma au akiwa amefariki.

Mpango huu unamuwezesha mzazi/mlezi kuweka fedha kidogo kidogo kutokana na mkataba atakaokuwa ameingia na benki kupitia kampuni ya Bima (kuanzia miaka 7 mpaka 18) ambazo zitamsaidia kulipa ada ya shule ya mtoto wake kuanzia elimu ya awali mpaka kidato cha sita na hata elimu ya juu.

Ikitokea mkataba umefika mwisho na mtoto amehitimu masomo yake, benki inampatia mzazi/mlezi mafao yote ya kiasi kilichobaki. Aidha ikitokea kwa bahati mbaya mzazi/mlezi amefariki kabla ya mkataba kufika mwisho, NBC Insurance Agency kupitia mshirika wake Sanlam Life Insurance company tutaendelea kumlipia mnufaika ada au michango ya kila mwezi kama mzazi/mlezi wake alivyokuwa analipia na hivyo mtoto kutimiza malengo yake ya shule.

Bima za afya

NBC Insurance Agency kwa kupitia mshirika wake Jubilee Insurance company inatoa huduma za bima za afya ambazo zinamuwezesha mteja kupata huduma katika hospitali yoyote hapa nchini. Bima hizi zinategemea na kiasi cha ada anacholipa mteja. Bima hizi pia zinagharamia gharama za malazi, yaani kama mtu atakuwa ameenda hospitali akalazwa, bima hizi zinaweza kumsaidia mteja kupata dawa pia kwenye maduka rasmi yanaouza dawa.

Bima za mali, ajali na amana

NBC Insurance Agency kupitia washirika wake inatoa bima mbalimbali za mali, ajali pamoja na amana. Bima hizo ni pamoja na bima za magari, bima za nyumba za makazi na biashara, bima za biashara, bima za ajali, bima za mitambo na mashine, bima za ujenzi, bima za usafiri n.k.

Ni kampuni gani ambazo NBC Insurance Agency inashirikiana nazo katika utoaji wa huduma hizi za bima?

NBC Insurance Agency inatoa huduma za bima kwa kushirikiana na kampuni kubwa tatu za bima hapa nchini ambazo ni Sanlam General, Sanlam Life pamoja na Jubilee Insurance Company Limited. Hizi ni kampuni kubwa na zenye uzoefu wa muda mrefu katika kutoa huduma za bima nje na ndani ya Tanzania.

Kampuni hizi zinatoa huduma bora kutokana na kuwa na wataalam wa kutosha na waliobobea katika masuala ya bima na ndiyo sababu iliyotufanya kuwachagua kwa ajili ya kufanya nao kazi.

NBC Insurance Agency inajitofautisha vipi kihuduma na benki nyingine ambazo zinatoa huduma hizi za bima?

Kwanza kwa Tanzania benki zinazotoa huduma za bima ni chache na sio kila benki inatoa huduma za bima. Kwa benki zinazotoa huduma za bima hapa nchini, NBC tunajitofautisha nao katika maeneo mbalimbali ambayo ni;

Utoaji wa elimu

Miongoni mwa vitu ambavyo vinaitofautisha NBC na benki nyingine zinazotoa huduma za bima ni utoaji wa elimu kwa wateja kabla ya kuwapatia huduma za bima. Wateja wengi wamekuwa wakikutana na changamoto ya kutokuwa na uelewa kuhusu bima.

Mfano; mtu akienda kukata bima ya gari hakuna mhudumu ambaye atamueleza namna ambavyo anaweza kunufaika, hakuna mhudumu atakaye muuliza kuhusu leseni ya udereva n.k, ikitokea amepata ajali ndiyo watamwambia gari lako limepata ajali hivyo ili tukutengenezee unahitaji kufanya hiki na hiki mwisho wa siku anaona kero na mpaka anafikia hatua ya kujuta kwanini amekata bima.

Hivyo kwetu jambo hili ni tofauti, sisi kabla ya kukuuzia aina yoyote ya bima tunakuelezea kwanza ili uweze kufahamu kila kitu kuhusu faida za bima unayotaka kukata. Hili limetufanya kuaminika sana na wateja wetu na ndio linatutofautisha na wengine.

Kutoa huduma bora na kwa haraka

Moja ya vitu ambavyo vinawavutia sana wateja wetu ni upatikanaji wa huduma bora ambazo zinatolewa kwa haraka. Hakuna mteja ambaye anapenda kukaa muda mrefu baada ya kufanya maombi ya bima ama baada ya kupata tatizo na kusubiri fidia yake, kwa kulifahamu hili, NBC kupitia washirika wetu tumekuwa tukijitahidi kuokoa sana muda wa wateja.

Kuwa na mteja pamoja wakati wa matatizo

Mtu anakata bima kwa ajili ya kupata fidia pale anapopata janga lolote, hivyo inapotokea mteja wetu amepata tatizo labda la kupotelewa na gari ama kuunguliwa na nyumba yake, NBC kupitia washirika wetu tunakuwa naye bega kwa bega mpaka tunahakikisha anapata kile anachostahili.

Hii ni kwa sababu NBC tunaamini kwamba mteja ni mshirika wetu hivyo tunapaswa kushirikiana naye kwenye kila hatua. Hivyo tunamsimamia na kumshauri vizuri ili apate malipo yake anayostahili kwa wakati.

Kutoa ushauri kwa wateja wetu

Mbali na kuwapa elimu, pia tumekuwa tukiwashauri wateja wetu kujikinga na majanga mbalimbali. NBC kabla ya kumkatia mtu bima mfano bima ya biashara tunakwenda kufanya Tathmini ya tatizo (Risk Survey) kwenye eneo lake la biashara kisha tunamshauri kama eneo hili siyo salama inabidi ufanye hivi, labda nyaya za umeme zimekaa vibaya, kufuli zimechakaa inabidi abadilishe, ajikinde na moto kupitia zana kujikinga na moto kama fire extinguisher.  n.k.

Mambo mengine yanayotutofautisha na wengine ni pamoja na kufika mahali ambapo wenzetu wengine hawafiki katika kutoa huduma, kwenye maeneo ambayo kuna mzunguko mkubwa wa biashara huduma zetu zinapatikana hadi siku ya Jumapili, kwa baadhi ya matawi yetu.

Utaratibu wa kupata huduma za bima kutoka NBC uko vipi?

Utaratibu wa kupata huduma za bima kutoka NBC ni kama ambavyo mteja anaingia benki kutoa ama kuweka fedha. Mteja anaweza kwenda kwenye tawi letu lolote kisha atataja aina ya bima anayoitaka, atakatiwa bima yake na atapewa na nyaraka zake zote. Kwenye matawi yetu yote, mteja anapata huduma ya bima, anapata ushauri na anapata elimu ya bima.

Mapokeo ya huduma zenu za bima yapo vipi mpaka sasa?

Mapokeo ni mazuri na makubwa sana, wateja wetu wametuamini sana kutokana na ubunifu wetu pamoja na huduma tunazowapa. Wateja wanafurahia huduma zetu kwa sababu wanatuona tofauti kutokana na kuwaelimisha, kuwashauri na kuwapatia huduma bora na kwa haraka.

Kitu kingine kinachosababisha mapokeo ya huduma zetu kuwa mazuri ni ushirikiano mzuri kutoka kwa washirika wetu ambao ni Sanlam General, Sanlam Life na Jubilee Insurance Company Limited ambao wamekuwa washirika wetu wa karibu.

Pia, wateja wametuamini na kupokea huduma zetu vizuri kutokana na misingi imara ya utendaji kazi wa benki yetu kuanzia kwenye nidhamu, misingi bora ya uwajibikaji n.k.

Ni kitu gani mnajivunia tangu mlipoanza kutoa huduma hizi za bima?

Kwa kweli tunajivunia vitu vingi sana, lakini kikubwa ni ukuaji wa uwakala wetu kuanzia tulipotoka mpaka hapa tulipo sasa kuanzia kwenye aina ya huduma, idadi ya wateja tunaowahudumia n.k, hii inaashiria namna gani wateja wametuamini na kuwa na sisi katika kipindi chote hicho.

Tunajivunia kuuza bima pamoja na faida za bima kwa sababu tunampa mteja kitu ambacho kinamfaidisha kutokana na fedha anayolipa. Kingine ni kuwa na bidhaa ambazo zinakidhi mahitaji ya wateja wetu katika maeneo matatu ambayo ni huduma bora, bidhaa bora, ushauri na elimu.

Kutokana na kuingia kwenu kwenye biashara ya bima, mnalizungumziaje soko la bima Tanzania na mnaiona wapi sekta ya bima nchini ndani ya miaka mitano ijayo?

Soko la bima linakuwa siku hadi siku, hii ni kutokana na kukua kwa sekta ya bima tofauti na miaka kadhaa iliyopita. Kukua huku kumechangiwa na juhudi za Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA) ambao wamefanya kazi kubwa sana kuhakikisha sekta hii inakua kubwa.

Kutokana na mikakati mizuri ya Serikali tumeshuhudia mapinduzi makubwa ya kibiashara kwenye sekta ya bima na ipo mikakati ambayo inaendelea kufanywa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania ili kuhakikisha sekta hii inakua kwa sababu hatujafika tunapotaka kufika kutokana na kuwepo kwa kiwango kidogo cha watumiaji wa bima Tanzania.

Katika kipindi cha miaka mitano ijayo sekta ya bima itakua kwa kasi kutokana na mikakati ya kimaendeleo iliyopo sasa hususani sera ya uchumi wa viwanda kwa sababu bima ni nguzo muhimu katika uchumi wa viwanda hivyo fursa kwenye sekta ya bima zitazidi kuongezeka.

Ni ipi mikakati ya NBC katika utoaji huduma za Bima?

Mikakati iliyopo ni kuendelea kutanua wigo wa utoaji wa huduma zetu, kuwa wabunifu kwa kuja na bidhaa nyingi zitakazokidhi matakwa ya wateja, kuendelea kuboresha huduma zetu na kufikia watu wengi zaidi kuliko ilivyo kawaida.

Wito wa NBC kwa wadau na wateja wa bima

Washirika wote tuliopo kwenye sekta ya bima kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima tunatakiwa kuwekeza sana katika kutoa elimu ya bima kwa wananchi kwa sababu wapo watu wengi wenye uwezo wa kuwa na bima lakini bado hawajapata uelewa wa kutosha.

Serikali na taasisi binafsi ziweke mikakati ya kuanzisha taasisi nyingi zinazofundisha elimu ya bima kwa sababu Tanzania kwa sasa ina chuo kimoja tu kinachofundisha elimu ya bima.

Bima ni muhimu sana kwenye maisha yetu hivyo wananchi wasione kama kuwa na bima ni gharama sana au ni kitendo cha anasa, wajitokeze kukata bima, waje NBC tutawapatia huduma bora za bima zenye elimu na ushauri ndani yake.