Usalama wa Chakula, jukumu la kila mtu


Usalama wa Chakula, jukumu la kila mtu

Kila mtu ana haki ya kupata chakula salama, chenye lishe bora na cha kutosha. Siku ya Usalama wa Chakula Duuniani iwe ni fursa ya kuimarisha juhudi zetu kuhakikisha kuwa chakula tunachokula ni salama kuanzia uzalishaji had mezani. Kila mtu katika mnyororo wa chakula anawajibika kwa ajili ya usalama wa chakula. Ni muda wa kwenda kutekeleza haya sasa.

Kutokomeza njaa inahusu watu wote kuweza kupata chakula salama, chenye viini lishe vyote muhimu na cha kutosha mwaka mzima, hivyo hatuwezi kuwa na uhakika wa chakula bila kuwepo na usalama wa chakula.

Chakula kisipokuwa salama, watoto hawawezi kujifunza na watu wazima hawawezi kufanya kazi. Maendeleo ya binadamu hayawezi kutokea. Kupatikana kwa chakula salama cha kutosha na chenye viini lishe vyote muhimu ni muhimu kwa ajili ya kuchochea afya njema.

Usalama wa chakula una athari za moja kwa moja kwenye afya za watu na matumizi ya vyakula vyenye lishe. Una nafasi kubwa katika kuhakikisha kuwa chakula kinabakia kuwa salama katika hatua zote za mnyororo wa thamani – kuanzia kwenye uzalishaji hadi uvunaji, uchakataji, uhifadhi, usambazaji, hadi katika uandaaji na ulaji.

Katika dunia ambapo mnyororo wa usambazaji umekuwa mkubwa sana, tukio lolote baya dhidi ya usalama wa chakula linaweza kuwa na athari kubwa kabisa ulimwenuni kwenye ngazi ya afya ya umma, Biashara na uchumi. Hivyo kuboresha usalama wa chakula unachangia kwa namna chanya katika Biashara, ajira na utokomezaji umaskini.

Nchi zimapoimarisha uwezo wao wa kusimamia, kisayansi na teknolojia kuhakikisha kuwa chakula ni salama na chenye ubora unaotegemewa katika mnyororo wote wa chakula, huwa zinaelekea katika uzalishaji endelevu wa chakula na utumiaji.

Leo, Kamisheni ya Codex Alimentarius ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Shirika la Afya Duniani (WHO) wanatekeleza hatua muhimu za viwango vya kimataifa vya vyakula kulinda afya za walaji na kuhakikisha ushindani mwema katika Biashara ya chakula. FAO na WHO wanatekeleza wajibu huu muhimu wa kujengea uwezo nchi ili kuhakikisha kuwa zinatekeleza mifumo yao ya kuhakikishausalama wa chakula.

Hapa Tanzania utaalam wa FAO katika masuala ya usalama wa chakula umekuwa ukitolewa katika kusaidia nchi kupata misaada ya kifedha duniani kwa ajili ya kudhibiti tatizo la sumukuvu.

Hii pia ilijumuisha kuimarisha uwezo wa serikali kuu na zile za mitaa katika kukabiliana na changamoto zinazotokana na tatizo la sumu kuvu kwa kuhakikisha njia sahihi na bora za uhifadhi sahihi wa mazao baada ya mavuno ili kuepuka uwezekano wa kuvamiwa na sumu kuvu.

Kama sehemu wa Mpango wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Sweden (SIDA), FAO inatoa msaada wa kitaalam kuptia mikakati ya kitaifa ya kudhibiti usambaaji wa magonjwa ya mimea na kukuza uwezo wa Serikali kutoa huduma za mazuio na udhibiti wa usamaaji wa magonjwa ya mimea ili kukabiliana na hatari inayoletwa na visumbufu na magonjwa katika kilimo na minyororo ya chakula.

Kupitia Mfuko wa Fleming chini ya Wizara ya Afya ya Serikali ya Uingereza, FAO imekuwa ikifanya kazi na Serikaliya Tanzania katika kukuza uelewa na kuweka mifumo kwa ajili ya matumizi sahihi ya vijuasumu (antibayotiki) katika chakula na kwenye kilimo yaani ufugaji, uzalishaji mazao, uvuvi na ufugaji wa samaki ili kuhakikisha usalama wa chakula.

Pia, FAO kwa sasa inatoa misaada ya kitaalam kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinisa, Wazee na Watoto kupitia mradi wa miaka miwili ‘Kukuza Usalama wa Chakula cha Mitaani’ ili kuboresha usalama wa chakula hapa Dar es Salaam. Mradi unakuza uelewa kwa wauzaji chakula wa mtaani kuhusu viwango vya ubora, urasimishaji wa Biashara zao na umuhimu wa kuweka uwiano wa lishe katika vyakula vyao ili kuhakikisha afya ya umma.

Utekelezaji wa azimio la Afya Moja kwa kiwango kikubwa unaongeza umbora wa usalama wa chakula, kwani afya ya watu inahusishwa na afya za wanyama na mazingira. Vimelea vya magonjwa vinavyopitishwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa wanyama kwa kugusana au kupitia chakula, majim na mazingira vina athari kwa afya ya umma na ukuaji na ustawi wa kiuchumi na kijamii. Kwa pamoja Serikali, Wasomi, wataalam, mashirika yasio ya kiserikali na mashirika ya kimataifa wanaweza kudhibiti hataro za usalama wa chakula.

Kila mtu ana haki ya kupata chakula salama, chenye lishe bora na cha kutosha. Siku ya Usalama wa Chakula Duuniani iwe ni fursa ya kuimarisha juhudi zetu kuhakikisha kuwa chakula tunachokula ni salama kuanzia uzalishaji had mezani. Kila mtu katika mnyororo wa chakula anawajibika kwa ajili ya usalama wa chakula. Ni muda wa kwenda kutekeleza haya sasa.

*Makala hii imeandikwa na Mwakilishi wa FAO hapa nchini Tanzania*