Mafanikio ya DUWASA katika kuimarisha huduma ya maji Makao Makuu ya nchi


Mafanikio ya DUWASA katika kuimarisha huduma ya maji Makao Makuu ya nchi

Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Mjini Dodoma (DUWASA) ilianzishwa mwezi Julai, 1998 kwa mujibu wa kifungu na 3(1) cha sheria No.8 ya mwaka 1997 ambayo ilibadilishwa kwa sheria Na. 05 ya mwaka 2019 ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira. Jukumu la msingi la DUWASA ni kutoa huduma endelevu ya usambazaji majisafi na usafi wa mazingira kwa wakazi wa mjini Dodoma.

Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Mjini Dodoma (DUWASA) ilianzishwa mwezi Julai, 1998 kwa mujibu wa kifungu na 3(1) cha sheria No.8 ya mwaka 1997 ambayo ilibadilishwa kwa sheria Na. 05 ya mwaka 2019 ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira.

Jukumu la msingi la DUWASA ni kutoa huduma endelevu ya usambazaji majisafi na usafi wa mazingira kwa wakazi wa mjini Dodoma.

DUWASA ilianzishwa ikiwa moja ya Mamlaka ya daraja ‘C’ ikitegemea ruzuku ya Serikali (Wizara ya Maji) katika uendeshaji hasa gharama za umeme na mishahara ya watumishi.

Hata hivyo, ilipanda kutoka daraja ‘C’ hadi ‘A’ mnamo mwaka 2003 na hivyo kujitegemea kwa asilimia mia (100%) katika gharama za uendeshaji na sehemu ya uwekezaji.

Hali ya huduma ya majisafi na uondoshaji majitaka mjini Dodoma

Huduma ya majisafi

Mahitaji ya maji

Utafiti na stadi za karibuni juu ya mahitaji ya maji kwa wakazi wa mji wa Dodoma ulifanywa mnamo mwaka 2002/2003 na Mhandisi mshauri SEURECA/NETWAS na kupitiwa (reviewed) na Mhandisi mshauri COWI Consult (2009).

Kwa mujibu wa stadi hizo, mahitaji ya maji mjini kwa sasa ni zaidi ya meta za ujazo 48,000 kwa siku. Kiasi hiki kinajumuisha mahitaji ya Chuo Kikuu cha Dodoma yanayofikia wastani wa mita za ujazo 3,000 kwa siku.

Hata hivyo, kufuatia ujio wa Serikali Makao Makuu ya Nchi - Dodoma, mahitaji ya maji yamekuwa yakiongezeka kwa kasi hali inayoashiria stadi hizi kupitwa na wakati na kuhitaji mapitio.

Vyanzo na uwezo wa uzalishaji maji

Chanzo pekee cha uzalishaji maji kwa matumizi ya wakazi wa mji wa Dodoma ni visima virefu vilivyochimbwa katika bonde la Makutupora. Bonde hili lipo takribani kilomita 30 kutoka mjini Dodoma.

Jumla ya visima vya uzalishaji maji 24 na visima vitano (5) vya kuchunguza mwenendo wa maji ardhini (observation boreholes) vimechimbwa katika bonde hilo. Uwezo wa visima vilivyopo kwa sasa pamoja na uwezo wa usafirishaji maji ni meta za ujazo zipatazo 61,500m3 kwa siku.

Uwezo huu wa uzalishaji maji umefikiwa mwaka 2015 baada ya uwekezaji mkubwa wa mradi wa kuboresha huduma ya upatikanaji wa majisafi kwa wakazi wa mjini Dodoma.

Mradi huu umeongeza uwezo wa uzalishaji na usafirishaji wa maji kutoka kwenye chanzo (Mzakwe) kutoka wastani wa mita za ujazo 32,000 kwa siku hadi kufikia mita za ujazo 61,500 kwa siku.

Gharama za mradi zilikuwa Dola za Marekani Milioni 49.623 zilizotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mkopo wenye masharti nafuu kutoka Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia Shirika lake la Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi (Economic Development Cooperation Fund – EDCF).

Uzalishaji halisi

Hivi sasa DUWASA inazalisha, kusafirisha, na kusambaza wastani wa meta za ujazo 52,000 kwa siku. Kiasi hiki cha uzalishaji kimekuwa kikiongezeka kwa kasi siku hadi siku na hivyo tunatarajia kufikia kiasi cha meta za ujazo 61,500 kwa siku katika kipindi kifupi kijacho. Hali hii imechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuhamishia Makao Makuu ya Serikali Jijini Dodoma.

Usafirishaji na Usambazaji maji mjini

Maji yanaposukumwa kutoka visimani hukusanywa kwenye matanki mawili yenye ujazo wa mita 680 na mita 800 yaliyopo Mzakwe. Ndani ya matanki hayo, maji hutibiwa kwa kutumia chlorine (Chlorination) iliyo katika mfumo wa Calcium Hypochlorite. Baada ya kutibiwa, maji huruhusiwa kuingia kwenye vituo vya kusukuma (kusafirisha) maji (pumping stations) kwenda mjini.

Kuna mabomba makuu mawili ya kusafirishia maji (transmission mains) kutoka kwenye chanzo eneo la Mzakwe kuja mjini yenye vipenyo vya mm 600 (inchi 24) kila moja. Mabomba hayo yana uwezo wa kusafirisha zaidi ya mita za ujazo 60,000 kwa siku kwa pamoja.

Aidha, kuna vituo wiwili vikubwa vya kusukuma maji kutoka Mzakwe vinavyoweza kusukuma zaidi ya mita za ujazo 60,000 kwa siku.

Mtandao wa kusambazia majisafi kwa sasa una jumla ya urefu wa kilomita zipatazo 516.69. Mtandao huu pia unajumuisha matenki makubwa mawili yenye ukubwa wa meta za ujazo 36,000 kila moja pamoja na matenki mengine manane (8) yanayotumika kuhifadhi na kusambaza maji yenye jumla ya meta za ujazo 20,030 hivyo kufanya jumla ya matenki yote kuwa na ujazo wa 90,470. Mtandao huu pia unajumuisha vituo sita (6) vya kusukumia maji.

Kwa sasa takribani asilimia 80 ya wakazi wa mjini Dodoma wanaokaribia kufikia 500,000 wanapata maji ya DUWASA. Hata hivyo, kufuatia ujio wa Serikali Makao Makuu - Dodoma, Mji wa Dodoma umekuwa ukipanuka kwa kasi na hivyo uhitaji wa kusogeza huduma za majisafi na majitaka kuongezeka.

Huduma ya Majitaka

Mfumo wa kukusanya na kusafirisha majitaka

Mnamo mwezi Februari 2002, DUWASA ilikabidhiwa dhamana ya kuendesha na kuhudumia mfumo wa majitaka mjini Dodoma kutoka CDA ambapo jumla ya wateja wapatao 2,000 walikuwa wamejiunga.

Mpaka sasa mtandao una urefu wa km 86 ambao unajumuisha mabomba makubwa ya kusafirishia majitaka (trunk sewer & sub trunk) yenye kipenyo cha mm 1100 na urefu wa km 24.3 na (lateral sewers) wenye jumla ya urefu wa km 61.7.

Mtandao mkuu wa kusafirishia majitaka (Main trunk) umesanifiwa kuhudumia watu wapatao 423,000. Hata hivyo, mtandao huu unahudumia takribani asilimia 20 tu ya wakazi kutokana na ukosefu wa mitandao midogo ya mabomba ya kukusanyia majitaka (lateral sewers).  Mitandao ya kukusanyia majitaka imeenea kikamilifu (comprehensive reticulation sewers network) kwenye maeneo matatu tu ya mji.

Maeneo hayo ni Mlimwa West (Area C), Mlimwa East (Area D) na Central Business Area. Maeneo mengine ya mji yaliyofikiwa na mtandao wa kukusanyia majitaka japo kwa kiasi kidogo ni kata za Makole, Viwandani, Madukani, Kizota, Chamwino, Kikuyu Kaskazini, Uhuru na Tambukareli.

Kwa maeneo ambayo mtandao wa majitaka hauyajafikia, wananchi wamekuwa wakitumia njia za septic na soak pit. DUWASA ina gari maalum la kunyonya majitaka (Cesspit emptiertruck) ambalo hutumika kuhudumia maeneo hayo yasiyo na mfumo wa uondoshaji majitaka. Huduma hii pia hutolewa na Manispaa pamoja na watu binafsi.

Mabwawa ya kutibu Majitaka

Mfumo uliopo wa kutibu majitaka ni mabwawa (Waste Stabilization Ponds - WSPs) yaliyopo kilometa zipatazo sita (6) toka mjini. Mabwawa haya yapo manne (4) kila moja likiwa na ukubwa wa meta 200 X 200. Mabwawa haya yalisanifiwa kwa muda ili kuhudumia watu 68,000 tu. Kwa sasa mabwawa haya yamezidiwa kutokana na kuhudumia watu wanaozidi usanifu wake. Mpango wa kujenga mabwawa mengine ya kudumu katika eneo la Nzuguni upo katika hatua ya kutafuta fedha za ujenzi.

Upimaji wa ubora wa majisafi na majitaka

DUWASA inatumia maabara yake mpya ya kisasa kwa ajili ya kupimia ubora wa majisafi na majitaka. Sampuli za majisafi kutoka kwenye maeneo mbalimbali ya mjini huchukuliwa na kupimwa mara mbili (2) kila mwezi ambazo hujumuisha Physical, Chemical pamoja na Bacterilogical parameters. Vilevile, sampuli za majitaka huchukuliwa na kupimwa toka katika mabwawa ya kutibu majitaka mara mbili (2) kila mwezi.

Kwa mujibu wa matokeo ya vipimo vya majisafi, maji yanayozalishwa na kusambazwa na DUWASA ni safi na salama kwa matumizi ya binadamu. Hii imethibitishwa pia na EWURA ambayo kwa wakati wake imekuwa ikifanya upimaji wa ubora wa majisafi katika maeneo mbalimbali ya mji na kuridhika kuwa ni safi na salama.

Mafanikio ya mamlaka toka kuanzishwa kwake

Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa DUWASA hadi sasa ni pamoja na:

   I.        Kuongeza uwezo wa uzalishaji maji kutoka lita 24,000,000 (1998) hadi kufikia lita 61,500,000 (2019) hivyo kuondoa migao mikali ya maji iliyokuwepo wakati huo.

II.        Kupunguza upotevu wa maji kutoka wastani wa 80% (1998) hadi kufikia wastani wa 26% kwa sasa.

III.        Kuongeza makusanyo ya maduhuli yatokanayo na huduma za majisafi na uondoshaji wa majitaka kutoka wastani wa TSh 14M= kwa mwezi (1998) hadi kufikia wastani wa TSh 1.6BN/= kwa mwezi (2019).

IV.        Kuongeza idadi ya wateja (maunganisho) wanaopata huduma majisafi kutoka 4,800 (1998) hadi kufikia maunganisho 41,740 (2019).

V.        Kuongeza idadi ya wateja (maunganisho) wanaopata huduma ya uondoshaji majitaka kutoka majisafi kutoka 2,000 (2000) hadi kufikia maunganisho 5,765 (2019).

VI.        Kumudu kutoa huduma ya majisafi kwa wakazi wa mji wa Dodoma bila ya kuteteleka.

Aidha katika kipindi cha hivi karibuni, DUWASA imepata mafanikio yafuatayo:

   I.        Kuongeza mtandao wa majisafi kutoka kilomita 303.6 (Julai, 2014) hadi kufikia kilomita 516.69 (Aprili, 2019) kwa kutekeleza miradi ya maji kwenye maeneo ya Mwangaza, Kisasa, Chidachi, Mlimwa, Kizota, Makulu, Ndachi, Nzuguni, Itega, Miganga, Mkalama, Swaswa, Ilazo extension, Miyuji, Mipango, Kinyambwa, Mapinduzi, Msalato, Veyula na Mbwanga.

II.        Kuongeza mtandao wa majitaka kutoka kilomita 79.3 (Julai, 2014) hadi kufikia kilomita 113.294 (Aprili, 2019) kwa kutekeleza miradi ya majitaka kwenye maeneo ya Area C-extension, Kigamboni, Bahi road, Kikuyu, Ipagala, barabara ya sita na Makole.

III.        Kupunguza upotevu wa maji (NRW) kutoka 30.5% (Julai, 2014) hadi kufikia 26.57% (Aprili, 2019).

IV.        Kuongeza wateja wa majisafi kutoka 28,833 (Julai, 2014) hadi kufikia wateja 42,829 (Aprili, 2019).

V.        Kuongeza Wateja wa Majitaka kutoka 4,922 (Julai, 2014) hadi kufikia wateja 5,779 (Aprili, 2019).

VI.        Kuongeza muda wa upatikanaji wa maji kwa wateja kutoka saa 16.8 (Julai, 2014) hadi kufikia saa 20 (Aprili, 2019).

VII.        Kuboresha mfumo wa kuchakata na kutuma Ankara kwenda kwa wateja ambapo kabla ya mwaka 2014 wasoma mita walikuwa wanaenda kwa wateja kuchukua usomaji wa dira kwa kuandika kwenye daftari na kisha kuja ofisini kuziingiza kwenye mfumo wa kuchakata Ankara hii ilikuwa inasababisha makosa ya kukosea Ankara za wateja kuwa mengi,  lakini kwa sasa  Mamlaka imeboresha mfumo kwa wasoma mita kuchukuwa usomaji kwa kutumia simu za mikononi na usomaji kutumwa moja kwa moja kwenye mfumo wa kuchakata Ankara, hii imesaidia kupunguza makosa ya kukosea Ankara za wateja kwa kiasi kikubwa. Halikadhalika Mamlaka imeboresha usambazaji wa Ankara za wateja ambapo kwa sasa Ankara za wateja zinatumwa kwa njia ya sms moja kwa moja kwenye simu ya mteja, hii imesaidia kufikisha Ankara kwa wateja kwa muda mfupi.

VIII.        Kuboresha njia za kufanya malipo ya Ankara za maji kwa kuhamia katika mfumo wa kielektroniki wa malipo wa Serikali kwa asilimia 100 ambapo kwa kutumia mfumo wa malipo wa Serikali wa GePG mteja anaweza kulipa ankara yake kwa kutumia matawi benki za NMB, CRDB, NBC na Benki ya Posta. Vile vile mteja anaweza kulipa kwa kutumia mitandao ya simu ya Vodacom, Tigo, Airtel, TTCL na Halotel, pia malipo yanaweza kufanywa kupitia mawakala wa mabenki waliopo kila kona. Hii imewasaidia wateja kupunguza muda waliokuwa wanaupoteza wakati wa kufanya malipo.

IX.        Kuongeza collection efficiency toka 77% mwezi June 2014 mpaka kufikia 91.4% mwezi   Aprili,  2019.

X.        Kuboresha njia za kupokea malalamiko / taarifa toka kwa wateja wake kwa kuanzisha kituo cha miito ya simu (Call centre) ambapo wateja wanaweza kupiga simu bila malipo yoyote na kufikisha taarifa /malalamiko yao. Kituo hiki kwa sasa kinafanya kazi kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 3:00 usiku.

Haya ni baadhi tu ya mafanikio ambayo DUWASA imeyapata tangu kuanzishwa kwake ambayo kimsingi yametokana na ushirikishwaji wa wadau katika kuandaa mipango mbalimbali ya DUWASA,  Uwekezaji katika miradi mbalimbali ya majisafi na majitaka kwa kushirikiana na Serikali pamoja na usimamizi makini wa utekelezaji wa mipango ya kibiashara ya Mamlaka.

Changamoto zinazoikabili mamlaka

Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana toka kuanzishwa kwa DUWASA na kupitia utekelezaji wa mpango wa kibishara, Mamlaka inakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na:-

(i)   Gharama kubwa za nishati ya umeme wa kuzalisha, kusafirishia na kusambazia maji, ambazo sasa zinafikia wastani wa TSh 490M/= kwa mwezi. Hii inachangiwa kwa kiasi kikubwa na asili ya chanzo cha maji (visima), na hali ya miinuko iliyopo katika mji wa Dodoma. Mamlaka inaendelea na jitihada za kupunguza kwa kufunga vifaa vyenye kupunguza matumizi ya umeme.

(ii)   Kubomoka kwa mitandao ya majitaka iliyojengwa kwa zege kwenye maeneo ya Area C na D, hivyo kusababisha mfumo wa kusafirisha majitaka katika maeneo hayo kuziba mara kwa mara na kutoa harufu mbaya.  Katika maeneo hayo, jumla ya km zipatazo 19 zimekwisha kuwa dhaifu na zinatakiwa kubadilishwa kwa gharama ya Sh 4.5bn/=. Changamoto hii pia imeanza kuyakuta maeneo mengine ya mji ikiwa ni pamoja na Mjini Kati na Uhindini.

Katika kutatua changamoto hiyo, mwaka wa fedha 2018/2019 DUWASA inatarajia kufanya ukarabati wa mtandao wa majitaka kwa maeneo ya area C na D kwa gharama ya Sh 4.5bn/= fedha ambayo inatolewa na Wizara ya Maji.

(iii)  Ufinyu wa mtandao wa kusambazia majisafi ambapo, zaidi ya kilometa 400 zinahitajika kujengwa ili kuyafikia maeneo mapya yasiyo na mitandao na yale yanayoendelea kuendelezwa. Pia urefu wa mtandao wa majitaka ni kilometa 89 tu ikilinganishwa na takribani kilometa 250 zinazohitajika. Ili kuendana na kasi ya ukuaji wa Jiji la Dodoma, DUWASA kwa kushirikiana na Wizara ya Maji imemuajiri Mhandisi Mshauri kampuni ya Norplan ambao wanafanya stadi ya mahitaji halisi ya huduma ya majisafi na uondoshaji wa majitaka kwa Jiji la Dodoma pamoja na Chamwino Ikulu ili baada ya hapo iandaliwe nyaraka ya zabuni kwa ajili ya kumpata Mkandarasi atayetekeleza kazi hizo.

(iv)  Wizi wa Maji unaofanywa na baadhi ya wateja wasio waaminifu hali inayosababisha upotevu wa maji na kuikosesha DUWASA mapato ya kuweza kujiendesha na kuhudumia wananchi kwa hali endelevu. Changamoto hii inatatuliwa kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali kama vile wananchi, viongozi na vyombo vya Dola.

Mipango ya DUWASA ya kuboresha zaidi huduma ya usambaji majisafi na uondoshaji wa majitaka

Mamlaka kwa kutumia bajeti yake ya ndani ina mpango wa kuendelea kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma za majisafi na uondoshaji majitaka kwa kutekeleza mipango ya muda mfupi, mipango ya muda wa kati na Mipango ya muda mrefu.  

Umuhimu wa kutekeleza mipango hii unasukumwa kwa kiasi kikubwa na uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano (5) kuamua kuhamia Makao Makuu ya Nchi, Dodoma.

Kwa mawasiliano:

Mkurugenzi Mtendaji

DUWASA

S.L.P 431

Tovuti: www.duwasa.go.tz

Simu: +255 26 2324245

Faksi: +255 26 2320060

Simu ya Taarifa (Bure): 0800110078

DODOMA