Tuzo za OSHA zaendelea kuiongezea thamani Kampuni ya NEWL


Tuzo za OSHA zaendelea kuiongezea thamani Kampuni ya NEWL

Makampuni mengi  yalishiriki kwenye tuzo za OSHA za mwaka huu kuliko miaka ya nyuma. Makampuni mengi yamekuwa na hamasa ya kushiriki na kujua umuhimu, usalama na afya mahala pa kazi.

Kampuni ya Northern Engineering Works Limited (NEWL) ilianzishwa mwaka 1987 kama kiwanda kidogo cha kuchomelea vyuma.

Ndani ya miaka zaidi ya thelathini, mfumo wa kazi zetu umebadilika kwani sasa kampuni imejiongeza na kujiimarisha kwenye kazi kadhaa za umeme, zaidi kuhusiana na kujenga, kuimarisha na kuhudumia minara ya simu nchi za Tanzania, Malawi na hivi karibuni nchini Kenya.

Kampuni imejikita kutoa ufumbuzi wa teknolojia ya uhandisi kwenye utekelezaji wa mawasiliano ya mbali, uunganishaji wa gridi ya taifa na huduma za umeme na mitambo.

Mnazizungumziaje Tuzo za OSHA za mwaka huu ukilinganisha na miaka iliyopita?

Tuzo za OSHA za mwaka huu kaulimbiu yake ilikuwa ni Usalama na Afya na mustakabali wa kazi kuelekea uchumi wa viwanda. Makampuni mengi  yalishiriki kwenye tuzo za OSHA za mwaka huu kuliko miaka ya nyuma. Makampuni mengi yamekuwa na hamasa ya kushiriki na kujua umuhimu, usalama na afya mahala pa kazi.

Je, hii ni mara ya ngapi mnashiriki katika Tuzo za OSHA?

Hii ni awamu ya tatu kwa kampuni ya NEWL kushiriki katika tuzo za OSHA.

Ni imani ya makampuni mengi kuwa ushiriki wao katika tuzo mbalimbali ni sehemu ya kuingozea thamani kampuni hizo. Je, tangu muanze kushiriki katika tuzo hizi, thamani yenu imepanda kwa kiasi gani?

Thamani imeongezeka kwa sababu kupitia tuzo hizi tumeweza kupata wateja wengi kwa kutuamini kuwa tunajali usalama wa wafanyakazi wetu mahala pa kazi.

Kabla ya ushindi wa mwaka huu, mlishawahi kushinda tuzo hizi miaka iliyopita mara mbili katika vipengele tofauti tofauti. Nini siri ya mafanikio haya?

Tumeshawahi kushinda mara mbili. Siri ya mafanikio ni kwamba sisi tuliopewa dhamana ya kitengo hiki cha usalama kazini ni kuhakikisha muajiri anafuata sheria zinazotolewa na OSHA na kuhakikisha zinafanyiwa kazi na wafanyakazi wote.

Pia, mnamo mwaka 2017 tulifanya mafunzo, uandaaji wa taarifa mbalimbali na hatimaye kufanyiwa ukaguzi wa OHSAS 18001:2007 na kutunukiwa cheti.

Nini ambacho kampuni imekuwa ikijifunza kutokana na ushiriki wake katika Tuzo za OSHA?

Kampuni imekuwa inaendelea kujifunza kutunza usalama mahala pa kazi, zaidi kupitia kampuni shiriki. Kutengeneza mahusiano mazuri na kampuni nyingine.

Mnautumiaje ushindi wa mwaka huu kuwa kama chachu ya maandalizi ya ushiriki wenu kwa miaka ijayo?

Tunahakikisha tunaendelea kutunza nafasi yetu ya ushindi na kuhakikisha wenzetu watajifunza vizuri kwenye nafasi yetu.

Kwa nini mmekuwa mkishiriki mara kwa mara katika tuzo hizi za OSHA? Yapi malengo ya kampuni ya kushiriki katika tuzo hizo?

Kulingana na kazi tunazofanya, OSHA inatusaidia kuboresha ufanisi wa kazi zetu na kuepukana na madhara katika maeneo yetu ya kazi.

Mnajiona wapi katika tuzo za mwakani za OSHA?

Tunajiona kuendelea kujitahidi zaidi na kutokupoteza nafasi yetu ya ushindi.

Kwa kiasi gani kampuni hiyo imekuwa ikizingatia kanuni za usalama na afya mahali pa kazi?

Kwa kutoa mafunzo mara kwa mara kwa wafanyakazi, wageni na wanajamii inayotuzunguka.

Ukipewa, fursa ya kutoa mapendekezo kwa waandaaji ya wapi pa kuboresha katika tuzo za miaka ijayo za OSHA, itakuwa nini?

Tunaomba mboreshe mabanda ya ushiriki na T-shirt zitolewe kwa washiriki wote kwa wakati.

Mwisho kabisa una ujumbe gani unataka kuwaambia Watanzania?

Kila mtu anawajibu wa kujifunza umuhimu wa usalama mahali popote kwa kufikiria kwanza usalama na kutenda kiusalama.