TFDA imeweka mifumo ya ufuatiliaji wa bidhaa za chakula kuhakikisha usalama wa afya ya mlaji


TFDA imeweka mifumo ya ufuatiliaji wa bidhaa za chakula kuhakikisha usalama wa afya ya mlaji

Tafiti zinaonyesha kuwa watu wengi duniani wanakula chakula ambacho si salama kwa afya zao jambo linalochangia maambukizo ya maradhi mbalimballi ikiwamo magonjwa ya mlipuko kama kuhara, matumbo na kipindupindu.

Chakula ni uhai. Lakini je, umeshawahi kujiuliza chakula unachokula ni salama kiasi gani?

Tafiti zinaonyesha kuwa watu wengi duniani wanakula chakula ambacho si salama kwa afya zao jambo linalochangia maambukizo ya maradhi mbalimballi ikiwamo magonjwa ya mlipuko kama kuhara, matumbo na kipindupindu.

Pia, ikumbukwe kuwa chakula sal­ama ni muhimu katika kulinda afya ya jamii, kuwa na uhakika wa chaku­la, kukuza uchumi kupitia kilimo na biashara ya mazao ya chakula, kuku­za utalii na hivyo kuleta maendeleo endelevu.

Ili kupunguza athari za chakula kisicho salama, Umoja wa Mataifa (EU) uliamua kuanzisha Siku ya Chakula Salama Duniani (World Food Safety Day), maadhimisho ambayo yaliridhiwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (United Nations General Assembly) ulio­fanyika tarehe 20 Decemba, 2018.

Pamoja na mambo mengine, mku­tano huu ulipitisha Azimio Namba 73/250 lililotangaza Siku ya Chakula Salama Duniani ambayo itakuwa iki­adhimishwa kila tarehe 7 ya mwezi Juni na hivyo maadhimisho haya yanafanyika duniani kote kwa mara ya kwanza mwaka huu, 2019 yakiwa na kauli mbiu ‘‘Chakula salama, juku­mu la kila mmoja wetu’’.

Lengo la maadhimisho haya ni kuhamasisha wadau na wananchi ili kuchukua hatua stahiki katika kuzuia athari zitokanazo na chakula kisicho salama, ikiwa ni pamoja na magon­jwa yatokanayo na chakula.

Katika maadhimisho ya siku ya Chakula Salama Duniani hapa nchi­ni, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ambayo ina jukumu la kusimamia usalama wa bidhaa za chakula nchini Tanzania imejipanga kuadhimisha siku hii kwa namna mbalimbali.

Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania, Gaudensia Sim­wanza anaeleza namna TFDA itaka­vyoadhimisha siku hiyo.

Kwa mujibu wa Simwanza, TFDA imeandaa vipindi na makala juu ya usalama wa chakula ambavyo vita­rushwa katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwamo magazeti, radio na televisheni kuanzia tarehe 7 Juni, 2019 kwa lengo la kuelimisha umma wa Tanzania juu ya siku hii muhimu na pia kukumbusha wajibu wa kila mmoja wetu katika kuhakiki­sha kuwa chakula ni salama katika mnyororo mzima wa chakula (Food chain).

“Kwa kutambua umuhimu wa wanahabari katika kuelimisha umma, TFDA imeandaa semina kwa waandishi wa habari na wahariri juu ya usalama wa chakula. Hii ita­saidia kwa kiwango kikubwa kufiki­sha ujumbe huu nchi nzima kupitia vyombo hivi,” anasisitiza.

Simwanza anasema kwa kipindi cha miaka mitano, TFDA imekuwa ikiratibu maadhimisho ya Wiki ya Chakula Salama nchini, ambapo makala mbalimbali zimekuwa ziki­andikwa katika magazeti na kurusha vipindi kuhusu usalama wa chakula katika vyombo vya habari, kuandaa maonyesho, kusambaza vielelezo vya uelimishaji jamii (vipeperushi, posters na mabango) na kufanya mikutano na midahalo katika mae­neo mbalimbali nchini kwa kengo la kuelemisha jamii juu ya chakula salama.

Uingizwaji na uuzwaji wa bidhaa zisizo na ubora

Akizungumzia hali ya uingiwaji na uuzwaji wa bidhaa, Simwanza anasema TFDA imeweka mifumo ya kufanya uhakiki na ufuatiliaji wa bidhaa za chakula zinazoingizwa na hata zinazozalishwa nchini ili kuhakikisha kuwa chakula kilichopo katika soko la Tanzania ni salama kwa afya ya mlaji.

Anaongeza kuwa mifumo hii ni pamoja na kufanya tathmini ya bidhaa za chakula kabla ya kutoa kibali cha kuingiza nchini shehena ya chakula husika. Vilevile, kila she­hena ya chakula inayoingizwa nchini hukaguliwa, kabla ya mfanyabi­ashara kuruhusiwa kuingiza chakula hicho nchini.

Anasema TFDA imeweka mifumo ya ufuatiliaji wa bidhaa katika soko, ili kubaini hali ya usalama wa bidhaa zinapokuwa katika soko na endapo itabainika kuwa bidhaa zilizoko katika soko sio salama kwa afya ya mlaji kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuisha muda wake wa matumizi au uhidadhi mbovu, TFDA inayo mifumo kwa ajili ya kuhakisha kuwa bidhaa hizo zinateketezwa na hazimfikii mlaji.

Hatua ambazo mamlaka inazitumia kufanya ukaguzi

Meneja huyo anasema TFDA ina jukumu la kufanya ukaguzi wa chakula nchini ili kuhakikisha kuwa bidhaa za chakula zinazozalishwa na kuuzwa hapa nchini ni salama kwa afya ya mlaji. Ukaguzi hufanyika nchi nzima kwa kutumia Wakaguzi wa Chakula walioko katika Ofisi za Kanda za TFDA. Aidha, ili kufikisha huduma karibu zaidi na wanan­chi, TFDA imekasimisha baadhi ya majukumu katika Halmashauri zote nchini, hivyo Maafisa wa Afya kati­ka ngazi za Halmashauri hufanya ukaguzi wa chakula katika mae­neo yaliyokasimishwa katika hal­mashauri zao.

Anasema ukaguzi wa chakula hufanyika katika hatua tofauti, ikiwa ni pamoja na katika viwanda, ambapo ukaguzi wa mazingira ya uzalishaji, malighafi, hatua za uzal­ishaji pamoja na uhifadhi wa chakula hufanyika.

“Ukaguzi hufanyika pia katika vituo vya forodha ili kuhakikisha kuwa chakula kinachoingizwa nchini ni salama na kimesajiliwa na kuid­hinishwa kuingizwa nchini. Aidha, TFDA hufanya ukaguzi katika mae­neo ya uuzaji na utayarishaji wa vyakula ili kuhakikisha kuwa chakula kinachomfikia mlaji kinatunzwa katika hali ambayo haitahatarisha afya ya mlaji,” anaongeza,

Hatua za kisheria dhidi ya wauza bidhaa zisizo na ubora

Simwanza anasema kwa mujibu wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura 219, zipo adhabu mbalimbali kulingana na kifungu cha sheria kilichovunjwa, ikiwa ni pamoja na faini, kifungo au vyote kwa pamoja.

Simwanza anasema TFDA ime­kuwa ikitoa elimu kwa umma juu ya masuala ya usalama wa chakula mara kwa mara kupitia njia mbalim­bali, ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari (radio, televisheni, magazeti) ambako vipindi hurekodiwa na kuru­shwa, mfano kipindi cha TFDA na Jamii lakini pia kuwa na vipindi vya moja kwa moja ambavyo wasikilizaji na watazamaji hupata nafasi ya kuu­liza maswali na kupata ufafanuzi.

Anataja jitihada nyingine kuwa ni kupitia ofisi za Kanda za TFDA ambako elimu hutolewa wakati wa ukaguzi lakini pia wamekuwa waki­toa elimu juu ya masuala muhimu ya kuzingatia ili kuhakikisha usalama wa chakula katika shule, masoko, magulio na minada.

Anasema vilevile TFDA imekuwa ikitoa elimu kwa wasindikaji wadogo wa chakula (wajasiriamali) pamoja na watayarishaji wa chakula juu ya namna ya kuhakikisha kuwa chakula wanachosindika au kinachoandaliwa ni salama kwa afya ya mlaji.

“Mafunzo haya kwa wajasiria­mali wa chakula yamekwishafanyika katika mikoa 25 ya Tanzania Bara, ambako wajasiriamali takriban 1400 wamefikiwa. Kwa kuzingatia kuwa asilimia 74 ya viwanda vya usindikaji wa chakula nchini ni wajasiriamali wadogo hivyo mafunzo haya siyo tu kwamba yatasaidia katika kuhakiki­sha usalama wa chakula, bali pia kue­ndeleza juhudi za Rais John Magu­fuli ya kufikia uchumi wa viwanda.”

Anasema pia TFDA imekuwa iki­andaa vielelezo mbalimbali vya ueli­mishaji kama vipeperushi, mabango, majalada na miongozo ambayo hugawanywa wakati wa mafunzo na mikutano na vingine kubandikwa katika maeneo ya mikusanyiko kama ikiwa ni pamoja na katika mbao za matangazo katika ofisi za vijiji, kata, zahanati, shule na mashine za kus­aga nafaka kwa lengo la kuelimisha jamii.

TFDA inavyoshirikiana na wadau

Simwanza anasema TFDA pia imekuwa ikitoa elimu kwa wafanya­biashara wa chakula juu ya uzinga­tiaji wa sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura 219.

Anasema pia kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikiandaa vielelezo mbalim­bali vya uelimishaji kama miongozo, vipeperushi na mabango mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabi­ashara kutambua mambo ya kuz­ingatia katika kuhakikisha chakula wanachouza ni salama kwa afya ya jamii.

Anasema TFDA hufanya vikao na wadau wakiwamo wafanyabi­ashara ili kujadiliana juu ya masuala yanayohusu usalama na ubora wa chakula.

“Ni jambo lisilopingika kwamba bidhaa zisizo na ubora husababisha kurudisha nyuma maendeleo ya mtu mmoja mmoja, jamii na hata nchi kwa ujumla. Hii ni kwa sababu, huko­sa soko au kuuzwa kwa bei ya chini kutegemea na hali ya bidhaa husika.”

Anasema bidhaa za chakula ambazo siyo salama kwa mlaji huteketezwa na kuongeza gharama kwa mzalishaji, mjasiriamali na mfanyabiashara.

“Ikiwa chakula kisicho salama kitamfikia mlaji kinaweza kusababi­sha magonjwa na hivyo kupelekea gharama za matibabu, jamii yenye magonjwa haiwezi kufanya kazi hivyo, uzalishaji mali utashuka, nchi itatumia fedha nyingi kununua madawa kwa ajili ya kutibu wag­onjwa hali ambayo huzorotesha uchumi wa nchi,” anasisitiza meneja huyo.

Simwanza anasema TFDA inao wadau wengi inaoshirikiana nao wakiwamo, wizara na idara mbalim­bali za Serikali kama wizara zinazo­husika na Kilimo, Mifugo na Uvuvi, TAMISEMI, Shirika la Viwango Tan­zania (TBS), Taasisi ya Chakula na Lishe, Taasisi ya Viuatilifu na Taasisi ya Mionzi.

Anasema pia yapo mashirika ya kimataifa kama WHO, FAO na UNI­CEF pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali na vikundi mbalimbali kama MVIWATA, wasimamiaji wa sheria, vyombo vya habari na vyama vya wafanyabiashara wa bidhaa zin­azodhibitiwa na mamlaka.

Simwanza anasema usalama wa chakula ni suala endelevu, kwa maana kuwa ili kulinda afya ya jamii chakula kinapaswa kuwa sal­ama wakati wote na kwa kutambua jukumu iliyokabidhiwa na Serikali la kulinda afya ya jamii dhidi ya mada­raka yatokanayo na chakula kisicho salama, TFDA ina wajibu wa kufanya ukaguzi wa chakula kinachosindik­wa, kuingizwa nchini au kutayarish­wa na kuuzwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu ili kuhakikisha usalama wake.

Changamoto katika ukaguzi wa bid­haa

Anataja changamoto hizo kuwa ni pamoja na wadau kutokutii sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura 219 kwa hiyari (voluntary compli­ance), uelewa mdogo wa jamii juu ya masuala ya usalama wa chakula, uchache wa rasilimali watu na rasili­mali fedha.

“Wito wangu kwa jamii ni kuwa kila mmoja katika mnyororo wa chakula atekeleze jukumu lake ili kuhakikisha kuwa chakula ni sala­ma kwani ni mtambuka, linahitaji ushirikiano wetu sote; mamlaka za udhibiti, wazalishaji wa chakula, wafanyabiashara na walaji.”

Wadau wengine ni wazalishaji, wasafirishaji, wahifadhi wa chakula, wafanyabiashara, watayarishaji na walaji ambao kwa pamoja wanapas­wa kutekeleza wajibu wao wa kuhakikisha kuwa chakula hakicha­fuliwi na vihatarishi vinavyoweza kuathiri afya ya jamii.

Mambo ya kuzingatia

Hata hivyo, Simwanza anasema yapo mambo mengi ya kuzingatia ili kuhakikisha usalama wa chakula ikiwamo kuzingatia usafi inayohusi­sha usafi binafsi wa mwili na mavazi yanayotumika wakati wa kuandaa chakula.

Anasema jambo lingine ni kunawa mikono kabla ya kugusa chakula kab­la ya kula au kuandaa na kutayarisha chakula, baada ya kutoka chooni, kuosha maeneo yanayogusa chakula mfano meza na vyombo vinavyotu­mika kuandalia chakula, kuepuka wadudu au wanyama kama mende na panya kuingia katika jiko au eneo la kuandalia chakula.

“Hii ni itasaidia kuepuka uchafuzi wa vimelea vya magonjwa ambavyo hupatikana katika mazingira kama udongo, maji, wanyama na binad­amu ambavyo huweza kuwa katika mikono, vyombo au meza za kuanda­lia chakula na kuingia katika chakula na kusababisha madhara kwa mlaji,” anasema.

Simwanza anasema pia waaandaji wa chakula wanapaswa kutengani­sha chakula kibichi na kilichopikwa ikiwa ni pamoja na nyama mbichi, kuku na samaki na vyakula vingine lakini pia kutumia vyombo tofauti vya kukatia vyakula hivyo visitumike kukatia vyakula vilivyoiva.

“Hii ni kwa sababu vyakula vibi­chi hasa nyama, kuku na samaki huwa na vimelea vinavyosababisha magonjwa ambavyo huweza kucha­fua chakula kilicho tayari kwa kuli­wa, hivyo kusababisha madhara kwa mlaji.”

Simwanza anasema wapishi pia wanashauriwa kupika chakula mpa­ka kiive vizuri hasa nyama, kuku, samaki na mayai lakini pia kuchem­sha kiporo hadi kichemke kwa kuwa moto wa kupika chakula huua vime­lea vya magonjwa vinavyoweza kuwepo katika chakula husika.

Anasema pia waandaaji wanapas­wa kuweka chakula katika joto sta­hiki badala ya kuacha katika joto la kawaida kwa zaidi ya saa mbili kwani vyakula vilivyopikwa vina uweze­kano wa kuharibika mapema hivyo inashauriwa kuhifadhiwa katika jokofu.

Anasema pia inashauriwa kuhakikisha chakula kinakuwa cha moto kabla ya kuliwa lakini pia kisi­achwe kwa muda mrefu hata kama kimehifadhiwa katika jokofu

“Hii ni kwa sababu vimelea vya magonjwa huzaliana na kuongezeka kwa haraka kama chakula kitahi­fadhiwa katika joto la kawaida. Kwa kuhifadhi chakula katika nyuzijoto chini ya 50C au juu ya 600C husaid­ia kupunguza kasi ya kuzaliana na kuongezeka kwa vimelea vya magon­jwa. Hata hivyo, baadhi ya vimelea vya magonjwa huweza kuzaliana na kuongezeka katika nyuzijoto chini ya 50C,” anaeleza.

Kwa mujibu wa Simwanza waan­daaji wa chakula wanapaswa kutu­mia maji na malighafi salama wakati wa kuanda chakula, matunda pamoja na mboga ambazo huliwa bila kupik­wa.

Kwa mujibu wa Simwanza, malighafi, ikiwa ni pamoja na maji na barafu huweza kuwa vimechafu­liwa na vimelea vya magonjwa au kemikali hatarishi kwa afya ya jamii.

“Usitumie chakula ambacho kimepita muda wake wa matumizi (expired food) kwani madhara yake ni makubwa,” anasisitiza Simwanza.

Meneja Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Gaudensia Simwanza.