Tanzania ilivyoandika historia Afrika na duniani


Tanzania ilivyoandika historia Afrika na duniani

Julai 26, 2019 Tanzania iliandika historia mpya kwa kufunga mjadala uliokuwa unaendelea ukihusisha athari za mazingira zinazoweza kutokea kutokana na ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115) Katika Eneo la Rufiji ambalo liko ndani ya Pori la Akiba la Selous, mkoani Pwani.

Julai 26, 2019 Tanzania iliandika historia mpya kwa kufunga mjadala uliokuwa unaendelea ukihusisha athari za mazingira zinazoweza kutokea kutokana na ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115) Katika Eneo la Rufiji ambalo liko ndani ya Pori la Akiba la Selous, mkoani Pwani.

Hata hivyo, kwa staili ya aina yake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli alishuhudiwa na mamia kwa maelfu ya Watanzania na wageni wa nje, akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo utakaogharimu Sh6.5 trilioni hadi kukamilika kwake.

Mjadala kuhusu mradi huo ulitokana na wanaharakati wa mazingira kueleza kuwa ujenzi wa bwawa hilo kwa ajili ya kuzalisha umeme ungehusisha ukatwaji mkubwa wa miti na hivyo kuharibu uasilia wa eneo hilo ambalo mwaka 1982 lilitambuliwa rasmi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Utamaduni (Unesco) kuwa ni urithi wa dunia kutokana na kuwa na viumbe tofauti na asili ambavyo havijabughudhiwa.

Lakini Rais Magufuli akihutubia Taifa na wananchi waliohudhuria hafla ya uwekaji wa jiwe hilo la msingi kwa ajili ya kuanza rasmi kazi ya ujenzi, alisema pori hilo linaongoza kwa ukubwa likifuatiwa na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Serengeti na hifadhi ya Burigi na ni kubwa kuliko nchi za Rwanda, Burundi, Uswisi na Uholanzi. Pori hilo lina ukubwa wa kilomita za mraba 50,000.

Anasema mradi wa ujenzi wa bwawa hilo ulianza kupigiwa chapuo na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, lakini ulipigwa vita karibu kila kona na hata baadhi ya wafadhili walitishia kuinyima Tanzania fedha za misaada.

“Kama mlivyosikia, mradi huu unakwenda kutekelezwa na fedha za Serikali ya Jamhuri kupitia kodi zenu ninyi wananchi wa Tanzania tunazokusanya,” amesema Rais Magufuli.

Nini azma ya mradi huo?

Akijibu hilo kupitia hotuba yake, Rais Magufuli anasema azma ya Serikali kwa sasa ni kutaka kuwatoa Watanzania hapa walipo na kuwapeleka katika uchumi wa kati ambao utategemea viwanda zaidi, hivyo kuna haja kubwa ya nchi kuwa na umeme wa uhakika na wa bei nafuu.

Hata hivyo, wajuzi wa mambo wanasema ujenzi wa mradi huo mkubwa wa kufua umeme wa maji wa MW 2,115 ni moja pia ya vielelezo vya kwamba, nchi za Afrika zinaweza kutekeleza miradi mikubwa kama hiyo zenyewe na hivyo jumuiya za kimataifa kutakiwa kuunga mkono juhudi za maendeleo barani humo.

Historia inaonyesha utafiti wa ujenzi wa mradi huo ulianza miaka 40 iliyopita.

Akizungumza na Mwananchi katika eneo la mradi, mkazi wa Kijiji cha Kisaki, Justin Lyasa (65) anasema akiwa na umri wa miaka 20, baba yake aligongwa na nyoka na kufariki dunia alipokuwa akifanya kazi ya kuwasindikiza wataalamu waliofika katika eneo hilo kufanya utafiti wa kujenga bwawa la umeme.

“Sherehe hii leo inanikumbusha mambo mengi, nilimpoteza baba yangu mzazi kwa kugongwa na nyoka kifutu. Yeye alikuwa anafanya kazi ya kibarua ya kubeba vifaa vya wataalamu wazungu waliokuwa wanakuja huku kupima ili wajenge bwawa la umeme.

“Enzi hizo eneo hili lilikuwa pori zito, wanyama wengi lakini wale jamaa walikuja na serikali ya kijiji ikatutangazia kuwa wanakuja kujenga bwawa kubwa sana litakalokuwa likizalisha umeme na sisi tutafaidika. Walikuwa wanakuja wanapima wanaondoka baadae tukaona kimya kabisa. Mwaka jana mwishoni tukaambiwa tena bwawa hili sasa linajengwa, hatukuamini tukasema ngoja tusubiri tuone, sasa leo tunaona Rais anaweka jiwe hili la msingi, hili ni jambo jema la kujivunia,” alisema Lyasa.

Safari rasmi ya ujenzi wa bwawa hili ilianza lini?

Ilikuwa Desemba 12, 2018, Rais Magufuli alitia saini na kampuni ya Arab Contractors ya Misri inayojenga mradi huo jijini Dar es Salaam, huku akisema mradi huo unakwenda kuboresha mazingira ya eneo hilo.

 

Anasema alitumia muda kutafakari kuhusu mradi huo kwa sababu Tanzania imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi vya uzalishaji umeme kama maji, gesi asilia, upepo, joto ardhi, makaa ya mawe na madini ya urani.

Ili kufikia uamuzi, anasema waliangalia vigezo vikubwa vinne ambavyo ni uhakika wa chanzo cha maji, gharama za utekelezaji, uzalishaji umeme, tija au manufaa yanayotarajiwa na mwisho wakagundua kuwa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115) Katika Eneo la Rufiji ndiyo unafaa zaidi kwa nyakati za sasa kwa Tanzania.

Waziri wa Nishati, Medard Kalemani aliliambia Mwananchi kuwa baada ya tafakari ya Serikali kuhusu chanzo kipya cha kuzalisha umeme wa maji ambao ni nafuu, walibaini maji ya Mto Rufiji  ni cha uhakika kwa sababu maji yake yanatoka katika mito inayotoa wastani wa mvua na kuna uwezo wa kuzalisha umeme kwa zaidi ya miaka 60 ijayo .

"Mradi huu utatumia fedha kidogo kuliko vyanzo vingine vya umeme, Uniti moja inayozalishwa na umeme wa maji ni Sh36 na huku umeme unaotengenezwa na nyuklia ni Sh 65 kwa uniti moja wakati umeme wa jua ni Sh103.05, upepo ni Sh103.05, makaa ya mawe Sh118, Gesi asilia Sh147 na mafuta ni Sh426 kwa uniti moja. Hivyo utofauti ni mkubwa sana kati ya maji na vyanzo vingine,” amesema Dk. Kalemani.

Hata hivyo, mradi huo umekuwa ukipingwa vikali na wanaharakati na mashirika ya mazingira ndani na nje ya Tanzania. Wanasema ujenzi huu unaweza kuleta madhara makubwa kwa viumbe hai pamoja na binadamu wanaoishi katika eneo hilo.

Mfuko wa Mazingira wa Kimataifa (WWF), umeshatoa ripoti inayoonyesha madhara ya kimazingira na uhifadhi wa mradi huo.

“Kuna matokeo makubwa zaidi ya mafuriko ya kilometa za mraba 1,200 za eneo linalohitajika na ujenzi wa bwawa hilo. Kutakuwa na ongezeko la mmomonyoko wa ardhi utakaosababisha kukauka kwa vyanzo vya maji yanayotegemewa na wanyamapori, hivyo kuathiri sekta ya utalii.

“Itapunguza rutuba katika ardhi na mazingira ya delta ya Rufiji na upatikanaji wa samaki aina ya kamba kochi na samaki wengineo wanaopatikana katika eneo hilo na hivyo kuathiri maisha ya wananchi wapatao 200,000 wanaoishi maeneo hayo,” imesema ripoti hiyo.

Hata hivyo, Dk Kalemani na Rais Magufuli wanasema mradi huo wa umeme utaleta manufaa makubwa kwa nchi tofauti na madai ya baadhi ya watu na mashirika ya nje kuwa utaharibu mazingira.

“Umeme wa maji ni rafiki wa mazingira na utapunguza ukataji wa miti na kutunza mazingira yetu na utaokoa miti inayokatwa kwa ajili ya kuni na mkaa kwa watu kutumia umeme...Tani milioni 2.3 za mkaa kwa mwaka zitatumia miti milioni 30 hivyo basi uwepo wa mradi huu utasaidia kupunguza ukataji wa miti.Hivi sasa kila siku kunavunwa hekta 583 ya miti kwa mwaka, eneo la Selou lina ukubwa wa hekta mil.5 hivyo kwa ukataji huu wa miti baada ya miaka kumi na tano tu, Selou inaweza kupotea.

“Mradi huu ni muhimu sana kutunza mazingira ya nchi yetu hivyo basi wapenda mazingira wote inabidi waunge mkono jambo hili. Uwepo wa umeme wa uhakika utasaidia watu wasikate miti na kutumia umeme,” amesema Dk. Kalemani.

Utofauti wa gharama za umeme katika mataifa mengine

Kwa sasa Tanzania inalipa Dola za Marekani senti 10.7 kwa uniti kiasi ambacho ni kikubwa tofauti na nchi nyingine huku Misri ikilipa Dola za Marekani senti 4.6, Korea ya Kusini na China ni ya Dola za Marekani senti8, Afrika Kusini Dola za Marekani senti 7.4, India Dola za Marekani senti 6.8, Ethiopia Dola za Marekani senti 2.4, Uingereza Dola za Marekani senti 0.15 na Marekani senti 0.12.

Bei ghali ya umeme inaelezewa kuwa inasababisha kuwepo pia kwa gharama kubwa kwa bidhaa za Tanzania kutokana na gharama kubwa za uzalishaji zinazochangiwa na bei hiyo.