NEMC: Mifuko ya Plastiki inaathiri vyanzo vya maji, viumbe vya majini, mifugo na binadamu


NEMC: Mifuko ya Plastiki inaathiri vyanzo vya maji, viumbe vya majini, mifugo na binadamu

"Kufikia  mwaka 2050 kutakuwepo na mifuko ya plastiki mingi zaidi ndani ya bahari, maziwa na mito kuliko samaki na viumbe vingine vya majini. Ndiyo kusema kwa mwaka huo ukienda kuvua kuna uhakika wa kuvua mifuko ya plastiki 400 na kupata samaki wawili tu" UNEP.

Tanzania ni miongoni mwa mataifa yaliyobarikiwa utajiri mkubwa wa rasilimali mbalimbali zinazotumika kwa shughuli za maendeleo ambazo leo hii zimeiweka katika ramani ya dunia ya mataifa yanayokuwa kwa kasi kiuchumi.

Rasilimali zote hizo za vyanzo vya maji (bahari, maziwa na mito), hifadhi za wanyama, misitu n.k zinaweza kutoweka endapo hakutakuwa na mipango sahihi ya kuzilinda kwa vizazi vijavyo.

Katika juhudi za kuhakikisha rasilimali zilizopo nchini zinalindwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Waziri wake wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mh. Januari Makamba, ilitangaza kuwa ifikapo Juni 1, matumizi ya mifuko ya plastiki yatafika kikomo.

Ni kwa muda mrefu sasa, mifuko ya plastiki imekuwa ikiharibu mazingira ambayo yanabeba rasilimali ardhi na vyanzo vya maji.

Serikali imezuia matumizi ya mifuko ya plastiki na utekelezaji wa jambo hilo unafanywa na taasisi za Serikali ikiwemo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ambalo ndiyo msimamizi wa masuala ya mazingira hapa nchini.

Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Wakili Manchare Heche anatoa elimu kwa umma kuhusiana na zoezi hilo na hatua zitakazochukuliwa na Serikali wakati wa uendeshaji wa zoezi hilo.

Tueleze kuhusu majukumu ya NEMC kufuatia agizo hilo?

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilianzishwa mwaka 1983 mara baada ya Tanzania kutunga sheria ya Mazingira namba 19 ya mwaka 1983.

Majukumu ya Baraza hilo ni pamoja na usimamizi endelevu wa mazingira, kuzuia na kudhibiti uchafuzi wa mazingira, usimamizi wa taka, viwango vya ubora wa mazingira, ushirikikishaji wa umma, ufuataji sheria na usimamizi wa utekelezaji.

Aidha, kuhakikisha sheria zinafuatwa, ukaguzi na ufuatiliaji wa tathmini ya athari za mazingira, utafiti, kuwezesha ushiriki wa umma katika ufanyaji maamuzi juu ya masuala ya mazingira, kuongeza uelewa wa mazingira na kukusanya na kusambaza habari za mazingira.

Baraza hilo kupitia Kanuni za Uzuiaji wa Matumizi ya Mifuko ya Plastiki namba 394 za mwaka 2019 zinalipa wajibu baraza hilo kuwa miongoni mwa taasisi za Serikali zinazosimamia uagizaji, utengenezaji, usafirishaji, uuzaji, na utumiaji wa mifuko ya plastiki.

Kwa hiyo wajibu wetu kwa kipindi hiki ni kuwafikia Watanzania wote kwa sasa katika kukomesha matumizi ya mifuko ya plastiki na hata ukisoma kanuni ya 15 ya Kanuni za Uzuiaji wa Matumizi ya Mifuko ya Plastiki, inatoa wajibu kwa Serikali za Mitaa kusimamia shughuli hizo.

Jambo hili ni la kila mamlaka za Serikali, ndiyo maana Wakuu wote wa Mikoa, Wilaya, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa wanabeba jukumu hili la kuhakikisha wanatekeleza agizo hili kikamilifu kwa sababu maagizo yametoka kwa viongozi wetu wakuu wa nchi. Na NEMC tunabakia kuwa kama mratibu wa namna gani zoezi hili lifanyike kwa nchi nzima.

Kwa nini katazo hili limekuja sasa hivi na si kipindi kingine?

Kwa faida ya watu wengi, ni kwamba Januari 1 mwaka 2017 ndiyo iliazimiwa kuwa mwisho wa matumizi ya mifuko ya plastiki nchini lakini kwa kujali, Serikali ilitoa nafasi mpaka mwezi Juni ili watu waweze kujiandaa.

Kimsingi, Serikali ilianza mchakato wa kuachana na matumizi ya mifuko ya plastiki tangu mwaka 2003 ukiwa kama mpango mkakati wa uhuishaji na uokoaji wa vyanzo vya maji katika taifa hili. Mpango huo uliweza kugundua kuwa tatizo la mifuko ya plastiki hapa nchini ni kubwa na hatua za makusudi zilihitajika kuchukuliwa.

Ukiangalia taifa la Rwanda lilifungia rasmi matumizi ya mifuko ya plastiki mwaka 2008, Kenya ilifanya hivyo mwaka 2017 na Zanzibar mwaka 2011, hii ina maana ya kuwa Tanzania ilianza mapema mchakato huo ingawa hatukuweza kuutekeleza kwa kipindi kile. Hivyo Watanzania wasione kuwa jambo hili kama vile geni kabisa hapa nchini hapana, jambo hili ni la muda tu na sasa umefika wakati wake wa utekelezaji.

Wadau gani mnashirikiana nao katika kuhakikisha kuwa agizo hilo la Serikali linafanikiwa kwa asilimia 100?

Kwa kwa sasa mdau mkuu ni vyombo vya habari kwa maana ya redio, magazeti, televisheni na blog mbalimbali ambao wao tumekuwa tunashirikiana nao bega kwa bega katika kipindi hiki, na hii inachagizwa na ukweli kwamba vyombo hivi vimekuwa vikitusaidia kufikisha habari kwa wahusika kwa usahihi zaidi.

Wadau wengine wakubwa ni wafanyabiashara, wazalishaji, wasambazaji, wauzaji, watumiaji na wananchi kama ambavyo unafahamu kuwa Serikali haifanyi biashara, hivyo tunazungumza nao na kuwasihi kuacha mara moja kuzalisha mifuko hiyo ya plastiki na badala yake wabadili teknolojia na wazalishe mifuko mbadala ambayo kimsingi ipo mingi tu.

Kwa kiasi gani vifungashio hivyo mbadala vinaweza kuleta tija, ufanisi na kulinda afya ya walaji na mazingira yake kwa ujumla?

Jambo hilo tulililiangalia katika maeneo makuu matatu, awali ni upatikanaji wake, pili uwezo wa kumudu kununua na tatu, ni ufanisi wake katika kutunza mazingira.

Katika kuona namna bora ya upatikanaji wa mifuko hiyo mbadala na katika bei nafuu, NEMC imeweka masharti rahisi, kwa mfano; leo ukija hapa NEMC na ukasema unataka kuanzisha kiwanda chako cha kutengeneza mifuko mbadala, sisi hatutakuwekea kinyongo tutakupa kibali mara moja uanze kufanya hivyo. Sababu kubwa kwanza soko la mifuko mbadala limekuwa kubwa, watu wengi wanahitaji mifuko hiyo hivyo ni fursa ambayo inakwenda kuondoa changamoto ya uwepo wa mifuko ya plastiki. Pili, ni mabadiliko, bahati mbaya kwa nchi zetu hizi kama Tanzania watu wengi wamekuwa na uoga wa kubadilisha mfumo wa maisha. Uzalishaji wa Mifuko mibadala unaendelea nchini ndani ya muda mfupi itakwepo yakutosha katika soko kutokana na mahitaji.

Katika ufanisi wa utunzaji wa mazingira, bado hatukatai kuwa hata mifuko hiyo mbadala inapomalizika kutumika na isipohifadhiwa vyema itageuka kuwa takataka na kuleta athari katika mazingira. Faida ya mifuko hii mingine huwa ikishatumika na ukaitupa inaoza, hali hii pekee inasaidia kutunza mazingira tofauti na mifuko ya plastiki ambayo huchukua mpaka miaka 500 kuja kuoza.

Je, vifungashio hivyo mbadala vinavyohitajika kutumika kwa sasa ni vipi?

Sheria yenyewe imeeleza wazi aina ya vifungashio vinavyohitajika kutumika kwa sasa tunapotokomeza matumizi ya mifuko ya plastiki. Sheria imetaja vifungashio vya woven Mifuko iliyotengenezwa kutokana na malighafi inayooza au inayoweza kurejeleshwa na isiyokuwa na malighafi yoyote ya plastiki (woven, non-woven) na vitu asilia (organic). Mimea au vitu asilia kama vile mihogo hutengeneza vifungashio vizuri, lakini pia vitu kama ukindu huweza kutengeneza vikapu, miti nayo hutengeneza karatasi ngumu ambazo huzalisha mifuko ya kaki.

Utekelezaji wa agizo hilo huko mitaani kwa wauzaji na watumiaje unaendeleaje?

Kusema kweli zoezi linakwenda vizuri tu, kata zote za Jiji la Dar es Salaam zipatazo 96, kwa kila kata kuna mwakilishi kutoka NEMC. Tanzania nzima, kuanzia ngazi ya chini mpaka Mkoa tuna wawakilishi wetu na tumekuwa tukifanya nao mazungumzo mara kwa mara, hivyo taarifa tunazozipata ni nzuri na nimeona mpaka Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri naye anaandamana mkoani kwake kwa kweli mambo yanakwenda vizuri.

Yumkini mamia kwa maelfu ya Watanzania hawana ufahamu na sababu za kwa nini mifuko ya plastiki imepigwa marufuku. Unaweza kutuambia nini sababu na kwa kiasi gani inaathiri mazingira?

Tunapiga marufuku kwa sababu mifuko ya plastiki imekuwa na madhara makubwa sana sio tu kwa mazingira bali hadi kwa baadhi ya viumbe hai pamoja na binadamu.

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mazingira duniani (UNEP) zinasema kuwa, viumbe hai wa majini wapatao 100,000 mpaka 150,000 hupoteza maisha kwa mwaka mmoja kutokana na mifuko ya plastiki.

Takwimu nyingine zinaeleza kuwa, ndege aina ya sea bird zaidi ya milioni moja hupoteza maisha kutokana na mifuko ya plastiki kwa mwaka mmoja.

UNEP hawakuishia hapo wanaendelea kutoa takwimu nyingine zenye kuogofya zaidi ambapo zinasema, kufikia  mwaka 2050 kutakuwepo na mifuko ya plastiki mingi zaidi ndani ya bahari, maziwa na mito kuliko samaki na viumbe vingine vya majini. Ndiyo kusema kwa mwaka huo ukienda kuvua kuna uhakika wa kuvua mifuko ya plastiki 400 na kupata samaki wawili tu.

Takwimu nyingine za UNEP zinaeleza kuwa, asilimia 80 ya mifuko ya plastiki inaingia mitaani huku asilimia moja tu ya mifuko hiyo ikirudi kiwandani kwa ajili matumizi mengine. UNEP pia inatuambia kuwa dunia nzima inatumia mifuko ipatayo bilioni 500 mpaka trilioni 1.

Mwaka 2017 Ranchi ya Kongwa ilitupa taarifa kuwa vilitokea vifo vya ng’ombe 156. Kati ya ng’ombe 156, ng’ombe 58 waliripotiwa kupoteza maisha kutokana na mifuko ya plastiki.

Labda nieleze kwa namna gani vifo vya ng’ombe hutokea kutokana na kula mifuko ya plastiki, ni kwamba anatafuna mfuko ule wa plastiki, kwa kawaida mifuko hiyo huwa inatoa chumvi na baadae humeza ambapo kwa bahati mbaya mfuko ule hauozi unasababisha ng’ombe yule kushindwa kupumua kutokana na mapafu kuzibwa na baadae kupoteza maisha.

Sababu nyingine ya msingi ya kwa nini mifuko hii ya plastiki inapigwa marufuku ni kuwa mifuko hii inatumia miaka mpaka 500 kuoza kwa maana ni vizazi kwa vizazi.

Ukiachana na ripoti hizo, mifuko hii ya plastiki imekuwa ikiathiri vyanzo vikuu vyote vya maji kama vile mito, bahari, maziwa n.k. Tukiweza kukabiliana na mifuko hii ya plastiki tutaweza kuokoa uchumi wa bluu (blue economy).

Sheria inazungumza nini? Na hukumu gani inatoa kwa wakiukaji wa agizo kwa wadau wote wa mifuko hiyo?

Sheria imeweka wazi kila kitu kuanzia kwa watengenezaji, wauzaji, wasafirishaji, wasambazaji na watumiaji. Sheria hiyo pia imetaja maeneo ambayo matumizi ya mifuko ya plastiki yatakuwa yanaruhusiwa.

Kanuni namba 394 zimempa wajibu mtumiaji, mtengenezaji, msafirishaji, msambazaji, muagizaji na muuzaji wa mifuko ya plastiki. Kanuni ya 9 ya kanuni hizi imeainisha maeneo 6 ambayo matumizi ya mifuko ya plastiki yameruhusiwa:-

Eneo la kwanza, ni vifungashio vya sekta ya kilimo. "vifungashio kwa ajili ya sekta ya kilimo" maana yake ni vifungashio vilivyotengenezwa kwa malighafi ya plastiki mahsusi kwa ajili ya kuhifadhi unyevu shambani au kufungashia miche ya mazao mbalimbali kwenye vitalu au kufunika vijumba kwa ajili ya kukuzia mazao au kilimo cha umwagiliaji au kukusanya, kuhifadhi na kusafirishia mazao.

Eneo la pili ni vifungashio kwa ajili ya sekta ya ujenzi" maana yake ni vifungashio vilivyotengenezwa kwa malighafi ya plastiki mahsusi kwa ajili ya kubebea bidhaa na vifaa vya ujenzi au kuzuia unyevu kupenya kwenye majengo au mabomba au nyaya au vigae au matanki au majengo ya muda au shughuli nyingine zinazohusiana na sekta ya ujenzi.

Eneo la tatu,"vifungashio kwa ajili ya bidhaa za viwandani" maana yake ni vifungashio vilivyotengenezwa kwa malighafi ya plastiki mahsusi kwa ajili ya kuhifadhi ubora wa bidhaa za viwandani. Vifungashio hivyo vitakuwa na lakiri au alama inayotambulisha bidhaa iliyofungashwa kabla ya kuuzwa au kusambazwa.

Eneo la nne, vifungashio kwa ajili ya vyakula" maana yake ni vifungashio vilivyotengenezwa kwa malighafi ya plastiki mahsusi kwa ajili ya kuhifadhi ubora wa chakula ambavyo vitakuwa na lakiri au alama inayotambulisha aina ya bidhaa ya chakula iliyofungashwa kabla ya kuuzwa, kusambazwa au kuingizwa sokoni.

Eneo la tano, "vifungashio kwa ajili ya huduma za afya" maana yake ni vifungashio vilivyotengenezwa kwa malighafi ya plastiki mahsusi kwa ajili ya kufungasha madawa au vifaa vya upasuaji au matibabu au vifaa vya huduma ya meno au huduma ya macho au huduma yoyote ya afya.

Eneo la sita ni, "vifungashio kwa ajili ya usafi na usimamizi wa taka" maana yake ni mifuko ya plastiki iliyotengenezwa kwa ajili ya kukusanya au kubebea taka ngumu ambapo ukubwa na unene wake utaainishwa kwa amri ya Waziri.

Kanuni ya 10 ya Kanuni hizo inatoa wajibu kwa wale wote ambao wamesamehewa katika Kanuni ya 9 juu ya matumizi ya mifuko ya plastiki, katika kuhakikisha hawageuzi msamaha huo kuwa sehemu ya utupaji ovyo wa mifuko hiyo. Zipo adhabu kwa yule atakayekiuka kanuni ya 10 ya wajibu juu ya matumizi ya mifuko hiyo ambazo huwa ni kubwa zaidi ya yule ambaye hakupewa msamaha wowote wa kisheria. Adhabu hizo ni kama ifuatavyo:-

Kwa mtu yeyote aliyesamehewa na kanuni ya 9, na akapatwa na kosa la kutupa ovyo vifungashio vya plastiki, atalipa faini ambayo si chini ya Tsh. 200,000 kwa mtu binafsi na kama kampuni si chini ya 5,000,000 kama ilivyoainishwa kwenye kanuni za usimamizi wa taka ngumu za mwaka 2009 (Solid Waste Regulation 2009).

Pia, zipo adhabu kwa wale ambao hawakusamehewa na sheria na wakakiuka, nao pia wana adhabu zao zinazojitegemea.

Kwa sasa Serikali imezuia utengenezaji na uagizaji wa mifuko hiyo ya plastiki kutoka nje ya nchi, hivyo mtu yeyote atakayekamatwa akiagiza au kutengeneza mifuko hiyo adhabu yake faini si chini ya milioni TSh. 20 mpaka bilioni 1 au kifungo cha miaka 2 jela au vyote kwa pamoja.

Kitendo cha kusambaza au kuhifadhi, akikamatwa adhabu faini si chini ya TSh. 5 milioni mpaka milioni 50 au miaka miwili jela au vyote viwili kwa pamoja.

Kwa muuzaji wa mifuko ya plastiki, akikamatwa adhabu yake faini si chini ya TSh, 100,000 mpaka 500,000 na kifungo cha miezi 3 jela.

Kwa upande wa mtumiaji yeye akikamatwa na mfuko wa plastiki adhabu yake si chini ya TSh. 30,000 au jela siku 7 au vyote viwili kwa pamoja.

Wapi mtu anatakiwa kupeleka mifuko hiyo ya plastiki katika kipindi hiki?

Mtu yeyote mwenye mifuko hiyo ya plastiki kabla ya tarehe anatakiwa kuiwasilisha katika Ofisi za Serikali ya mtaa wake husika, huko ndipo zilizpo ofisi za umma zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya kukusanya mifuko ya plastiki kwa nchi nzima. Pia, kama anaona haelewi cha kufanya anaweza kuja katika Ofisi za NEMC zilizopo katika mikoa uya Mbeya, Mtwara, Dar es Salaam, Dodoma, Arusha Mwanza na Kigoma.

Mnatoa wito gani kwa Watanzania wote?

Sisi tunatoa wito kwa Watanzania wote kwamba nchi yetu hii ni ya kipekee na hatuna mahali pengine pa kusema tunaweza kukimbilia tukiharibu hapa tulipo. Tumebarikiwa kuwa na utajiri wa vitu vingi sana kama vile mito, bahari, maziwa, milima na mbuga mbalimbali, tunachotakiwa kuvitunza vitu hivi kwa kila hali na mali, na moja ya jitihada tuanze na ukomeshaji wa matumizi ya mifuko ya plastiki.

Wananchi wametoa ushirikiano mzuri katika zoezi hili na tunawaomba sasa waache kutumia mifuko hiyo ili kuepuka adhabu tajwa hapo juu.