ELERAI ni kampuni bora ya ujenzi yenye hadhi ya daraja la kwanza nchini


ELERAI ni kampuni bora ya ujenzi yenye hadhi ya daraja la kwanza nchini

Mafanikio ya kampuni ni makubwa kwani tangu kuanzishwa kwake imeweza kusajiliwa daraja la kwanza mnamo Julai 3, 2007 daraja ambalo tumesimamia hadi leo na limetuwezesha kufanya miradi mikubwa nchi nzima.

ELERAI Construction Company Ltd ni Kampuni ya ujenzi daraja la kwanza nchini ambayo inahusika na ujenzi wa barabara na majengo.

Kampuni hii ilisajiliwa mnamo mwaka 1991, ambapo Makao makuu ya kampuni hii yapo Sakina, Arusha na pia kuna ofisi katika mikoa mingine kama Mwanza na Dar es Salaam.

Kampuni hii inafanya kazi za ujenzi wa barabara na majengo ya Serikali, taasisi za Serikali, mashirika ya umma, makampuni binafsi, wafanyabiashara, taasisi za kidini na mtu mmoja mmoja.

Yapi Malengo ya uanzishwaji wa kampuni hii nchini

Lengo kuu la kuanzishwa kwa kampuni hii ni kufanya kazi za ujenzi wa majengo na barabara kwa ubora wa hali ya juu na kutimiza matakwa ya wateja wetu kwa kiwango cha kupitiliza kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi.

Vipi kuhusu soko la sekta ya ujenzi nchini? Je, kuna fursa yoyote ya kukua kwa soko hilo kwa siku zijazo?

Sekta hii ya ujenzi wa barabara na majengo hapa nchini ni sekta endelevu ambayo inakua siku hadi siku. Kazi za ujenzi kiujumla kila wakati kunaibuka mitindo mipya ya ujenzi hususani wa majengo na miundombinu mingine jambo linalofanya kila wakati wateja kufikiria design/mitindo mipya ya kupata huduma husika. Soko la sekta hii bado ni kubwa na litaendelea kukua japo kuna Changamoto nyingi za hapa na pale.

Tueleze kwa ufupi kuhusiana na baadhi ya miradi ya ujenzi ambayo mmeweza kuifaniskisha chini ya kampuni hii?

Tangu kuanzishwa kwake kampuni hii imefanikisha ujenzi wa miradi mingi ya Serikali, taasisi za Serikali, Makampuni na taasisi binafsi n.k Mfano Ujenzi wa Chuo Kikuu cha Mandela Arusha, ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, ujenzi wa visima mbalimbali vya mafuta vya BP (Puma), ujenzi wa mahoteli kama vile Joshmal Hotel, A1 Hotel- Arusha, ujenzi wa stendi za mabasi kama Morogoro, Dodoma, Tanga, Tabora; ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Manyara, ujenzi wa hospitali ya Mkoa wa Manyara, ujenzi wa jengo la TRA Manyara, ujenzi wa jengo la BAWASA Manyara, ujenzi wa jengo la TBA Arusha, ujenzi wa jengo la Umoja wa Makanisa Maji ya Chai Arusha, ujenzi wa makazi ya wafanyakazi (staff houses) wa TANAPA Serengeti, Arusha Park, Tarangire na Mkomazi; mradi wa umeme (TANESCO) Biharamulo, TANESCO Ngara na TANESCO Mpanda.

Na sasa kuna miradi inaendelea kama vile mradi wa soko la kisasa Kibaha, Mradi wa Maghala ya kuhifadhia chakula NFRA Babati-Manyara na Mpanda.

Kipi ambacho kampuni kinaitofautisha na makampuni mengine ya ujenzi wa majengo hapa nchini?

Kampuni hii imeweza kujipambanua vizuri katika namna bora zaidi ya ufanyaji kazi wake kwa kushirikisha timu ya wataalamu wa kutosha katika Idara zote zinazohusiana na ujenzi na Idara shirikishi/saidizi na ina vitendea kazi vya kutosha na ofisi za kutosha maeneo mengi nchini.

Kampuni imeweza kuwa na akiba ya vifaa na malighafi nyingi za ujenzi kama vile nondo, saruji (cement), mchanga, matofali, mitambo ya kisasa ya kufyatulia tofali na paving, mitambo ya ujenzi (earth moving equipments), Magari ya kazi na ya operations ya kutosha, karakana za Aluminium, za uchomeleaji, za mbao vyote hivi vinafanya kazi zifanyike kwa uharaka na wepesi na kwa gharama nafuu zaidi ndani ya kampuni yetu badala ya kutafuta kandarasi saidizi.

Pia, kampuni ina kampuni dada zingine kama Northern Engineering Works Ltd na Joshmal Investment ambazo zinasaidia sana katika kusaidia (backup) huduma mbalimbali. Kampuni ina ofisi nzuri na za kisasa Dar es Salaam na Arusha na kote kuna watumishi. Kampuni ina mafunzo kwa wafanyakazi wake mara kwa mara na inashiriki vikao vya bodi za kitaalamu mara kwa mara.

Pia, tunapata fursa ya kujifunza kutoka kwa wakandarasi wengine ndani na nje ya nchi na kupitia mitandao kama google, You Tube n.k. Pamoja na mambo mengine, sehemu kubwa ya faida inatumika kuboresha huduma za kampuni ili kuweza kuendelea kutoa ushindani katika soko kwa kutoa huduma bora zaidi kwa gharama nzuri.

Kampuni hii imeweza kutoa ajira kiasi gani hapa nchini?

Kampuni hii imeweza kutoa ajira nyingi sana tangu kuanzishwa kwake kwa makundi tofauti tofauti kuanzia kwa watu wa kawaida hadi kwa watu wenye fani zao (professionals).

Kuna wafanyakazi wa kudumu na wa mikataba ya miaka 2 au 3, pia kuna wanafunzi wanaofanya mafunzo tarajali (field). Pia, kuna ajira zinazotolewa kupitia kwa makampuni ya ulinzi, na kupitia wakandarasi wadogo (sub-contractors) na hata kwa mama wa nyumbani ambao huwa wanatoa huduma za chakula na usafi katika maeneo ya miradi na ofisi.

Kiujumla maisha, afya na hali za wafanyakazi wetu zinaonesha jinsi gani kampuni imeweza kutoa ajira tena ajira zenye tija kwa maisha yao, ndugu zao na hata watoto na wategemezi wao wengine. Michango ya kampuni hii kwenda mifuko ya kijamii pia na kodi ya mishahara (PAYE) inadhihirisha mchango wa ajira wa kampuni hii kwa Serikali na watumishi wengine wa taasisi mbalimbali.

Nini kinaweza kusimama kama alama ya mafanikio ya kampuni tangu kuanza kwa Shughuli zake hapa nchini?

Mafanikio ya kampuni ni makubwa kwani tangu kuanzishwa kwake imeweza kusajiliwa daraja la kwanza mnamo Julai 3, 2007 daraja ambalo tumesimamia hadi leo na limetuwezesha kufanya miradi mikubwa nchi nzima. Pia, kwa miaka takribani 25 iliyopita kazi zote zilizofanywa na kampuni kwa watu binafsi, taasisi za serikali, mashirika ya dini na miradi ya wafadhili imekuwa imara kwa wakati wote na bila kasoro kujitokeza baadae.

Mambo gani yakirekebishwa sekta ya ujenzi itaweza kustawi zaidi ya hapa?

Sera, na mikataba ya kazi hususani kwa kazi zinazotolewa kwa makampuni ya kigeni (ya nje), hapa tunashauri Serikali na bodi husika ziweke utaratibu jumuishi (joint venture) kwa miradi yote inayotolewa kwa makampuni ya kigeni.

Hii itasaidia kuongeza ajira kwa wazawa, kupata na kujifunza teknolojia mpya kutoka kwa makampuni ya kigeni na pia kuongeza pato la makampuni ya ndani ya nchi (wazawa).

La pili, tungetamani kuona TBA wanabaki kuwa wasimamizi na waangalizi wa kazi za ujenzi za Serikali na wakandarasi waendelee kushindana katika kazi hizi.

Utitiri wa kodi mbalimbali, Serikali kupitia taasisi husika iliangalie upya na kwa mapana yake suala la kodi mbalimbali katika sekta ya ujenzi.

Kwa namna gani mnashiriki katika ajenda ya uchumi wa viwanda ya Rais John Pombe Magufuli?

Uchumi wa viwanda unakwenda bega kwa bega na upatikanaji wa umeme wa uhakika. ELERAI Construction Company Ltd imejenga vituo vikubwa sana vya kuzalisha umeme Wilaya ya Biharamulo na Ngara mkoani Kagera na Mpanda.

Umeme unaopatikana kutoka kwenye vituo hivi vya umeme wa mafuta vinafanya kuwe na umeme wa uhakika katika maeneo ya viwanda vidogo, vikubwa na vya kati katika maeneo husika.

Uchumi wa viwanda pia unakwenda bega kwa bega na uboreshaji wa miundombinu ya barabara kutoka maeneo mengi ya uzalishaji malighafi kwenda maeneo yenye viwanda. ELERAI Construction Company Ltd imekuwa ikiboresha barabara nyingi vijijini kupitia kandarasi zake na Tanroad. Kazi hizi zimekuwa zikifanywa kwa ubora mkubwa na kwa wakati jambo linalofanya urahisi wa mawasiliano ya barabara wakati wote.

Uchumi wa viwanda pia unategemea mawasiliano ya simu katika kuunganisha ufanisi wake. ELERAI Construction Co. Ltd kupitia kampuni dada yake Northern Engineering Works Ltd wamekuwa wahudumiaji wakubwa wa minara ya simu kwa miaka zaidi ya 15 ndani na nje ya nchi, na ili limesaidia kufanya uwepo wa mawasiliano kwa maeneo mengi kwa muda wote hivyo kurahisisha shughuli za viwanda kupata malighafi, masoko na watumishi wakati wote.

Changamoto gani mnazokabiliana nazo? Na kwa namna gani mnageuza changamoto hizo kuwa fursa ya kusonga mbele?

Kwa sasa sekta yetu ya ujenzi inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuyumba kwa mitaji kwa kuwa kazi nyingi kubwa zinafanywa na wakandarasi wa kigeni ambao kwa sasa hakuna sheria yoyote inayowalazimisha kuingia utaratibu wa pamoja (joint venture) na wakandarasi wazawa. Hivyo fedha zetu zote wanabeba wao.

Pia, kazi nyingi za Serikali kwa sasa zinafanywa na taasisi za Serikali tu kama JKT na TBA na ikumbukwe kuwa Serikali ndiye alikuwa mteja mkubwa kwa kazi hizi za ujenzi. Namna mojawapo ya kukabiliana nazo changamoto hizi ni pamoja na kuiomba Serikali itazame upya namna bora ya kushirikisha wakandarasi wazawa kwa kazi wanazopewa wageni na pia TBA na JKT.

Changamoto nyingine inatokana na mifumo yetu ya kodi, kodi nyingi zinazolipwa siyo rafiki na ni kubwa kulingana na hali halisi.

Gharama za uendeshaji kampuni za ujenzi ni kubwa hasa ukizingatia mifumo ya ulipaji ilivyo ni kwa njia ya vyeti (certificates). Hivyo inakulazimu muda wote uwe na fedha au malighafi hitajika wakati wote.

Namna tunavyogeuza changamoto hizi kuwa fursa ya kusonga mbele ni kwa kuendelea kuzifanya kazi hizi katika mazingira haya haya na huku tukiendelea kuiomba Serikali na taasisi husika katika mifumo hii ili kuweza kuboresha zaidi mazingira husika.

Wapi mnaiona kampuni yenu baada ya miaka mitano?

Katika miaka mitano ijayo, kama kutakuwa na mabadiliko katika maeneo yenye changamoto na vikwazo, tunaamini kampuni yetu inaweza kuwa miongoni mwa makampuni makubwa sana ya ujenzi hasa katika kitengo cha majengo na ili linaweza kusaidia kupunguza mwanya wa makampuni ya kigeni kuja kwa wingi katika sekta hii.

Mnatoa ujumbe gani kwa Watanzania wote?

Fursa bado zipo katika sekta ya ujenzi kwa kuwa bado kuna maeneo mengi sana bado yanahitaji kujengwa na idadi ya watu inazidi kuongezeka.

Kila jengo lililojengwa miaka 10, 20 au 30 iliyopita kwa sasa sehemu kubwa linaweza onekana limepitwa na wakati. Hivyo linaweza vunjwa tena likajengwa jengo jingine jipya na la kisasa zaidi au likaboreshwa (renovation) ambapo kwa sasa wengi wanafanya renovations.

Vivyo hivyo, barabara zilizojengwa miaka 10, 15 iliyopita tayari zinahitaji kubomolewa na kujengwa zingine au kuboreshwa zaidi.

Fursa kwenye sekta ya ujenzi bado ni kubwa na itaendelea kuwa kubwa kadri watu wanavyozidi kuongezeka.