Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) laadhimisha Siku ya Mabaharia duniani


Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) laadhimisha Siku ya Mabaharia duniani

Kuridhiwa kwa Mkataba wa Kazi wa Kimataifa wa mwaka 2006 (Maritime Labour Convention, 2006) na Serikali ya Tanzania pamoja na kutungwa kwa kanuni mbalimbali na TASAC juu ya usimamizi wa shughuli za masuala ya bahari ni miongoni mwa hatua chanya za kutambua mchango wa sekta ya bahari na mabaharia kwa ujumla nchini Tanzania

Mnamo mwaka 2010 mkutano wa kidiplomasia uliyofanyika Manila, Philippines, Shirika la Bahari Duniani (IMO) liliazimia na kuitenga siku ya tarehe 25 ya mwezi Juni kila mwaka kuwa ni Siku ya Mabaharia duniani ikiwa ni kutambua kuwa kila ambacho tunatumia katika maisha yetu ya kila siku kimehusisha sekta ya bahari ama moja kwa moja au vinginevyo katika usafirishaji wa bidhaa hiyo.

Dhumuni la maadhimisho haya ni kutambua mchango wa mabaharia katika uchumi wa dunia na kutambua madhara (risks) wanayokabiliana nayo.

Tukirejea nyuma hadi mwaka 2016, ambapo kauli mbiu ilikuwa “baharini kwa wote” ikiunganishwa na kauli mbiu iliyotolewa na IMO katika kuadhimisha Siku ya Bahari Dunia isemayo “shipping indispensible to the world”, ikiwa na maana “shughuli za Usafiri wa bahari haziepukiki katika dunia,” kauli mbiu hiyo ilisisitiza juu ya jinsi gani mabaharia ni muhimu katika maisha yetu ya kila siku.

Kwa mujibu wa takwimu za IMO, takriban asilimia 90 ya shehena kwa matumizi ya jamii mbalimbali duniani inasafirishwa kwa njia ya bahari.

Katika kuadhimisha umuhimu wa siku hii , MKurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) anasema” tunapo sherehekea siku hii muhimu, tunawafikiria na kuwakumbuka mabaharia zaidi ya milioni 1.2 ulimwenguni kote ambao wanafanya shughuli zote za kiuchumi duniani zifanyike, maisha yetu yawe na furaha, ikiwa ni pamoja na chakula tunachokula, kahawa, chai pamoja na vinywaji vingine tunywavyo, magari tunayoendesha, Mafuta na gesi vitupavyo joto na kuendeshea mitambo yetu, kutupatia mwanga, biashara tufanyazo, simu za mkononi na kompyuta ambavyo haviepukiki katika maisha yetu ya kila siku. 

Wakati teknolojia ikirahisisha maisha na mawasiliano katika jamii, mabaharia wengi kwa muda mwingi huwa mbali na familia zao na wakati mwingine hakuna mtandao (network) na hivyo kutonufaika kwa kiasi kikubwa na  fursa hii muhimu ya kupata mawasiliano na familia zao.

Mabaharia wanahusika na shughuli za uongozaji meli pamoja na kusimamia upakiaji na upakuaji wa mizigo mbalimbali melini. Siku ya mabaharia si tu kutambua thamani ya kazi ya mabaharia bali inalenga kuielimisha jamii juu ya changamoto zinazowakabili mabaharia pamoja na masuala kama vile ya uharamia na majanga mengine wanayokabiliana nayo mabaharia pindi wawapo melini au bandarini duniani kote.

Kwa mara ya kwanza maadhimisho haya ya siku ya mabaharia duniani yalifanyika tarehe 25 Juni 2011 na mwaka huu maadhimisho haya yanafanyika yakiwa yamebeba kauli mbiu inayohimiza usawa wa kijinsia.

Ndani ya mwaka mzima wa 2019, kutakuwa na msisitizo mkubwa wa juu ya umuhimu ushiriki wa wanawake katika masuala ya bahari duniani pamoja na thamani ya mwanamke katika ngazi mbalimbali za sekta ya bahari.

Msisitizo huu juu ya kampeni ya kumuinua mwanamke katika sekta ya bahari umepewa msukumo mkubwa na kauli mbiu ya Siku ya Bahari duniani (World Maritime Day) ya mwaka huu 2019 iliyotolewa na Shirika la Bahari Duniani (IMO) isemayo “empowering women in the Maritime Community” ikiwa na maana ya “kumwezesha mwanamke katika jamii ya sekta ya bahari." IMO imesisitiza kuwa, kauli mbiu hii ina nguvu sana na inasikika na kupokelewa mbali zaidi.

Kauli mbiu hii hutoa mwanya wa kuonesha nafasi kwa wanawake pamoja na kutambua mchango wao ambao wameendelea kutoa kupitia fani mbalimbali za masuala ya bahari.

Katika kuunga mkono jambo hili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikiwawezesha wanawake bila kuchoka katika kada mbalimbali ikiwemo uongozi ndani na nje ya sekta ya bahari.

Kuridhiwa kwa Mkataba wa Kazi wa Kimataifa wa mwaka 2006 (Maritime Labour Convention, 2006) na Serikali ya Tanzania pamoja na kutungwa kwa kanuni mbalimbali na TASAC juu ya usimamizi wa shughuli za masuala ya bahari ni miongoni mwa hatua chanya za kutambua mchango wa sekta ya bahari na mabaharia kwa ujumla nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na kutambua mhanga wanaojitolea mabaharia wakati wakitekeleza majukumu yao ya kila siku wawapo melini.

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) linapenda kuchukua nafasi hii kutoa shukrani za dhati kabisa na kuwapongeza mabaharia wote duniani kwa ujasiri wao katika kuhakikisha uchumi wa taifa hili na wa dunia kwa ujumla unasonga mbele.  

Mwisho kabisa, tunawatakia mabaharia wote afya njema na heri ya Siku ya Mabaharia Duniani kwa mwaka 2019.