Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115) katika eneo la Rufiji hauna madhara


Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115) katika eneo la Rufiji hauna madhara

Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115) katika maporomoko ya Mto Rufiji yaliyoko katika eneo maarufu la Stiglers Gorge, uliwekwa jiwe la Msingi Julai 26, mwaka huu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.

Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115) katika maporomoko ya Mto Rufiji yaliyoko katika eneo maarufu la Stiglers Gorge, uliwekwa jiwe la Msingi Julai 26, mwaka huu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.

Mradi huo unajengwa mpakani mwa mikoa miwili ya Pwani na Morogoro katika Pori la Akiba la Selous.

Ni mradi ambao ulianzishwa na wazo lilitolewa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika miaka ya 1970, lakini utekelezaji wake haukuwezekana wakati huo kutokana na sababu kuu mbili.

Sababu hizo ni mahitaji ya umeme nchini yalikuwa madogo kiasi cha MW 100 na gharama za ujenzi kuwa kubwa ikilinganishwa na hali ya uchumi kwa wakati huo.

Hata hivyo, moja ya ahadi zake kwa Watanzania, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Magufuli, iliahidi wananchi kuwapatia umeme wa uhakika ili wafanye shughuli za kiuchumi kwa kuanzisha viwanda vikubwa, vya kati pamoja na vidogo na hivyo kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Serikali hiyo ya awamu ya tano iliweka vipaumbele katika kuboresha sekta ya nishati kwa lengo la kuwa na umeme wa uhakika na wenye ubora unaoweza kukuza uwekezaji wa viwanda na wa Taifa.

Ikumbukwe kuwa Serikali imeweka azma ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaojengwa kwa viwanda ifikapo mwaka 2025.

Na mojawapo ya nyenzo kuu ya kufikia uchumi huo ni upatikanaji wa umeme wa kutosha na uhakika wakati wote ili viwanda vilete ufanisi.

Hivyo, taratibu za uendelezaji wa mradi huo zilianza rasmi ilipofika Desemba 12, 2018 mikataba ya ujenzi wa mradi huo ilisainiwa kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na mkandarasi ambaye ni Kampuni ya Arab Contractors ikiwa ni JV na Elsewedy Electric, zote za Misri.

Tukio hilo lilishuhudiwa na Rais Magufuli na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Misri, Dk. Mostafa Madbouly katika Ikulu ya Dar es Salaam.

Baada ya mkataba taratibu nyingine zikafuatia na ujenzi ukaanza rasmi Juni 15, 2019 ambao unatarajia kukamilika ndani ya miaka mitatu ijayo.

Hata hivyo kumekuwa na maneno mengi kuhusu mradi huo mkubwa, ambao faida zake kwa Tanzania ni nyingi.

Licha ya maneno hayo, Rais Magufuli alisema Tanzania itatekeleza mradi huo kwa sababu umefanyiwa utafiti kitaalamu na hakuna tatizo lolote kimazingira katika kuendeleza mradi huo.

Akizungumza wakati wa uwekaji wa Jiwe la Msingi la mradi huo Julai 26, mwaka huu katika eneo la Mradi, Rais Magufuli alisema walitumia muda kutafakari kuhusu mradi huo kwa sababu Tanzania imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi sana vya uzalishaji umeme, kama vile gesi asilia, maji, upepo, joto ardhi, madini ya Urani na makaa ya mawe.

Alisema katika kufikia uamuzi huo, waliangalia vigezo vikubwa vinne ambavyo ni uhakika wa chanzo, gharama za utekelezaji, uzalishaji wa umeme na tija au manufaa yanayotarajiwa.

Alieleza kuwa mwisho waligundua kuwa mradi wa maji ya Rufiji ndiyo unaifaa zaidi Tanzania kwa muda huu; na sababu chanzo chake ni cha uhakika na maji yake yanatoka katika mito inayotoa wastani wa mvua.

Pia, kuna uwezo wa kuzalisha umeme kwa zaidi ya miaka 60 ijayo. “Mradi huu utatumia fedha kidogo kuliko vyanzo vingine vya umeme, uniti moja inayozalishwa na umeme wa maji ni Sh36 na huku umeme unaotengenezwa na nyuklia ni Sh65 kwa uniti moja wakati umeme wa jua ni Sh103.05, upepo ni Sh103.05, makaa ya mawe ni Sh118, gesi asilia ni Sh147 na mafuta ni Sh426 kwa uniti moja. Hivyo utofauti ni mkubwa sana kati ya maji na vyanzo vingine,” alisema Rais Magufuli.

Lakini siku chache kabla ya uwekaji wa jiwe la msingi, wataalamu wabobezi wa Tanzania wa masuala ya uhifadhi, mazingira na uchumi walizindua na ripoti yao ya utafiti wa kitaalamu kuhusu faida na madhara ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme wa Mto Rufiji.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa siku chache kabla ya uwekaji huo wa jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo unaotekelezwa na Kampuni inayomilikiwa na Serikali ya Misri, Arab Contractors kwa ubia na Elsewedy pia ya Misri, akizungumza wakati wa uzinduzi huo Jijini Dar es Salaam, kiongozi wa timu hiyo ya wataalamu, Saleh Pamba alisema utafiti wao ulilenga kuangalia madhara na faida za ujenzi wa mradi baada ya mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa kujitokeza hadharani kupinga azma ya Rais Magufuli, kuutekeleza mradi huo unaotarajiwa kuzalisha MW 2,115 za umeme na kuifanya Tanzania kujitosheleza na kuwa na ziada ya nishati hiyo.

Pamoja na Pamba, wataalamu wengine katika timu hiyo ni Abubakar Rajab, Abdulkarim Shah, Dk. Magnus Ngoile na Dk. Thomas Kashililah.

Pamba aliyataja mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyojitokeza kupinga mradi huo na kusambaza taarifa zake duniani kote zikieleza athari zitakazojitokeza iwapo utatekelezwa kuwa Shirika la Umoja wa Taifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyama Pori (WWF).

Alisema hoja za upinzani huo dhidi ya uamuzi wa Rais Magufuli zilizosambazwa duniani kote kwa njia ya maandishi kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kabla ya kubebwa na baadhi ya wapinzani wa maendeleo wa ndani ya Tanzania, zilianza kujenga taswira mbaya dhidi ya mradi wenyewe na Rais Magufuli aliyeapa kuutekeleza.

“UNESCO na WWF walitushtua sana baada ya kusoma maandiko yao yaliyokuwa yakipinga Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115) katika eneo la Rufiji, waliandika hoja nyingi zilizokuwa zikipinga uamuzi wa Rais kutekeleza ujenzi wa mradi huo wakitaka jumuiya za kimataifa kupaza sauti kwa pamoja ili usitekelezwe, sisi tulishtuka kwa sababu hizo hoja zao nyingine zilikuwa haziingii akilini lakini nyingine zilikuwa zinafikirisha,” alisema Pamba.

Aliongeza, “Tukaona kama wasomi wa Kitanzania ni wajibu wetu kujiridhisha ili kama kuna hizo hatari walizoziainisha tuishauri Serikali ifanye vinginevyo, tumefanya utafiti wa kina kweli kweli, tumegusa kila kipengele walichokipigia kelele, lakini sasa ajabu tulichokigundua ni kwamba, kelele zote za hawa wazungu ni uwongo mtupu.

Wanatishwa na kasi ya Rais Magufuli kuliletea maendeleo Taifa letu.

Kwa mujibu wake, haina shaka hata kidogo kuwa mataifa ya Magharibi yamejaribu kutumia kisingizio kuwa Pori la Akiba la Selous ambalo linatambulika kama eneo la urithi wa dunia na mahali unapojengwa mradi huo, Serikali imekusudia kupaharibu, lakini ukweli hofu kubwa ya magharibi ni kasi ya Tanzania kuelekea kwenye uchumi wa kati na kujitoa kwenye utegemezi wa mataifa hayo na taasisi zake za misaada.

Pamba aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Katibu Tawala wa Mkoa, alisema katika utafiti wao wamebaini kuwa eneo la Selous lililotumika kujenga mradi ni asilimia mbili tu ya kilometa za mraba 50,000, hivyo, sehemu kubwa ya hifadhi haitaguswa na kwamba hata eneo ambalo mradi unatekelezwa halitaathirika na uharibifu wa mazingira au kuhatarisha ustawi wa wanyama.

“Lakini sisi katika utafiti wetu tulibaini kuwa hawa jamaa ajenda yao ni kuhakikisha Tanzania haifikii malengo ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo 2025.

“Umeme wa Mto Rufiji utasaidia kukua haraka kwa sekta ya viwanda, madini, uendeshaji wa treni za kisasa za umeme, upatikanaji wa umeme vijijini na wafanyabiashara wadogo watakuwa na uhakika wa kupata umeme wa bei nafuu, uchumi wetu utapaa kwa kasi ya ajabu,” alisema Pamba.

Alisema, “Ripoti hii ambayo tunaitoa kwenu waandishi wa habari, nendeni mkaisome na mtakubaliana na sisi kuwa uamuzi wa ujenzi wa mradi huo ulifikiwa miaka ya 1960 na 1970 huko, lakini uamuzi wa kuifanya Selous kuwa eneo ka urithi wa dunia ulichukuliwa mwaka 1982.

Hizi taasisi za kimataifa zilikuwa na taarifa kuhusu uamuzi wetu huo.

“Sasa katika hoja zao za sasa wanasema ujenzi wa mradi huo utahatarisha hali ya usalama na utasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, siyo kweli hata kidogo.

Sisi tumebaini katika utafiti kuwa utekelezaji wa mradi utalinda mazingira na tumefafanua vizuri katika ripoti kuwa hali ya usalama itaimarika mno kwa sababu kutakuwa na ulinzi wa kutosha katika eneo zima la mradi, hivyo hata wawindaji haramu hawata sogelea huko.

“Hawa wazungu wanasema wakati wa utekelezaji wa mradi, kutakuwa na kelele na uchafuzi wa hela, hoja za kitoto kabisa kwa sababu sisi katika uchunguzi wetu, tumebaini kuwa kabla ya mradi kuanza kutekelezwa, hivi sasa kuna viwanja vya ndege vidogo, hizi airstrips 38 na kati ya hizo 33 zinafanya kazi kila uchao kusafirisha watalii, hapo hawaoni kelele hizo za ndege kupaa na kutua.

“Sasa utafiti hupingwa kwa utafiti, ripoti ya utafiti wetu tumeiweka mezani kama wao wana yao mpya ya utafiti wa kweli siyo ya kuchafua nchi au Rais, nao waiweke mezani.

Wapeni Watanzania ripoti yetu wajue kuwa mradi huu una manufaa makubwa kwa nchi yetu na hao wazungu lengo lao tusiutekeleze ili tuendelee kuwategemea wao.

“Kwetu sisi tunaiomba Serikali ichukue hatua madhubuti za ujenzi wa vyanzo vipya vya uzalishaji umeme wa uhakika ili iepuke kushindwa kufikia malengo ya kuwa Taifa lenye uchumi wa kati ifikapo 2025.”

Pia, Tanzania inapaswa kuwa na vyanzo vipya vya umeme wa uhakika ili kuepuka hatari ya maeneo ya misitu kugeuka jangwa na kuepuka athari ya mabadiliko ya tabia,” alisema Pamba.

Alisema kupatikana kwa umeme wa uhakika kutaepusha kuteketezwa kwa kilomita za mraba 412,000s za misitu kila mwaka kwa ajili ya shughuli za kibinadamu na hivyo kuongeza ustawi wa maeneo ya uoto wa asili na mapori mengi zaidi.