Miradi ya Maendeleo ya Vijiji wilayani Moshi iliyotekelezwa na FTK Mwaka 2017 na 2018


Miradi ya Maendeleo ya Vijiji wilayani Moshi iliyotekelezwa na FTK Mwaka 2017 na 2018

Kwa kutumia malengo haya na madhumuni thabiti yanayohusiana na utekelezaji, FTK imeweka mpango ambao umelenga kuwaalika wadau wengine, ikiwa ni pamoja na Jumuiya, Mamlaka za chini za Serikali na Mashirika yasiyo ya kiserikali, kutambua ni malengo gani na sekta zinazofanana na malengo yao na kufikiria namna bora ya kufanya kazi kwa kushirikiana na FTK, kuelekea kufanikisha malengo hayo ya pamoja.

FT Kilimanjaro (FTK) ni Shirika lisilo la Kiserikali lililosajiliwa hapa Tanzania. FTK ni mpango wa pamoja baina ya Dutch FEMI Foundation na Kampuni ya TPC Ltd. Lengo la FTK ni kuboresha ustawi wa jamii mbalimbali zilizopo katika lindi la umaskini katika eneo la Moshi Chini.

Shirika hilo linakusudia kujenga jamii ambazo watu wote (wanawake kwa wanaume, vijana na wazee) watapata huduma za msingi za afya, elimu na fursa sawa za kuwa wazalishaji na kukimu maisha yao na familia zao na linakusudia kulitekeleza hilo katika njia tegemezi na mazingira endelevu.

Moshi Chini inapatikana Kusini mwa Wilaya ya Moshi Vijijini, sehemu ya Mkoa wa Kilimanjaro Kaskazini mwa Tanzania. Eneo hilo liko Kusini mwa Mji wa Moshi na limezungukwa na takriban hekta 16,000 ya shamba la miwa la kampuni ya kuzalisha sukari ya TPC.

Watu wapatao 75,000 wanakadiriwa kuwa wanaishi na kuzunguka eneo hili, ikiwa wameenea zaidi katika Kata tatu za Arusha Chini, Mabogini na Kahe katika Wilaya ya Moshi Vijijini na idadi ndogo ya vijiji katika Wilaya za karibu na Mkoa mwingine.

Wakiongozwa na dhana ya mbinu jumuishi ya maendeleo, hatua zinazotumika mara kwa mara na katika sekta nyingi, kazi zao kubwa zimejengwa kuzungukia malengo ya muda mrefu katika sekta nne (Elimu, Afya, Mapato na Miundombinu) ambazo zina uhusiano wa moja kwa moja.

Kwa kutumia malengo haya na madhumuni thabiti yanayohusiana na utekelezaji, FTK imeweka mpango ambao umelenga kuwaalika wadau wengine, ikiwa ni pamoja na Jumuiya, Mamlaka za chini za Serikali na Mashirika yasiyo ya kiserikali, kutambua ni malengo gani na sekta zinazofanana na malengo yao na kufikiria namna bora ya kufanya kazi kwa kushirikiana na FTK, kuelekea kufanikisha malengo hayo ya pamoja.

Katika kufanikisha malengo haya, FTK kwa kushirikiana na wadau mbnalimbali ikiwemo kampuni ya sukari ya TPC imetekeleza miradi mbalimbali ambayo imesaidia katika kubadili maisha ya wakazi wa eneo la Moshi Chini na maeneo ya jirani katika kipindi cha mwaka 2017 na 2018. Baadhi ya miradi hiyo ni kama ifuatavyo:

Katika kipindi cha mwaka 2017, taasisi ya FTK imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali katika maeneo yake ya kimkakati ambayo ni Elimu, Afya, Kipato na Miundombinu.

Elimu

Kwenye eneo hili la elimu taasisi hii imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo; ujenzi wa jiko la shule, ukarabati wa majiko ya kupikia kwenye shule mbili za Msingi, utoaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi 242,400 kwenye shule mbalimbali kwa kushirikiana na wazazi, kufanikisha wanafunzi 80 kurudi shule kutokana na kupatiwa huduma ya chakula cha mchana kwenye shule ya ChemChem.

Mingine ni; utoaji wa fedha Tsh 5,970,000 kwa shule za Msingi za Ronga, Mikocheni na Chemchem kutokana na kupata madaraja ya A 25 na B 218 kwenye mtihani wa Taifa wa darasa la saba, ufadhili wa kimasomo ya Sekondari na vyuo vya ufundi kwa wanafunzi 205, idadi ya wanafunzi wa kike 810 walidahiliwa kwenye darasa la mradi wa Binti Shupavu, utoaji wa huduma ya usafiri wa kwenda na kurudi shuleni kwa wanafunzi 260 wa shule za Sekondari.

Uzalishaji wa kipato

Ujenzi wa kisima kwenye mashamba kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa maji ya kutumia na kumwagilia mazao, kuongezeka kwa mavuno ambapo ekari 80 zimeongezeka kuvunwa kutokana na ujenzi wa kisima, kutoa fedha za mitaji ya kuanzia biashara kwa wajasiriamali wapatao 85, zaidi ya tani 250 za mazao ya shamba zimevunwa kwenye shamba la Mtakuja na uandaaji wa semina 8 za kilimo kuhusu njia bora za kilimo.

Afya

Utoaji wa vipimo vya kwa watoto wapatao 1,716 waliohudhuria kambi ya afya, utoaji wa vidonge vya kinga ya minyoo kwa wanafunzi wapatao 4,186 kutoka kwenye shule 16, utoaji wa huduma za vipimo na matibabu kwa watoto 12 wenye ulemavu.

Maeneo mengine

Mbali na maeneo hayo ya kimkakati taasisi ya FTK pia ilitekeleza mambo mbalimbali kwa lengo la kusaidia jamii za Moshi Chini katika kipindi cha mwaka 2017.

Mambo hayo ni pamoja na; utoaji wa mikopo midogo kwa akina mama 15 wanaolea watoto bila baba (Single mothers), utoaji wa mikopo na mafunzo kwa akina mama 33 wanaolea watoto bila baba (Single mothers).

Nyingine ni utoaji wa baiskeli mpya 22 za kubebea mizigo, kukabidhi nyumba mbili za makazi zilizojengwa na C-re-Aid, kutoa mikopo ya biashara kwa waombaji 85, ukarabati wa kilomita 19 za barabara (barabara ya shamba la Mtakuja, Mikocheni, Kahe na barabara ya Kikavu).

Katika kipindi cha mwaka 2017 taasisi ya FTK ilitumia kiasi cha EURO 600,000 ambazo ni sawa na fedha za Kitanzania TSh 1,600,000,000 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Mwaka 2018, taasisi ya FTK ilikuwa inatimiza miaka 10 toka ilipoanza kufanya shughuli zake hapa nchini, ndani ya mwaka huo, FTK ilifanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali pamoja na kusaidia jamii nyingi zenye uhitaji. Miongoni mwa shughuli walizofanya katika maeneo yake ya kimkakati ni kama ifuatavyo:

Elimu

Kwenye eneo hili la elimu taasisi hii imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo; ujenzi wa jiko la shule, kutoa huduma ya chakula cha mchana kwa wanafunzi 119,531 kwenye shule za; Londoto wanafunzi 19,486, Chemchem wanafunzi 53,595 na Mikocheni wanafunzi 46,450, ukarabati wa majiko ya kupikia kwenye shule mbili za Msingi, utoaji wa fedha TSh 3,600,000 kwa shule za Msingi za Ronga, Mikocheni na Chemchem kutokana na kupata madaraja ya A 25 na B 218 kwenye mtihani wa Taifa wa darasa la saba.

Kazi nyingine ni pamoja na; ufadhili wa kimasomo ya Sekondari na vyuo vya ufundi kwa wanafunzi 49 na utoaji wa huduma ya usafiri wa kwenda na kurudi shuleni kwa wanafunzi 300 wa shule za Sekondari.  

Uzalishaji wa kipato

Ujenzi wa kisima kwenye mashamba kwa ajili ya kusaidia upatikanaji wa maji ya kutumia na kumwagilia mazao, kuongezeka kwa mavuno ambapo ekari 80 zimeongezeka kuvunwa kutokana na ujenzi wa kisima, kutoa fedha za mitaji ya kuanzisha biashara kwa wajasiriamali wapatao 85, kuanzisha biashara kwa wajasiriamali wapatao 85, zaidi ya tani 250 za mazao ya shamba zimevunwa kwenye shamba la Mtakuja na uandaaji wa semina 8 za kilimo kuhusu njia bora za kilimo.

Afya

Utoaji wa vipimo vya afya kwa watoto wapatao 1900 waliohudhuria kambi ya afya, utoaji wa vidonge vya kinga ya minyoo kwa wanafunzi wapatao 3433 kutoka kwenye shule 16 na kutoa matibabu kwa wagonjwa 44 walioko katika hali mbaya ya afya kupitia mfuko wa matibabu ya dharura pamoja na kutoa misaada kwa watu 109 kupitia program ya Mama Bus.

Maeneo mengine

Maeneo mengine ambayo taasisi ya FTK ilitoa misaada katika kipindi cha mwaka 2018 ni pamoja na; kutoa mikopo midogo kwa akina mama 33 wanaolea watoto bila baba (Single mothers), semina 3 za mafunzo ya kuongeza uwezo ziliendeshwa kwa wanajamii, utekelezaji wa ujenzi na ukarabati wa kilomita 30.6 za barabara (Londoto 8.8 km, Mikocheni 9 km, Newland 4 km na Mtakuja 8.8 km).

Katika kipindi cha mwaka 2018 taasisi ya FTK ilitumia kiasi cha EURO 460,000 ambazo ni sawa na fedha za Kitanzania TSh 1,210,000,000 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.