Mchanga pekee ni kampeni ya mwaka mzima inayolenga kuhamasisha ukusanyaji wa chupa za plastiki na uhifadhi wa fukwe za bahari


Mchanga pekee ni kampeni ya mwaka mzima inayolenga kuhamasisha ukusanyaji wa chupa za plastiki na uhifadhi wa fukwe za bahari

MCHANGA PEKEE ni Kampeni ya miezi 12 iliyobuniwa, kuasisiwa na inayosimamiwa na Kampuni ya Coca-Cola Kwanza Kampuni Tanzu ya Coca-Cola Beverages Africa ikiwa imeanza mwezi Februari mwaka 2019 yenye malengo na madhumuni ya kuelimisha, kufundisha, kushirikisha na kuhimiza uhifadhi wa plastiki taka (mazingira) katika jamii zetu ikiwa imejikita katika usafishaji wa fukwe zetu, ukusanyaji wa chupa za plastiki, uchakataji na njia bora ya uhifadhi wa chupa za Plastiki nchini Tanzania.

Uchafu upatikanao baharini asilimia kubwa unatokea nchi kavu kupitia mito, mifereji, na fukwe zetu, ambapo inakadiriwa kuna vipande 13,000 vya plastiki kwa kila kilometa za mraba katika bahari na utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na shirika la “International Council of Beverages Associations (ICBA)” unaonyesha kuna vipande vya plastiki vipatavyo millioni 15 baharini mpaka leo.

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Ocean Conservancy’s 2018 International Costal Cleanup inaonyesha vipande vya sigara vinaongoza kwa kuokotwa kwenye fukwe pale usafi wa fukwe unapofanyika ikiwa na wastani wa vipande millioni 2.4, ikifuatiwa na vifungashio vya chakula (Food wrappers) wastani wa millioni 1.7, Chupa za plastiki (millioni 1.6), vizibo vya plastiki (millioni 1.1) na mifuko ya plastiki /Rambo (757,523) ambapo inatengeneza idadi ya makundi matano makubwa ambayo yaliokotwa kwenye zoezi la usafishaji wa fukwe lililofanyika kwenye nchi zaidi ya 100 duniani.

Kwa Tanzania, hali ni hiyo hiyo katika fukwe zetu za Mtwara, Dar es Salaam, Bagamoyo, Tanga na Zanzibar ambapo asilimia kubwa ya taka za plastiki hutokana na shughuli za kibinadamu na utupaji holela wa chupa za plastiki kwenye vyanzo vya maji kama mito na mifereji.

Endapo hali hii ikiendelea hivi pasipo kuchuliwa hatua yoyote, inakadiriwa kuwa ifikapo 2050 kutakuwa na vipande vingi vya plastiki baharini kuliko samaki.

Kwa kupitia tafiti hizi na Makala mbalimbali zihusuzo mazingira ndipo kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-Cola kwanza ikaamua kuja na kitu kiitwacho “MCHANGA PEKEE”

MCHANGA PEKEE

MCHANGA PEKEE ni Kampeni ya miezi 12 iliyobuniwa, kuasisiwa na inayosimamiwa na Kampuni ya Coca-Cola Kwanza Kampuni Tanzu ya Coca-Cola Beverages Africa ikiwaimeanza mwezi Februari mwaka 2019 yenye malengo na madhumuni ya kuelimisha, kufundisha, kushirikisha na kuhimiza uhifadhi wa plastiki taka (mazingira) katika jamii zetu ikiwa imejikita katika usafishaji wa fukwe zetu, ukusanyaji wa chupa za plastiki, uchakataji na njia bora ya uhifadhi wa chupa za Plastiki nchini Tanzania.

MCHANGA PEKEE ni kampeni ya mazingira yenye malengo ya usafishaji wa fukwe nchini Tanzania kwa kushirikisha jamii husika kuziweka katika mandhari salama, endelevu na zenya kuvutia ambapo lengo kuu likiwa ni ubaki mchanga peke yake kwenye fukwe kwa kuondoa vitu visivyostahili kuwepo (uchafu-plastiki).

Kampeni hii imejikita katika ukusanyaji wa chupa za plastiki katika mazingira yetu ili kuwezesha mazingira kuwa salama na yenye kuweza kuhifadhi ekolojia ya mazingira yaliyopo.

Kampeni ya MCHANGA PEKEE imegawanyika katika shughuli kuu mbili zenye lengo moja la uelimishaji wa jamii kwa njia ya ushiriki wa jamii kwenye kuhifadhi na kutunza mazingira. Majukumu ya kampeni ya MCHANGA PEKEE ni “Usafishaji wa Fukwe” na “Ununuaji wa chupa za Plastiki kwa malengo ya kuchakatwa”.

Kampeni ya MCHANGA PEKEE imejikita mahsusi katika kuwezesha, kujenga morali na kusimamia usafishaji wa fukwe zetu nchini ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu ya njia bora na salama za uhifadhi wa chupa za plastiki.

MCHANGA PEKEE ni jukwaa lenye malengo ya kukuza uelewa kwa jamii kuhusu njia bora za uhifadhi wa mazingira hasa hasa taka zitokanazo na plastiki na kuikumbusha jamii umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.

Kampeni ya MCHANGA PEKEE imekuja kwa malengo na madhumuni ya kuwaleta pamoja wadau wa sekta ya viwanda na wazalishaji wa chupa za plastiki kujumuika pamoja katika uhifadhi wa mazingira.

Usafishaji fukwe

Kampeni ya MCHANGA PEKEE imefanikiwa kuajiri wanawake vijana wanne katika fukwe ya Coco, ambapo wanawake hao wana jukumu kuu la kusafisha fukwe hiyo mara 5 kwa wiki masaa 8 kwa siku husika kwa mwaka mzima wa 2019-2019 ambapo wanawake hao wamepatiwa mikataba ya kazi, vitendea kazi na kupewa elimu ya mazingira.

Kampeni hii ya MCHANGA PEKEE husafisha fukwe ya Coco kila siku za Jumamosi, Jumapili, Jumatatu, Jumatano, Ijumaa kwa masaa 8 kila siku mara 5 kwa wiki kwa muda wa mwaka mzima kuanzia Februari 2019 mpaka Februari 2020.

Kupitia kampeni hii ya MCHANGA PEKEE, Coca-Cola Kwanza imefanikiwa kuweka vifaa vya kutupia uchafu vipatavyo kumi katika maeneo tofauti tofauti kwenye fukwe ya Coco ambapo kila dumu la kutupia uchafu lina ujumbe wenye malengo ya kumkumbusha mwananchi kutupa taka kwenye eneo hilo.

Kazi hii imetokana na makubaliano kati ya kampuni ya Coca-Cola kwanza (Kupitia Kampeni ya MCHANGA PEKEE) na Serikali (upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni) ya kufanya usafi wa fukwe na fukwe ya Coco (Coco Beach) kama eneo la kuanzia kampeni hii.

Matokeo ya usafishaji fukwe ya Coco

Kupitia timu ya wasafishaji fukwe inayofanya kazi kupitia kampeni ya MCHANGA PEKEE, imeweza kubaini mambo mbalimbali kwenye usafishaji wao wa fukwe kwa kipindi chote walichofanya usafi kwenye fukwe hiyo, ambapo kwa uchunguzi wao, taka nyingi zikusanywazo kila siku wafanyapo usafi vipande vya chupa za plastiki vinaongoza kwa kuokotwa, ambapo pamoja na mambo mengine taka nyingine wakutanazo kila mara wafanyapo usafi ni pamoja na pini, sindano za mahospitalini, vifungashio vya chakula, mirija, vizibo vya plastiki, mifuko ya plastiki /Rambo, pamoja na mabaki ya vyakula mbalimbali.

Athari chanya za kampeni ya MCHANGA PEKEE kwa fukwe

Ni ukweli usiopingika kampeni ya MCHANGA PEKEE imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufikia kundi kubwa la jamii kama lengo lake la kuelimisha jamii kuhusu usafishaji wa fukwe.

Fukwe ya Coco kwa siku za wikiendi inapokea wastani wa watu 300 mpaka 500 kwa nyakati tofauti, kwa kila ambaye amefika fukwe hiyo, hufanikiwa kukutana na wasafishaji wetu wakiwa kazini kusafisha na kwa kila eneo ambalo watu hufika hukutana na jumbe mbalimbali za kampeni hii kwenye ndoo maalumu za kutupia uchafu ambazo humkumbusha mtumiaji wa fukwe kuhakikisha anayatunza mazingira husika kwa manufaa yake na vizazi vijavyo.

Mpaka sasa kupitia jumbe hizo, zaidi ya watu 5000 wameweza kuzisoma na wameweza kutumia ndoo maalumu za utupaji wa taka kuhifadhi taka baada ya matumizi.

Kupitia kikosi kazi chetu cha usafishaji kwa siku hukusanya wastani wa chupa za plastiki zipatazo 150, vizibo vya plastiki zaidi ya 250 na uchafu mwingine mwingi sana ambao hutokana na kusukumwa na mawimbi ya bahari kuja ufukweni.

Uchafu wote ukusanywao na kikosi kazi cha MCHANGA PEKEE unahifadhiwa kwenye mazingira salama kusubiri magari ya Manispaa ya Kinondoni kuchukuliwa kwa ajili ya uhifadhi salama.

Chupa zikusanywazo kwenye zoezi hilo huchukuliwa na kupelekwa kwa wachakataji wa chupa kwa lengo la kupatikana mbao zitokanazo na plastiki.

Kupitia ushuhuda wa jamii inayofanya kazi kwenye fukwe ya Coco, vijana wa ufukweni wameeleza wazi kuwa kwa sasa idadi ya watalii wa fukwe ya Coco imeongezeka kutokana na eneo hilo kuwa safi na muonekano mpya kulinganisha na zamani ilivyokuwa, wameenda mbali kwa kusema hii imekuja kutokana na kampeni ya MCHANGA PEKEE ambayo imebuniwa, kuasisiwa na kusimamiwa na kampuni ya Coca-Cola Kwanza.

Mpaka sasa kikosi kazi cha MCHANGA PEKEE kimeweza kukusanya jumla ya chupa taka za plastiki kwenye fukwe ya Coco zaidi ya 8500 na zote zimechukuliwa na kupelekwa kwenye kampuni ya uchakataji ili kupatikana mbao zitokanazo na plastiki.

Pamoja na mambo mengine, kikosi kazi kina majukumu ya kuhakikisha kinatoa elimu ya uhifhadhi wa mazingira na kwa muktadha huu elimu ya uhifadhi wa fukwe zetu nchini.

Trash for Cash (Pesa kwa Taka)

MCHANGA PEKEE kama kampeni mama ina kipengele ndani yake kiitwacho Trash for Cash (Pesa kwa Taka), ikiwa ni kampeni maalumu yenye madhumuni ya kuelimisha jamii yote kwa ujumla kwenye makazi yao na mitaa yao umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na ushiriki wao wa moja kwa moja kusafisha mitaa yao kwa uondoaji wa chupa za plastiki ikiwa ni sehemu ya kuweka mitaa yetu safi na jamii yote kwa ujumla.

Trash for Cash (Pesa kwa Taka)ni kampeni iliyo chini ya kampeni mama ya MCHANGA PEKEE ambayo imebuniwa, kuasisiwa na inayosimamiwa na kampuni ya Coca-Cola Kwanza yenye malengo ya utoaji wa elimu kwa jamii kwa njia ya ushiriki wao katika ukusanyaji wa chupa za plastiki ambapo kampuni ya Coca-Cola Kwanza inazinunua chupa hizo kwa kila chupa moja inanunuliwa kwa kiasi cha Shilingi 50 ambapo kwa kila mwezi kampuni imeweka malengo ya kununua chupa 15,000 kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Kampeni hii iliyo chini ya MCHANGA PEKEE, huchagua maeneo ya makazi ya jamii na kwenda kufunga kambi kwenye makazi ya watu kwa kwenda na magari ya uelimishaji, magari ya ukusanyaji wa chupa taka pamoja na kikosi kazi cha uelimishaji wa mazingira na ukusanyaji wa chupa za plastiki kwa jamii.

Zoezi hili liliasisiwa mwezi Februari na kampeni imelenga kufikisha elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa rika zote za jamii na mikoa mbalimbali nchini.

Kampeni hii inanunua chupa moja (1) kwa kiasi cha Shilingi 50 na kampeni imejiwekea kila mwezi kununua zaidi ya chupa 15,000 kwenye makazi ya jamii, ambapo kila mwezi kikosi kazi huchagua eneo la kwenda kutoa elimu ya uhifadhi bora wa chupa za plastiki.

Mpaka sasa kampeni imefanikiwa kwenda maeneo mbalimbali katika jiji la Dar es Salaam ikiwemo Mbagala (Wilaya ya Temeke), Manzese (Wilaya ya Ubungo), Tandale (Wilaya ya Kinondoni) na Mwanyamala-CCM Mwinjuma (Wilaya ya Kinondoni), ambapo kwa kila eneo ambalo kampeni hii imeweza kupita imefanikiwa kutoa elimu ya mazingira kwa wakazi takribani 5000 ambapo mpaka sasa zaidi ya chupa za plastiki 60,000 zimeweza kununuliwa kwa kiasi cha Shilingi 50 kwa kila chupa.

Bei inayotumika kwenye ununuaji wa chupa kwenye kampeni hii ni mara nne ya bei ya soko ambapo kwa soko la chupa za plastiki kwa sasa mfumo unaotumika ni ule wa kununua kwa njia ya kupima kwa uzito (Kilogramu) ambapo kwa kila Kilo 1 ya chupa ya plastiki bei ni kiasi cha wastani wa Shilingi 200 mpaka 250 ambapo kwenye kilo 1 ya chupa ni wastani wa chupa 25 mpaka 30 ambazo kwa kampeni yetu mkazi angeweza kujipatia kiasi cha Shilingi 1000 mpaka 1500.

Lengo la kampeni yetu hii si kuja kuharibu soko, hapana bali imekuja kutoa elimu ya mazingira na umuhimu wa uhifadhi wa chupa za plastiki kwenye makazi yetu ambazo ndiyo chanzo cha kuziba mifereji na kupelekea yote kupita kupitia mito na kwenda kuathiri bahari zetu.

Kampeni hii ina sura ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kwani pale kampeni hii ifikapo kwenye makazi ya jamii mara zote imepokelewa na jamii kwa mwitikio ulio mkubwa sana na kupelekea kupata watu wengi sana wenye chupa za plastiki ambapo huipa kikosi kazi tathmini kuwa chupa za plastiki ni kazi kubwa sana na inahitaji kazi za ziada kufanyika kuhakikisha tuinatokomeza changamoto hii yote.

Namna kampeni hii inavyofanyika

Punde mkazi wa eneo husika anapoleta chupa za plastiki hukutana na kikosi kazi cha Coca-Cola Kwanza ambapo uhesabiwa idadi za chupa alizokuja nazo na kupewa kuponi maalumu yenye kumuwezesha yeye kwenda kuchukua pesa kwenye gari maalumu la utoaji wa fedha. Zoezi hili limetengenezwa kuwa rahisi sana na lenye kumuwezesha mleta chupa kupata fedha zake kwa haraka na uwazi mkubwa. 

Faida na umuhimu wa Kampeni (MCHANGA PEKEE)

1.   Ufahamu na uelimishaji wa Uhifadhi na utunzaji endelevu wa mazingira yetu kwa ujumla.

2. Kuunga mkono juhudi za Serikali katika kujenga jamii bora yenye kutambua umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na usimamizi endelevu wa mazingira.

3. Ukuzaji wa sekta ya utalii wa fukwe kwa kuwezesha utunzaji wa fukwe wa muda wote na kufanikisha mvuto wa fukwe kama sehemu mojawapo ya kipato cha taifa kupitia sekta ya utalii.

4. Uwezeshaji wa kiuchumi na kifursa (ajira) kwa vijana na wanawake kupitia mradi huu (MCHANGA PEKEE)

5. Kupunguza ongezeko la chupa za plastiki katika jamii na kuifundisha jamii njia bora za uhifadhi na ubadilishi bora wa matumizi ya chupa za plastiki.

6. Ulinzi na uhifadhi wa ekolojia ya viumbe vya baharini na nchi kavu pia kuwezesha jamii kuishi kwenye maeneo yaliyo huru na uchafu na maradhi yatokanayo na uchafuzi wa mazingira.

Hitimisho

Kampuni ya Coca-Cola Kwanza kama sehemu ya jamii na mdau mkubwa wa Serikali na jamii katika uhifadhi wa mazingira imejipanga kuendeleza kampeni hii na kubuni kampeni nyingine tofauti tofauti zenye lengo la kuiwezesha jamii kuishi kwenye jamii iliyo salama na endelevu ili kuwezesha shughuli za maendeleo kufanyika kwenye mazingira yaliyo bora na salama.

Imeandaliwa na

Idara ya Masuala ya Umma na Mawasiliano

Coca-Cola Kwanza