iCHF ni mkombozi wa upatikanaji wa huduma za afya kwa jamii za wafugaji mkoani Manyara


iCHF ni mkombozi wa upatikanaji wa huduma za afya kwa jamii za wafugaji mkoani Manyara

Uanzishwaji wa iCHF ni matunda mazuri ya ushirikiano wa Serikali na taasisi binafsi pamoja na wadau wa maendeleo kwenye kuboresha maisha ya wananchi.

Afya ni kitu muhimu katika maisha ya binadamu kwa kuwa ni kichocheo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi. Mtu anapokuwa na afya njema, anakuwa na nafasi kubwa ya kuzalisha mali na hata kuongeza pato binafsi na familia kwa ujumla.

Pia, afya ni hali ya ukamilifu kimwili, kiakili, kijamii na kutokuwepo kwa maradhi. Afya bora ni nguzo na rasilimali muhimu katika kuchangia maendeleo ya mtu binafsi, familia na nchi hususan katika kuleta maisha bora na kupunguza umaskini.

Upatikanaji wa afya bora unahitaji uwezeshaji wa jamii iwe na uwezo wa kushiriki, kuamua, kupanga na kutekeleza mikakati yao ya kuwaletea maendeleo katika ngazi mbalimbali.

Kwa kulitambua hili, jamii ya wafugaji mkoani Manyara wamesema wako tayari kujiunga na Mpango wa Kitaifa wa Bima ya Afya Iliyoboreshwa (iCHF), baada ya kuridhika na maboresho yaliyofanyika kwenye mpango huo.

Akiongea katika uzinduzi wa iCHFya kitaifa Mkoa wa Manyara, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mheshimiwa, Jackson Sipitieck alisema kuwa Mpango huu umezingatia hali halisi ya wafugaji ambao huwa wana familia kubwa na mara kwa mara huwa wanahama na mifugo yao.

“Mkoa wa Manyara tuna bahati kuwa tulishaanza kutekeleza hii CHF iliyoboreshwa tangu mwaka 2015, ambapo tulikuwa tunalipa shilingi 30,000 kwa kaya na kutibiwa wilayani, sasa kwa hii ni kama imeboreshwa zaidi maana tutatibiwa hata hospitali ya rufaa ya Mkoa ambako kuna huduma nyingi zaidi,” alisema.

Pia aliongeza kwamba, kwa Wilaya ya Simanjiro, wangependa pia hospitali za dini zijumuishwe kama ilivyokuwa kwenye CHF iliyoboreshwa (iCHF), “Ukiangalia zamani tulikuwa tunatibiwa kwenye hospitali ya dini, sasa huu mpango mpya ni lazima uendeleze mazuri ya zamani, ili haya yaliyoboreshwa zaidi yaweze kuleta matokeo chanya,” alisema.

Mkoa wa Manyara (pamoja na Kilimanjaro) ni moja kati ya mikoa miwili ambayo Shirika lisilokuwa la serikali la PharmAccess kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) waliendesha kwa majaribio CHF iliyoboreshwa (iCHF) kuanzia mwaka 2015 na kupata mafanikio makubwa.

Katika majaribio hayo yaliyopelekea kuanzishwa kwa iCHF ya kitaifa, Shirika la PharmAccess na NHIF walianzisha utaratibu wa fedha zinazokusanywa toka kwa wananchi waliojiunga na kukusanywa kwenye akaunti moja ya mkoa ambapo kila mwisho wa mwezi malipo yalifanyika kwenda kwenye vituo vya kutoa huduma kulingana na huduma waliyotoa kwa wanachama.

Majaribio haya yaliendeshwa kwenye mikoa ya Manyara na Kilimanjaro kwa sababu, PharmAccess walipoanza mradi wa kusaidia upatikanaji wa huduma bora za afya kupitia bima, walitafuta vikundi vilivyosajiliwa ambavyo vina idadi kubwa ya watu kwa ajili ya majaribio.

Wanachama wa FINCA na wale wa chama cha KNCU ndio walioonekana wanafaa. FINCA iliisha baada ya mwaka wa kwanza kutokana na matatizo kwenye uongozi, wakati bima ya KNCU iliendelea.

CHF iliyoboreshwa Kilimanjaro ni muendelezo wa bima ya afya ya KNCU. Baada ya mafanikio ya bima ya KNCU, kwenye mikutano ya uhamasishaji na hata kupitia vikao vya madiwani watu waliomba nao wajiunge na bima ya KNCU hata kama sio wanachama wa KNCU. Ili kufanikiwa hilo, ndio majadiliano yakaanza kusaidia kuboresha CHF kutumia mfano wa bima ya KNCU ili watu wote waweze kujiunga.

Baada ya kuanza mkoa wa Kilimanjaro, Manyara iliingia kutokana na mapendekezo ya NHIF, ambao ndio wadau katika utekelezaji wa ICHF kwa PharmAccess.

Pia, katika majaribio hayo ndipo ulianzishwa utaratibu wa makusanyo yote ya Halmashauri kuwekwa kwenye chungu kimoja (risk pooling at regional level) hivyo kuwezesha ustahimilivu wa mfuko kuwa mkubwa.

Ni kutokana na mabadiliko hayo ndipo majaribio hayo yaliweza hata kuingia mkataba wa huduma na vituo vya afya vya binafsi na vile vya dini. Katika mfumo huu wa majaribio, bei ya kujiunga kwa kaya ilikuwa ni TSh. 30,000, kiasi ambacho pia ndicho kinachotumika katika CHF iliyoboreshwa ya kitaifa.

Mwaka 2018, Serikali ilipokea sehemu kubwa ya mabadiliko haya na kuyatumia kwenye kuanzisha CHF iliyoboreshwa ya kitaifa ambayo imezinduliwa rasmi mikoa ya Manyara, Kilimanjaro, na mikoa mingine zaidi ya 20 Tanzania Bara.

Uzinduzi wa CHF iliyoboreshwa ya kitaifa mkoani Manyara ulihudhuriwa na wakuu wa Wilaya zote, Wenyeviti wa Halmashauri zote saba, Wakurugenzi wa Halmashauri zote, Mganga Mkuu wa Mkoa, Waganga Wakuu wa Halmashauri, Waratibu wa CHF wa Halmashauri zote na wageni waalikwa mbalimbali ikiwemo wadau wa maendeleo wanaofanya kazi mkoa wa Manyara.

Akielezea historia ya iCHF katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Kimataifa la PharmAccess, Dk. Heri Marwa alisema uanzishwaji wa iCHF ni matunda mazuri ya ushirikiano wa Serikali na taasisi binafsi pamoja na wadau wa maendeleo kwenye kuboresha maisha ya wananchi. 

Mwaka 2011 PharmAccess ilikubaliana na chama kikuu cha ushirika cha KNCU kuanzisha bima ya afya kwa ajili ya wanaushirika ambao wengi walikuwa wakitumia gharama kubwa ya mapato yao kwenye matibabu.  Bima hiyo iliyoitwa KNCU Health Plan iliendeshwa kwa muda wa miaka mitatu ya mafanikio hata kuweza kufikia malengo ya uandikishaji kwa asilimia 70.

Mafanikio ya bima ya wakulima ya kahawa yalipelekea wananchi ambao siyo wanaushirika kuanza kulazimisha wapewe nafasi ya kujiunga na bima hiyo.

Mafanikio hayo ndiyo yalipelekea PharmAccess kuanza majadiliano na Serikali ambapo walielekezwa kushirikiana na NHIF kutumia misingi iliyowekwa kwenye bima ya wakulima wa kahawa kuanzisha majaribio ya kuboresha bima ya afya ya jamii (CHF) ambayo ilikuwepo tangu mwaka 2001.

Huo ndio ukawa mwisho wa KNCU Health Plan na mwanzo wa iCHF ambayo ndiyo imekuja kutuletea mfumo huu wa kitaifa.

Akizungumzia manufaa ya mpango huu kwa jamii ya wakulima, Dk. Marwa alisema, “Duniani inakadiriwa kuwa watu milioni 100 wanaingia kwenye umaskini kila mwaka kutokana na kulipa gharama za matibabu (taarifa ya WHO). Haina tofauti na hapa kwetu, wafugaji hulazimika kuuza mifugo yao kwa bei rahisi pale wanapokuwa wanaumwa ili kulipia gharama za matibabu, wengine wakilazimika kuuza ardhi au hata mali kama nyumba. Kuwa na bima itawasaidia kuondoa majanga kama haya. Jamii yenye afya bora, uzalishaji mali huongezeka.”

Kuhusu mikakati ya PharmAccess na NHIF katika kuhakikisha mpango huu unafika kwenye mikoa mingine, Dk. Marwa alisema, kwa sasa wanashirikiana na NHIF na wadau wengine wa maendeleo kutoa ushauri wa kiufundi (technical assistance) kwa mikoa inayohitaji ili iweze kuanza utekelezaji.

Katika uzinduzi huo, PharmAccess ilikabidhi simu janja (smartphone) 610 kwa ajili ya uandikishaji wa wanachama kwenye  kila kijiji na pikipiki thelathini na mbili (32), ikiwa ni pikipiki moja kwa kila tarafa ndani ya mkoa ili zitumike na maafisa tarafa wa NiCHF katika kuhamasisha na kufuatilia utekelezaji wa NiCHF.

“Mmekuwa Mkoa wa kwanza kuwa na pikipiki za tarafa kwa ajili ya NiCHF na kama zikitumika vizuri, tunaamini Manyara utakuwa ni Mkoa wa kwanza kwenye uandikishaji,” alisema Dk. Marwa.

Pamoja na vifaa hivyo, PharmAccess wamegharamia pia mafunzo ya waandikishaji wawili kwa kila kijiji cha Mkoa wa Manyara, Wenyeviti na Watendaji wa vijiji, Waganga Wafawidhi wa Zahanati, vituo vya afya na hospitali zote za Mkoa wa Manyara.

Dk. Marwa alimalizia kwa kuwataka watu wa Mkoa wa Manyara kuonyesha kwa vitendo kuwa wao ndio waanzilishi wa mpango huu kwa kujiunga kwa wingi kwa kuwa sababu na uwezo wa kufanya hivyo wanao.

Akipokea simu na pikipiki hizo kwa niaba ya mkuu wa mkoa, Mkuu wa wilaya ya Babati, Elizabeth Kitundu alilishukuru Shirika la PharmAccess kwa kusaidia kwao kuanzisha iCHF mkoa wa Manyara na pia kutoa nyenzo hizo ambazo zitasaidia sana kwenye utekelezaji. Kitundu alisema lengo la mpango huo ni kusogeza huduma karibu kwa wananchi na kutoa huduma bora zenye viwango vinavyokubalika.

“Mkoa wa Manyara ulijiwekea malengo mawili mahsusi ya kuboresha huduma za afya na kuhakikisha usajili wa NiCHF unafikia asilimia 50 ya kaya hadi kufikia Desemba mwaka huu. Tunanuia pia gharama za matibabu zisiwe kikwazo cha kufanya wananchi wasifikie huduma au kuwadumbukiza zaidi katika umaskini,” alisema.

"Tangu mwaka 2018 Serikali imeanzisha mfuko wa afya ya jamii ulioboreshwa wa Taifa na mkoa wetu una bahati kubwa ya kupata mdau wetu wa PhamAccess International aliyeshirikiana na Manyara kuanzisha iCHF iliyoboreshwa tangu mwaka 2015 hivyo mkoa wetu una uzoefu kiasi hivyo umeweza kuanza kuitekeleza iCHF mpya ya kitaifa ikiwa na uzoefu," alisema Kitundu.

Akitoa maoni yake katika uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga alisema mpango huu ili upate mafanikio ni lazima uendelee kushirikiana na vituo vya kutolea huduma vya binafsi, hasa vya dini kutokana na wingi wa wananchi kupenda kutumia vituo hivyo zaidi au kutokana na ukaribu au huduma zinazotolewa.

“Wananchi wanapendelea kutumia huduma hii kwa kupatiwa matibabu katika eneo lolote wanaloishi bila kuambiwa hapo ni kwenye taasisi ya serikali au taasisi ya kidini ili mradi apate tiba,” alisema Mofuga.

Kwa upande wake Meneja wa Mfuko wa Bima ya Afya nchini (NHIF) mkoani Manyara, Hans Mwankenja alisema asilimia 23 ya kaya za Mkoa huo zimeshajiunga kwenye mfuko wa iCHF tangu mfuko huo ulivyoanzishwa mwaka 2015.

”Itakuwa ni ajabu kama baada ya kuiboresha na kuwa iCHF ya kitaifa, uandikishaji wetu upungue toka asilimia 23 ambayo tulikuwa tumefikia, ni lazima tujiwekee malengo ya kwenda mbele Zaidi,” alisema.

Mkoa wa Manyara umejiwekea kufikia lengo la uandikshaji wa asilimia 50 kufikia mwisho wa mwaka 2019 na asilimia 80 ifikapo mwisho wa mwaka 2020.

Wasemavyo wananchi kuhusu iCHF

Mkazi wa Majengo mapya mjini Babati, Chambalo Mchele anasema alinunua kadi ya iCHF kwa Sh30, 000 ambayo hutumia kupata matibabu na kaya yake pindi wakiugua.

Mkazi wa mtaa wa Mruki mjini Babati, Anna Qambalali alisema alipata kadi hiyo bila gharama kwa sababu yeye ni mjamzito.

Shirika la PharmAccess lina mradi wa kutoa kadi za iCHF kwa wajawazito wanaoenda kliniki mapema kuhudhuria mahudhurio yote manne katika kliniki ya mama na mtoto.