Serikali ya Awamu ya Tano inavyotimiza ndoto ya Mwalimu Nyerere


Serikali ya Awamu ya Tano inavyotimiza ndoto ya Mwalimu  Nyerere

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, imeanza kutimiza ndoto za Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere alizokuwa amezianza katika miaka ya 1970.

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, imeanza kutimiza ndoto za Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere alizokuwa amezianza katika miaka ya 1970.

Akiwa Rais wa Awamu ya Kwanza ya Tanzania, Mwalimu Nyerere alipania kujenga mradi mkubwa wa kufua umeme wa maji katika bonde la Mto Rufiji eneo la Stieglers Gorge (Hivi sasa unaitwa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115) Katika Eneo la Rufiji).

Mwaka 1976, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Norway ziliipa kazi ya kufanya upembuzi yakinifu Kampuni ya Norplan & Hafslund ya nchini Norway.

Kazi hiyo ilikamilika mwaka 1980. Upembuzi huo yakinifu uliangalia mradi mzima ambao ulihusisha uzalishaji wa umeme, kudhibiti mafuriko na kuendeleza kilimo katika ukanda wa chini wa bonde pamoja na kuendeleza shughuli za uvuvi na utalii.

Pia, kazi hiyo ilibainisha katika eneo hilo kuwa kunaweza kujengwa mradi wa kufua umeme wa Megawati 2,115, ambao ungetekelezwa katika awamu tatu ambazo ni moja uzalishaji wa megawati 400, awamu ya pili megawati 800 na awamu ya tatu megawati 900.

Kwa wakati huo, gharama za ujenzi wa mradi ziliainishwa kuwa ni Dola 1.380 za Marekani. Hata hivyo, mradi huo haukuweza kuendelea kwa sababu mahitaji ya umeme kwa kipindi hicho hayakuwa makubwa. Zilikuwa zikitumika MW 100.

Lakini pia gharama za ujenzi zilionekana kuwa kubwa ikilinganishwa na hali ya uchumi wa wakati huo ambao si sawa na wa sasa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, kwa sasa mahitaji ya umeme nchini yamekuwa yakiongezeka kwa kasi na hiyo inatokana na utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme vijijini ambayo inaendelea nchi nzima ambayo inasambazwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Alipoingia madarakani Novemba, 2015, Rais Dk. Magufuli alisema moja ya jambo analotamani kulitekeleza katika kipindi chake cha uongozi ni kuona Watanzania wote wanapata umeme wa uhakika kusudi lengo la kufikiwa kwa Tanzania ya viwanda litimie.

Alisema Tanzania ikiwa na umeme wa uhakika na wenye gharama nafuu, uhakika wa watu au wawekezaji kuanzisha viwanda vikubwa, vya kati na vidogo litatimia na hivyo kuongeza pato kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Rais Dk. Magufuli alisema azma ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaojengwa kwa viwanda ifikapo 2025 inawezekana kabisa. Na mojawapo ya nyenzo kubwa ya kuwezesha hilo kufanyika ni kwa nchi kuwa na umeme wa uhakika wa gharama nafuu.

Hivyo, utekelezaji wa azma hiyo ni kuanza kwa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115) katika mapromoko ya Mto Rufiji na miradi mingine inayoendelea nchini ambayo itawezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Hivyo, Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), iliamua kutekeleza mradi huu mkubwa wa kufua umeme kwa kutumia maji katika mapromoko hayo ya Mto Rufiji ambayo yapo katika Pori la Hifadhi ya Taifa ya Selous mpakani mwa mikoa ya Morogoro na Pwani eneo la Stiglers Gorge.

SAFARI YA UJENZI WA MRADI ILIVYOANZA

Ilikuwa Desemba 12, 2018, TANESCO wakishuhudiwa na Rais Magufuli na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Misri, Dk. Mostafa Madbouly ilitiliana saini na makandarasi wanaojenga mradi huo Kampuni ya Arab Contractors ya Misri na kampuni mbia ya Jv Elsewedy Electric, zote za Misri, Ikulu jijini Dar es Salaam.

TANESCO ilikabidhi rasmi eneo la mradi kwa makandarasi hao Februari 14, 2019 ambao wanatakiwa kuujenga kwa miezi 42 ambayo imegawanywa.

Miezi 36 ni ya ujenzi wa mradi mzima na miezi sita ni kwa ajili ya maandalizi.

Hata hivyo, tayari miezi sita ya maandalizi ilishakamilika na Julai 26, Rais Magufuli aliweka rasmi jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo ambao tayari umeshaanza kutekelezwa kwa kasi kubwa.

Miongoni mwa kazi zilizokwishatekelezwa kabla ya mradi kuanza ni pamoja na ujenzi wa miundombinu wezesheji ambayo ni umeme wa msongo wa Kilovoti 32, maji na mawasiliano ya simu.

Nyingine ni ujenzi wa barabara ya Kibiti – Mkongo – Mloka –Stiglers Gorge kwa kiwango cha changarawe na sehemu maalumu ya kushushia mizigo katika kituo cha treni ya Tazara Fuga.

Kazi nyingine ni ujenzi wa nyumba ya mitambo (power house) itakayokuwa na uwezo wa kuweka mashine sita zenye uwezo wa Megawati 235 kila moja hivyo kufanya uwezo wa kufua umeme wa mradi kuwa megawati 2,115, kituo cha kupoza na kukuza umeme cha kilovoti 400 kutoka eneo la mradi kwenda Chalinze na Kibiti ambazo zitaungwa kwenye mfumo wa umeme wa Gridi ya Taifa na daraja la kuvuka Mto Rufiji.

Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, kazi kuu za mradi huo zitahusisha ujenzi wa kuta za kuzuia maji (Dam) wenye urefu wa mita 1,025 na kimo cha mita 131, wenye matoleo ya maji kwa ajili ya matumizi ya eneo la chini ya bwawa na milango saba ya kutolea maji ya mafuriko.

Ujenzi wa kuta nne za kuzuia maji ya bwawa kutoroka, migodi minne, mmoja wa kuchepusha maji wakati wa ujenzi na mitatu ya kupeleka maji kwenye tabaini za maji, ujenzi wa daraja la kuvuka Mto Rufiji, ujenzi wa nyumba za mashine tisa zenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 235 na ujenzi wa njia mbili za kilovoti 400, RHPP – Chalinze kilometa 60 na RHHP –Kibiti kilometa 174.

Kazi nyingine ni ujenzi wa kituo cha kupoza na kukuza umeme cha msongo wa kilovoti 400 cha kuunganisha umeme wa maji wa Julius Nyerere (Mw 2115)  na Gridi ya Taifa na ujenzi wa nyumba za kudumu za wafanyakazi na barabara za ndani.

Bwawa litakuwa na uwezo wa kutunza maji lita 35.2 bilioni wakati wa mafuriko.

Wakati wa ujazo wake wa juu kufua umeme, bwawa litakuwa na eneo la kilometa za mraba 914 sawa na asilimia 1.8 ya eneo lote la Pori la Akiba la Selous lenye eneo la kilometa za mraba 50,000.

Kidakia maji cha mradi ina eneo la kilometa za mraba 158,420 likiwa na mikoa 10, wilaya 29 na mapori ya akiba matano.

Aidha mradi huu unahusisha ujenzi wa njia za umeme wa msongo wa Kilovoti 400 na msongo wa Kilovoti 220 pamoja na vituo vya kupoozea ukiwamo ujenzi wa njia ya umeme wenye urefu wa kilometa 162 ya msongo wa kilovoti 400, kutoka Rufiji hadi Chalinze.

Ujenzi wa njia ya umeme yenye urefu wa kilomita 181 ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Segera, ujenzi wa njia ya umeme yenye urefu wa kilometa 342 ya msongo wa Kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, na ujenzi wa njia ya umeme yenye urefu wa kilometa 162 ya msongo wa Kilovoti 220 kutoka Segera hadi Tanga.

Kwa mujibu wa utekelezaji wake, hadi sasa upembuzi yakinifu wa njia ya Msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma umekamilika.

Pia, hatua za manunuzi za kumpata Mhandisi mshauri kwa ajili ya kupata upembuzi yakinifu wa njia za umeme za msongo wa Kilovoti 400 kutoka Rufiji hadi Chalinze, Chalinze hadi Segera pamoja na njia za umeme za Msongo wa kilovoti 220 kutoka Segera hadi Tanga mjini zimeanza.

Ujenzi wa njia ya umeme unatarajiwa kuanza Februari, 2020 na kukamilika Desemba 2021.

Gharama za mradi huo mkubwa wa kufua umeme katika Mto Rufiji ni Sh6.558 trilioni. Fedha hizi zitalipwa na Watanzania wenyewe.

Na hadi sasa, Serikali imekwisha lipa mkandarasi jumla ya Sh983.7  bilioni ambayo ni sawa na asilimia 15 za gharama za mradi.

Hili litakuwa Bwawa kubwa la 60 duniani na la nne barani Afrika, likizidiwa na mabwawa yaliyopo Ethiopia (2) na moja la Nigeria huku Grand Renaissance (zaidi ya MW 6,000) linaloendelea kujengwa Ethiopia likiwa ndilo kubwa zaidi.

Akihutubia Taifa katika sherehe ya uwekaji wa jiwe hilo la msingi, Rais Dk. Magufuli alisema alitumia muda mrefu kutafakari kuhusu mradi huu, kwa sababu Tanzania imebarikiwa kuwa na vyanzo vingi vya uzalishaji umeme kama maji, gesi asilia, upepo, joto ardhi, makaa ya mawe na madini ya urani.

Lakini aliona huu wa kujenga Bwawa la Rufiji (Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115) Katika Eneo la Rufiji) unafaa zaidi kwa sababu unakwenda kuzalisha umeme wa maji ambao gharama zake ni nafuu zaidi.