Rais JPM azindua barabara Mbeya


Rais JPM azindua barabara Mbeya

“Naishukuru Wizara ya Ujenzi kwa kunialika kwenye hafla hii ya ufunguzi wa barabara ya Mbeya hadi Chunya, yenye urefu wa kilometa 72, na uwekaji wa jiwe la msingi kwenye barabara ya Chunya-Makolongolosi yenye urefu wa kilometa 39” Rais Magufuli.

Mbeya - Chunya yazinduliwa Chunya -Makongolosi yawekwa jiwe la msingi

 “Naishukuru Wizara ya Ujenzi kwa kunialika kwenye hafla hii, ya ufunguzi wa barabara ya Mbeya hadi Chunya, yenye urefu wa kilometa 72, na uwekaji wa jiwe la msingi kwenye barabara ya Chunya-Makolongolosi yenye urefu wa kilometa 39”

Ni kauli ya Rais Dkt. John Magufuli, aliyoitoa wakati anazungumza na maelfu ya wananchi wa Chunya,waliojitokeza kumsikiliza katika viwanja vya Saba Saba, vilivyopo wilayani humo, akiwa katika ziara yake ya kikazi ya siku tisa mkoani Mbeya.

Anasema wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, yapo mambo ambayo Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia Ilani yake ya Uchaguzi, kiliyaahidi na moja ya ahadi hizo ukisoma kwenye ukurasa wa 55, ilikuwa ni kukamilisha ujenzi wa barabara ya Mbeya-Chunya, Makongolosi yenye jumla ya kilometa 111.

Rais Dkt. Magufuli anaongeza hivyo amefurahi kufika wilayani humo, kufungua kipande cha barabara ya Mbeya-Chunya na pia kuweka jiwe la msingi la barabara ya Chunya-Makongolosi.

“Huu ni uthibitisho mwingine kuwa ahadi huwa ni deni, na deni tumelitimiza. Napenda niwapongeze watanzania wote,kwa kufanikisha utekelezaji wa miradi hii” anasema Rais Dkt. Magufuli.

Anaongeza ujenzi wa barabara hiyo ya Mbeya hadi Chunya, umegharimu shilingi bilioni 139.997, na ujenzi wa barabara ya Chunya kwenda Makongolosi, unagharimu shilingi bilioni 62.678” anasema Rais Dkt. Magufuli.

Kiongozi Mkuu huyo wa nchi, anasema hivyo jumla ya shilingi bilioni 202.675, zimetolewa na serikali na fedha hizo asilimia 100, zimetolewa na serikali waliyoichagua watanzania.

Anaongeza hiyo maana yake kwamba barabara hiyo imejengwa na watanzania, walipa kodi wakiwemo wananchi wa wilaya ya Chunya na kuwa barabara hiyo itaendelea kuleta mchango mkubwa katika kuchochea maendeleo ya wananchi wa Mbeya na Chunya kwa jumla.

Rais Dkt. Magufuli anasema anafahamu wananchi wa Chunya, ni wakulima wazuri wa mazao ya chakula na biashara, na pia Chunya ni maarufu kwa madini hususani dhahabu.

Hivyo basi ana matumaini makubwa kwamba wananchi wa Chunya, wataitumia vizuri barabara hiyo, kujiletea maendeleo, na kwamba kama wajuavyo serikali imechukua hatua mbalimbali za kukuza sekta ya madini, kwa kufuta kodi nyingi kwenye madini.

“Wilaya ya Chunya ya mwaka 2015, siyo Chunya ya leo niliyoiona, hongereni sana. Chunya imebadirika sana sana, imebadirika sana vile vijiji njiani ambavyo havikuwepo, ama vilikuwa vinaonekana kama maporini, leo nimekuta vijiji vimekua”anasema Rais Dkt. Magufuli.

Rais Dkt. Magufuli anasema anakumbuka akiwa Waziri wa Ujenzi, wakipirta kwenye barabara ya Mbeya-Lwanjilo na kutoka Lwanjilo hadi Chunya, walikuwa wakipita njiani wakikutana na wananchi, kwanza.

Barabara ya Kikusya - Ipinda – Matema

Lwanjilo hadi Chunya, walikuwa wakipita njiani wakikutana na wananchi, kwanza wakikuangalia walikuwa wamechoka, wamechukia halafu wanakuonyesha chini.

Kwa mujibu wa Rais Dkt. Magufuli, maana yake wananchi walikuwa wanaonyesha wanataka barabaraya kiwango cha lami, na alipopita safari hiiwananchi hawakumuonyesha hivyo, lakini kila alipokuwa akiangalia njiani mazao mazuri yamelimwa, nyumba nzuri za bati zimejengwa na mji umebadirika.

Rais Dkt. Magufuli anasema maendeleo hayo wameyafanya wananchi wa wilaya ya Chunya, wameibadirisha wilaya yao, Chunya imeanza kuwa wilaya ya mfano.

“Miaka hiyo nisingeweza kuona jengo la ghorofa, leo naona majengo ya ghorofa, Chunya jamani Chunya hongereni sana…” anasema Rais Dkt. Magufuli.

Naibu Waziri wa Ujenzi

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa anasema barabara ya kutoka Mbeya- Lwanjilo hadi Chunya, yenye urefu wa kilometa 72, na barabara ya Chunya- Makongolosi yenye urefu wa kilometa 39, ni sehemu ya barabara iliyo katika ushoroba wa kati magharibi, yaani Mbeya-Rungwa- Ipole-Tabora hadi Nzega.

Anaongeza barabara hiyo ni sehemu ya barabara kuu ya Mbeya-Chunya, Makongolosi-Rungwa hadi Mkiwa, yenye urefu wa kilometa 522, ambayo ni kiungo muhimu kwani inaunganisha mikoa mitatu ya Mbeya, Tabora na Singida.

“Mheshimiwa Rais Dkt.Magufuli, ukitoka Makongolosi kwenda Lupa zipo kilometa 182, ambazo na zenyewe zinaendelea kushughulikiwa.Lakini kutoka Rungwa kwenda Ipole mkoani Tabora, urefu wa kilometa 172” anasema Kwandikwa.

Kwandikwa anaongeza kwa maana hiyo anawahakikishia wananchi wa wilaya ya Chunya, kuwa serikali inaendelea kuwaunganisha vizuri namikoa ya Tabora pamoja na Singida.

Naibu Waziri Ujenzi anasema madhumuni ya ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami, ni kuwaondolea wananchi kero ya usafiri na usafirishaji, hususani katika msimu wa masika,ambapo mkoa wa Mbeya ni maarufu kwa kilimo cha mazao ya misitu, mazao mengine pamoja na uchimbaji wa madini.

Kwandikwa anasema wananchi wanahitaji kuunganishwa na maeneo ya masoko, ya mikoa ya kati ikiwemo Tabora, Singida, Arusha na Dodoma.

Mtendaji Mkuu wa Tanroads

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, anasema barabara ya kutoka Mbeya-Makongolosi, ni sehemu ya barabara ya kutoka Mbeya-Makongolosi, Lupa, Itigi hadi Singida yenye urefu wa kilometa 522.

Mhandisi Mfugale anasema serikali iliamua, kuanza kuijenga barabara hiyo, kwa kiwango cha lami na sehemu ya kwanza iliyoanza ndiyo inatoka Mbeya- Chunya hadi Makongolosi.

“Ili barabara hii ijengwe haraka, tuliigawanya katika sehemu tatu, ambazo ni Mbeya hadi Lwanjilo urefu wa kilometa 36, halafu Lwanjilo hadi Chunya yenye urefu kilometa 36, na ya mwisho ni Chunya hadi Makongolosi urefu wa kilometa 39” anasema Mhandisi Mfugale.

Barabara ya Kikusya-Ipinda Matema

Rais Dkt. Magufuli anasema matokeo ya barabara hizo na miradi mbalimbali, ni matokeo ya wananchi wa Kyela na watanzania kwa jumla, kuchagua kwao kuzuri.

Anaongeza anataka kuwaeleza ukweli kwamba hakuna siri ya hilio, kwani huwezi ukapeleka chakula kwa jirani wakati mtoto wako ana njaa na huo ndiyo ukweli wala hataki kuwaficha.

Anasema wananchi walimchagua yeye anayetokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), na asingepitishwa na CCM, asingekuwa Rais kwa hiyo viongozi hao wa Chama walipendekeza jina lake, wakampitisha na yeye akawa na deni moja tu la kuwafanyia kazi watanzania wote.

“Hata ukiwa siyo mwana-CCM, nikisema CCM oyeee wewe sema tuu, sababu utakapopita barabarani hii, barabara limejengwa kwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, sema CCM oyeee. Ninawashukuru sana ndagha ndagha ndagha fijho …” anasema Rais Dkt. Magufuli na kushangiliwa na wananchi.

Rais Dkt. Magufuli wananchi walipowachagua, yapo mambo ambayo yameainishwa vizuri kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM, klwamba ni lazima wayatekeleza katika kipindi cha miaka mitano, lakini mengine yatatekelezwa kipindi cha miaka kumi.

Anaongeza katika maendeleo yoyote huwezi kuyamaliza kwa siku moja, hata Mungu alitumia siku sita ya saba akapumzika, sembuse ya binadamu na kwamba anachotaka kuwaambia wananchi Ipinda ni kuwa wameanza vizuri.

Rais Dkt. Magufuli anasema mbunge Dkt. Mwakyembe alikuwa ni Naibu wake Wizara ya Ujenzi, na inawezekana historia hiyo wana-Kyela hawaijui, lakini baadaye Dkt. Mwakyembe akawa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi.

“Akaleta mapendekezo mazuri, akaingiza mikakati yake, meli zile zikaanza kutengezwa lakini inawezekana wapo wanaoweza kusema huyu siyo lolote, sababu shukrani ya Punda huwa ni mateke, unaweza ukambeba mtu ukampitisha kwenye shimo au barabara ama mto, ukiishafika kule akasema li mgongo lake lina jasho kwanza linanuka” anasema Rais Dkt. Magufuli.

Mbunge wa Jimbo la Kyela

Mbunge wa jimbo la Kyela na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, anasema wananchi wa Kyela watakuwa watu wa ajabu kama wasipomshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa barabara ya Kikusya-Ipinda hadi Matema.

Dkt. Mwakyembe anasema Rais Dkt. Magufuli alipofika wilayani Kyela, kuomba kura wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, aliwaahidi wananchi wilayani humo kuimalizia barabara hiyo na ni kweli ameimaliza kwa kiwango cha hali ya juu sana.

“Tunakushukuru sana tulikuwa tunachukua zaidi ya saa 6 kutoka Kikusya kwenda Matema, sasa hivi tunatumia dakika 30…” anasema Dkt. Mwakyembe.

Naibu Waziri wa Ujenzi

Naye Naibu Waziri wa Ujenzi, Kwandikwa anasema kukamilika kwa barabara hiyo ya Kikusya-Ipinda hadi Matema, itasaidia sana wananchi wa wilaya ya Kyela, sababu Matema ni mji wa kitalii.

Anaongeza lakini vile vile pamoja na serikali kuendelea kujenga miundombinu ya barabara, pia inakamilisha ujenzi wa meli moja ya abiria, na mbili za mizigo kila moja yenye uwezo wa kubeba tani 100, ambazo zitawaunganisha wananchi wa Mbeya na mikoa ya Ruvuma.

“Tunategemea wananchi hawa wataweza kubeba mazao yao na kuyapeleka mikoa mingine…tunaendelea kuwaunganisha wakazi wa mkoa huu wa Mbeya na mikoa mingine, ambapo tunaendelea kufanya usanifu kutoka Isyonje kwenda Makete” anasema Kwandikwa.

Kwandikwa anasema serikali imejipanga ili kuwahudumia watanzania kwa barabara nzuri, ili uchumi ukue na wananchi waweze kuboresha maisha yao.

Barabara ya Katumba-Mbambo hadi Tukuyu

Rais Dkt. Magufuli anasema barabara ya kutoka Katumba kwenda Busokelo wilayani Rungwe kufika hadi Tukuyu Kyela, kuna karibu kilometa 81.

Anasema serikali imetengeneza kilometa 10 eneo la Busokelo, na kuwa wananchi wake ni wakulima wazuri mno, wanalima maparachichi, ndizi, tangawizi, mahindi na chai.

“Serikali ninayoingoza haiwezi ikawaacha watu wa namna hii waendelee kuhangaika, kwa hiyo nimeamua leo kwamba nah ii barabara tunaitandika iwe ya kiwango cha lami moja kwa moja” anasema Rais Dkt. Magufuli na kuufanya umati wa wananchi kulipuka kwa shangwe.

Anaongeza kwa watu wachapakazi lazima wapate matunda ya kazi zao, hivyo anachotaka kuwaambia wana-Busekelo na Tukuyu kwa jumla, yapo mambo mengi yanafanyika na kazi zinafanyika, anachowaomba ni kuvumiliana na kikubwa waendelee kuliendeleza Taifa.