Uchambuzi wa HakiRasilimali kuhusu bajeti ya Wizara ya madini na Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2018/19 na 2019/2020


Uchambuzi wa HakiRasilimali kuhusu bajeti ya Wizara ya madini na Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2018/19 na 2019/2020

Sekta ya uziduaji (Mafuta, Madini na gesi asilia) ni eneo muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla, takwimu zinaonesha kuwa sekta ya uziduaji nchini inakadiriwa kuchangia takribani asilimia 5 (2018) ya pato la Taifa ambapo, Dira ya Taifa ya maendeleo inakadiria kwamba hadi kufikia Mwaka 2025 mchango wa sekta ya madini unatarajiwa kuongezeka hadi kufikia asilimia 10 ya pato zima la Taifa.

UTANGUILIZI

Sekta ya uziduaji (Mafuta, Madini na gesi asilia) ni eneo muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla, takwimu zinaonesha kuwa sekta ya uziduaji nchini inakadiriwa kuchangia takribani asilimia 5 (2018) ya pato la Taifa ambapo, Dira ya Taifa ya maendeleo inakadiria kwamba hadi kufikia Mwaka 2025 mchango wa sekta ya madini unatarajiwa kuongezeka hadi kufikia asilimia 10 ya pato zima la Taifa.

Kwa kuzingatia umuhimu wa Sekta ya uziduaji nchini, HakiRasilimali (Mtandao wa Asasi za Kiraia unaofanya kazi za uchambuzi wa Sera na Uchechemuzi katika sekta ya Uziduaji), umekuwa ukifuatilia kwa karibu na kwa umakini Mwelekeo wa Kisera, mipango, matamko na bajeti ya Wizara husika, na hatimaye kufanya uchambuzi katika maeneo tajwa, hasa kwa kulinganisha hatua mbalimbali za utekelezaji wa sheria, sera, mipango na bajeti husika kwa mwaka uliopita na mwaka uliopo na hatimaye kutoa mapendekezo kuhusu maeneo ya vipaumbele ambayo tunaona yanafaa kuwa sehemu ya mipango na utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha unaofuatia.

Kwa minajili hiyo, kama ilivyo kwa miaka iliyopita, mwaka huu pia HakiRasilimali imefanya mapitio ya utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka uliopita na hatimaye kujadili na kuchambua kwa kina mwelekeo wa kisera na maeneo mengine pendekezwa kwa lengo la kutoa maoni yetu na pia kuainisha maeneo ya kipaumbele katika bajeti za Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati kwa mwaka 2019/2020. Lengo kuu la maoni haya ni kuboresha usimamizi na utekelezaji wa sera, mipango na mikakati mbalimbali ya Wizara ya Madini na Nishati ili kuleta matokeo yenye tija na endelevu kwa manufaa ya Taifa letu.

Mapitio ya bajeti ya taifa 2018/2019 na 2019/20 kwa ujumla;

Katika kipindi cha Mwaka 2018/19 Serikali ilipanga kutumia bajeti ya jumla ya Shilingi bilioni 32,476.0 ambapo, Shilingi bilioni 20,468 ilitengwa Kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida (recurrent expenditures) na Shilingi bilioni 12,007 ikitengwa kwa ajili ya bajeti ya Maendeleo (Development expenditures).

Kwa kipindi cha kuanzia Julai 2018 hadi Januari 2019, jumla ya Shilingi bilioni 11,006.5 zilikusanywa ikiwa ni pamoja na mapato ya kodi na maduhuli mbalimbali, hii ikiwa ni sawa na asilimia 52.7 ya shilingi bilioni 20,890 zilizopangwa kukusanywa kwa mapato ya ndani. Katika kipindi hicho pia, jumla ya shilingi 13,750.6 ziliidhinishwa kutolewa na Serikali ambapo, Shilingi bilioni 10,962.1 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 2,788.5 kwa ajili ya maendeleo. Kwa minajili hiyo, hadi kufikia januari, 2019, ambayo ni robo tatu (3/4) ya mwaka wa utekelezaji, ni asilimia 23.2 tu ya bajeti nzima ya maendeleo ilikuwa imetolewa kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Mwaka 2019/2020:

Katika Makadirio ya bajeti ya mwaka 2019/2020, Serikali imepanga kukusanya na kutumia Shilingi bilioni 33,105.4 kati ya hizo, Shilingi bilioni 23,045.3 zinatarajiwa kukusanywa kutoka katika mapato ya ndani, na tofauti yake itakusanywa kutoka vyanzo mbalimbali vikiwemo mikopo na misaada kutoka ndani na nje ya nchi. Halikadhalika, Serikali inakadiria kutumia Shilingi bilioni 20,856.8 kwa Matumizi ya kawaida, na Shilingi bilioni 12,248.6 kwa ajili ya Matumizi Maendeleo, ambapo, katika bajeti ya maendeleo Shilingi bilioni 9,737.7 zitakuwa ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 2,510.9 zitatoka nje ya nchi.

Kwa ujumla, makadirio ya bajeti ya Mwaka wa fedha 2019/20 ina tofauti ya ongezeko la takribani Shilingi bilioni 629.4 ikilinganishwa na bajeti ya Mwaka 2018/2019. Kwa upande wa bajeti ya maendeleo, Serikali inakadiria kutumia shilingi bilioni 12,248.6 ilinganishwa na Shilingi bilioni 12,007.0 kwa Mwaka wa fedha uliopita, hii ikiwa ni ongezeko la shilingi Milioni 241.6.

Changamoto katika bajeti ya taifa kwa ujumla:

Mwenendo wa utekelezaji wa bajeti ya maendeleo kwa mwaka wa fedha uliopita na miaka mingine iliyopita, fedha ya bajeti ya maendeleo imekuwa ikitolewa kidogo ukilinganisha na bajeti ya matumizi ya kawaida. Kwa mfano, hadi kufikia Januari 2019, robo ya tatu ya utekelezaji wa mwaka wa fedha husika, ni shilingi bilioni 2,788.5 tu zilitolewa katika shughuli za miradi sawa na asilimia 23.2 ya bilioni 12,007 iliyoidhinishwa na bunge. Ufinyu wa bajeti ya maendeleo ni kikwazo kwa miradi mingi yenye maslahi kwa wananchi ambayo iwapo rasilimali fedha hazitatolewa inaweza isitekelezeke kabisa au isitekelezwe kwa wakati.

Tunaitaka na kuishauri Serikali, kuipa kipaumbele bajeti ya maendeleo sambamba na kutoa fedha zinazohitajika kwa wakati. Vivyo hivyo, tunasisitiza Serikali kuendelea kutengeneza mazingira ya kuvutia ya kibiashara na kutanua wigo wa kodi na vyanzo mbalimbali vya mapato ili kukidhi mahitaji ya kibajeti.

Makadirio na utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Madini na Wizara ya Nishati kwa mwaka 2018/2019 na 2019/2020

Wizara ya Madini

Makadirio ya bajeti iliyopitishwa na Bunge kwa ajili ya Wizara ya Madini kwa Mwaka 2018/2019 yalikuwa ni jumla ya Shilingi 58.9 Bilioni, ambapo Shilingi 39.2 Bilioni sawa na asilimia 66.7 ilikuwa ni kwa ajili ya bajeti ya matumizi ya kawaida na Shilingi 19.6 Bilioni sawa na asilimia 33.3 ikiwa ni kwa ajili ya Matumizi ya maendeleo.

Hadi kufikia Februari, 2019, kiasi cha shilingi 23.4 Bilioni kilipokelewa kwa ajili ya Matumizi ya kawaida na Matumizi mengineyo, ikiwa ni sawa na asilimia 59 ya lengo la bajeti nzima ya Matumizi ya kawaida (39,287,517,992) ikilinganishwa na Shilingi 100,000,000 zilizopokelewa kwa ajili ya shughuli za maendeleo ambayo ni sawa na asilimia 0.5 ya lengo la bajeti nzima ya maendeleo. Hata hivyo, Wizara ya Madini ilipokea ruzuku ya shilingi 1, 000, 0000,000 kwa ajili ya ujezi wa ofisi za madini ambazo hazikuwepo katika bajeti ya mwaka husika. Ufinyu wa bajeti kwa ajili ya maendeleo unakwamisha mipango mingi ya maendeleo ya wizara kwa mwaka kutokutekelezeka au ikatekelezeka kwa kiwango cha chini kama ilivyotarajiwa. Hii haitakuwa na tija kwa miradi ambayo inagusa uwezeshaji wananchi hasa wachimbaji wadogo wadogo.

Taarifa ya Mkaguzi na Mdhitbiti wa Hesabu za Serikali inayoishia Juni 2018, iliyotolewa rasmi Machi 2019, inaonesha kuwa, hadi kufikia June 30, 2018, kulikuwa na baki ya Dola za Marekani 622,175 na Shilingi 130,331,274.45 katika Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) zilizobaki kutoka sehemu ya ruzuku ya Dola za Marekani 3,000,000, ambazo zilitolewa na Benki ya Dunia kwa Wizara ya Nishati na Madini (2015/16) kwa ajili ya kuendeleza Rasilimali madini nchini ili zitolewe kama ruzuku kwa wachimbaji wadogo wa madini ili kuendeleza uchimbaji mdogo. Hata hivyo, hakukuwa na maelezo yoyote kutoka Wizarani kuhusu fedha hizo ambazo zingeweza kuwa msaada kwa wachimbaji wadogo.

PENDEKEZO: Tunaishauri Serikali kuendelea kutafuta rasilimali za kutosha kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo na kuzikabidhi fedha hizo chini ya uangalizi wa mamlaka ya STAMICO ili ziweze kuratibiwa kwa kuwawezesha wachimbaji wadogo nchini.

Mapitio ya makadirio ya bajeti ya taasisi za Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na 2019/2020

Tume ya Madini

Tume ya Madini imeundwa kwa mujibu wa Sheria ya madini 2010, Sheria ya marekebisho Anuai No. 7 ya Mwaka, 2017. Mamlaka ya kuianzisha Tume na majukumu yake yameainishwa katika kifungu cha 21 na kifungu cha 22, ambapo, miongoni mwa majukumu ya Tume hiyo ni kusimamia, kuratibu, kupanga, kudhibiti na kutekeleza masuala na shughuli zote zinazohusu madini na pia kuishauri Serikali kuhusiana na shughuli zote zinazohusu Sekta ya Madini nchini. Halikadhalika, Tume ya madini ni chombo chenye mamlaka kamili ya kushitaki au kushitakiwa pale inapobidi.

Katika Mwaka wa fedha wa 2018/19, Tume ya Madini ilikuwa na bajeti ya jumla ya shilingi 12.5 Bilioni, ambapo, shilingi 8.6 Bilioni ikiwa ni kwa ajili ya Matumizi mengineyo na shilingi 3.9 Bilioni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Tume. Hadi kufikia Disemba 2018, Tume ilipokea jumla ya shilingi bilioni 8.2 ikiwa ni sawa na asilimia 94 ya lengo la nusu Mwaka wa bajeti husika. 

Katika makadirio ya Mwaka wa fedha 2019/20, Tume ya Madini inatarajia kutumia shilingi 21,404,963,891 kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Hii inajumuisha shilingi 13,396,281,500 kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi 8,008,682,391 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Tume ya Madini.

Changamoto kubwa ambayo inaikabili tume ni kutokueleweka kwa sheria ya madini kwa wadau wa madini na wafanyabiashara ambao husababisha ugumu kwa Tume kukusanya baadhi ya tozo mbalimbali zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria ya Madini.

PENDEKEZO: Tunashauri Tume ya Madini kuwa na mkakati kabambe wa kutoa elimu kwa Umma mara kwa mara na kutumia njia mbalimbali kama vile televisheni, redio za kitaifa na kijamii pamoja na mitandao ya kijamii n,k. ili Umma wa Watanzania uelimike kuhusu Sheria ya Madini na kazi na mamlaka ya Tume ya Madini.

Taasisi ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia Tanzania (TEITI)

Mpango wa Uwazi na Uwajibikaji Tanzania katika sekta ya Mafuta, gesi na madini, umeanzishwa chini ya Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji ya Mwaka 2015 kwa lengo la kukuza na kuboresha Uwazi na uwajibikaji katika uvunaji wa rasilimali madini, mafuta na gesi asilia.

Mpango huu unaratibiwa chini ya Wizara ya Madini. Tangu kuanzisha kwake, taasisi hii imekuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kutokuwa na vyanzo vya uhakika vya fedha katika kutekeleza mipango na shughuli zake mbalimbali.

Katika mapitio ya taarifa ya shughuli zilizotekelezwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019, taasisi hii imeshindwa kutekeleza shughuli nyingi zilizopagwa kutekelezwa kwa mwaka husika kutokana na uhaba wa rasilimali fedha. Katika mwaka wa Fedha wa 2018/2019 jumla ya shilingi 1,629,379,543 zilipitishwa na Bunge kupitia Wizara ya Madini, ambapo, matumizi mengineyo yalikuwa ni Shilingi 243,415,543 na matumizi kwa ajili ya maendeleo ilikuwa ni shilingi 1,3385,964,000. Hata hivyo, hadi kufikia Februari, 2019, inaonekana hakukua na fedha yoyote iliyotolewa kwa ajili ya maendeleo kwenda TEITI.

Halikadhalika, baadhi ya shughuli zilizotekelezwa kupitia TEITI hazina maelezo ya kutosha kuhusu vyanzo vya fedha vilivyofanikisha utekelezaji huo. Kwa ujumla, taarifa ya utekelezaji ya shughuli za taasisi kwa mwaka ulipita haikutoa ufafanuzi wa kina kwa baadhi ya masuala ambayo ni muhimu kujulikana na wadau mbalimbali wa maendeleo. Baadhi ya masuala yaliyojitokeza katika taarifa ya taasisi ni kama yafuatayo;-

1)Taarifa haikuonesha au kufafanua kwa kina kuhusu matumizi mengineyo katika bajeti (OC) yalitumika katika matumizi gani hasa kutokana kwamba taasisi haikupokea kiasi chochote cha fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

2)Taarifa kuu ya TEITI ya utekelezaji kwa mwaka 2016/17 na 2017/18 hazijatolewa hadi leo, ingawa, kuna maelezo ya kuanza kwa utaratibu wa kumtafuta mtaalamu mshauri wa kuandaa taarifa husika. Ingekuwa vyema kwa TEITI kutoa mrejesho wa hatua zilizofanyika katika kutekeleza jukumu la utolewaji wa taarifa tajwa.

3)Kuanzishwa kwa rejista ya taarifa kwa Umma kuhusu wamiliki wa hisa katika kampuni za madini, mafuta na gesi asilia ni moja kati ya shughuli iliyopaswa kutekelezwa, ila hakuna maelezo yoyote katika taarifa kuhusu hatua za utekelezaji wa uanzishwaji wa rejista hiyo kama ilivyosisitizwa na aliyekuwa Waziri wa Madini, Mh. Angella Kairuki tarehe 25/10/2018, jijini Dodoma wakati akizindua kamati ya tatu ya TEITI. Rejista ina umuhimu mkubwa katika kuboresha uwazi katika sekta hii na pia itasaidia kuzuia upotevu wa rasilimali na mapato yatokanayo na rasilimali madini, mafuta na gesi asilia. TEITI haina budi kutoa mrejesho kwa Umma kuhusu hatua iliiyofikiwa ya uanzishwaji wa rejista.

4)Taarifa ya TEITI imeonesha miongoni mwa mafanikio kwa mwaka 2018/19 ilikuwa ni kuongezeka kwa uwazi wa matumizi ya mapato ya halmashauri yanayotokana na tozo kutoka kampuni za uchimbaji madini, mafuta na gesi asilia. Ingawa hakuna maelezo ya kutosha kuonesha ni halmashauri zipi na iwapo ongezeko hilo ni kwa kiasi gani ukilinganisha na mwaka wa fedha uliopita. Ni vizuri kwa TEITI kutoa taarifa zenye maelezo ya kutosha ili kusaidia watumiaji wa taarifa kuelewa kwa kina.

Changamoto zinazoikabili TEITI

Kama ilivyoainishwa, miongoni mwa changamoto kuu zinazoikabili TEITI ni uhaba wa rasilimali fedha za kutekeleza shughuli za maendeleo iliyojipangia na pia upungufu wa rasilimali watu kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya taasisi. Vivyo hivyo, muundo na mfumo wa kimamlaka, kiutendaji, kimaamuzi na utashi wa kisiasa vinaweza pia kuwa sehemu ya changamoto za kufikia azma na lengo la kuanzishwa TEITI.

Mapendekezo na Ushauri kuhusu TEITI

Awali ya yote, tunaipongeza sana Serikali kwa dhamira njema ya kuanzisha na kulea mpango huu kabambe wenye tija kwa nchi yetu, tuna imani kubwa na nia ya Serikali na wadau wengine wa maendeleo katika kuifanya TEITI kuwa imara zaidi na yenye kuwajibika ipasavyo. Ni imani yetu kwamba, changamoto zilizojitokeza zimetoa fursa ya kujitathmini na kujipanga vyema kwa ajili ya kufikia malengo tarajiwa. Kwa minajili hiyo, tunapenda kupendekeza yafuatayo;

a) Serikali ifanye marekebisho ya Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia ya Mwaka 2015 ili kuiwezesha TEITI kuwa Taasisi iliyo huru na yenye muundo na mfumo mpana unaoiwezesha kuwa na mamlaka katika kukusanya rasilimali fedha na kutekeleza  majukumu yake kikamilifu na kwa wakati.

b) Pamoja na kutumia televisheni, na redio, TEITI inapaswa Kutumia njia mbadala katika kuhabarisha na kutaarifu Umma na wadau mbalimbali kuhusu kazi, wajibu na shughuli za TEITI, ingekuwa vyema kuanza kutumia mitandao ya kijamii na redio za kijamii (social media and community redio) ambazo zipo karibu na watu wa rika tofauti na pia hutumiwa na watu wengi zaidi.

c)  Serikali (kupitia Wizara ya madini) iharakishe mchakato wa upatikanaji wa taarifa na Uwazi wa Mikataba ya Madini, gesi na rasilimali zingine kwa kuzingatia kwamba, msingi mkuu wa kuanzishwa TEITI ni kwa ajili ya kukuza na kuboresha Uwazi na uwajibikaji katika uvunaji wa rasilimali madini, mafuta na gesi asilia.

d) TEITI itoe taarifa kuhusu maendeleo ya uchunguzi wa ukaguzi maalum wa Shilingi bilioni 30.5 kama ilivyojitokeza katika taarifa ya mshauri mwelekezi.

e)  TEITI iharakishe upatikanaji wa watumishi wenye uwezo na sifa zinazohitajika katika kutekeleza majukumu ya TEITI katika ngazi tofauti.

f)   Wizara ya madini iwajibike ipasavyo kufanikisha upatikanaji wa rasilimali fedha ili TEITI iweze kuwa na fedha zinazohitajika kutekeleza shughuli za maendeleo kama ilivyopangwa.

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)

STAMICO ni moja kati ya Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini. Hili ni shirika linalomilikiwa na Serikali kwa asilimia mia moja, ambalo lilianzishwa rasmi mwaka 1972 chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma (1969). 

Mwaka 2015 Shirika lilifanyiwa marekebisho makubwa ya kimuundo (restructuring) chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma (mabadiliko ya uanzishwaji wa mashirika ya Umma) 2015. STAMICO inamiliki makampuni kadhaa ya madini yakiwemo STAMIGOLD, Buhemba Gold, Makaa ya Mawe Kiwira n.k, kwa lengo la kuyaendesha kifaida.

Changamoto zinazoikabili STAMICO

Miongoni mwa changamoto zinazoikabili STAMICO ni (1) uhaba wa rasilimali fedha zinazohitajika kuendesha shirika. Kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG 2019) STAMIGOLD kampuni tanzu ya STAMICO, imekuwa inajiendesha kwa hasara takribani miaka 3 iliyopita kutokana na madeni, uwekezaji mdogo na kampuni kutofanya shughuli za uzalishaji.

(2) Na kwa miezi kadhaa STAMIGOLD Kampuni tanzu ya STAMICO pia imekua inafanya shughuli zake kwa inakadiliwa kutumia mafuta ya petrol kisasi cha lita 450 kwa mwezi. Hii ni baada ya kukosa umeme kuendesha shughuli zao.

(3) Vivyo hivyo, Kifungu namba 9 cha marekebisho ya Sheria ya Madini 2010, kupitia Sheria ya marekebisho Anuai sheria No. 7, 2017, Sheria inaelekeza umiliki wa Serikali usiopungua asilimia 16 katika makampuni ya madini, ingawa, sheria au kanuni hazitoi mwongozo kuhusu mamlaka ipi ya Serikali itahusika na jukumu la kusimamia umiliki huo.

Katika makadirio ya mwaka wa fedha wa 2018/2019, jumla ya shilingi bilioni 13.6 ziliombwa kupitia Wizara ya Madini kwa ajili ya maendeleo, ambapo, takribani shilingi bilioni 9 zikiwa kwa ajili ya maendeleo ya miradi ya Kiwira na Buhemba na shilingi bilioni 4 na zaidi zikiwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Hata hivyo, katika kipindi hadi kufikia Februari, 2019, STAMICO ilipokea shilingi bilioni 2.7 tu ambazo zilikuwa ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi na matumizi mengineyo. Hii ina maana kuwa, ni asilimia 32.6 tu ya fedha zote zilizopokelewa kwa mwaka wa fedha uliopita.

Mapendekezo/ ushauri kuhusu STAMICO

Pamoja na changamoto zinazolikabili Shirika la Madini la Taifa, tunaona mustakabali mzuri wa Shirika katika miaka ijayo, hata sasa, tunatambua jitihada za Wizara na Serikali kwa kulihuisha Shirika hadi kufika hapo lilipo, bado tunaamini kuwa kuna nia ya dhati ya kulifanya Shirika kuwa imara zaidi na kujiendesha kwa faida. Hivyo basi, kwa kutambua umuhimu wa STAMICO katika maendeleo ya rasilimali madini nchini, tunapenda kutoa mapendekezo yetu kama ifuatavyo;-

a) Serikali ifanye uwekezaji mkubwa kwa STAMICO (pamoja na kuipa ruzuku ya upendeleo) na pia kuchukua dhamana ya madeni yanayoikabili ili iweze kuwa na uwezo wa kujiimarisha kifedha ili kumudu gharama za uzalishaji.

b) Tunapendekeza kuwa STAMICO ifanyiwe mabadiliko makubwa ya kimuundo na kimfumo ili iwe kampuni hodhi (Holding company) inayoweza kumiliki hisa au sehemu ya umiliki katika makampuni mengine ya migodi na pia iweze kukuza mtaji kwa kuingia makubaliano ya kimkakati na ya kiuwekezaji, ikiwezekana, kukopa na hata kukaribisha wadau (hasa wananchi) wenye nia ya kuwekeza katika vipaumbele vya Shirika.

c)  Tunaamini kuwa, iwapo STAMICO itabadilishwa na kuwa kampuni hodhi, itasaidia kukuza mtaji wake kwa haraka, pia itamwezesha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Serikali kufanya ukaguzi (katika mashirika ya Umma na makampuni binafsi (kwenye sekta ya madini, mafuta na gesi asilia) na hatimaye kuweza kujiridhisha na mwenendo wa mapato na matumizi ya makampuni hayo ambayo kwa sasa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Serikali hana uwezo wa kuyakagua kwa mujibu wa sheria.

d) Tunapendekeza kuwa, STAMICO ifanyiwe mabadiliko na ipewe jukumu la kusimamia na kuratibu umiliki wa asilimia 16 za Serikali katika makampuni ya madini kwa niaba ya Serikali.

e) Tunapendekeza pia, STAMICO ijitanue na kufanya utafiti na uwekezaji katika aina tofauti za madini kama vile “graphite", coal” na mengineyo kuliko kujielekeza zaidi katika dhahabu.

Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2018/2019 na 2019/2020

Katika mwaka wa Fedha wa 2018/2019, Wizara ya Nishati ilikadiria kukusanya na kutumia Shilingi 1.69 Trilioni, katika makadirio hayo, shilingi 1. 665 trilioni zilitengwa kwa ajili ya Maendeleo na Shilingi 27,145,014,000 zikiwa ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida. Hadi kufikia Disemba 2018, kiasi cha shilingi bilioni 275.40 zilikuwa zimepokelewa kwa ajili ya shughuli za maendeleo, hivyo hivyo, Shilingi bilioni 12.1 zikiwa zimepokelewa kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

Katika Mwaka wa fedha 2019/2020, Wizara imekadiria kutumia Shilingi 2.142 trilioni ambapo kati ya makadirio hayo, Shilingi 2.116 trilioni ni kwa ajili ya maendelo na shilingi 26.339 bilioni kwa ajili ya Matumizi ya kawaida. Vyanzo vya mapato ya bajeti vinatarajiwa kuwa vya ndani na pia kutoka nje ya Nchi, ambapo, Serikali inatarajia kukusanya shilingi 1,956,372,000,000 kutoka vyanzo vya ndani na pia Shilingi 160,082,000,000 kutoka nje ya Nchi.

Kwa mujibu wa takwimu za wizara, makusanyo ya Maduhuli yanayotarajiwa kukusanywa kwa mwaka wa Fedha 2019/20 ni bilioni 612,370,725,000, ikiwa sawa na ongezo la asilimia 55.5 kwa mwaka wa Fedha 2018/19 (Bilioni 394,450.860, 600). Hata hivyo, taarifa ya Wizara haioneshi ni kiasi gani cha Maduhuli kimekusanywa kwa mwaka wa Fedha uliopita. Tunaishauri Wizara itoe taarifa ya utekelezaji wa Bajeti na makusanyo ya maduhuli kwa mwaka wa Fedha 2018/19.

Makadirio ya bajeti kwa mwaka huu wa fedha, yameongezeka kwa takribani asilimia 26 ikiwa ni kutokana na kiasi kikubwa kwenda katika mradi wa Rufiji unaotarajia kuzalisha Megawati 2,115, ambapo gharama za mradi zimepanda kutoka shilingi 700,000,000 kwa Mwaka 2018/2019 hadi Shilingi 1,443,264,000,000 ambalo ni ongezeko la asilimia 106.2.

Hivyo basi, tafsiri ya bajeti kwa Mwaka huu inaonesha kwamba, zaidi ya nusu ya bajeti ya Wizara nzima ya Nishati, yaani asilimia 74 imeelekezwa katika mradi wa Rufiji ambao ni mradi kwa ajili ya maendeleo. Tunapenda kuipongeza Wizara kwa kuwa ya mfano kwa kutenga kiasi kikubwa katika bajeti ya maendeleo kwa miaka miwili mfululizo, pia pongezi kwa Serikali kwa nia njema ya kuwekeza katika mradi wenye lengo la kuondoa changamoto za umeme Nchini.

Mapendekezo:                                           

Pamoja na kutambua jitihada njema za Serikali, Tunashauri kuwa Serikali itoe kipaumbele katika kutenga rasilimali fedha za kutosha katika miradi mingine ambayo ipo katika hatua tofauti tofauti za utekelezaji hasa miradi ya gesi asilia, ili utekelezaji wake uende sambamba na miradi mingine.

Tathimini ya baadhi ya taasisi chini ya Wizara ya Nishati

1.Shirika la Taifa la Maendelo ya Petroli (TPDC)

Sheria ya Petroli ya Mwaka 2015, inatoa madaraka kwa TPDC kufanya na kusimamia shughuli za utafutaji, uendelezaji na usambazaji wa Mafuta na Gesi Asilia Nchini. Pamoja na umuhimu wa mamlaka ya TPDC bado inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo zifuatazo;

Changamoto za Madeni na Ukusanyaji usioridhisha wa wadaiwa:

(a)    Uendeshaji kiasara: Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG): Taarifa yaMdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonesha kuwa hadi kufikia Juni 30, 2018, TPDC ilipata hasara ya Shilingi 64,543,000,000 huku ikiwa na madeni yanayofikia shilingi 3,544,892,000,000 hivyo kuwa katika moja ya mashirika yenye hali mbaya ya kifedha. Hali kadhalika, taarifa ya kamati ya Bunge ya Nishati na Madini inaonesha kuwa, hadi kufikia Disemba 2018, TPDC ilikuwa inadai (TANESCO, SONGAS, Ndovu Resource ltd, Kilimanjaro Oil ltd n.k) jumla ya shilingi bilioni 527.096. deni ambalo limesababisha makampuni yenye mkondo wa juu kutishia kuzuia kuuza Gesi Asilia kwa TPDC kwa sababu ya kushindwa kulipia Ankara zake kwa wakati.

(b)    Uwekezaji kwa ajili ya shughuli za Maendeleo:

       i.        Ufinyu wa bajeti na uwekezaji mdogo TPDC: Hii changamoto ni miongoni mwa sababu zinazokwamisha ufanisi katika utekelezaji wa mikakati inayojiwekea. Mwaka 2016, TPDC iliandaa Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi Asilia (NGUMP 2016 – Natural Gas Utilization Master Plan). Mpango huu ulioainisha kwa kina usambazaji wa Gesi Asilia Nchini. Hata hivyo, mpango huu umekua ukisuasua kutekelezeka hadi leo kwa sababu ya ukosefu wa rasilimali fedha.

    ii.        Majadiliano yasiyo na kikomo: kwa kipindi kirefu sana, kupitia taarifa zinazotolewa na Wizara ya Nishati, kumekuwepo kwa majadiliano yasiyo na kikomo kwa Serikali na Wawekezaji. Hii inaathiri utekelezaji wa mikakati ya baadhi ya shughuli za Gesi Asilia iliyopo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.  Kwa Mfano Utelezaji wa Mradi wa Kusindika Gesi Asilia kwenye Hali ya Kimiminika (Liquefied Natural Gas Plant-LNG).

Vivyo hivyo majadiliano haya yasiyo na kikomo, yanasababisha ucheleweshwaji wa uwekezaji wa mitaji ya kigeni (FDI) ambayo ni kichocheo cha uchumi na maendeleo ya miradi mbalimbali nchini. Lakini pia upatikanaji wa FDIs ungeisaidia Serikali kuelekeza rasilimali zaidi katika sekta zilizo na ufinyu wa Bajeti hasa katika maeneo ya kimkakati ya kijamii.

MAPENDEKEZO: Tunaishauri Serikali kuipa TPDC kipaumbele katika uwekezaji ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kisheria kama inavyotakiwa, ufinyu wa bajeti na uhaba katika uwekezaji kutaifanya TPDC kuwa tegemezi na kushindwa kuhimili ushindani kwa kasi inayohitajika katika biashara.

(C)  Utekelezaji wa miradi ya Gesi Asilia na Makadirio yake 2018/2019 – 2019/20

i.        Mradi wa kusindika Gesi Asilia kwenye hali ya kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG): Mradi huu umepangwa kutekelezwa kwa Mwaka 2019/20, ambapo bajeti ya Shilingi bilioni 6.5 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza ulipaji fidia, kufanya tafiti mbalimbali za kiuchumi ili kusaidia timu ya Serikali katika majadiliano na wawekezaji. Mradi huu ulipendekezwa kama ulivyo kwa Mwaka 2018/19 kwa bajeti ya Shilingi bilioni 6.5.

Mradi huu umekuwa katika majadiliano tangu miaka 2 iliyopita na hakuna taarifa za kutosha kuhusu maafikiano na hatua zilizofikiwa katika majadiliano baina ya Serikali na wawekezaji. Tunaishauri Serikali kuzingatia muda na pia tunaitaka Serikali kutolea ufafanuzi wa bajeti inayopangwa kila mwaka na ufanisi wake.

ii.        Ujenzi wa Miundombinu ya Usambazaji wa Gesi Asilia katika Jiji la Dar es Salaam: Mradi huu unalenga kujenga miundombinu ya kusambaza gesi asilia katika jiji la Dar es Salaam. Bajeti ya Shilingi 1,100,000,000 zimetengwa kwa Mwaka 2019/20. Ingawa mradi kama huu uliwekwa pia katika bajeti ya Mwaka 2018/19 ambapo bajeti ya Shilingi Bilioni 2 zilitengwa. Hadi sasa hakuna maelezo wala taarifa ambayo imetolewa kuhusu hatua za usambazaji wa gesi asilia katika maeneo husika.

iii.        Mradi wa Kusafirisha Gesi Asilia kutoka Dar es Salaam Tanzania hadi Uganda: Mradi huu unahusisha ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asilia kwenda Nchini Uganda kutokea Dar es Salaam, bomba hilo litakwenda sambamba na bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki linalotoka Hoima Uganda hadi Chongoleani-Tanga (Tanzania). Bajeti ya Shilingi 800,000,000 zimetengwa kwa Mwaka 2019/20. Hatahivyo, mradi huu pia ulitengewa Shilingi Bilioni 1.5 katika Mwaka 2018/19 kwa ajili ya Upembuzi Yakinifu. Tunashauri Serikali kufafanua bajeti nzima kwa ajili ya mradi huu na pia kutoa ufafanuzi wa hatua za utekelezaji wa bajeti zinazopangwa kila mwaka.

iv.        Mradi wa bomba la kusafirisha Mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Uganda hadi Tanga Tanzania (EACOP): Mradi huu ni mwendelezo wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Nchini Uganda hadi Tanzania, ambapo, bajeti ya Shilingi 7,000,000,000 zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha majadiliano ya kimkataba kati ya Nchi washirika Uganda na Tanzania) na makampuni yaliyowekeza kwenye mradi huu (Total SA na Tullow Plc). Hata hivyo, katika bajeti ya Mwaka 2018/19, Shilingi bilioni 54 zilitengwa kwa ajili ya kazi na majukumu yanayofanana na mwaka huu. Pamoja na jitihada za Serikali katika mradi huu, ili kukuza Uwazi na Uwajibikaji katika utekelezaji wa mradi huu, tunafahamu majadiliano haya yamechukua sura mpya na hivyo basi tunaishauri Serikali iweke wazi hatua za makubaliano zilizofikiwa hadi sasa, na kipi kinakusudiwa kwenye majadiliano haya mapya. Pia ijulikane jumla ya fidia zitakazolipwa na mchango wa kila Nchi wabia katika utekelezaji wa Mradi.

Mwelekeo wa Kisera

HakiRasilimali inatoa pongezi nyingi kwa Serikali na Mamlaka zake kwa hatua mbalimbali ambazo zimechukuliwa katika Utungaji na utekelezaji wa Sheria na Kanuni zinazogusa Sekta ya madini, mafuta na gesi asilia nchini. Katika hatua tofauti, tumeshuhudia Maelekezo kadhaa yakitolewa na Viongozi wa Serikali yenye lengo la kurekebisha kasoro mbalimbali zilizokuwepo pia na kuharakisha utekelezaji wa maudhui yaliyomo katika Sheria ya Madini ya 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017.

Pia tunatambua na kupongeza hatua ya Serikali ya kukutana na wadau na wachimbaji wadogo wa Madini nchini kwa lengo la kusikiliza kero, changamoto na maoni yao kuhusu uendelezaji wa Sekta ya Madini. Vivyo hivyo, hatua zilizochukuliwa hadi za kufuta Kodi ya ongezeko la thamani (VAT) 18% na Kodi ya zuio (withholding tax 5%) kwa wachimbaji wadogo, Kufungua na kujenga masoko ya madini katika mikoa yenye uzalishaji wa madini, pia, tamko la Serikali la kurudisha Umiliki wa machimbo ya Makaa ya Mawe Kiwira Serikalini sambamba na kulipa malimbikizo ya Madeni yaTANCOAL Co.

Hata hivyo, tunaona umuhimu wa kuzidi kusisitiza na kushauri Serikali kufanyia marekebisho kwa baadhi ya Sheria zinazogusa maendeleo ya Sekta ya Madini, na vilevile, msukumo zaidi uwekwe katika uwezeshaji wa kifedha na kiufundi na pia usimamizi katika utekelezaji wa Sheria na Kanuni mbalimbali za Madini ili kutekeleza usimamizi madhubuti wa rasilimali madini kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi na Nchi kwa ujumla.

Kwa hiyo basi, matarajio yetu kama Asasi ni kuona maamuzi na uelekeo wa kisera katika sekta ya madini, mafuta na gesi asilia unalenga kujenga mifumo imara na taasisi endelevu, inayotoa wigo mpana wa ushiriki wa wananchi kwa ujumla.

 Ukaguzi wa fedha na taarifa kwenye sekta ya uziduaji

Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, imebaini Changamoto kwa ofisi yake Kupata taarifa za kifedha na kimikataba kutoka katika mashirika na makampuni kwenye sekta ya madini, mafuta na gesi asilia. Changamoto hizi zimesababisha ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za Serikali kushindwa kufanya ukaguzi wake kwa mujibu wa Sheria.

Hivyo basi , ili kuweza kuchochea ongezeko la uwazi na uwajibikaji kwenye sekta, kuna haja ya kupitiwa upya kwa sheria ya madini,  mafuta na gesi asilia ili kumpa mamlaka ya moja kwa moja Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali kupata taarifa zitakazosaidia ukaguzi wake kwa maslahi mapana ya nchi.

D.   UWEZESHAJI WAZAWA (LOCAL CONTENT)

Kwa kupitia Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na kanuni zake, kampuni za uchimbaji madini Tanzania zinapaswa kuandaa na kuwasilisha mpango wa uwezeshaji wazawa katika baraza la uwezeshaji wananchi kiuchumi. Pamoja na masuala mengine, mpango huo utapaswa kuonesha namna kampuni za wananchi (wazawa) zitapata vipaumbele katika zabuni na bidhaa zinazopatikana nchini, upatikanaji wa ajira kwa Watanzania na utoaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo zaidi waajiriwa wazawa. Hatua hii ina nia njema na yakupongezwa kwa sababu inalenga kuwashirikisha wananchi kuwa sehemu ya uchumi wa madini ya nchi yao.

Changamoto tunazoziona ni uwezo na umahiri/ushindani usioridhisha wa kampuni za wazawa kushiriki kikamilifu katika fursa hizo, na pia kukosekana kwa muunganiko (Link) wa mnyororo wa thamani baina ya kampuni za madini na sekta zingine za kiuchumi, kama kilimo, uvuvi, elimu na ufundi n.k, pia uelewa mdogo wa wananchi kuhusu uwepo wa fursa hizo.

Pendekezo letu ni kwa Serikali kuweka mifumo na mikakati inayotekelezeka kwa ajili ya kuwaandaa wananchi na kuwajengea uwezo ili washiriki kikamilifu katika sekta ya madini kwa kushirikiana na wadau na taasisi mbalimbali za maendeleo zikiwemo asasi za kiraia.

UWAJIBIKAJI WA MAKAMPUNI KWA JAMII (Corporate Social Responsibility)

Katika suala la uwajibikaji wa makampuni kwa jamii, kifungu cha 102 cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, (Kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria ya Marekebisho ya Sheria Anuai Na. 7, 2017) kinafafanua wajibu wa makampuni kujihusisha katika huduma za kijamii katika maeneo ambayo shughuli za uziduaji zinafanyika. Sheria pia inaelekeza kuwa, Kila mwaka kampuni hizi zinapaswa kuandaa Mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (Plan for Corporate Social Responsibilty), ambao utapelekwa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa/ Vijiji/ Halmashauri kwa ajili ya majadiliano na kupitishwa ili uanze kutekelezwa katika eneo husika.

Ni jambo jema na lenye nia nzuri la kuwawezesha wananchi kupata huduma za kijamii zinazohitajika katika maeneo yao. Ingawa, changamoto kubwa zilizopo zinahusisha baadhi ya makampuni kutokutekeleza majukumu yao kama inavyotakiwa kisheria, pia, uwepo wa migongano ya uelewa kwa baadhi ya makampuni na halmashauri, ambapo, baadhi ya makampuni hudhani suala la mipango ya nini kifanyike ni suala lao pekee, ilhali, baadhi ya Halmashauri zikiamini kuwa wao ndio wanaopaswa kupanga na kupeleka mipango yao katika kampuni husika ili zitoe fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mipango yao. Hali kadhalika, kutokuwepo kwa kikomo (asilimia) cha kiwango kinachotakiwa kutumika katika shughuli za uwajibikaji wa makampuni kwa jamii inapunja jamii za maeneo husika kufaidika na rasilimali zao.

Hivyo basi, tunashauri na kupendekeza, kuandaliwa kwa kanuni/ Mwongozo wa ngazi ya Taifa utakaofafanua masuala kadhaa yakiwemo majukumu na wajibu wa wadau mbalimbali katika jamii yakiwemo makampuni na halmashauri husika.

UCHIMBAJI MDOGO

Uwezeshaji wa wachimbaji wadogo ni moja kati ya maeneo muhimu na ya vipaumbele katika Sheria ya Madini ya mwaka 2010, (Kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria ya Marekebisho ya Sheria Anuai Na. 7, 2017). Uchimbaji mdogo umetengeneza ajira kwa watu wengi na unaweza kunufaisha zaidi wananchi wengi na nchi kupata mapato yatokanayo na kodi na tozo mbalimbali katika rasilimali madini. Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Madini, kati ya Julai, 2018 hadi Februari, 2019, leseni za uchimbaji mdogo 4,497 zilitolewa na Tume ya madini kwa wachimbaji wadogo.

Hatua ya Serikali kupitia Wizara ya madini ya kuanzisha utoaji wa ruzuku kwa wachimbaji wadogo na wakati na pia kufuta kodi ya ongezeko la thamani na kodi ya zuio kwa wachimbaji wadogo, ni hatua za kupongezwa kwani zinalenga kuwawezesha wachimbaji wadogo. Hivyo basi, pamoja na jitihada zinazochukuliwa na Serikali za kushughulikia kero zinazowakabili wachimbaji wadogo ili kuondokana na kutumia zana duni katika uchimbaji, ukosefu wa masoko ya uhakika ya madini, maeneo madogo, migogoro, ukosefu wa mitaji, n.k. Itakuwa ni vyema kwa Serikali kupitia Wizara, Tume ya Madini na STAMICO, kuendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwakopesha zana za uchimbaji, kuwapatia utaalamu na matumizi ya teknolojia katika uchimbaji na uchenjuaji wa madini, pia, kuwapatia mafunzo ya ujuzi, huduma za utafiti, teknolojia, mitaji na hasa kuanzisha benki ya madini au kuwadhamini ili waweze kupata mikopo yenye masharti na riba zisizoumiza.

Mapendekezo ya jumla ya vipaumbele

Kwa kuzingatia umuhimu wa Sekta ya madini, mafuta na gesi asilia nchini pia manufaa ambayo yanaweza kupatikana kwa ajili ya nchi na wananchi katika eneo hili tunapenda kutoa mapendekezo yetu katika maeneo ambayo tunaamini yatakuwa na manufaa makubwa katika vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2019/2020, kama ifuatavyo;-

 MGAWANYO WA BAJETI YA TAIFA KWA UJUMLA:

Hofu yetu ni kwamba uelekezaji wa rasilimali nyingi kwenye miradi michache kunaweza kusababisha kudumaa kwa miradi mingine ya maendeleo utakaosababishwa na ufinyu wa mgawanyo wa rasilimali.

Kuwepo na utaratibu unaozingatia mgawanyo wa rasilimali wenye uwiano unaofaa ili kutoa fursa kwa sekta zingine kushamiri. Kwa mafano, Makadirio ya bajeti ya 2019/2020 katika sekta ya Nishati na ujenzi yanachukua zaidi ya asilimia 50 ya bajeti yote ya nchi, hii inaweza kufanya sekta zingine kutopata rasilimali fedha za kutosha kwa shughuli za maendeleo. Hali kadhalika, pamoja na kutambua umuhimu wa sekta husika, tunashauri utekelezaji wa miradi hiyo kugawanywa katika vipindi vya muda ili kuruhusu mgawanyo wa wastani kuelekezwa katika miradi hiyo.

 UTUNZAJI WA MAZINGIRA:

1) Tunashauri kuwa Wizara ya Nishati na Serikali kutekeleza mpango kabambe wa TPDC (NGUMP 2016) ili kuwezesha miundombinu ya gesi asilia kujengwa ili kuharakisha matumizi ya gesi asilia katika kaya na pia kupunguza mahitaji na matumizi ya Mkaa na Kuni hasa kwa mikoa mikubwa ambapo mahitaji huongezeka kila siku kwa ajili ya shughuli za kiuchumi. 

2) Kwa kutambua kuwa kuna baadhi ya migodi inatarajia kufungwa, mathalani, Bulyanhulu, n. k. Tunaishauri Serikali kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya tathmini ya athari za kimazingira katika meneo ya miradi mikubwa na taarifa za athari hizo ziwekwe bayana ili kuelimisha wananchi hasa wanaoishi kando kando ya miradi hiyo kuchukua tahadhari za kiafya na maisha yao. Vivyo hivyo taasisi zingine kama Asasi za Kiraia (AZAKI) na Taasisi za kitaaluma pia wafanye tafiti sambamba zenye lengo la kubaini athari za kimazingira ili kuchangia katika juhudi za Serikali katika utunzaji wa Mazingira.

2) Kwa kuzingatia mwenendo wa mabadiliko ya tabianchi (trends of climate change), na jitihada za Serikali kufufua na kuwekeza katika eneo la madini ya makaa ya Mawe, tunaishauri Serikali kupitia upya Sheria za usimamizi wa mazingira ili kuepusha madhara/athari hasi zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.

MRADI WA KUSAMBAZA NA KUUZA GESI

a) Tunashauri kwamba kwa maeneo ambayo gesi ilishaanza kuvunwa ambako ni Mnazi Bay na Songosongo, Serikali iwe na mkakati kabambe wa kuuza gesi kwa ajili ya matumizi mbalimbali, takwimu zinaonesha kuwa gesi inayotumika kwa mwaka mzima ni kati ya asilimia 4.18 na 6 tu ya uwezo wa bomba. Hii ni hasara kwa taifa ikizingatiwa kuwa bomba la gesi limejengwa kwa mkopo na tayari mkopo na riba umeanza kulipwa. 

Pia, Serikali itoe kipaumbele katika uwekezaji wa vitalu vya kimkakati vya gesi asilia vilivyopo chini ya mamlaka ya TPDC kwa kuharakisha mazungumzo na wawekezaji ili kufikia muafaka wa kupata uwekezaji wenye manufaa na pia kujali muda kwa kutumia fursa ipasavyo.

a) Kuendelea kuchelewa kuwekeza kunaweza kutoa fursa kwa nchi zingine zenye gesi kama Msumbiji kukosesha taifa faida nono.

b) TPDC iweke juhudi za kutosha katika utafutaji wa masoko ya uhakika kwa ajili ya usambazaji wa Gesi Asilia. Katika bajeti ya mwaka 2018/19 takribani viwanda 10 vilikuwa vimeunganishwa au vilikuwepo katika majadiliano. Pia kwa mwaka huo kulikuwa na Matarajio ya kuunganisha kaya/nyumba Zaidi ya 2000 katika miundombinu ya gesi asilia.  Kwa vyovyote vile, shabaha hizo bado haziridhishi ukizingatia wingi wa viwanda vilivyopo Nchini na idadi ya kaya zilizopo. Tunashauri Serikali iwekeze na kuiwezesha TPDC kufikia malengo zaidi.

Mpango wa taifa wa uwajibikaji wa makampuni (CSR) na uwezeshaji wazawa (Local Content)-(National Local Content and CSR Plan):

Ili nchi iweze kunufaika na rasilimali zake, tunaishauri Serikali kundaa mpango kabambe utakao toa mwongozo kuhusu uwajibikaji wa makampuni kwa jamii na Uwezeshwaji wazawa. Tunaamini kuwa kama Mpango huu utafikiwa, utaweza kutoa viwango elekezeki vitakavyoweza kuunganisha sekta zote na faida jumuishi kwa Taifa.

Muundo wa Wizara ya Madini

Kuna haja ya kupitia upya muundo wa Wizara ya Madini na kufanya marekebisho katika idara au taasisi ambazo zinaonekana kuwa na majukumu yanayofanana. Kwa minajili hii, kuanzishwa kwa Tume ya Madini kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria ya Madini 2010, inapokonya mamlaka na kazi ambazo idara ya madini chini ya kamishna wa madini alikuwa nazo. Kuendelea kuwa na idara na taasisi ambazo zinafanya kazi zinazofanana siyo tu kwamba zinatoa taarifa ya utendaji unaofanana ila pia ni kuingia gharama zisizo na tija.

Matamko ya kisiasa na utekelezaji wa bajeti

a) Kwa kuzingatia utawala wa Sheria, taratibu na kanuni za nchi, matumizi yote ya Bajeti ya Serikali yanapaswa kupitishwa na Bunge kwa niaba ya Wananchi. Kupitia vyombo mbali mbali vya Habari, mawasilisho Bungeni, kumekuwa na matamko mbalimbali ya kisiasa yenye athari kwenye Utekelezaji wa Bajeti kama zinavyopitishwa na Bunge. Kwa mantinki hiyo ni kwamba Bajeti elekezi zimekuwa hazifikii lengo husika. Ili kuwepo na bajeti inayozingatia ukomo na uhalisia endelevu, tunashauri kuwa matamko ya kisiasa yanayoongeza gharama na bajeti ambazo hazikuwepo awali kudhibitiwa ili rasilimali fedha zitumike kwa vipaumbele vinayotakiwa na siyo vinginevyo

a) Hivyo basi wanasiasa, watendaji wa Serikali hawana budi kuzingatia Sheria, taratibu na kanuni za nchi katika usimamizi na Utekelezaji wa Bajeti.

b) Ukinzani wa uhalisia wa Bajeti na matamko ya kisiasa siyo tu husababisha hasara, lakini pia huondoa imani ya wananchi kwa viongozi wao na Serikali kwa Ujumla.

Tamko Hili limeandaliwa na kutolewa na HakiRasilimali

Kwa maelezo Zaidi, wasiliana nasi kupitia

Simu: +255 (0) 745 655 6555

www.hakirasilimali.or.tz