Chuo Kikuu Mzumbe chaboresha miundombinu ili kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia


Chuo Kikuu Mzumbe chaboresha miundombinu ili kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia

Chuo Kikuu Mzumbe kimeboresha miundombinu ya mabweni, kumbi za mihadhara, madarasa, ofisi na nyumba za wafanyakazi kwa ajili ya kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Chuo Kikuu Mzumbe kimeboresha miundombinu ya mabweni, kumbi za mihadhara, madarasa, ofisi na nyumba za wafanyakazi kwa ajili ya kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Pia, Chuo kimetekeleza miradi mitatu mikubwa ya ujenzi pamoja na miradi mbalimbali ya ukarabati iliyofanyika katika Kampasi zote tatu za Chuo Kikuu Mzumbe.

Akizungumza katika mahojiano na gazeti la hili hivi karibuni, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chuo Kikuu Mzumbe, Rainfrida Ngatunga alisema kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kimeboresha miundombinu hii kwa ufadhili mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Tano na kwa kutumia mapato ya ndani.

Ngatunga alisema kwa Kampasi Kuu, Chuo kinajenga majengo manne ya mabweni yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1024 kwa ufadhili wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Alisema Serikali imetoa fedha shilingi bilioni 6.5 na mradi huu unajengwa na mkandarasi “National Service Construction Department” (SUMA JKT). Alisema mradi huu unatarajiwa kukamilika tarehe 19 Oktoba 2019 na unategemewa kupunguza tatizo la uhaba wa mabweni kwa wanafunzi wa Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu Mzumbe.

Pia, alisema Chuo kimeanza mradi wa ujenzi wa kumbi za mihadhara na madarasa kuanzia tarehe 21 Juni 2019 na utatekelezwa kwa muda wa miezi 13 na SUMA JKT kwa gharama ya shilingi bilioni 3.12. Katika mradi huu, madarasa manne ambayo kila moja litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 100, kumbi mbili za mihadhara ambazo kila moja itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 300 na ofisi zitakazoweza kutumiwa na wafanyakazi 50 kwa wakati mmoja.

Aidha, Chuo kimekarabati mabweni ya wanafunzi  na nyumba za wafanyakazi katika bajeti yake kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 hadi 2018/2019 kwa kutumia mfumo wa force account unaosimamiwa na wataalamu kutoka Kurugenzi ya Majengo na Miliki. Mpaka sasa mabweni sita na nyumba za wafanyakazi 22 zimekamilika wakati nyumba nne za wafanyakazi zinaendelea kukarabatiwa.  

Kwa upande wa Kampasi ya Mbeya, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (MOEST) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) zimefadhili ujenzi wa jengo la ghorofa tatu la utawala na taaluma. Jengo hilo litakapokamilika litakuwa na ofisi za utawala 14 zenye uwezo wa kuchua wafanyakazi 32, madarasa  matatu yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 100 kila mmoja na kumbi za mihadhara mbili zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 300 kila mmoja. Mradi huu umeshafikia hatua za mwisho kukamilika na jengo hili linatarajiwa kuanza kutumika katika mwaka wa masomo 2019/2020. Mradi huu unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 3 na utakiwezesha Chuo kupanua miundombinu yake katika Kampasi ya Mbeya.

Kwa upande wa Kampasi ya Dar es Salaam, Ngatunga alisema Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea na ukarabati wa iliyokuwa Shule ya Sekondari ya Tegeta kwa ajili ya upanuzi wa Kampasi ya Dar es Salaam. Mpaka sasa ukarabati unaendelea na unafanywa kwa kutumia mfumo wa force account unaotekelezwa na wataalamu wa Kurugenzi ya Majengo na Miliki ya Chuo Kikuu Mzumbe.

Aidha Chuo kimekarabati jengo moja kati ya majengo matatu yaliyonunuliwa kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa ajili ya kuongeza ofisi kwa wafanyakazi wa Kampasi ya Dar es Salaam.

Ngatunga alisema kuwa uimarishaji wa miundombinu hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Nne wa Chuo Kikuu Mzumbe wa mwaka 2017/2018-2021/2022 ambapo moja ya malengo yake makuu ni kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Mkurugenzi huyo alisema uimarishaji wa mabweni na madarasa katika kipindi hiki ni mkubwa kuliko iliyowahi kufanywa na Serikali ya Tanzania katika kipindi chote Chuo hicho kiwepo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1953 ikiwa ni Shule kwa ajili ya watoto wa Machifu na Waafrika waliotumika katika Serikali ya Mkoloni.