Mikakati ya NIT katika kuleta mapinduzi ya sekta ya uchukuzi nchini


Mikakati ya NIT katika kuleta mapinduzi ya sekta ya uchukuzi nchini

Katika dhamira hiyo ya kuifanya nchi kuwa ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, kunahitaji maandalizi stahiki ya mazingira yatakayohakikisha dhamira hiyo inafanikiwa kwa wakati

Tanzania inalenga kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na moja ya njia ya kufikia lengo hilo ni kuwa na uchumi unaotegemea viwanda kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli  inavyolipa kipaumbele suala la uanzishwaji wa viwanda vingi nchini.

Msisitizo wa serikali hii katika kuanzisha viwanda mbalimbali ni kukuza uchumi kwa namna tofauti, kama vile kuwatengenezea wananchi ajira zitakazowawezesha kuwa na kipato cha kukidhi mahitaji yao na familia zao.

Pia, kutokana na ajira za wananchi hao, Serikali itakuwa na wigo mpana wa kukusanya kodi ikiwa ni pamoja na kodi za mali zao zisizohamishika, kama ardhi na majengo.

Hata hivyo, katika dhamira hiyo ya kuifanya nchi kuwa ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, kunahitaji maandalizi stahiki ya mazingira yatakayohakikisha dhamira hiyo inafanikiwa kwa wakati.

Mazingira mojawapo ya kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati ni kuwa na sekta imara ya uchukuzi.

Sekta imara ya uchukuzi itatengeneza mazingira rahisi katika muktadha wa usafirishaji wa malighafi kutoka shambani kwenda viwandani na kutoka viwandani kwenda sokoni.

Hivyo, kutokana na umuhimu huo ni lazima kuweka mikakati ya kuhakikisha sekta hiyo inakuwa imara na endelevu ili kukidhi mahitaji haya ya mapinduzi ya kiuchumi.

Katika kuhakikisha suala la uchukuzi nchini linafanikiwa, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) chini ya uongozi imara wa Mkuu wa Chuo hicho, kimejipanga kuhakikisha kinaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya uchukuzi kwa kufundisha wataalam wa kada mbalimbali za sekta hiyo.

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Mhandisi Profesa Zacharia Mganilwa anaeleza mikakati mbalimbali ya chuo hicho ikiwemo miradi wanayoitekeleza yenye lengo la kuboresha sekta ya uchukuzi nchini katika mahojiano maalum na gazeti hili yaliyofanyika ofisini kwake hivi karibuni.

Tunaomba utueleze mikakati ya NIT katika kuboresha sekta ya uchukuzi nchini

Chuo kama kitovu cha sekta ya uchukuzi nchini kina mikakati mingi ya kuhakikisha kwamba sekta hii inakuwa imara na endelevu ili kusaidia juhudi za kufikia mapinduzi ya kiuchumi hapa nchini. Miongoni mwa mikakati hiyo ni kuifanya NIT kuwa kituo cha Umahiri wa Mafunzo ya Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji (Centre of Excellence in Aviation and Transport Operations).

Unamaanisha nini unaposema NIT kuwa kituo cha umahiri?

Nikisema NIT kuwa kituo cha umahiri wa mafunzo namaanisha chuo kuwa na uwezo wa kutoa mafunzo ya kada mbalimbali za usafiri kwa kutumia teknolojia za kisasa na zenye viwango vya kimataifa.

Kwa namna gani NIT mnalitekeleza jambo hili?

Katika jitihada za kusaidia mapinduzi ya kiuchumi hapa nchini, Benki ya Dunia waliona kuna upungufu wa watu wenye maarifa na ujuzi hususan katika sekta ya uchukuzi pamoja na changamoto mbalimbali katika nyanja ya elimu ya ufundi (Technical Education) hivyo wakatoa fedha kwa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ili kutatua changamoto hizo.

Fedha hizo zilitolewa kwa kuzingatia maeneo makuu matano ambayo ni: TEHAMA (ICT), Uzalishaji (Manufacturing), uchakataji wa bidhaa za kilimo (Agro-processing), Nishati (Energy) na Usafiri (Transport).

Baada ya hapo Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ikachagua vyuo 8 kwa ajili ya kuandika pendekezo (Proposal) la eneo ambalo chuo kinaweza kumudu kuzalisha wataalam wabobezi.

NIT tuliandika katika eneo la usafiri na tukafanikiwa kushinda katika eneo hilo, hivyo tukafanikiwa kupata fedha kiasi cha Dola za Kimarekani 21.5 milioni. Fedha hizi ndizo tumezielekeza kwenye utekelezaji wa mradi huu wa kuanzisha kituo cha umahiri wa mafunzo ya usafiri wa anga na operesheni za usafirishaji (Center of Excellence in Aviation and Transport Operations).

Mradi huu utahusisha ujenzi wa Miundombinu, Ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuwajengea uwezo wanataaluma.

Hivyo kutakua na ununuzi wa ndege tatu kwa ajili ya mafunzo ya urubani, vifaa vya kufundishia Wahandisi wa matengenezo ya ndege na vifaa vya Mock-up kwaajili ya mafunzo ya wahudumu ndani ya Ndege (Cabin crew)  

Kwa upande wa uboreshaji wa miundombinu ya Chuo kutakua na ujenzi wa utawala kwa ajili ya kituo hiki, mabweni ya wasichana na wavulana, maabara na karakana za kisasa zenye teknolojia ya hali ya juu na majengo kwa ajili ya kuhifadhia vifaa vya kufundishia. Miundombinu hii itajengwa hapa makao makuu ya chuo.

Pia, tutajenga karakana (Hangar) kwa ajili ya ndege zetu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Vilevile tumepewa eneo la hekta 60 kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ambapo nako tutajenga karakana ya ndege, madarasa, mabweni ya wanafunzi wa kike na kiume na nyumba za wafanyakazi, hii ni katika upande wa usafiri wa anga (Aviation).

Upande wa shughuli za usafiri (Transport Operations) tutaanzisha program mbalimbali za usafiri wa majini, barabara na reli.

Miongoni mwa kozi mpya tutakazoanzisha ni pamoja na Stashahada ya Usimamizi wa Kampuni ya Meli na Bandari (Diploma in Shipping and Port Management), Stashahada ya Usimamizi wa Usafiri wa Reli na Barabara (Diploma in Logistics and Rail-Road Transport Management), Shahada ya Kwanza ya Usimamizi wa Meli na Bandari (Bachelor Degree in Shipping and Port Management) na Shahada ya Kwanza ya Usafiri wa Reli na Barabara (Bachelor Degree in Rail-Road Logistics).

Mwanafunzi anayesoma kozi ya Rail-Road atabobea kwenye usafiri wa reli na barabara ambao kwa sasa unasimamiwa na Taasisi ya Usafiri wa Ardhini yaani Land Transport (LATRA).

Kwa upande wa kozi ya Shipping and Port mwanafunzi atabobea kwenye Usafiri wa majini na atakuwa na uwezo wa kufanya kazi kwenye makampuni ya Meli yanayosimamiwa na Shirika la Usimamizi wa Meli (TASAC). Huku wale wa Uhandisi matengenezo ya ndege wakibobea kwenye sekta ya anga chini ya usimamizi wa Tanzania Civil Aviation Authority TCAA.

Mradi huu tumeanza kuutekeleza mwaka huu na ukikamilika utakuwa na manufaa makubwa kwa taifa kwani tunategemea kuzalisha wataalam zaidi ya 4000 wa sekta za usafirishaji wakiwemo marubani, wahudumu wa ndani ya ndege, wataalam wabobezi wa usimamizi wa Usafiri wa Barabara, Reli, Kampuni za Meli, Bandari n.k

Tueleze kuhusu mpango wa kuibadili NIT kuwa Chuo Kikuu

Wazo la kukipandisha hadhi Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kuwa Chuo Kikuu cha Usafirishaji (NUT) lilianza mwaka 2015 katika kikao cha ushirikiano kati ya China na Afrika kilichofanyika nchini Afrika ya Kusini (Forum on China–Africa Cooperation, FOCAC) ambapo Rais wa China, Xi Jinping aliwambia wakuu wa nchi za Afrika waliohudhuria kikao kile kuwa hamuwezi kulifanya bara la Afrika kuwa la uchumi wa viwanda bila kuwa na vyuo vikuu vya usafirishaji.

Hivyo Rais huyo akatoa ahadi ya Serikali ya China kujenga vyuo vikuu 5 vya usafirishaji barani Afrika. Baada ya hapo Rais Xi Jinping akatoa nafasi kwa nchi za Afrika kuandika mapendekezo kupitia mabalozi wa China kwenye nchi hizo ili wapate ufadhili huo wa kujengewa Chuo Kikuu cha Usafirishaji.

Tanzania ikiwa ni moja ya nchi iliyohudhuria mkutano ule tukiwakilishwa na Makamu wa Rais, Serikali ilikichagua Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kuandika pendekezo hilo.

Baada ya kuandika, mapendekezo hayo yalishindanishwa na sisi tukashinda hivyo tunasubiri kupokea fedha kiasi cha Dola za kimarekani milioni 62 ambazo zitaweza kukipandisha hadhi Chuo kuwa Chuo Kikuu cha Usafirishaji.

Baada ya kushinda walikuja wataalam kutoka Chuo Kikuu cha usafirishaji cha Southwest Jiaotong University cha China kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu ili kuandaa ripoti itakayosaidia utolewaji wa fedha hizo.

Kwenye mradi huu tunatarajia kuanzisha Ndaki tatu (3) na shule mbili (2): Ndaki ya Sayansi na Teknolojia ya usafiri wa Anga (College of Aerospace Science and Technology) kwa ajili ya kufundisha wataalam wa masuala ya anga ambayo   Miundombinu yake itajengwa kwenye eneo letu la Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA).

zingine ni Ndaki ya Usafirishaji na Teknolojia ya Uhandisi (Transportation Engineering and Technology sciences) na Ndaki ya Menejimenti ya Usafirishaji na Uchumi (Transportation Management and Economics) Shule zitakazoanzishwa ni Shule ya mafunzo ya ufundi katika Usafirishaji (Institute of Technical Training in Transport) na Shule ya Taaluma za Usafiri wa Majini na Menejimenti ya Bandari (Merchant Marine College) itakayojengwa katika eneo la Chuo lililopo mkoani Lindi eneo la Kikwetu.

Unatoa wito gani kwa Watanzania na wadau wa sekta ya usafiri?

Wazazi na vijana wa Kitanzania wanatakiwa kuchangamkia fursa hii ya mafunzo kwa sababu sekta ya uchukuzi inakuwa kwa kasi na ina uhitaji mkubwa wa rasilimali watu hivyo kusoma kozi hizi watajitengenezea mazingira mazuri ya kupata ajira na kujiajiri.

Kingine, wadau wa sekta ya usafiri wajitokeze kusaidia juhudi za kuboresha sekta hii kwa kutoa misaada mbalimbali ikiwemo vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ufadhili wa wanafunzi, kutoa nafasi kwa mafunzo ya vitendo n.k.