Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere chajikita kufundisha lugha ya kichina


Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere chajikita kufundisha lugha ya kichina

Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) ni miongoni mwa taasisi chache hapa nchini ambazo zimekuwa zikitoa mafunzo ya lugha ya Kichina kwa ustadi wa hali ya juu ili kumwezesha Mtanzania kutanua wigo wa kufanya shughuli za kijamii au kiuchumi na watu wanaotumia lugha ya Kichina.

China ni moja kati ya mataifa yenye nguvu za kiuchumi duniani kutokana na kuwekeza katika maeneo mengi kama vile viwanda, ujenzi wa barabara na majengo, biashara, teknolojia, n.k.

Kwa kiasi kikubwa uwekezaji wa China umefanywa katika mataifa mengi na hasa  katika mataifa yanaoendelea ili kuchagiza kasi ya maendeleo ya mataifa hayo.

Uwekezaji huu tumeushuhudia pia hapa kwetu Tanzania, kwani makampuni mbalimbali ya Kichina yamekuwa yakifanya kazi katika sekta tofauti mfano kilimo, ujenzi wa barabara, majengo, madaraja n.k. Pia kuna makampuni mengine mengi yamewekeza katika biashara, mabenki n.k

Sehemu yoyote yenye uwekezaji aghalabu huwa ni neema kwa wananchi wa eneo husika, hali hiyo pia ipo kwa Watanzania kwani wamesogezewa fursa ya ajira karibu kutokana na mwamko wa China kuwekeza hapa nchini.

Fursa hizi za ajira zinazoletwa na uwekezaji wa Wachina, zimefanya baadhi ya taasisi za elimu hapa nchini kuanza kufundisha lugha ya Kichina ili kuongeza wigo wa mawasiliano kati ya wawekezaji wa Kichina na Watanzania kwa sababu mawasiliano ni kitu muhimu katika uwekezaji.

Pia, kama ilivyokuwa kwa watu wengine, Wachina huvutiwa kwa urahisi mtu anapozungumza lugha yao, hivyo upo uhitaji mkubwa wa Watanzania kuijua lugha ya Kichina ili kuweza kuzitumia fursa zinazoletwa na Wachina ipasavyo.

Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) ni miongoni mwa taasisi chache hapa nchini ambazo zimekuwa zikitoa mafunzo ya lugha ya Kichina kwa ustadi wa hali ya juu ili kumwezesha Mtanzania kutanua wigo wa kufanya shughuli za kijamii au kiuchumi na watu wanaotumia lugha ya Kichina.

Uanzishwaji wa mafunzo ya lugha ya Kichina ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na China.

Mkuu wa kitengo cha Lugha na utamaduni wa Kichina katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Dkt. Phillip Daninga anaelezea kwa kina kuhusiana na lugha hiyo na faida zake kwa Watanzania.

Kwa nini mmefikiria kuanzisha mafunzo ya lugha ya Kichina?

Unajua China kwa sasa ni taifa ambalo uchumi wake unakua si tu ndani ya China pekee bali ukuaji wake unakwenda nje ya mipaka yake. Ukuaji huo ndio umesababisha leo hii kuna wafanyabiashara wengi wa Kichina hapa nchini, na pia wafanyabiashara wengi Watanzania kule China.

Hivyo, Chuo chetu kiliiona fursa hiyo na kuamua kuanzisha mafunzo ya lugha ya Kichina ili watu wajifunze lugha hii kwa kuwa lugha ni chombo muhimu katika kuleta maendeleo.

Mwitikio wa wanafunzi chuoni hapo upo vipi?

Mwitikio ni mzuri sana ambapo kila mwaka zaidi ya wanafunzi 100 wanajiandikisha hapa kuja kujifunza lugha ya Kichina. Kozi hii ya lugha ya Kichina inatolewa kwa wafanyakazi na wafanyabiashara mbalimbali baada ya muda wa kazi/shughuli zao (jioni) na wanafunzi wetu wanaosoma hapa ambao wanasoma lugha hii kama somo mojawapo.

Kuna faida gani mtu anapojifunza lugha ya Kichina?

Kama nilivyotangulia kusema hapo awali kuwa uwekezaji wa China hapa nchini unakua kwa kasi na ni fursa kwa Watanzania. Kwa kuwa kuna uwekezaji wa viwanda vingi hapa nchini vinavyomilikiwa na Wachina, kwanza Watanzania wenye kuzungumza Kichina watapata fursa ya ajira kwenye viwanda, ujenzi wa miradi ya barabara, majengo, madaraja, n.k.

Kwa wale wanaozungumza Kichina na wana ujuzi fulani, lugha itakuwa kama kitu cha ziada katika ajira zao lakini wale wanaozungumza Kichina bila ya kuwa na ujuzi wowote wataweza kuwa wakalimani.

Faida nyingine ni kwa wafanyabiashara,  kwa kufahamu lugha ya Kichina inakuwa ni rahisi kuweza kufanya biashara na Wachina wenyewe moja kwa moja, kwakuwa wachina humfurahia zaidi mtu anayeongea lugha yakichina. Lakini ufahamu wa bidhaa zao utakuwa mkubwa na utaweza kutengeneza faida kubwa kutokana na uwezo wako wa kuwasiliana kibiashara.

Kwa upande wa wanafunzi, kuna fursa ya kwenda kusoma nje ya nchi (scholarship) kwa wale watakaofaulu vizuri zaidi katika mitihani ya lugha hiyo. Fursa hii ya kwenda kusoma nje ipo katika programu mbili yaani, masomo ya muda mfupi (short-term) mfano wiki tatu au miezi sita, na yale ya muda mrefu (long-term) kama vile masomo ya umahiri (masters) na uzamivu (PhD).

Je, mna mpango gani wa kuhuisha mtaala wa Lugha ya Kichina ili iweze kufundishwa katika madaraja yote?

Mpaka sasa tumeshaandaa mtaala huo katika ngazi ya Stashahada (Diploma) na Shahada (Degree) ambao tunashughulikia mchakato wa kuidhinishwa na lengo letu ni kufundisha wanafunzi waliopo na wanaokuja kusoma hapa chuoni lugha ya Kichina katika ngazi ya Stashahada na Shahada.

Pia, tunatarajia kuzalisha wataalamu wa lugha ya Kichina wazawa ambao watakuja kufundisha lugha ya Kichina kwa watu wengine wanaohitaji.

Ili mtu aweze kuzungumza vizuri Kichina anatakiwa kusoma hadi ngazi gani?

Kwanza kabisa napenda niseme jambo moja kuwa, kufahamu lugha ya Kichina hutegemea juhudi za mtu binafsi ndiyo maana wapo watu ambao unaweza kuwafundisha leo hii kesho akafanyia mazoezi ya kutosha akawa anazungumza vizuri kama Mchina mwenyewe.

Nikirejea katika swali lako la msingi, kuna hatua kama tano za kujifunza lugha ya Kichina. Hatua ya Kwanza, ni utangulizi ambapo mtu anafundishwa salamu na kujitambulisha.

Hatua ya pili, mambo yanatanuka zaidi na mtu akiweza kujifunza hatua ya tatu na ya nne, anakuwa katika nafasi nzuri ya kuizungumza lugha hiyo bila matatizo. Mwanafunzi anapofikia hatua hii anaweza kupata scholarship (ya muda mfupi au mrefu) kwenda kusoma nchini China. Mwanafunzi akifaulu hatua hii pia anaweza kupata ajira ya moja kwamoja kutoka katika makampuni tofauti tofauti yanayofanya kazi nchini au nje ya nchi.  Kikubwa katika Lugha ya Kichina ni idadi ya maneno ya Kichina ambayo mtu anaweza kuyamudu na kuyatumia mara kwa mara.

Je, kuna utaratibu wa watu wanaosoma lugha hiyo kufahamu tamaduni nyingine za China?

Licha ya lugha yenyewe ya Kichina kufundishwa ikibeba sehemu ya utamaduni wa China, pia wanafunzi wanapofika hapa hufundishwa programu nyingine ya utamaduni wa Kichina inayoitwa TAIJI.

Je, unapoongelea TAIJI unamaanisha nini hasa?

Taiji ni utamaduni wa Kichina unaohusisha mazoezi ya viungo vya mwili unaotumika kama sehemu ya mazoezi ambapo huimarisha afya ya mwili, akili na ukakamavu. Programu hii hushirikisha watu wa rika na jinsia zote.

Pia, kuna nyimbo ambapo wanafunzi hufundishwa kuimba kwa lugha ya Kichina. Nyimbo hizi huwa na maana mbalimbali na wanafunzi huelezwa waziwazi.

Mwisho kabisa kuna zoezi la ukataji na utengenezaji wa maumbo/sanamu mbalimbali ya Kichina yenye maana mbalimbali.

Changamoto gani mnakabiliana nazo katika uendeshaji wa kozi hii?

Kama unavyojua Chuo chetu kimekuwa kikikua kwa kasi sana kwa maana hata idadi ya wanafunzi tulionao ni wengi hivyo kulazimu kuongeza idadi ya madarasa. Inaweza kutokea madarasa kuingiliana, lakini hili linatatulika kwani kwa sasa Chuo kimezindua ukumbi mkubwa wa mihadhara ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto hiyo.

Mikakati gani Chuo inayo juu ya lugha hiyo?

Kwanza kabisa tunaendelea na mchakato wa kuhakikisha kuwa tunahuisha mtaala ili lugha ya Kichina iweze kufundishwa katika ngazi za Stashahada na Shahada.

Pia, tutaendelea kuwatangazia Watanzania wote kuhusiana na kozi hii yenye fursa mbalimbali za ukuaji wa kiuchumi ili waweze kuijua na kuitumia ipasavyo.

Mwisho kabisa nini unaweza kuwaambia Watanzania?

Kwanza naomba niwathibitishie kuwa lugha ya Kichina ni rahisi kujifunza na hata mimi nilipopata fursa ya kwenda kusoma China lugha hii nilikuwa na mtazamo kama huo lakini baadae nikajifunza kwa bidii nikaona hakuna kinachoshindikana.

Sambamba na hilo niwatake Watanzania kuja katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) kujifunza lugha hii kwani ni sehemu sahihi na gharama zake ni za kawaida.