Haya ndiyo manufaa ya Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115) kwa Taifa


Haya ndiyo manufaa ya Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115) kwa Taifa

Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115) katika eneo la Rufiji maarufu kama Stieglers Gorge, licha ya kutarajiwa kufua umeme wa MW 2,115 za umeme, pia utakuwa na faida lukuki.

Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115) katika eneo la Rufiji maarufu kama Stieglers Gorge, licha ya kutarajiwa kufua umeme wa MW 2,115 za umeme, pia utakuwa na faida lukuki.

Wakizungumza wakati wa kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi huo Desemba 12, mwaka jana Ikulu Jijini Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli alieleza kwa kina mradi huo una manufaa yake kwa Tanzania.

Mradi huo umetajwa kuwa ni wa manufaa makubwa kwa upande wa uchumi wa nchi, wananchi mmoja mmoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa ujumla.

Kwa upande wa uchumi wa nchi, mradi utawezesha nchi kuwa na umeme mwingi na unaokidhi mahitaji na kuvutia uwekezaji wa miradi mikubwa na ya kati ya uzalishaji mali.

Aidha, kwa upande wa wananchi, mradi huo unategemea kuchochea ukuaji wa huduma za kiuchumi na kijamii kwa ujumla kama vile afya, elimu, maji, pamoja na sekta muhimu ya viwanda na shughuli nyingine za kijamii zinazotegemea umeme.

Kwa TANESCO ambao ndiyo wasimamizi wa mradi kwa niaba ya Serikali, mradi utasaidia kuimarisha sekta ya uzalishaji umeme na hata kuongeza mapato ya shirika kwa kuuza umeme mwingi zaidi ukilinganisha na awali, na pia kupunguza gharama za uzalishaji umeme kwa sababu umeme wa maji ni wa gharama nafuu zaidi ikilinganishwa na vyanzo vingine vinavyotumika hivi sasa.

Katika hotuba yake wakati wa kushuhudia utilianaji saini wa ujenzi wa mradi huo, baina ya TANESCO na kampuni mbili kutoka Misri mwaka jana, Rais Magufuli alisema Serikali imefanya uchambuzi wa kina kabla ya kuamua kuutekeleza na kubaini kuwa utakuwa suluhu kwa mahitaji ya sasa ya nishati.

Kampuni ya Arab Contractors ikishirikiana na Elsewedy Electric zimepewa kandarasi ya kujenga mradi wa umeme katika Bonde la Mto Rufiji na kugharimu Dola 2.9 bilioni za Marekani sawa na zaidi ya Sh6.5 trilioni.

Rais Magufuli anasema waliangazia vyanzo vyote vya nishati vilivyopo nchini kama upepo, makaa ya mawe, madini ya urani, gesi asilia na mafuta na kulinganisha na mahitaji ya sasa ya nishati hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda.

“Baada ya kutafakari kwa kina hususan kwa kutumia vigezo vikubwa yaani uhakika wa chanzo chenyewe, gharama za utekelezaji, gharama za uzalishaji pamoja na tija tulibaini kuwa mradi huo ndiyo unaifaa zaidi nchi yetu kwa sasa,” alisema Rais Magufuli.

Alisema mradi huo ni wa uhakika kwa kuwa una uwezo wa kuzalisha umeme kwa zaidi ya miaka 60 na utatumia maji yanayotoka katika mtandao wa mito iliyopo kwenye mikoa yenye wastani mkubwa wa mvua.

“Gharama zake za utekelezaji siyo kubwa sana ukilinganisha na vyanzo vingine.” Kama nilivyosema mradi huu utagharimu Sh6.5 trilioni ukitumia vyanzo vingine kutekeleza mradi huu kuzalisha MW 2,115 tungetumia fedha nyingi sana,” alisisitiza.

Kuhusu gharama za kuzalisha, alisema uniti moja ya umeme wa maji ni Sh36 ukilinganisha na vyanzo vingine ambavyo ni ghali ikiwemo mafuta ambayo hugharimu Sh446 ikiwa ni mara 12 zaidi ya ule unaozalishwa kwa maji.

Kutokana na uwekezaji huo, amesisitiza uzalishaji wa umeme nchini utaongezeka zaidi kutoka uzalishaji wa sasa wa MW 1,560 na utakapokamilika bei ya umeme itapungua na kuwaletea wananchi unafuu wa upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa kuchochea shughuli za uchumi ikiwemo viwanda kilimo, umwagiliaji na michezo.

Mpango wa Serikali ni kufikia uzalishaji wa umeme wa MW 5,000 ifikapo mwaka 2020 na hatimaye MW 10,000 itakapofika 2025.

Rais Magufuli alitupilia mbali maoni ya wakosoaji wa mradi huo wanaouhusisha na uharibifu wa mazingira akieleza kuwa, “Umeme wa maji ni rafiki wa mazingira” na kwamba eneo litakalotumika kutekeleza mradi huo ni dogo kati ya asilimia 1.8 hadi asilimia 2 na eneo lote la Akiba la Selous.

Sambamba na hilo, utapunguza ukataji wa miti inayotumika katika vyanzo vya kuni na mkaa zaidi na wakazi wa mijini katika matumizi ya nyumbani.

Inakadiriwa kuwa watu laki sita hupoteza maisha kutokana na matumizi ya mkaa, kuni na mafuta ya taa, hivyo kukamilika kwa mradi huo utaokoa maisha ya wengi pamoja na uteketezaji wa miti.

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani aliyataja manufaa ya mradi huo ikiwamo kuifanya nchi kuwa na umeme wa uhakika na wa kutosha utakaosaidia maendeleo ya uchumi wa viwanda na maendeleo endelevu ya wananchi.

Mbali na hilo pia nchi itakuwa na maji ya uhakika kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao na ufugaji kwenye eneo lililo chini ya eneo la mradi na maporomoko ya Mto Rufiji.

“Kuboresha shughuli za utalii katika Pori la Akiba la Selous kwa kuwapo mazingira mazuri ya ustawi kwa wanyama pori kutokana na uhakika wa maji wakati wote wa bwawa litakalotokana na ujazo wa maji.

“Kuongeza mapato ya nchi kutokana na kustawi kwa shughuli za kitalii katika eneo la mradi. Kuvutia uwekezaji kwenye sekta ya viwanda na sekta mbalimbali za uchumi kutokana na uwepo wa umeme wa uhakika na wa bei nafuu hivyo kupunguza tatizo la ajira. “Kupunguza athari za mafuriko ya Mto Rufiji kwa wakazi waliopo maeneo ya Rufiji chini hadi delta ya Mto Rufiji na kuongeza pato la Taifa na lishe kutokana na mazao ya uvuvi,” alisema Dk. Kalemani.

Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115) katika eneo la Rufiji umelenga katika kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa gharama nafuu kwa Taifa kwa kuongeza chanzo kipya cha kufua umeme kwa njia ya maji katika Mto Rufiji.

Kupitia mradi huu, Tanzania itaongeza jumla ya MW 2,115 katika gridi ya Taifa, aidha, kupitia mradi huo Tanzania itakuza kiwango cha ufuaji umeme hivyo kukuza uwekezaji katika shughuli za kiuchumi na kibiashara kwa jamii na kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika, ambao utakuwa kichocheo cha nchi kufikia uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Kukuza na sekta ya uwekezaji katika kilimo kwa kuongeza viwango vya ubora wa mazao ya kilimo kwa kuyaongezea thamani kupitia viwanda, moja ya malengo makuu ya mradi ni kupunguza madhara ya mafuriko katika maeneo ya mashamba yaliyo katika Bonde la Mto Rufiji.

Pia, utaboresha kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la mto Rufiji kwa kutumia hifadhi ya maji yatakayokuwa yamekwishatumika katika kufua umeme.

Kuboresha sekta ya uvuvi katika Bonde la mto Rufiji hususan katika bwawa litakalojengwa ili kuhifadhi maji yatakayotumiwa katika kufua umeme.

Pia, faida nyingine za mradi huo ni kutoa ajira zaidi ya 10,000 na kusaidia kuzuia mafuriko.

Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115) katika eneo la Rufiji ni mradi mkubwa wa kwanza wa kufua umeme kusimamiwa na wazawa.