Fursa na mikakati ya CRASA katika kukuza mtandao mkubwa wa mawasiliano SADC


Fursa na mikakati ya CRASA katika kukuza mtandao mkubwa wa mawasiliano SADC

Makubaliano ya nchi wanachama wa SADC ifikapo 2027, ni kuhakikisha huduma za intaneti ndani ya mtangamano huo zinafikia angalau asilimia 20 na simu za mkononi asilimia 80 hadi 90.

Tarehe 29 Machi, 2019 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi James M. Kilaba alianza kuongoza Umoja wa Mamlaka za Udhibiti wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA) unaolenga kuwa na ‘Jamii ya Kieletroniki’ ndani ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

CRASA inayo Katiba inayoiongoza katika utendaji wa majukumu yake. Aidha, CRASA kwa sasa ina nchi wanachama 13 kati ya 16 za Jumuiya ya SADC, ambao ni Angola, Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusi-ni, Eswatini, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.

Malengo makuu ya CRASA ni:-(i) Kuendeleza mfano wa kuigwa katika usi-mamizi wa TEHAMA na Posta na kuwezesha utekelezaji katika nchi wanachama;(ii) Kukuza na kuratibu utekelezaji wa Kanuni za TEHAMA na Posta, Viwango na uthibiti wa ubora wa vifaa vya mawasiliano ili kubore-sha uwekezaji wa biashara katika Jumuiya ya SADC; (iii) Kukuza uwezeshaji kwa nchi wanachama kushiriki katika sekta za TEHAMA na Posta pamoja na kuboresha ushawishi wa huduma kwa watunga Sera kitaifa na kikanda; (iv) Kubadilishana uzoefu na mawazo kuhusu maendeleo katika uthibiti wa sekta ya mawasiliano.

CRASA inao mfumo wa kujiendesha wenye Mkutano Mkuu (Annual General Meeting) ambao ndicho chombo cha juu cha maamuzi na chini yake ipo Kamati ya Utendaji (Executive Committee) inayoongozwa na Mwenyekiti, Makamu Wenyekiti wawili na Mweka Hazina.

Aidha, zipo pia Kamati Maalumu na Sekretariati. Kuanzia mwezi Machi, 2019 Tanzania kupitia TCRA ilipokea jukumu la kuongoza Kamati ya Utendaji (Executive Committee) ambayo inatekeleza maamuzi ya Mkutano Mkuu wa CRASA na maamuzi mengine ya SADC. Aidha, Kamati ya Utendaji kwa sasa inao Makamu Mwenyekiti wa kwanza, Zambia, Makamu Mwenyekiti wa pili Eswatini na Mweka Hazina, Botswana. CRASA inajiendesha kupitia Kamati mbalimbali na imejikita kwenye malengo kadhaa ikiwemo kuoanisha Kanuni, Sera kati-ka huduma za Posta na Teknolo-jia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) miongoni mwa nchi 16 wanachama wa jumuiya hiyo ili kuimarisha mazingira ya uwekezaji na biashara.

 Kwa mujibu wa CRASA, hadi sasa inatekeleza majukumu yake kwa kutumia Kamati zifuatazo:-(i) Kamati ya Mawasilia-no ya Kieletroniki ina jukumu la kuhakikisha kuwa, mawasiliano ya kielektroniki yanazidisha mchango wake katika uchumi wa Jumuiya ya SADC. Kamati inalo pia jukumu la kukuza Maendeleo sawa ya matumizi ya TEHAMA na kuweka msingi wa utafiti na Maendeleo ya Sekta ya Mawasiliano kwenye eneo lote la SADC. Kamati hii inaongozwa na Afrika Kusini na Tanzania ni Mjumbe. (ii) Kamati ya Mawasiliano ya Posta yenye jukumu la kuwezesha kuwepo mfumo wa pamoja wa kiudhibiti wa sekta ya Posta na kuhakikisha kwamba huduma za Posta zinatolewa kwa ubora wa hali ya juu na kwa bei nafuu kwenye Jumuiya ya SADC.

Kamati hii inaongozwa na Zimbabwe na Tanzania ni Makamu Mwe-nyekiti na Mjumbe.(iii) Kamati ya Masuala ya Walaji yenye lengo kubwa la kuunganisha utaratibu wa kutetea haki za wateja na utetezi wao. Aidha, Kamati inalo kusudi la kuhakikisha kwamba uhuru wa biashara katika sekta ya Mawasiliano na kuna fursa zinazotakiwa za uchaguzi kwa walaji katika eneo la SADC. Kamati hii inaongozwa na Mauritius na Tanzania ni Mjumbe.(iv) Kamati ya Rasilimali Watu imewekwa na jukumu la kusaidia nchi wanachama waweze kuwa na watumishi wanaojitosheleza kwa kuzingatia Maendeleo ya udhibiti wa TEHAMA na kusaidia Kamati ya Utendaji kutimiza majukumu yake yahusuyo watumishi wa CRASA. Kamati hii inaongozwa na Afrika Kusini na Tanzania ni Mjumbe.(v) Kamati ya Mawasiliano kwa Wote imewekwa kuhakikisha kwamba uhuru wa soko la Mawasiliano unaendana na ushirikiano wa kuwezesha huduma za Posta na kielektroniki zinawafikia wananchi walio wengi katika SADC.

Kamati hii inaongozwa na Lesotho na Tanzania ni mjumbe. (vi) Kamati na Sheria na Sera yenye lengo kuu la kutoa huduma za ushauri wa Kisheria na Kisera kwa Mkutano Mkuu wa Kamati zote za CRASA na mahusiano ya kimataifa, Kanda na ndani ya nchi wanachama. Kamati hii inaongozwa na Zambia na Tanzania ni Mjumbe. (vii) Kamati ya Fedha na Ukaguzi ina jukumu la kutathmini na kutoa mapendekezo kuhusu fedha na kuishauri Kamati ya Utendaji na Mkutano Mkuu wa CRASA. Aidha, Kamati inahakikisha kuwepo kwa utaratibu thabiti wa utawala bora na uthibiti wa ndani na usimamizi wa viashiria vya hatari. Kamati hii inaongozwa na Msumbiji na Tanzania ni Mjumbe kwa nafasi yake ya Mwenyekiti CRASA.

Utekelezaji wa majukumu ya CRASA chini ya Mwenyekiti wake Mhandisi Kilaba ni sehemu ya kusaidia utekelezaji wa malengo ya SADC kwa mwaka mmoja chini ya Mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo, Rais Mheshimiwa Dk John Pombe Joseph Magufuli aliyekabidhiwa kijiti Agosti 17, mwaka huu na Rais wa Namibia, Mheshimiwa Hage Geingob. Katika mahojiano maalumu na Mhandisi Kilaba ofisini kwake, anasema mawasiliano ni msingi unaochagiza ufanikishaji wa malengo na mikakati mbalimbali ya Jumuiya hiyo ikiwamo ukuaji wa shughuli za kibiashara kupitia mtandao wa taarifa za masoko kwa mawasiliano nafuu, ubora, uhakika na salama. “Ajenda ya kwanza nitakayoitetea ni nchi zote tuhakikishe huduma zinakwenda kieletroniki ndani ya SADC, hilo litafanikiwa kwa kuwa na ‘Smart Society’, na hili linafanikiwa baada ya kuwa na miundombinu yenye kasi ya mawasiliano (broadband), tuwe na njia inayosafirisha mzigo mkubwa wa mawimbi kwa kasi na ufanisi.

 

Hili ni eneo la kwanza na muhimu katika kutengeneza Smart Region ya SADC,” anas-ema Mhandisi Kilaba. Mhandisi Kilaba aliyechukua majukumu ya CRASA kutoka Eswatini anasema, harakati hizo zimeshaanza ndani ya TCRA kupitia uhamasishaji wa kui-marisha miundombinu hiyo kwa kila nchi mwanachama. “Ajenda ya pili tunayoifanyia kazi ni kuhakikisha usalama wa miundombinu hiyo ya mawasiliano ya broadband na watumiaji wake. Na jambo la tatu ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma kwa watu wa jumuiya hiyo kupitia miundombinu hiyo, sasa inabidi kila raia awe na simu janja ili apate huduma hiyo,” anasema Kilaba.

Aidha, nitakazania utekelezaji wa miradi mitatu ya kimkakati itakayoleta maendeleo ya haraka hasa katika kujenga uchumi wa viwanda katika nchi za SADC na hususan Tanzania:(i) Kuweka Viwango vya upigaji wa simu katika mzunguko (roaming) ndani ya nchi za SADC. Kwa sasa tumeona upo utofauti mkubwa sana wa tozo za utumiaji wa simu kwa wananchi wa SADC wanapokuwa wametembelea nchi zingine. Ni nia yetu kupunguza utofauti wa tozo hizi ili isiwe kikwazo kwa Mawasiliano kwa watu na wafanyabiashara wanapotembelea nchi zingine ndani ya SADC;(ii) Kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vya vifaa vya Mawasiliano hapa nchini kwetu; (iii) Kuweka Utaratibu wa pamoja wa Mwongozo na Viwango vya kusajili vifaa ya mawasiliano kwa matumizi ndani ya SADC ili kuondoa simu feki;(iv) Kusisitiza uanzishwaji na matumizi ya Anwani za Kitaifa na Postikodi ili kuongeza fursa za biashara kupitia mtandaoni kutoka nchi za SADC.Akitaja mikakati iliyopo katika utekelezaji wa majukumu ndani ya CRASA, Mhandisi Kilaba anasema kwanza ni kupunguza gharama za mawasiliano kwa wananchi wake kupitia tozo (Roaming Tariffs/charges), zinazotokana na huduma mbalimbali za ujumbe mfupi wa maneno, kupiga simu na kutumia data kwa njia ya simu janja.

“Mfano wewe ukitoka Tanzania hadi nchi nyingine ndani ya SADC ukiwa na simu na laini yako ya hapa Tanzania, changamoto unayoweza kukumbana nayo ni gharama za kutumia laini yako hiyo (roaming tariffs/charges) kuwa kubwa ukilinganisha na za nyumbani. Gharama hizi mara nyingine zinategemeana na mtandao wa huduma za kampuni ya simu unayotumia kwamba imefika nchi ngapi za SADC,” anasema.

“Kwa hiyo tunataka tuweke viwango vya tozo za pamoja unapokuwa nchi za SADC, tusiumizane pale Mtanzania akipiga simu ndani ya nchi au nje ya nchi yake.”Mhandisi Kilaba anasema viwango vya tozo za pamoja itakuwa ni ajenda mojawapo kupitia kikao cha Kamati ya Utendaji (Executive Committee) Agosti 30, 2019, kitakachofanyika Jijini Dar es Salaam. Anasema tayari vikao vya watalaamu vimeshafanyika na kutoa mapedekezo ya viwango hivyo. Kuhusu udhibiti wa simu feki chini ya CRASA, Mhandisi Kilaba anasema kila Mdhibiti ndani ya nchi mwanachama anawajibika kupitia vituo vya utambuzi wa IMEI za Simu za Mkononi (CEIR) kufuatilia ubora wa simu zinazoingia na kutumika nchini mwake.

Anasema mpango uliopo ni kuunganisha mtandao wa kusoma CEIR zote katika nchi za jumuiya hiyo ili kuthibiti wizi na ubora wa simu, na kwamba simu iliyofungiwa Tanzania haitatumika nchi zote za SADC. Kwa mujibu wa TCRA, Mfumo wa Kusimamia Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TTMS), umeambatanishwa na mfumo mdogo wa CEIR unaofuatilia utambuzi wa IMEI zote nchini Tanzania. Pia, TTMS inabadilis-hana takwimu za IMEI zote na kanzidata ya GSMA ambaye ni msimamizi wa IMEI zote za simu duniani. “Hata akibadilisha laini ya Voda, atumie Tigo hawezi. Ndiyo maana mtu akishuka na simu yake feki uwanja wa Ndege haitafanya kazi, akiweka laini simu inasema IMEI hii haipo, au ziko mbili, kwa hiyo tunataka kuthibiti simu feki ndani ya SADC,” anasema Kilaba.

“Tumeshaanza kujadili Machi mwaka huu, bado tuko katika mwendelezo wa majadiliano katika ratiba za mikutano ya CRASA, mkwamo unaweza kuwa mtazamo tu katika biashara. Mikakati iliyopo tunatakiwa kuiendeleza na kipindi cha uon-gozi ni mwaka mmoja tu ambao ni mfupi sana.Tutajitahidi kuwa na kasi.

Kasi ya Tanzania

CRASA tumekubaliana kutelekeza mipango hiyo, kwa mfano tunapokubaliana jambo fulani, tunaoanisha sera zetu ili kila mtu atekeleze katika nchi yake,” anasema Mhandisi Kilaba. Kwa Tanzania kila inapoingia makubaliano, huanza kutekele-za jambo hilo kwa wakati iki-wa ni sehemu ya kuchochea na kuhamasisha nchi nyingine kutekeleza kwa wakati ili kuwanufaisha wananchi wa SADC. “Kwa mfano, Tanzania imeshafikisha huduma za Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa katika kila mpaka wa nchi jirani ili kurahisisha uunganishaji wa huduma za data kwa ufanisi na gharama nafuu. Ingefaa kwa nchi ambazo bado kujiunganisha, wote wajiunganishe kuanzia Malawi, Zambia, Msumbiji, Burundi, Rwanda, Uganda, Kenya,”anasema Kilaba. “Hata roaming sisi tunao Mfumo wa Kusimamia na Kuratibu Mawasiliano ya Simu (TTMS), baadhi ya wenzetu nchi za SADC hawana. Tanzania tunaweza kujua watu wangapi wa nje wanapata huduma hizo wakiwa nchini.

Marejeo ya gharama hizo yanaweza kuwa na changamoto zake kimapato, mfano kama nchi inakusanya dola ya Kimarekani moja (1) kwa simu inayotoka, tukikubaliana ipungue hadi nusu dola maana yake itapunguza mapato ingawa muhimu inaweza kuwa ni kupunguza gharama kwa wananchi wetu wa SADC.”

Fursa za CRASA kwa Tanzania

Pamoja na kasi hiyo ya utekelezaji wa mikakati ya CRA-SA, Mhandisi Kilaba anabaini-sha fursa ambazo Watanzania na wawekezaji nchini wanaweza kutumia katika sekta ya mawasiliano inayohusisha soko la watu milioni 350 wa jumuiya hiyo. Mpango wa kidijitali wa SADC 2027, unatekelezwa na sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kupitia Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Miundombinu katika mtangamano (RIDMP), unaohu-sisha pia sekta za usafirishaji, nishati, vyanzo vya maji na hali ya hewa.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mawasiliano Duniani (International Telecommunication Union - ITU), za mwaka 2011, idadi ya watumiaji wa simu za mkononi nchi za SADC walikuwa ni asilimia 60 huku Intaneti ikiwa asilimia nne tu. Makubaliano ya nchi wanachama wa SADC ifikapo 2027, ni kuhakikisha huduma za intaneti ndani ya mtangamano huo zinafikia angalau asilimia 20 na simu za mkononi asilimia 80 hadi 90. Kwa takwimu za Disemba mwaka jana, makadirio ya huduma za simu za mkononi ilikuwa ni asilimia 72.2, huku Botswana, Namibia, Afrika Kusini, Seychelles na Mauritius zikiwa na asilimia 100. Mhandisi Kilaba anasema mahitaji ya simu janja ni makubwa ndani ya jumuiya hiyo na hakuna nchi yoyote yenye kiwanda mahsusi cha kuunganisha simu janja za mkononi.

“Sasa Mabalozi wa Tanzania walikuja katika Mkutano Mkuu wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali, nikawaambia watutafutie wawekezaji huko nje watakaokuja kuwekeza kiwanda cha kuunganisha simu janja Tanzania,”anasema.“Kwa sasa wote tunaagiza tu China na nchi zingine wakati Tanzania iko kwenye mazingira mazuri ya kuanzisha kiwanda hicho. Tuna mipaka ya nchi nane ikiwemo DRC, tunaweza kusambaza katika nchi nyingine zote kwa hiyo ni fursa tunayotakiwa kuichangamkia, inabidi tuanze hapa ndani kuhimiza matumizi ya simu janja.”Fursa nyingine inayoendelea katika mipango ya TCRA ni kuanzisha kiwanda cha kufanya matengenezo, kuchenjua madini yaliyopo katika taka za kielektroniki zikiwemo simu au kuziharibu ili kuepusha madhara kwa mazingira. “Simu zinapomaliza muda wake hatujui zinaenda wapi, lakini kuna madini ya dhahabu, shaba, silver, bati, Iridium, n.k kwa hiyo kuchenjua madini na kuuza bidhaa mpya, au kuziharibu taka zake ili kutengeneza bidhaa nyingine kama vile mabomba. Huu ni mpango katika fikra na tayari tumeshaanza muda kutafuta wawekezaji,” anasema Mhandisi Kilaba.

Fursa ya tatu ni kuandaa kiwanda kitakachokuwa kin-azalisha Radio za kidijitali kwa mahitaji ya nchi za SADC, ingawa si zote zimefanikiwa kuhama kutoka Mfumo wa Utangazaji wa Analojia Kwenda Dijitali.“Kwa upande wa TV tulishazima mfumo wa analojia, sasa tutazima mfumo sauti upande wa Radio ingawaje itachukua muda mrefu. Hadi sasa hakuna nchi yenye kiwanda cha kuzalisha Radio za kidijitali, kwa hiyo ni fursa, Tanzania itakuwa mhudumiaji wa soko la nchi zote za SADC, tulishawaambia mabalozi pia watutafutie wawekezaji,” anasema Mhandisi Kilaba. “Kwa kumalizia, ningependa kutoa pongenzi nyingi kwa nchi yetu chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Rais Dk John Pombe Joseph Magufuli kwa kuonyesha umahiri wa hali ya juu kuongoza Mkutano wa wakuu wa nchi za SADC. Sisi tunaongoza taasisi zilizo chini ya SADC hatuna mashaka kwamba tuna uongozi imara wa jumuiya hii na kwa hivyo tunaahidi kutoa mchango wetu mkubwa kuhakikisha ajenda zilizopo zinatekelezwa kikamilifu.”