Japan inajiandaa kwa ajili ya mkutano muhimu wa kimataifa kwa maendeleo ya Afrika (TICAD)


Japan inajiandaa kwa ajili ya mkutano muhimu wa kimataifa kwa maendeleo ya Afrika (TICAD)

Azimio la Tokyo la Maendeleo ya Afrika ambalo lilipitishwa na mkutano huo wa kwanza , lilirudisha suala la misaada na maendeleo kwa ajili ya Afrika kuwa ajenda ya kimataifa. Tangu hapo kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20,TICAD imekua na  historia ya kuboresha mazingira ya kijamii na kiuchumi ndani ya Afrika kwa kutumia rasilimali za umma na binafsi ikijumuisha misaada ya kiufundi kutoka Japan, utaoji wa misaada, na mikopo ya kawaida.

Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo wa Maendeleo ya Afrika (TICAD) ni mkutano wa kimataifa unaoongozwa na Serikali ya Japan na kushirikiana katika udhamini na Umoja wa Mataifa, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) na Benki ya Dunia.

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, azma ya nchi zilizoendelea kuzisaidia nchi nyingi za Kiafrika ilianza kufifia.  Katika mazingira hayo, Japan ndiyo ilikuwa nchi mwasisi wa wazo la kuona umuhimu wa kuisaidia Afrika, na kuanzia hapo mkutano wa TICAD ulikuwa ni  sehemu ya mchango wa  Japan kutekeleza kwa vitendo azma hiyo.

Mkutano wa kwanza wa TICAD ulifanyika mnamo mwaka 1993 ukiongozwa na Japan ikishirikiana kwa karibu na Umoja wa Mataifa na taasisi ya Global Coalition for Africa, na kuwavutia washiriki kutoka nchi 48 za Kiafrika, ikijumuisha wakuu wa nchi wapatao watano (5).

Azimio la Tokyo la Maendeleo ya Afrika ambalo lilipitishwa na mkutano huo wa kwanza , lilirudisha suala la misaada na maendeleo kwa ajili ya Afrika kuwa ajenda ya kimataifa. Tangu hapo kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20,TICAD imekua na  historia ya kuboresha mazingira ya kijamii na kiuchumi ndani ya Afrika kwa kutumia rasilimali za umma na binafsi ikijumuisha misaada ya kiufundi kutoka Japan, utaoji wa misaada, na mikopo ya kawaida.

Kuanzia mwaka 2016 na kuendelea, mikutano ya TICAD hua inafanyika kila baada ya miaka mitatu (3) barani  Afrika na Japan. Mkutano wa TICAD wa sita (6) ulifanyika Kenya na mkutano ujao wa TICAD wa saba (7) utafanyika Yokohama kuanzia Agosti 28 mpaka Agosti 30, 2019.

Kauli mbiu ya mkutano ujao wa TICAD wa saba (7) ni  “Kuendeleza  Maendeleo ya Afrika kupitia Watu, Teknolojia na Ubunifu”Kauli mbiu hiyo inaendana na umahiri wa Japan katika uendelezaji wa rasilimali watu sambamba na sayansi, teknolojia na uvumbuzi. Katika kauli mbiu hii, Japan inalenga kuboresha maendeleo ya Afrika kupitia misaada mbalimbali ambayo ni ya kipekee kwa Japan. Kupitia kauli mbiu hii ya mkutano wa saba wa TICAD Japan inatarajia thamani ya bara la Afrika  itaongezeka katika ngazi zote za kitaifa na kimataifa. 

TICAD na JICA

Mkutano wa TICAD kufanyika Afrika kwa mara ya kwanza ulikuwa ni ule uliofanyika jijini Nairobi, Kenya mwezi Agosti 2016. Azimio la Nairobi liliubeba mkutano huo wa sita (6) wa kihistoria wa TICAD uliosisitiza mabadiliko ya muundo wa kiuchumi kupitia uchumi mseto, viwanda, mifumo ya afya endelevu kwa ubora wa maisha na utulivu wa jamii kwa ustawi wa pamoja ndio masuala makuu ya kushughulikia changamoto mpya ambazo Afrika imekuwa ikikabiliana nazo. Kwa changamoto hizo, Serikali ya Japan ilijitolea katika mkutano wa sita (6) wa TICAD kuwekeza kwa mustakabali wa Afrika kwa kuunga mkono ujenzi wa miundombinu bora, kujenga mfumo wa afya thabiti, na kuchagiza amani na utulivu kuanzia mwaka 2016.

Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) ambalo ni Shirika la Serikali ya Japan linalosimamia  Misaada ya Maendeleo (ODA),  inayotolewa na Serikali hiyo, limekuwa likichukua hatua kadhaa na kuonyesha matokeo madhubuti kwa mustakabali wa Afrika, kwa lengo la kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). JICA imekuwa ikichukua hatua hizo kupitia njia tatu ambazo ni: ushirikiano wa kiufundi, utoaji wa mikopo ya masharti nafuu (ODA concessionary loans), na  utoaji wa misaada isiyokua na sharti la kulipa (grant-aid) kwa nchi za Kiafrika sanjari na dira  yake ya "Kuongoza dunia  kwa uaminifu".

Pamoja na malengo ya TICAD, mipango ya JICA barani Afrika imejengwa kupitia  nguzo tatu kama ifuatavyo: Afrika Bora, Afrika yenye Utulivu na Afrika Thabiti.

Afrika bora

Kutokana na  kuporomoka kwa bei ya bidhaa za ulimwengu baada ya 2013, JICA inawezesha mabadiliko ya muundo wa uchumi kupitia ujumuishaji wa uchumi na masuala ya viwanda barani Afrika. Kutekeleza hilo JICA inakuza maendeleo ya miundombinu bora kwa kuwekeza takriban dola bilioni 10 katika maendeleo ya  rasilimali asili na maendeleo ya nishati, na maendeleo ya miji.

JICA pia inakuza shughuli za sekta binafsi kupitia ukuzaji rasilimali watu na stadi za kiutendaji kwa viwanda vya Kiafrika ambavyo pia vinakidhi mahitaji ya kampuni za Japan. Hii ni pamoja na programu za mafunzo ya waalimu wa hesabu na sayansi, msaada wa mafunzo ya ufundi na elimu ya juu, na juhudi za KAIZEN katika viwanda vya utengenezaji/uzalishaji wa bidhaa na sekta ya biashara. Kwa kuongezea, JICA inatoa fursa kwa vijana wa Kiafrika kusoma katika kozi za shahada ya uzamili huko Japan na kupata mafunzo tarajali ya uzoefu katika kampuni za Kijapani kupitia mpango wa ABE Initiative (African Business Education).  JICA pia inafuatilia vijana hawa baada ya kurudi katika nchi zao, kwa lengo la kukuza rasilimali watu ambao wanaweza kuwezesha  Makampuni ya Japan kupanua biashara zao katika bara la Afrika.

Afrika yenye utulivu

JICA inatilia mkazo katika kujenga mfumo wa afya bora kwa maisha bora. Wakati ikizingatia haki ya kila nchi kumiliki shughuli zake,   JICA inasaidia Mpango wa Afya kwa Wote (UHC) kupitia ushirikiano wa kifedha na kiufundi kwa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa huduma ya afya na kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma ikiwa ni pamoja na fedha za afya. JICA pia inasaidia afya ya mama na mtoto, afya ya uzazi, na hatua za magonjwa ya kuambukiza na yasiyoweza kuambukiza kufikia  Mpango wa Afya kwa Wote (UHC).

Afrika thabiti

JICA inasaidia katika kujenga msingi madhubuti wa utulivu wa kijamii katika kukabiliana na ukuaji wa vurugu zinazotokana na  siasa za misimamo mikali, vita na mabadiliko ya hali ya hewa. Katika suala hili, JICA inakusudia kuongeza uzalishaji wa mpunga maradufu katika miaka 10 kupitia Mipango ya Maendeleo ya Mpunga ya Kitaifa ya kila nchi chini ya mpango wa Jumuiya ya Maendeleo ya Mpunga Afrika (CARD) ambayo ilianzishwa mnamo 2008. Aidha  JICA inasaidia mnyororo mzima wa thamani kama upanuzi, uzalishaji, utunzaji baada ya mavuno na utafutaji masoko kupitia ushirikiano wa kiufundi na kifedha na shughuli za utafiti kwa kushirikiana na washirika wengine wa maendeleo.

 

JICA nchini Tanzania

Ili kufikia malengo ya TICAD, JICA Tanzania inafanya shughuli katika sekta mbalimbali nchini ambazo ni Kilimo, Sekta Binafsi na Maendeleo ya Viwanda, Umeme na Nishati, Uchukuzi, Maji, Serikali za Mitaa, Usimamizi wa Fedha za Umma na Afya. Kwa kuongezea, JICA imekuwa ikipeleka watu wa kujitolea zaidi ya 1,500 nchini Tanzania tangu 1967. Zaidi ya hayo, JICA ina program ya mafunzo ambayo zaidi ya Watanzania 3,500 wametembelea Japan na takriban watu 100 kila mwaka wanashiriki katika programu hiyo. Kwa sababu ya nafasi, katika makala haya  tunataja shughuli chache tu ambazo husaidia maendeleo ya nchi: miongoni mwa mambo hayo, ni maendeleo ya uchukuzi wa mijini, uwezo wa uwezeshaji wa biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki, uboreshaji wa ubora na tija katika viwanda vya uzalishaji "5S KAIZEN", na mafunzo ya shahada ya uzamili katika mpango wa African Business Education (ABE Initiative),  na Kilimo.

Maendeleo ya usafirishaji mijini

Maendeleo ya usafirishaji wa mijini ni muhimu katika maendeleo ya nchi yoyote. Tanzania imebarikiwa kuwa na Bahari ya Hindi huku ikiwa na nchi tano za jirani zisizokuwa na bahari. Kwa maana hii, ina faida ya kijiografia kama kitovu cha usafirishaji wa kikanda. Ukizingatia ukuaji endelevu wa uchumi ulioshuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni na kuongezeka kwa kasi kwa shehena, changamoto ya msingi ni kusaidia kukuza mitandao ya barabara, reli na bandari kwa kanda kwa kutumia fursa ya jiografia ya Tanzania kikamilifu.

Misaada wa JICA katika sekta hii ilianza mnamo mwaka 1980 kwa ujenzi wa Daraja la Selander, ikifuatiwa na ukarabati wa barabara nyingi katika eneo la Kariakoo la Dar es Salaam na katika Wilaya ya Kati ya jiji hilo la kibiashara katika miaka ya 1990. Katika siku za hivi karibuni, barabara kama vile Kilwa, Ali Hassan na Kawawa  za jijini Dar es Salaam zilijengwa kwa msaada wa JICA. Hivi majuzi, JICA ilichangia katika   ujenzi wa Daraja la Juu la kwanza nchini Tanzania (Mfugale Flyover) kwenye makutano ya Tazara ambalo lilikamilika mnamo Septemba 2018. Kufuatia kukamilika kwa Daraja hilo la Juu, msongamano katika Makutano hayo (ambayo ni moja ya maeneo yenye shughuli nyingi zaidi nchini) umepunguzwa sana.

Muda wa kusafiri katika sehemu hii umepunguzwa sana; ni ahueni kwa wasafiri waliokuwa wakipata kizuizi/ugumu kwenda na kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA). Kwa kuongezea, eneo la ujenzi lilisimamiwa vizuri na mkandarasi na mshauri wa Kijapani. Mradi huo haukufanikiwa tu kuweka rekodi ya zaidi ya masaa milioni 2.5  bila ajali yeyote  lakini pia ulikamilishwa kama ilivyopangwa. Daraja hilo la juu (Flyover) ni ishara ya kudumu ya kumbukumbu ya ushirikiano na urafiki wa muda mrefu kati ya Tanzania na Japan. Miradi ya maendeleo ya mijini ambayo ipo katika hatua za utekelezaji ni pamoja na Mradi wa Upanuaji wa Barabara mpya ya Bagamoyo (Mwenge – Morocco)  na ujenzi wa mradi wa daraja la Gerezani jijini Dar es Salaam.

Ukuzaji uwezo wa uwezeshaji wa biashara katika Ukanda wa Afrika Mashariki

JICA Tanzania kwa kushirikiana na mamlaka za mapato tano (5) za nchi za Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda wamekuwa wakitumia mradi wa ushirikiano wa kiufundi unaojulikana kama "Mradi wa Kukuza Uwezo wa Uwezeshaji Biashara katika Afrika Mashariki" tangu 2017. Kusudi la mradi huu ni kuhakikisha utendaji kazi mzuri wa Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani "One-Stop- Border Post" (OSBPs) kwenye mipaka lengwa na kuboresha ujengaji uwezo wa shughuli za forodha katika udhibiti wa majanga /hatari na mipaka ndani ya Afrika Mashariki. Ili kuongeza uwezeshaji wa kibiashara ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki na zaidi, JICA ilichangia katika uanzishwaji wa OSBPs huko Rusumo kwenye mpaka wa Tanzania / Rwanda na Namanga kwenye mpaka wa Tanzania / Kenya. Kupitia vituo hivi vya OSBPs, muda wa uondoshaji mizigo katika mipaka hiyo umepungua sana. Kwa mfano huko Rusumo, muda wa uondoshaji wa mizigo umepunguzwa kwa takriban asilimia 73.

Mradi wa uboreshaji tija viwandani (KAIZEN)

Uboreshaji wa tija katika sekta ya uzalishaji ni moja ya shughuli kuu za JICA nchini Tanzania. Kutokana na ombi la Serikali, JICA ilianzisha Mradi wa Kuongeza Ubora na Uzalishaji Viwandani (KAIZEN) mnamo 2003. Hapo awali mradi huu ulishughulikia Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Morogoro. Kupitia mradi huu, kampuni zaidi ya 50 na zaidi ya watu 2000 walifundishwa kuhusu mkakati huo wa KAIZEN. Jambo hilo lilisababisha kuongezeka kwa tija sambamba na kuongezeka maradufu kwa uzalishaji na kampuni nyingine kumudu kupunguza kiwango cha uharibifu wa bidhaa  (defective rate) kwa asilimia 70.

Awamu ya 2 ya mradi huo itahusu Mikoa mingi zaidi na kampuni nyingi zaidi. Lengo la mwisho la mradi huu  ni kusambaza mbinu za mradi wa KAIZEN kwa kampuni 100 na kuzalisha wakufunzi 150 wa KAIZEN kote nchini. Wakati huo huo Kiwanda cha kutengeneza nguo kilichopo mkoani Arusha cha A to Z kiliibuka mshindi wa shindano la tuzo za KAIZEN za bara la Afrika. Kampuni hiyo iliyoko Arusha, ambayo inatumia mbinu ya KAIZEN katika shughuli zake, ilipewa tuzo hiyo katika shindano ambalo lilifanyika Tunis, Tunisia mnamo Juni 2019. Nchi nyingine ambazo zilishiriki katika mashindano hayo zilikuwa Tunisia, Kenya, Afrika Kusini, Ethiopia, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Namibia.

Programu ya Shahada ya Uzamili ya Mpango wa Elimu kwa  Afrika (ABE Initiative)

Mpango wa  ABE Initiative  ulianza mnamo 2014 kwa lengo la kuziba pengo/nafasi iliyopo baina ya Japan na Tanzania kupitia kuwajengea uwezo vijana wa Kiafrika. Kufikia sasa  vijana 85 wa Kitanzania wamefaidika na programu za shahada za uzamili zinazotolewa  katika Vyuo Vikuu vya Kijapani na mafunzo tarajali kutoka katika kampuni za kati za biashara za Kijapani huko Japan kupitia mpango huu. Wahitimu wa ABE wanatarajiwa kuchangia katika maendeleo ya viwanda nchini na kujenga mitandao na sekta binafsi ya Japan.

Kilimo

Katika kilimo, msaada wa JICA Tanzania  ulianza mnamo 1974 na "Mradi wa Maendeleo ya Kilimo Kilimanjaro". Hii ilifuatiwa na Mradi wa Umwagiliaji wa Moshi Chini  (Lower Moshi Irrigation Scheme) na Kituo cha Maendeleo ya Kilimanjaro na kwa sasa Kituo cha Mafunzo ya Kilimo Kilimanjaro (KATC). Tangu wakati huo, JICA imekuwa ikisaidia kilimo cha mpunga kupitia Mradi wa Maendeleo ya Sekta ya Mpunga (TANRICE 2) ambao sasa unahusisha Tanzania nzima.

Kupitia mradi huu zaidi ya wakulima 15,000 wamepatiwa mafunzo na kuanza kutumia teknolojia bora za kilimo cha mpunga. Zaidi ya hayo, wakulima ambao walishiriki katika mafunzo kama haya wameongeza mavuno yao ya mpunga kwa takriban asilimia 40. Katika miaka ya 2000, JICA ilipanua shughuli zake katika sekta ya kilimo kwa kuimarisha mfumo wa ukaguzi na utathmini wa Serikali (M&E). Hii ilisababisha maendeleo ya mfumo wa taarifa wa wavuti unaoitwa "Mfumo wa Takwimu za Kilimo (ARDS)". Mnamo mwaka 2017 zaidi ya 90% ya taarifa za  kilimo kote nchini zilisomwa na mfumo huo kila mwezi.

Mapema mwaka huu Mradi wa Uimarishaji wa Mipango na Uwezo wa Utekelezaji wa DADP kupitia Matumizi ya Njia ya SHEP (TANSHEP) ulianzishwa. Hii inakusudia kukuza sekta ndogo ya kilimo cha mbogamboga  inayolenga Mamlaka ya Serikali za Mitaa 12 katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga na katika maeneo mengine ya kipaumbele cha kilimo hicho kulingana na vipaumbele vya Serikali.  Madhumuni ya mradi huu ni kuwezesha Wilaya katika maeneo yaliyolengwa kuongeza kipato cha wakulima katika maeneo hayo kupitia njia ya "Kulima kwa ajili ya kuuza" na sio njia ya "Kulima na kuuza".

Ofisi ya JICA, Tanzania

Shughuli za Ofisi ya JICA Tanzania zilianza mnamo 1962, mwaka mmoja tu baada ya uhuru wa Tanganyika, wakati ambao ni Mtanzania mmoja tu alikubaliwa kujiunga na mafunzo ya ufundi huko Japan. Tangu wakati huo shughuli kama hizo ziliendelea kukua na kupanuka kwa miaka mingi na sasa hazijumuishi tu ushirikiano wa kiufundi lakini pia utoaji wa mikopo ya  masharti nafuu na misaada isiyokuwa na masharti ya kulipa (grant-aid).

Ili kufanya shughuli kama hizi, Ofisi ya JICA Tanzania imeajiri zaidi ya wafanyikazi 50 (wanaume kwa wanawake) ambao wanafanya kazi ili kuhakikisha kuwa shughuli za JICA nchini zinafanywa kwa ustadi kwa faida ya watu wa nchi zetu mbili za kirafiki za Tanzania na Japan.