VETA yalenga kudahili wanafunzi 700,000 kwenye vyuo vya ufundi stadi nchini


VETA yalenga kudahili wanafunzi 700,000 kwenye vyuo vya ufundi stadi nchini

Katika mwaka huu wa fedha (2019/2020), Serikali imejipanga kujenga vyuo vya VETA katika Wilaya 29, ambazo ni Nyasa, Chunya, Ukerewe, Kongwa, Korogwe, Ruangwa, Bahi, Igunga, Kasulu (Halmashauri ya Mji), Pangani, Mafia, Longido, Mkinga, Chemba, Uvinza, Lushoto, Mbarali, Monduli, Buhigwe, Ulanga, Masasi, Rufiji, Iringa, Ikungi, Kilindi, Kwimba, Kishapu, Uyui, na Butiama.   

Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania, chini ya uongozi thabiti wa Rais Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, inafanya jitihada kubwa na kuweka mikakati ya kujenga uchumi wa nchi kwa lengo la kufikia uchumi wa kati, unaoendeshwa na viwanda, ifikapo mwaka 2025.

Miongoni mwa mikakati muhimu ni kuhakikisha uwezo wa nguvukazi ya kutosha na yenye ujuzi wa kutosha kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kufikia lengo hilo la kitaifa. Nguvukazi yenye ujuzi huchangia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza tija na ufanisi katika maeneo ya uzalishaji, ikiwemo viwanda, kilimo na sekta nyinginezo.

Vilevile, huwawezesha wananchi kujiajiri kwa kuanzisha viwanda vidogovidogo na vya kati, wakiwa katika vikundi au mmoja mmoja. Hapo ndipo jukumu la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) la kuzalisha nguvukazi yenye ujuzi wa ufundi stadi linapojidhihirisha.

VETA inatambua kuwa katika kipindi hiki kunahitajika mikakati thabiti ya kupanua wigo na kuimarisha ubora wa mafunzo ili kwenda sambamba na mahitaji ya kuanzisha na kuendeleza viwanda ili kuifikisha Tanzania katika uchumi wa kati.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu anabainisha mikakati mbalimbali ambayo VETA inaendelea kuiweka na kuitekeleza ili kuendelea kuongeza uzalishaji wa nguvukazi yenye ujuzi katika ufundi stadi.

“Matamanio yetu ni kuona kila Mtanzania anayehitaji kupata ujuzi anapata fursa ya mafunzo ya ufundi stadi, yenye ubora unaokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa. Hilo linajibainisha katika Dira yetu ya sasa ambayo ni Tanzaniayenye Mafundi Stadi Mahiri na wa Kutosha,” anasema Dkt. Bujulu.

Anaongeza kuwa, “Shabaha yetu ni kuongeza udahili kwa vyuo vyote vya elimu na mafunzo ya ufundi stadi kutoka kiwango cha sasa cha wanafunzi 223,000 kwa mwaka hadi 700,000 kwa mwaka ifikapo 2021.”

Dkt. Bujulu anatanabaisha kuwa moja ya mikakati ya kuhakikisha VETA inafikisha fursa kwa Watanzania wengi zaidi ni kuendelea kujenga, kukarabati na kuimarisha vyuo vya Ufundi Stadi na miundombinu mbalimbali, zikiwemo karakana za mafunzo na maabara. Matarajio ni kuongeza vyuo vinavyomilikiwa na VETA kutoka 31 vya sasa na kufikia 42 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2019 na 45 ifikapo mwezi Juni 2020. Vilevile, VETA inaendelea kujenga karakana mpya, kuboresha zilizopo na kununua vifaa, mitambo pamoja na zana mbalimbali za kufundishia kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Dkt. Bujulu anabainisha zaidi kuwa hadi sasa kuna miradi ya ujenzi wa vyuo vitano (5) vya VETA vya ngazi ya Mkoa, iliyo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Mikoa hiyo ni Rukwa, Geita, Simiyu, Njombe na Kagera. Pia, kuna miradi mingine 11 ya vyuo vya Wilaya, ambayo ni Itilima, Ileje, Nkasi, Chato, Muleba, Simanjiro, Babati, Ngorongoro, Kilindi (World Vision), Newala na Kasulu.

Anataja baadhi ya mafanikio ya hivi karibuni katika juhudi za ujenzi wa vyuo vya VETA kuwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma ambacho kilizinduliwa rasmi tarehe 5 Aprili, 2019 na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli; na Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Urambo, mkoani Tabora, ambacho ilizinduliwa tarehe 9 Julai, 2019 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Joyce Lazaro Ndalichako.

Katika mwaka huu wa fedha (2019/2020), Serikali imejipanga kujenga vyuo vya VETA katika Wilaya 29, ambazo ni Nyasa, Chunya, Ukerewe, Kongwa, Korogwe, Ruangwa, Bahi, Igunga, Kasulu (Halmashauri ya Mji), Pangani, Mafia, Longido, Mkinga, Chemba, Uvinza, Lushoto, Mbarali, Monduli, Buhigwe, Ulanga, Masasi, Rufiji, Iringa, Ikungi, Kilindi, Kwimba, Kishapu, Uyui, na Butiama.   

Dkt. Bujulu anaongeza kuwa pamoja na ujenzi wa vyuo vipya, suala la uboreshaji wa karakana nalo linapewa kipaumbele kikubwa ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanajifunza kwa vitendo kwa kutumia vifaa bora na vya kisasa. Anasema kuwa VETA inajenga karakana na kununua vifaa mbalimbali vya mafunzo ili viweze kutumiwa na walimu na wanafunzi katika masomo ya vitendo.

Anazitaja juhudi za uboreshaji na uimarishaji wa karakana kuwa ni pamoja na ujenzi wa Karakana ya kisasa ya Useremala katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi Dodoma (VETA Dodoma); Ujenzi wa karakana za Useremala na umeme wa Magari VETA Kihonda; na ujenzi wa Karakana ya Umeme wa Viwandani katika Chuo cha VETA Mwanza. Ujenzi wa karakana unaendelea pia katika Vyuo vya VETA vya Manyara RVTSC, Arusha VTC (Oljoro), Pwani RVTSC na Lindi RVTSC.

Ili kukabiliana na mahitaji na gharama kubwa za mafunzo, Mamlaka inabuni mbinu na mifumo mingine ya kupanua fursa za mafunzo ya ufundi stadi ili iende sambamba na ujenzi wa vyuo. Miongoni mwa mbinu hizo ni pamoja na utoaji wa mafunzo kwa wajasiriamali (INTEP); Mafunzo ya Uanagenzi (yanayohusisha sehemu ya kazi); Mafunzo kwa Njia ya Simu (VSOMO) na Urasimishaji Ujuzi uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi (RPL).

Akizungumzia mafunzo ya INTEP, Dkt. Bujulu anaeleza kuwa VETA inatekeleza mpango huo wa kuboresha ujuzi katika sekta isiyo rasmi ujulikanao kama Mpango Jumuishi wa Mafunzo ya Kukuza Ujasiriamali (Integrated Training for Entrepreneurship Promotion).

Kupitia mpango huu mafunzo ya muda mfupi hutolewa kwa wajasiriamali katika jamii wanamofanyia shughuli zao na unalenga kupanua fursa za kujiajiri na kuongeza tija na ubora wa bidhaa au huduma zinazotolewa na walengwa kwenye sekta zisizo rasmi.

Kuhusu mafunzo ya uanagenzi, Dkt. Bujulu alisema kuwa ni mafunzo yanayohusisha chuo na mahala pa kazi. VETA inatekeleza mafunzo hayo kwa uratibu wa vyuo vya VETA Moshi na VETA Dar es Salaam. Katika Chuo cha VETA Moshi, mafunzo hayo yanaendeshwa kwa ushirikiano na Chemba ya Madini na Nishati Tanzania (TCME) na kampuni mbalimbali za uchimbaji wa madini.

Kwa upande wa Chuo cha VETA Dar es Salaam mafunzo haya yanahusisha ushirikiano kati ya Chuo hicho na kampuni mbalimbali katika maeneo ya ufundi umeme na magari, na huduma za hoteli.

Mpango mwingine anaoufafanua Dkt. Bujulu ni wa RPL, ambao ni Urasimishaji Ujuzi Uliopatikana Nje ya Mfumo Rasmi wa Mafunzo (Recognition of Prior Learning). Mpango huu unawalenga mafundi wenye ujuzi ambao wameupata sehemu za kazi, pasipo kupitia mafunzo yoyote yaliyo rasmi