Alama tano katika miaka 50 ya Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC)


Alama tano katika miaka 50 ya Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC)

Shirika hilo linalomiliki kisheria leseni zote katika shughuli za utafiti, uendelezaji na uzalishaji, lilianza kazi mwaka 1973 kabla ya kugeuzwa Kampuni ya Taifa ya Mafuta kupitia Sheria ya Petroli ya 2015.

Mei 30 mwaka huu, Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC) limetimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma namba 17 ya mwaka 1969.

Maadhimisho hayo ya kihistoria yaliyofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam yalitanguliwa na masimulizi, ushuhuda wa safari ya Shirika hilo kutoka Mwenyekiti wake wa Kwanza, Silyvesta Barongo kupitia matumaini ya ugunduzi wa kwanza wa gesi asilia mwaka 1974 katika kisiwa cha Songo Songo.

Pamoja na tukio hilo, Idara za watalaamu na watafiti wa Shirika hilo walitoa elimu mbalimbali ya shughuli za utafiti, uendelezaji, uzalishaji, biashara ya gesi, mafuta na matarajio ya mchango wa sekta katika mapato ya kodi katika mfuko wa Serikali na mfuko wa Mafuta na Gesi kwa miaka mitano ijayo.

Shirika hilo linalomiliki kisheria leseni zote katika shughuli za utafiti, uendelezaji na uzalishaji, lilianza kazi mwaka 1973 kabla ya kugeuzwa Kampuni ya Taifa ya Mafuta kupitia Sheria ya Petroli ya 2015.

Katika hotuba yake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Mhandisi Kapuulya Musomba anajivunia mbele ya hadhira hiyo kuwa shughuli za utafiti zimefanikisha upatikanaji wa gesi asilia zaidi ya futi za ujazo trilioni 57 iliyoko kwenye visima mbalimbali vinavyotumika na visivyotumika, eneo la Nchi kavu na maji ya kina kirefu.

“Rasilimali hii imekuwa msaada mkubwa hususani katika kuzalisha umeme unaotumika viwandani, majumbani na kuendeshea vyombo vya moto (magari), bado tutaendelea na miradi ya kuunganisha katika huduma hizo ili kupunguza bei za bidhaa na huduma kupitia matumizi ya gesi,”anasema Mhandisi Kapuulya.

Kaimu Meneja Mtafiti kutoka Idara ya Mkondo wa Juu wa Shirika hilo, Shigela Josephat anasema tangu kipindi hicho hadi sasa, jumla ya visima virefu 96 vimekwisha chimbwa vikijumuisha vya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji.

Anasema hadi sasa Taifa lina vitalu zaidi ya 20 vilivyopo wazi kwa ajili ya uwekezaji mpya kwa maeneo ya nchi kavu na baharini huku leseni 11 zikiendelea kufanya kazi chini ya umiliki wa TPDC.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), kampuni zinazofanya shughuli za utafiti, uendelezaji na uzalishaji kupitia leseni hizo ni pamoja na Kampuni ya Mafuta ya Shell Tanzania, Pan African Energy Tanzania (PAET), Heritage Oil, Ndovu Resources Ltd, Equinor na Swala.

Gesi viwandani

Katika hatua za kutekeleza azma ya kupunguza ukali wa maisha kwa Mtanzania ndani ya miaka hiyo, Muhandisi Kapuulya anasema alama ya kwanza ni kuunganisha gesi kwenye viwanda.

Anasema kuanzia kipindi cha 2006/07 hadi kufikia Agosti mwaka jana, tayari viwanda 44 vilikuwa vimeunganishwa na gesi inayofikia futi za ujazo milioni 15 tu wakati akiba ni futi za ujazo trilioni 57.

Awali Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo Mtwara, Jagat Rathee alinukuliwa na vyombo vya habari akisema baada ya kuunganisha gesi katika kiwanda hicho, uzalishaji wake utaongezeka kutoka wastani wa tani 2000 za saruji hadi tani 6000 kwa siku.

Aidha, uzalishaji wa umeme katika kiwanda hicho utaongezeka hadi Megawati 35 za umeme wa njia ya gesi asilia ikilinganishwa na wastani wa megawati 20 zilizotokana na matumizi ya lita 106,000 mafuta ya dizeli kwa siku.

“Kiwanda kilikuwa kinatumia gharama kubwa kwenye Dizeli ili kupata megawati 18 hadi 22 tu kwa siku, ilikuwa ni gharama sana ndiyo maana tulizalisha tani 2000 tu,” anasema Rathee baada ya kutiliana saini mkataba wa miaka 20 na TPDC kwa ajili ya kuwaunganishia gesi asilia kiwandani hapo.

Mtaji wa Gridi ya Taifa

Kwa mujibu wa TPDC, mitambo iliyokuwa inafua umeme kwa kutumia mafuta badala ya gesi asilia imekuwa ikiisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 1 bilioni kuanzia 2011 hadi 2014.  

Aidha, umeme huo ulikuwa ukiigharimu Serikali kati ya Dola senti 35 hadi 42 kwa uniti, wakati ule unaozalishwa kutokana na gesi asilia ukiuzwa kati ya senti 6 hadi 8.

Licha ya dosari za kukatika kwa umeme mara kadhaa wa Tanesco, Mkurugenzi wa Utafiti, Uendelezaji na Uzalishaji wa TPDC, Venosa Ngowi anasema matumizi ya gesi nchini yamepunguza gharama kwa sehemu kubwa.

Anasema gesi iliyopo itatoshereza mahitaji ya ndani kutokana na upatikanaji wa rasilimali hiyo ambayo kwa sasa inafikia futi za ujazo trilioni 57 huku ikiwa imetumika chini ya trilioni moja.

“Upatikanaji wa nishati ya umeme nchini zaidi ya asilimia 55 unaotokana na gesi asilia hatua iliyopunguza gharama za uzalishaji,” anasema.

Usambazaji wa gesi majumbani

Pamoja na mchango huo katika gridi ya Taifa, alama nyingine ni utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa gesi majumbani, ulioanza Julai mwaka jana katika kaya 15 za Mkoa wa Mtwara kwa bajeti ya Sh1.3 bilioni kupitia awamu ya kwanza.

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani anasema Serikali imetenga futi za ujazo trilioni 1.2 za gesi kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa usambazaji Gesi Asilia Dar es Salaam kupitia Kampuni yake tanzu ya GASCO.

Kaimu Mkurugenzi wa Mkondo wa Chini wa TPDC, Emmanuel Gilbert anasema mradi huo unaotarajiwa kutumia Dola 270 milioni (sawa na zaidi ya Sh623.97 bilioni) utatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara ukihusisha sekta binafsi. 

Raymond Kavishe, mkazi wa Kinondoni anayepika katika jiko la gesi katika baa iliyopo Mikocheni, anasema amekuwa akitumia mkaa wa Sh15, 000 kwa siku, lakini baada ya kuanza kutumia gesi hiyo imemsaidia kupunguza asilimia 40 ya gharama alizokuwa akitumia kwenye mkaa.

“Nimepunguza gharama mara mbili kwa matumizi ya gesi hii. Kabla ya gesi hii nilikuwa natumia hadi mkaa wa Sh15, 000 kwa siku, lakini sasa nimepunguza gharama hizo mara mbili,” anasema Kavishe.

Miradi mikubwa

Kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015, TPDC imepatiwa haki ya kushiriki katika miradi mikubwa ya gesi kwa ubia wa asilimia 25, hatua inayoelezwa na wachambuzi wa sekta hiyo kwamba itachagiza kukua kwa kasi kwa kampuni hiyo.

Baadhi ya miradi hiyo itakayoanza hivi karibuni ni pamoja na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania utakaoanza Juni mwaka huu kwa gharama ya Dola 3.5 bilioni pamoja na Mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kusindika gesi asili (LNG Plant) utakaogharimu zaidi ya Dola 30 bilioni.

Mchango wa TPDC kwa jamii

Katika utekelezaji wa dhana ya uwajibikaji kwa Jamii (CSR) Shirika hilo limekuwa likitekeleza miradi mbalimbali hususani katika Jamii  ambazo Shirika linatekeleza majukumu yake, au Miundombinu ya Shirika inapatikana hapo.

Kupitia mpango wa CSR, Shirika limekuwa likisaidia katika Sekta mbalimbali ikiwamo Afya, Elimu, Utawala bora, Maji na Michezo.

Kaimu Mkurugenzi wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba anasema kati ya mwaka 2014 hadi 2019, Shirika hilo limegusa vijiji vya mikoa mbalimbali ikiwamo Lindi kwa ujenzi wa miradi inayogharimu zaidi ya Sh500milioni.

Wakazi na viongozi katika vijiji vya Mikoa ya Lindi wamepongeza mchango huo, huku wakiomba kuwekeza zaidi katika huduma za maji na afya kupitia vipaumbele vya shirika hilo.

Afisa Elimu Kata ya Kivinje/Singino, Zulfa Makame anasema wanafunzi walikuwa katika mazigira magumu yanayohatarisha ushiriki wa vipindi vya masomo yao kutokana na changamoto za huduma ya vyoo.

Mbali na kata hiyo, Februari mwaka huu Shirika hilo limetoa Sh22milioni katika Shule ya msingi Kinyerezi, Dar es Salaam kwa ajili ya ujenzi wa madarasa pamoja na hundi ya Sh10 milioni kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Bungu “B” Wilayani Kibiti.

Mtendaji wa Kata ya Songosongo, wilayani Kilwa, Shamte Bungara anasema TPDC imesaidia mradi wa maji lita 60,000 za maji, uliopunguza uhaba wa maji katika kijiji cha Songosongo chenye mahitaji ya lita 200,000 kwa siku.

“Kipaumbele kijacho tunaomba kiwe katika vitongoji vitatu kati ya vinne vya kijiji cha Songosongo, ambavyo vinakabiliwa na uhaba wa maji.  

Tahadhali na matumaini yajayo

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Masoko na Uewekezaji wa  Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Mhandisi Godwin Samwel anasimulia hujuma zilizokwamisha ukuaji wa shirika hilo, huku akitoa tahadhali na mbinu kwa uongozi ili kulifanya shirika hilo liwe kimataifa.

Mhandisi Samweli aliyetumikia Shirika hilo kuanzia 1984 hadi 2007 anasema mwaka 1992 uongozi wa Shirika hilo uliandaa mpango wa kukusanya tozo katika bei ya mafuta ambayo ingetumika katika kuimarisha Shirika hilo lakini Serikali ilikataa.

Mbali na hilo, Mhandisi Samweli anasema TPDC ilipendekeza kununua depo mbili za kuhifadhia mafuta kwa fedha ya Shirika lakini Serikali pia ilikataa kwa wakati huo ikidai Serikali haitakiwi kujiingiza katika ushindani wa kibiashara.

“Kama hilo lingekubalika, TPDC leo ingekuwa imepiga hatua kubwa sana, ingekuwa na msingi wa kufanya biashara,” alisema Mhandisi Samweli.

Hata hivyo, wakati tahadhari hiyo ikitolewa tayari TPDC imechangia katika Mfuko wa Mapato ya Mafuta na Gesi kiasi cha Sh7.9bilioni (2016/17), Sh28bilioni (2017/18) na Sh66bilioni kwa mwaka huu wa fedha 2018/19 huku matarajio yakiwa ni Sh87.3 bilioni( 2019/20), Sh92.6 bilioni(2020/21), Sh98.2bilioni (2021/22) na Sh104 bilioni kwa mwaka wa 2022/23. Mfuko huo ulianzishwa chini ya Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi ya mwaka 2015.

Mhandisi Samweli anasisitiza jambo la msingi akisema kampuni za kimataifa zilifanikiwa kupata mitaji katika mkondo wa juu baada ya kuwezeshwa katika eneo la mkondo wa chini.

“Jambo la kwanza ni political will (utayari wa kisiasa), hali ambayo ninaiona kwa sasa, wanaotoa maamuzi waone umuhimu wa kuliwezesha TPDC ili liwe na nguvu.”