Miaka 60 ya Hifadhi ya Serengeti na Tuzo ya hifadhi bora barani Afrika


Miaka 60 ya Hifadhi ya Serengeti na Tuzo ya hifadhi bora barani Afrika

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ina ukubwa wa Kilometa za mra­ba 14,763, ambapo ni Hifadhi ya Taifa ya pili kwa ukubwa nchini ikitanguliwa na hifadhi ya Taifa ya Ruaha yenye ukubwa wa kilometa za mraba 20,226.

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mwaka huu, imeshinda tuzo ya hifadhi bora barani Afrika huku ikiwa katika maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa mwake.

Hifadhi hii, ilianzishwa mwaka 1959 na tangu wakati huo, hadi sasa imeendelea kuwa miongoni mwa hifadhi zinazovutia watalii wengi duniani.

Neno Serengeti linatokana na neno la kimasai la Sirenget lenye maana ya uwanda mpana wa nyasi fupi, malisho mengi na maji ya kutosha pengine ndiyo maana hifadhi hiyo inapewa majina men­gi kama vile lulu, bustani ya Afrika na Edeni ya Afrika kutokana na utajiri wa maliasili uliopo ndani ya hifadhi hii.

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ina ukubwa wa Kilometa za mra­ba 14,763, ambapo ni Hifadhi ya Taifa ya pili kwa ukubwa nchini ikitanguliwa na hifadhi ya Taifa ya Ruaha yenye ukubwa wa kilometa za mraba 20,226.

Umaarufu wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti unatokana na uwepo wa nyumbu wanaohama kwa makun­di na kuvuka mpaka wa Tanzania hadi hifadhi ya wanyama pori ya Maasai Mara nchini Kenya ambapo takwimu za TANAPA zinaonyesha kuwa kila mwaka zaidi ya nyumbu milioni moja, pundamilia 200,000, swala tomi zaidi ya 300,000 na pofu 12,000 huunga misafara ya kutafuta malisho na maji.

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni moja ya maajabu ya dunia kutoka­na na tendo la uhamaji wa Nyumbu kutoka Kusini hadi Kaskazini na kurudi, tendo ambalo linafanyika mara moja tu kwa mwaka, ambapo tendo hilo linaifanya hifadhi hii kuwa Eden ya Afrika na kupend­wa kutembelewa na watu wengi ulimwenguni kote.

Ukiacha Nyumbu, wanyama wengine maarufu walao nyama katika hifadhi ya Taifa ya Serenge­ti ni Chui na Simba, ambapo utafiti umebaini kuwa ukubwa wa hifa­dhi hii umesaidia kudumisha uhai wa wanyama waliokuwa katika hatari ya kutoweka duniani, kama Mbwamwitu, Faru na wengine.

Hifadhi ya Serengeti pia ni moja ya maeneo yaliyoshinda tuzo ya moja ya maeneo saba ya maajabu asili ya barani Afrika, ikiwa pia inatambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kama moja ya maeneo ya urithi wa dunia.

Tuzo ya Serengeti kupelekwa kwa Rais Magufuli

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangallah tayari ameka­bidhiwa na TANAPA tuzo ya Seren­geti kuwa hifadhi bora barani Afri­ka ili amkabidhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakuru­genzi wa Shirika la Hifadhi za Tai­fa Tanzania (TANAPA), Mkuu wa Majeshi Mstaafu Generali George Waitara alimkabidhi tuzo hiyo, Waziri Dk. Kigwangalla katika haf­la ambayo imefanyika viwanja vya TGT hivi karibuni.

Akikabidhi Tuzo hiyo, Generali mstaafu Waitara anasema ushindi wa Serengeti kuwa hifadhi bora ni ushindi wa Watanzania wote.

Anasema TANAPA inamkabidhi tuzo hiyo Waziri Kigwangallah ili aipeleke kwa viongozi wa juu wa Serikali.

Waitara aliongeza kuwa Bodi na Menejimenti ya TANAPA wataendelea kusimamia hifadhi kwa weledi zaidi, nidhamu, uza­lendo na kujituma katika kiwango cha hali ya juu.

Hifadhi Tano zilizoshindanishwa na Serengeti na kushindwa

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Profesa Adolf Mkenda anasema tuzo hiyo imepatikana baada ya Serengeti kushindanishwa na hifadhi kubwa tano barani Afrika baada ya watalii kupiga kura.

Anasema tuzo hiyo imetolewa na taasisi ya World Travel Award (WTA) Juni mosi nchini Mauritius baada ya kuona Serengeti ina sifa za kipekee duniani.

Profesa Mkenda alizitaja sifa hizo kuwa ni kuwa na idadi kubwa ya wanyama wahamao, kuwa na wan­yama wengi walao nyama na kuwa na Ukanda mrefu wenye wanyama wengi.

Profesa Mkenda anasema hifadhi tano ambazo zili­pambanishwa na Serengeti ni hifadhi ya Masai Mara ya nchini Kenya, hifadhi ya Kru­ger ya Afrika Kusini, Hifadhi ya Kalahari ya Botswana, hifadhi ya Kidepo ya Uganda na Etosha ya Namibia.

Anasema kuwa tuzo hiyo imeiletea Tanzania sifa ulimwenguni kote na inato­kana na jitihada kubwa za uhifadhi ambazo zinafany­wa na Serikali kwa kushiriki­ana na wananchi.

Tuzo ilivyopokelwa Mkoa wa Mara na Simiyu

Kabla ya tuzo hiyo kuka­bidhiwa kwa Rais John Magufuli, wakazi wa mikoa ya Simiyu na Mara ambapo hifadhi hiyo ipo wamepata fursa ya kuipokea tuzo hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka wanasema tuzo hiyo ni matokeo ya ushirikiano mzuri baina ya wahifadhi na wananchi wa Mara na Simiyu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Kigoma Malima anasema, Mkoa wa Mara umeanza kujiandaa kuipokea tuzo hiyo, hasa kutokana na umuhimu wake kwa wananchi ili kuendeleza uhifadhi.

Malima anasema tuzo hiyo siyo tu ni faraja kwa wakazi wa Mkoa wa Mara bali ni faraja kwa Watanza­nia wote.

“Mkoa wa Mara tut­aendelea kupambana ili kui­marisha ulinzi na uhifadhi wa Serengeti kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo,” anasema Malima.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antho­ny Mtaka anasema tuzo hiyo itaendelea kuhamasi­sha uhifadhi wa Serengeti kwani wananchi wameona umuhimu wa uhifadhi.

Tuzo kupelekwa kwenye maonyesho ya utalii

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Kigwangalla ame­agiza kutengenezwa bango maalum ambalo litaonyesha tuzo hiyo bora ya uhifadhi ya Serengeti barani Afrika ambalo litakuwa linapele­kwa kwenye maonyesho.

Tunataka katika maone­sho yote ya utalii bango hili lifikishwe ili watu waone kuwa Serengeti ndio hifadhi bora barani Afrika” ame­sema.

Amesema tuzo hiyo pia inapaswa kuwekwa kwenye banda la Tanzania ili watu wajuwe hakuna sababu ya kwenda kwingine.

“Pia tengenezeni bango la Mlima Kilimanjaro na kuon­esha imeshinda Mara tano kama hifadhi bora ili kila mtu aone kuwa mlima upo Tanzania sio nchi nyingine bila kuzungumza,” amese­ma.

TANAPA kuendelea kulinda hifadhi kwa maslahi ya Taifa

Kamishna Mkuu wa uhifa­dhi wa TANAPA, Allan Kijazi anasema wakati Serengeti ikitimiza miaka 60 na kush­inda tuzo ya hifadhi bora barani Afrika, wao kama TANAPA wataendelea kulin­da hifadhi na kuvutia watalii zaidi.

Anasema malengo ya TANAPA ambayo hivi kari­buni imezindua mkakati wa kufanyakazi kwa viwango vya kimataifa na mkakati ya kuboresha huduma kwawa­teja i kuhakikisha Serengeti inashinda kuwa hifadhi bora duniani.

“Tunataka hifadhi zetu zote 19 ziwe ni bora bara­ni Afrika na hili linaweze­kana kwani tumejipanga vizuri kupitia mfumo wetu wa jeshi usu ambao uta­ongeza utendaji kazi kwa weledi,uzalendo na kutii maagizo ya juu,” anasema

Hii ndio serengeti mwaka huu imetimiza miaka 60 huku ikipata heshma kubwa ya kushinda tuzo ya hifadhi bora barani Afrika na sasa kila mtanzania anafursa ya kwenda Serengeti kujionea maajabu ya dunia.

Kamishna wa Uhifadhi

Hifadhi za Taifa Tanzania

S. L. P 3134

ARUSHA.

Barua pepe: [email protected]­aparks.go.tz

Simu: +255 (27) 297 0404-07