Watanzania tulipe kodi ili kuisadia Serikali katika jitihada za kuleta maendeleo


Watanzania tulipe kodi ili kuisadia Serikali katika jitihada za kuleta maendeleo

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwa kutambua umuhimu wa kodi, imekuwa ikihimiza ukusanyaji wa mapato pamoja na kupambana na rushwa na ufisadi ili kupunguza ukali wa maisha kwa Watanzania.

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli kwa kutambua umuhimu wa kodi, imekuwa ikihimiza ukusanyaji wa mapato pamoja na kupambana na rushwa na ufisadi ili kupunguza ukali wa maisha kwa Watanzania.

Rais Magufuli amekuwa akisisitiza ulipaji wa kodi kwa kila mtu hasa wafanyabiashara akiamini kwamba, ndiyo njia pekee inayoweza kuiingizia Serikali mapato kwa urahisi ambayo yatatumika kwa ajili ya maendeleo.

Katika hilo, Rais Magufuli pia alikuwa akiwahimiza Watanzania wanaponunua bidhaa yoyote ile na kwa gharama yoyote, wadai risiti kama uthibitisho wa bidhaa waliyonunua ili kuweza kuwabana wafanyabiashara wote wanaokwepa kulipa kodi.

Serikali imekuwa ikitumia muda mwingi kuhamasisha Watanzania kuunga mkono jitihada za kukusanya kodi pale wanaponunua bidhaa ili kuiongezea Serikali mapato. Lakini pamoja na juhudi hizo za Rais na Serikali yake, bado kuna changamoto kubwa kufikia mafanikio kutokana na baadhi ya wananchi kushindwa kutimiza jukumu lao la kulipa kodi.

Hii inatokana na ukweli kwamba, baadhi ya Watanzania hawaelewi maana na umuhimu wa kulipa kodi au kwa makusudi wanakwepa kulipa kodi. 

Kuna msemo usemao “Mjenga nchi ni mwananchi”. Hakuna nchi inayoweza kupiga hatua ya maendeleo bila kutegemea wananchi wake. Mwananchi ndiyo msingi wa kila kitu.

Maendeleo ya uchumi kwa nchi yoyote yanategemea mapato yanayotokana na kodi, ushuru na tozo mbalimbali ambazo wananchi hulipa. Kupitia makusanyo ya kodi, huiwezesha Serikali na taasisi zake kutekeleza vyema jukumu la kuwapelekea maendeleo.

Utekelezaji wa ahadi zote za Serikali kwa asilimia kubwa hutegemea ukusanyaji sahihi wa mapato kutoka kwenye kodi.

Ili Serikali iweze kujitegemea na kujiamulia mambo yake kikamilifu, lazima iwe na uwezo wa kujiendesha hasa kwa kutegemea mapato ya ndani yanayotokana na kodi kuliko misaada na mikopo hasa kutoka nje.

Makusanyo ya ndani hutegemea wananchi wazalendo ambao hutimiza wajibu wao kwa kulipa kodi ili Serikali ipate fedha za kujiendesha na kutekeleza miradi ya maendeleo.

Hakuna mwananchi asiyehitaji miundombinu mizuri ikiwamo barabara, vivuko, madaraja, usafiri bora na gharama nafuu wa nchi kavu, angani na majini. Pia, hakuna mwananchi asiyehitaji huduma bora za afya, elimu, maji safi na salama, nishati na kilimo cha umwagiliaji.

Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikitekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ununuzi wa ndege, ujenzi wa reli ya kisasa, utekelezaji wa miradi ya barabara, ujenzi wa vivuko na madaraja, utoaji wa elimu bure, uzalishaji wa nishati ya umeme, ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali n.k.

Utekelezaji wa hayo na mengine yanategema makusanyo ya Serikali ambayo huchangiwa na kila mwananchi kupitia kulipa kodi na tozo nyinginezo. Kila unapolipa kodi unakuwa umetekeleza wajibu wako wa kujenga uchumi wa taifa lako.

Hii inaonyesha jinsi gani kodi ilivyo muhimu kwa taifa. Hivyo kwa kuangalia hayo ni lazima kila mwananchi kwa nafasi yake alipe kodi kwa hiari ili kusaidia juhudi za Serikali za kutuletea maendeleo.

Kodi hizi kwa kawaida hulipwa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambacho ni chombo maalum kilichopewa dhamana ya kikatiba kukusanya kodi hapa nchini.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hukusanya kodi kwa niaba ya Serikali. Mifumo ya ukusanyaji kodi kupitia mamlaka hiyo kwa sasa imeimarishwa ili kila mhusika aweze kulipa kodi kadri ya uzalishaji wake huku ikibana mianya yote ya ukwepaji.

Serikali hupanga bajeti kwa kutegemea mapato yanayokusanywa kutoka vyanzo mbalimbali. Kuweka malengo tusiyoweza kuyafikia au kuzembea kukusanya, husababisha baadhi ya miradi ya maendeleo kushindwa kutekelezwa kwa wakati uliobainishwa.

Ni vyema kila raia akawa na moyo wa kizalendo wa kulipa kodi ili Serikali iweze kutekeleza mipango yake kadri ilivyojipangia. Wapo baadhi ya watu wanaokwepa kodi kwa makusudi. Hii ni tabia inayopaswa kukemewa, badala yake wajisikie fahari kulipa.

Wapo wanaokwepa hata kwa kutoa rushwa. Kwa bahati mbaya baadhi ya watu wanashindwa kuelewa kuwa rushwa inaharibu uchumi wa nchi, kwani fedha wanayotoa haiendi kwenye mfuko wa Serikali itumike kutoa huduma bora kwa wananchi.

Badala yake, inakwenda kwenye mifuko ya watu binafsi ambao hawawezi kuzitumia kujenga barabara, shule, vituo vya afya au kuchimba visima vya maji kwa ajili ya kijiji au mtaa.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza kuwa ni kosa la jinai kukwepa kulipa kodi yoyote ya Serikali na kosa hilo linaambatana na kifungo ama faini, au vyote kwa pamoja.

Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kufikia uchumi wa kati inawezekana iwapo kila Mtanzania atalipa kodi. Kila mmoja ajivunie kulipa kodi na si kukwepa au kulipa kodi pungufu.

Wananchi waanze kutekeleza wajibu wao na kutoa muda kwa Serikali kuzitumia kwa manufaa ya umma, ili viongozi watakaobainika wanajinufaisha nazo wawajibishwe kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Juhudi za TRA katika kukusanya kodi

Baadhi ya watu wamekuwa wakibuni njia mbalimbali za kukwepa kodi hali ambayo inasababisha Serikali kukosa mapato yake kwa mujibu wa sheria.

Hali hiyo inatokana na watu kukosa uzalendo kwa nchi yao au yawezekana inatokana na kutokujua umuhimu wa kulipa kodi.

Kutokana na hilo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikitoa elimu ya kodi mara kwa mara kwa wadau mbalimbali ili kuhakikisha kila mlipa kodi anafahamu maana ya kodi na umuhimu wa kulipa kodi.

Pia, Mamlaka hiyo imejipanga kuhakikisha kila mmoja anaelewa umuhimu wa kodi ili waweze kulipa kwa hiyari bila shuruti kama ambavyo sheria inawataka kufanya. Kila mtu mwenye kipato anatakiwa kulipa kodi ambayo ndiyo itakayoiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake kwa wananchi wake.

Pia, mikakati mbalimbali imewekwa ili kuhakikisha kodi zinakusanywa ikiwa ni pamoja na kuziba mianya yote ya ukwepaji kodi na kuwachukulia hatua wale wote wanaokwepa kulipa kodi.

TRA imekuwa ikifanya doria mbalimbali katika mipaka isiyo rasmi, bandari bubu na sehemu ambazo zinaweza kutumika kama vichochoro vya kukwepea kodi ili kuweza kuwakamata wanaovunja sheria kwa kukwepa kulipa kodi.

Matumizi ya mfumo wa kielektroniki

Mwaka 2017, Rais Magufuli alizindua mfumo mpya wa ukusanyaji kodi kwa njia ya Kielektroniki (Electronic Revenue Collection System (e-RCS), mfumo ambao umeongeza mapato kwa kiwango kikubwa.

Mfumo huu ni sehemu ya mchakato wa ukusanyaji wa mapato unaojumuisha mifumo mbalimbali iliyowekwa pamoja kuweza kufanya ukadiriaji, tathmini na ukokotozi wa kodi kutoka kwenye miamala mbalimbali inayofanyika kielektroniki.

Ni mfumo ambao unahusisha moduli tisa zinazofanya kazi mwanzo hadi mwisho kuhakikisha kodi inakusanywa, inakadiriwa na kupelekwa moja kwa moja kwenye akaunti za Mamlaka ya Mapato Tanzania na Bodi ya Mapato Zanzibar ambazo zipo Benki Kuu.

Matumizi ya EFD

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa ikitilia mkazo mkubwa matumizi ya Mashine za Kielektroniki za Kodi (EFDs) katika manunuzi ya kila bidhaa na utoaji wa huduma ili kuhakikisha kila kodi inayolipwa inafika serikalini na kuiwezesha nchi kutekeleza wajibu wa kutoa huduma muhimu za kijamii kwa wananchi wake.

Kutokana na hilo, wafanyabiashara wengi wamejitokeza kununua EFDs kwa hiari. Mwamko huo si katika manunuzi tu bali kumekuwa na mwamko wa wafanyabiashara kutoa risiti kwa hiari hata pale ambapo hawajaombwa na wateja.

Matumizi ya mfumo wa Stempu za kielektroniki (ETS)

Juni mwaka 2018, Serikali kupitia TRA ilianzisha mfumo wa Stempu za kodi za Kielektroniki (ETS) kwa bidhaa zinazostahili kutozwa ushuru wa bidhaa badala ya stempu za karatasi za kubandika ambapo mfumo huo mpya ulianza kutumika rasmi Januari 15, mwaka huu.

Kutokana na changamoto za mfumo wa stempu za kodi za karatasi, Serikali iliamua kuanzisha mfumo wa stempu za kodi za kielektroniki, mfumo ambao unaendeshwa kwa ushirikiano wa TRA na kampuni ya SICPA SA yenye makao makuu yake nchini Uswisi.

TRA ilipiga marufuku matumizi ya stempu za karatasi kwa bidhaa zote za sigara, pombe kali, mvinyo, bia na aina zote za vileo zenye stempu zisizo za kielektroniki na zile zisizo za stempu kabisa, baada ya utekelezaji wa agizo hilo, Julai mwaka huu, Serikali imetangaza kuwa, kuanzia Agosti 2019, TRA itaanza kutumia mfumo wa stempu za kielektroniki (ETS) katika bidhaa za vinywaji baridi kama soda n.k.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo takwimu zinaonyesha kuwa, kuna ongezeko la ukusanyaji wa mapato kutokana na awamu ya kwanza ya matumizi ya mfumo huo.

“Tuna imani mfumo huu utaongeza mapato, kwa awamu ya kwanza tu tumefanikiwa kuongeza mapato ya ushuru wa forodha kutoka Sh. 24 bilioni Januari hadi Sh. 28 bilioni Aprili,” alinukuliwa Kayombo na gazeti la Mwananchi.

Mfumo wa kuingiza na kuondosha mizigo kwa njia ya Kielektroniki (TANCIS)

Katika jitihada za kuongeza ukusanyaji wa mapato, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatumia Mfumo wa Kuingiza na Kuondosha Mizigo kwa njia ya Kielektroniki (TANCIS).

Mfumo huo wa TANCIS ni kichocheo muhimu katika kuipa mamlaka teknolojia ambayo itaiwezesha kuendana na matakwa ya ukuaji wa biashara ya kimataifa. Lengo la matumizi ya mfumo huo ni kuwezesha mamlaka hiyo kukusanya mapato hadi kuvuka lengo, kurahisisha shughuli za forodha ikiwa ni pamoja na kuongeza tija.

Mfumo wa TANCIS unawezesha usimamizi wa mizigo tangu inapoingia hadi inapoondoshwa katika muda muafaka pia unatoa ripoti kamili ya utendaji na kutunza takwimu na hivyo kurahisisha shughuli za forodha na kuongeza mapato ya serikali ambayo hutumika katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Uboreshaji wa taarifa za walipakodi

Katika jitihada za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuongeza ufanisi katika usimamizi na ukusanyaji wa kodi kwa kiwango cha juu, ilizindua zoezi la uhakiki na uboreshaji wa taarifa za usajili wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) ambao umeisaidia mamlaka hiyo kujua idadi sahihi ya walipakodi halisi na kuondoa walipakodi hewa ili kuboresha huduma za ulipaji kodi kwa ujumla.

Baadhi ya miradi iliyotekelezwa kutokana na ukusanyaji wa kodi

Kupitia uboreshaji wa mifumo ya ulipaji kodi iliyosababisha kuongezeka kwa mapato yanayokusanywa na TRA kwa mwezi, Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kutekeleza miradi mikubwa na ya kihistoria ambayo imemalizika na mingine inaendelea kutekelezwa kama ifuatavyo;

Ununuzi wa ndege mpya

Kupitia mapato yatokanayo na kodi, Serikali ya Awamu ya Tano imefanikiwa kununua ndege kwa ajili ya kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na kuboresha sekta ya usafiria wa anga nchini. Ndege zilizonunuliwa ni pamoja na; Boeing 787-8 Dreamliner, Airbus A220-300 pamoja na ndege 3 aina ya Bombardier Q400.

Ujenzi wa reli ya kisasa (SGR)

Tanzania inatekeleza mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kwa kutumia fedha za ndani ambazo zinatokana na mapato yanayotokana na kodi inayolipwa na wananchi. Katika mradi huo wa kihistoria, kipande cha Morogoro -Makutupora kilianza kujengwa Februari 2018 na kitakamilika Februari 2021.

Utoaji wa elimu bure

Kupitia mapato yatokanayo na kodi, Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikitenga bajeti kila mwezi kwa ajili ya kugharamia elimu bila malipo kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Huu ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Magufuli aliyoitoa wakati wa kampeni za urais mwaka 2015.

Mbali na miradi hii, Serikali imekuwa ikitekeleza miradi ya upatikanaji wa maji safi na salama, ujenzi wa vituo vya afya na hospitali, ununuzi wa dawa na vifaa tiba, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara, ujenzi wa shule, utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu n.k.

Haya yote yanafanyika kutokana na mapato yatokanayo na kodi za wananchi. Ni muda sasa wa Watanzania kuamka na kuhakikisha kwamba kila mtu kwa nafasi yake anakuwa mlipaji kodi mzuri ili kusaidia juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo.

Serikali tumeichagua ili kusimamia sheria na kutuongoza, lakini jukumu la kujenga nchi na kujikwamua na umaskini tunalo sisi wananchi na tutaweza kufanikiwa kufanya hivyo endapo tutakuwa walipaji wazuri wa kodi.