ZFDA: Usalama wa bidhaa za chakula husaidia kulinda na kuimarisha afya ya jamii Zanzibar


ZFDA: Usalama wa bidhaa za chakula husaidia kulinda na kuimarisha afya ya jamii Zanzibar

ZFDA ilianza kufanya kazi zake katika kontena lililopo maeneo ya Majestic na mwezi Aprili 2009 kuhamishiwa kili­pokuwa kiwanda cha Dawa cha Zanzibar (Sasa M/Mmoja) kab­la ya kuhamia Mombasa kili­pokuwa kiwanda cha Uchapaji cha Al-Khayria mwezi Septem­ba 2014.

Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) ambao zamani ulitambulika kama Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDB) ni Taasisi iliyopo chini ya Wizara ya Afya Zanzibar yenye jukumu la kudhibiti ubora na usalama wa chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi.

Wakala huu unafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Chaku­la, Dawa na Vipodozi namba 2 ya mwaka 2006 na marekebi­sho yake ya Sheria namba 3 ya mwaka 2017. ZFDA ilianzishwa kwa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi namba 2 ya mwaka 2006 pamoja na marekebisho yake namba 3 ya mwaka 2017.

Sheria hii ilifuta Sheria ya Madawa na Madawa hatari namba 2 ya mwaka 1986 na Sheria ya Afya ya Jamii, sura ya 73/1947 iliyosimamia masuala ya Usalama wa Chakula Zan­zibar. ZFDA ilianza kufanya kazi zake rasmi mnamo mwezi Januari mwaka 2007.

ZFDA ilianza kufanya kazi zake katika kontena lililopo maeneo ya Majestic na mwezi Aprili 2009 kuhamishiwa kili­pokuwa kiwanda cha Dawa cha Zanzibar (Sasa M/Mmoja) kab­la ya kuhamia Mombasa kili­pokuwa kiwanda cha Uchapaji cha Al-Khayria mwezi Septem­ba 2014.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi (ZFDA), Dk Burhani O. Simai anaelezea baadhi ya majukumu yanayofanywa na ZFDA sambamba na mafanikio yaliyofikiwa na Wakala huo tangu kuanzishwa kwake.

Dira

Kuwa taasisi inayotoa hudu­ma kwa ufanisi katika kudhibiti usalama na ubora wa Chakula, Dawa, Vipodozi na Vifaa tiba.

Dhamira

Kulinda na kuimarisha afya ya jamii kwa kuhakikisha ubo­ra, usalama na ufanisi wa matu­mizi ya chakula, dawa, teknolo­jia, vipodozi na vifaa tiba.

Lengo

Kuhakikisha kuwa bidhaa za Chakula, Dawa, Vifaa tiba ni bora na salama kwa matumizi ya binaadamu.

Sifa za msingi za ZFDA

• Umoja

• Uwazi

• Uadilifu

• Hadhi

• Ahadi

• Uwajibikaji

Majukumu ya ZFDA

1. Kudhibiti utengenezaji, uingizaji, usambazaji na uuzaji wa vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba nchini.

2. Kutathmini na kusajili vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ili kuhakiki­sha vinafikia viwango vilivyowekwa kabla ya kuruhusiwa kwenye soko la Zanzibar.

3. Kukagua viwanda vya utengenezaji na maeneo ya mauzo ya bidhaa ili kuhakikisha viwango vili­vyowekwa vinafikiwa.

4. Kufanya uchunguzi wa kimaabara ili kuhakikisha kuwa bidhaa husika zin­afikia viwango vya ubora na usalama.

5. Kusimamia majaribio ya dawa mpya na vifaa tiba (Clinical trials).

6. Kutoa leseni na vibali mbalimbali kwa bidhaa vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ikiwa ni pamoja na leseni za kuin­giza na kutoa nje bidhaa husika.

7. Kudhibiti utoaji wa matangazo ya biashara ya bidhaa zinazodhibiti­wa na ZFDA.

8. Kuratibu madhara yato­kanayo na utumiaji wa vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba.

9. Kuelimisha jamii kuhusu ubora, usalama na matu­mizi sahihi ya vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba.

Ukaguzi wa Biashara za Chaku­la na Dawa Zanzibar

Ukaguzi ni kazi yetu ya kila siku na unaweza kufanyika wakati wowote ili kuona kama wafanyabiashara wanaende­sha biashara zao katika misingi inayokubalika.

Hii itajumuisha ubora wa majengo, mifumo na mazin­gira ya uzalishaji, usambazaji, uuzaji pamoja na ubora wa bid­haa zinazozalishwa au kuuzwa. Ukaguzi hufanywa na wak­aguzi walioteuliwa na ZFDA na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali.

Kazi za ukaguzi wa biashara za chakula zinasimamiwa na Idara ya Udhibiti wa Usalama wa Chakula. Maeneo yanayo­kaguliwa ni pamoja na Hoteli, Mikahawa, Ghala za Chakula, Viwanda, Machinjio, Mabucha, Maduka ya jumla na rejereja, magari ya kusafirishia chakula, Vinu vya kusaga nafaka na bek­ari.

Kwa upande mwengine Idara ya Dawa ina jukumu la kuhakik­isha kuwa inakagua maduka makubwa ya Dawa (Pharma­cy), Maduka ya Dawa Baridi (OTC), Maduka ya Vipodozi na Maduka ya Vifaa tiba. Lengo ni lile lile la kuhakikisha kuwa zinazosambazwa na kuuzwa Zanzibar zinakuwa na ubora unaokubalika na ni salama kwa mtumiaji na zina ufanisi.

Katika kufanikisha majuku­mu yake ya ukaguzi pia, idara hufanya ufuatiliaji wa dawa zilizokatazwa kama vile uuzw­aji wa dawa za Serikali au dawa bandia au dawa zisizoruhusi­wa kuwepo katika maduka ya dawa baridi ambazo hutakiwa kuuzwa kwa kuwepo cheti cha daktari.

Ukaguzi Maalum wa Viwanda vya Chakula na Dawa

Katika kuhakikisha kuwa bid­haa zinazozalishwa ndani na nje ya Zanzibar ni salama kwa matumizi ya binadamu, ZFDA inalazimika kwa mujibu wa sheria kufanyia ukaguzi viwan­da hivyo ndani na nje ya nchi.

Utaratibu huu huiwezesha nchi kupata dawa na vyakula ambavyo vinaleta uhakika wa ubora wake kwa kuhakikisha vinazalishwa kwa kufuata tara­tibu stahiki kulingana na mion­gozo bora ya uzalishaji. Hili kwa kiasi kikubwa litapunguza ongezeko la maradhi kama vile matumbo na kansa.

Hivi sasa kwa kuzingatia hali za kiuchumi za wafanya­biashara wetu, ZFDA imekuwa inafanya ukaguzi wa viwanda kwa bidhaa zote za Dawa, na kwa upande wa chakula hufan­ya kwa bidhaa zilizopo kwenye kundi la bidhaa hatarishi kama vile nyama na bidhaa za nyama, samaki, maziwa na bidhaa za maziwa, vyakula maalum vya watoto pamoja na bidhaa zin­azoliwa kwa wingi Zanzibar.

Tathmini ya Usajili wa Bidhaa za Chakula, Dawa na Vipodozi

Sheria ya ZFDA inazuia mtu yeyote kuzalisha, kuingiza, kusambaza na kuuza nchini chakula chochote kilichofun­gashwa bila ya chakula hicho kusajiliwa na ZFDA. Chakula kinachosajiliwa ni kile kilicho­sindikwa au kufungashwa kwe­nye kasha, kopo au chupa n.k.

Hivyo ZFDA huifanyia tath­mini bidhaa husika na ikiona kuwa imetimiza vigezo na viwango vinavyotakiwa huipa cheti cha usajili bidhaa hiyo.

Jambo hili hurahisisha ufua­tiliaji na utambuzi wa bidhaa za Chakula, Dawa, Vipodozi na Vifaa tiba zinapokuwa sokoni. Hii itaendelea kuthibitisha kuwa bidhaa zinakuwa salama muda wote zinapokuwa sokoni.

Uingizaji na usafirishaji wa bidhaa za chakula katika vituo vya forodha

ZFDA ina jukumu la kuhakik­isha kuwa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba vilivyopo nchini ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Huwasajili na kuwatam­bua waingizaji wa bidhaa hizo ambao kabla ya kuingiza au kusafirisha bidhaa hutakiwa kuomba kibali cha kufanya hivyo.

ZFDA imeweka mfumo

 wa udhibiti wa uingizaji na usafirishaji wa bidhaa katika vituo vya forodha vinavyot­ambulika kama vile bandari ya Malindi Mkokotoni, Mkoani Wete, Uwanja wa Ndege wa Unguja Kisauni na wa Pemba.

Baada ya kupokea maombi na kumpa kibali muingi­zaji /msafirishaji atalazimika kukaguliwa mzigo wake kwa ajili ya kuchukua sampuli kwa uchunguzi wa maabara.

Ikiwa majibu ya maabara yatathibitisha kuwa bidhaa hiyo inafaa kwa matumizi ita­ruhusiwa kuingizwa na kusam­bazwa au kusafirishwa.

Udhibiti wa bidhaa zisizofaa kwa matumizi ya binadamu

Mambo mbalimbali yame­kuwa yakichangia uwepo wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ambavyo havifai kwa matumizi ya bin­adamu ambavyo ZFDA hulaz­imika kuviteketeza au kuvirudi­sha katika nchi iliyotoka kama matakwa ya sheria.

Mambo hayo ni pamoja na bidhaa kumaliza muda wa matumizi, zimekatazwa, utunzaji mbaya, kughushi au usafirishaji mbaya.

Jambo hili hufanyika kwa mujibu wa sheria ambapo gharama za uteketezaji hutole­wa na mwenye mali. Zoezi hilo husimamiwa na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali iki­wemo vyombo vya usalama, idara ya mazingira, jeshi la polisi, waandishi wa habari, halmashauri, sheha wa mtaa pamoja na mfanyabiashara mwenyewe.

Pia mfanyabiashara hulaz­imika kulipia gharama za usafirishaji ikiwa bidhaa ita­rudishwa nchi iliyotoka.

Ukosefu wa elimu wa sheria, kanuni, miongozo na taratibu za ZFDA kwa wafanyabiashara zinachangia kwa kiasi kikubwa kuingiza na kuuza bidhaa za chakula zisizo na usalama hapa nchini.

Pia wapo baadhi ya wafanya­biashara ambao kwa makusudi hudhamiria kuingiza bidhaa zisizokuwa na ubora kwa saba­bu ya kutarajia faida kubwa na nyinginezo.

Ukaguzi ni kazi yetu ya kila siku na unaweza kufanyika wakati wowote ili kuona kama wafanyabishara wanaendesha biashara zao katika misingi inayokubalika, hii itajumuisha ubora wa majengo, mifumo na mazingira ya uzalishaji, usam­bazaji, uuzaji pamoja na ubora wa bidhaa zinazozalishwa au kuuzwa.

Ukaguzi hufanywa na wak­aguzi walioteuliwa na ZFDA na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali. Kazi za ukaguzi wa biashara za chakula zinasi­mamiwa na idara ya udhibiti wa usalama wa chakula.Mae­neo yanayokaguliwa ni pamoja na hoteli, migahawa, ghala, viwanda, machinjio, mabucha, maduka ya jumla na rejareja, magari ya kusafirishia chakula, vinu vya kusaga nafaka na bek­ari.

Ataweza kupata adhabu mbalimbali kama vile kutozwa faini, kufungiwa biashara yake kwa muda au moja kwa moja au kifungo ikibidi.

Kwa mujibu wa kifungu nam­bari (16) cha sheria ya chakula, dawa na vipodozi nambari 2/2006 hairuhusiwi kwa mtu yeyote kuzalisha bidhaa, kuuza, kusambaza au kuhifadhi bidhaa zinazodhibitiwa na ZFDA bila ya kibali.

Mtu atakayekiuka utara­tibu huu atawajibika kulipia faini isiyopungua milioni tatu (3,000,000) au kifungo kisicho­pungua miaka miwili au vyote kwa pamoja.

Katika kuhakikisha lengo la kulinda na kuimarisha afya ya jamii linafikiwa, ZFDA inaendelea kutoa elimu na taarifa mbalimbali kwa jamii zinazohusu ubora na usalama wa bidhaa za chakula, dawa na vipodozi kwa kupitia vyombo vya habari redio na televisheni, semina, mafunzo na mikutano. Pia, ZFDA hutoa habari zake kupitia tovuti yake (www.zfda. go.tz)

Pia, ZFDA hutoa taarifa za uwepo wa magonjwa au athari mbalimbali baada ya kufanya tathmini na ikithibitika kuwa zina athari tahadhari hutolewa kwa jamii. Maabara ndiyo mhi­mili mkuu wa kazi za ZFDA.

Kazi kubwa ni kufanya uchunguzi wa dawa, chakula, vipodozi na vifaa tiba. Wastani wa sampuli 2068 huchunguzwa kila mwaka.

Maabara inafanya kazi zake kwa kutekeleza mifumo ya kimataifa kwa kufuata muon­gozo wa “ISO/IEC 17025:2005” ambapo mwisho wa mwaka huu maabara ya ZFDA inatege­mea kupata ithibati ya kima­taifa (accreditation).

ZFDA inashirikiana na taa­sisi mbalimbali ambazo tuna­fanya kazi zinazofanana katika udhibiti wa bidhaa hizi na pia tunashirikiana na taasisi ambazo hatufanani nazo lakini wanatuwezesha kufanya kazi zetu kwa urahisi.

Miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja na TFDA, ZBS, TBS, Wizara za kilimo, Wizara za Mifugo, Wizara za Biashara, Taasisi ya Mionzi, Manispaa na Halmashauri, Jeshi la Polisi na vyombo vya habari.

Aidha ZFDA inashirikiana na taasisi za kimataifa katika mahusiano ya kikanda katika kudhibiti usalama wa dawa na chakula na tumekuwa tukishiri­ki katika shughuli mbalimbali katika jumuiya za kimataifa kama vile EAC, SADC, AU, NEPAD, GF, WHO na nyingi­nezo.

Tahadhari ya bidhaa hatarishi

ZFDA hutoa taarifa za uwe­po wa magonjwa au athari mbalimbali baada ya kufanya tathmini. Bidhaa hizi baada ya kuthibishwa kuwa na athari tahadhari hutolewa kwa jamii. Kwa mfano; ZFDA iliweza kubaini Dawa duni na Dawa bandia kutoka India na China sambamba na kuziondoa katika soko dawa zilizotolewa katika miongozo ya kitabibu.

Aidha ZFDA ilitoa tahadhari ya kuwepo kwa dawa za uzazi wa mpango zinazotokana na miti shamba zenye madhara kutoka Uchina. Na hivi kari­buni ZFDA imepiga marufuku uingizwaji wa bidhaa za nyama kutoka Afrika ya Kusini kuto­kana na kuwepo mlipuko wa ugonjwa wa Listeriosis mpaka pale ZFDA itakapotangaza tena.

Utoaji wa taarifa kwa jamii

Katika kuhakikisha lengo la kulinda na kuimarisha afya ya jamii linafikiwa, ZFDA inaendelea kutoa elimu na taarifa mbalimbali kwa jamii zinazohusu ubora na usalama wa bidhaa za Chakula, Dawa na Vipodozi.

Ili kufanikisha hilo, Bodi ime­kuwa ikitumia njia mbalimbali zikiwemo vyombo vya habari (redio na TV), semina, mafunzo na mikutano.

Pia, ZFDA hutumia tovuti yake (www.zfda.go.tz) kwa ajili ya utoaji habari wa mambo yote yanayohusiana na kazi za Wakala.

Mafanikio

Mafanikio yaliyopatikana ni mengi ikiwa ni pamoja na kupa­ta ofisi za kudumu, kupata ithi­bati ya kimataifa kwa kufuata muongozo wa ISO 9001:2015.

Kufanyika kwa marekebisho ya sheria ya chakula, dawa na vipodozi ili iendane na wakati uliopo, kuongeza idadi ya usa­jili wa bidhaa na biashara zin­azodhibitiwa na ZFDA, kuon­gezeka kwa uelewa wa wadau juu ya kazi za ZFDA.

Mwisho kabisa ni kush­iriki katika miradi mbalimbali (EAC, SADC na AU) na kufanya makubaliano kati ya ZFDA na TFDA na kuweka utaratibu mzuri wa wafanyabiashara kusafirisha bidhaa zinazozal­ishwa nchini bila ya bughudha yoyote.

Changamoto

Pamoja na mafanikio tuli­yokuwa nayo, bado tunakabili­ana na changamoto mbalimbali ikiwemo:

Wafanyabiashara kughushi nyaraka za kuingizia bidhaa nchini, uwepo wa bandari bubu jambo ambalo linahatarisha usalama wa bidhaa zinazoingia nchini, uhaba wa vitendea kazi ikiwemo vifaa na mashine za uchunguzi za maabara na usafi­ri kama gari na pikipiki kwa ajili ya kazi za ZFDA.

Changamoto nyingine ni uhaba wa wataalamu na wafanyakazi wa ZFDA, uhaba wa nafasi za ofisi kwa ajili ya wafanyakazi na uhaba wa elimu kwa jamii na wananchi kwa ujumla kuhusu kazi za ZFDA.

Wito

Tunapenda wananchi wafa­hamu kuwa suala la usalama wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba siyo la ZFDA peke yao bali ni la kila mtu, hivyo tunapenda kuwaom­ba ushirikiano zaidi kwa kutu­letea taarifa pindi wanapoona tatizo lolote linalohusiana na bidhaa zinazodhibitiwa na ZFDA au pale wanapodhurika na matumizi ya chakula, dawa au vipodozi.

Aidha ZFDA inatoa wito kwa wafanyabiashara kufuata tara­tibu zilizowekwa ili kuepuka usumbufu wakati wanapoin­giza na kusafirisha bidhaa zao pamoja na kuhakikisha usalama wa bidhaa wanazoziuza kwa wananchi ili kuepusha madhara yatakayoweza kutokea.