Siku ya bima ina umuhimu mkubwa katika kuongeza uelewa kwa wananchi


Siku ya bima ina umuhimu mkubwa katika kuongeza uelewa kwa wananchi

Maadhimisho ya siku ya bima hufanyika kila ifikapo mwezi Septemba ya kila mwaka. Maadhimisho haya yalianza kuadhimishwa miaka 21 iliyopita na mwaka huu yanatimiza mwaka wa 22.

Bima ni mpango unaotoa fidia endapo janga litatokea kwa mkata bima. Fidia hiyo hutolewa kutoka kwenye michango ya wakata bima wanaounda umoja wa kukabiliana na majanga.

Bima imegawanyika katika makundi mawili ambayo ni: bima za maisha ambazo ni bima za muda mrefu zaidi ya mwaka mmoja na kuendelea pamoja na bima za kawaida ambazo ni za muda mfupi ambazo ni mikataba ya mwaka mmoja.

Kwa kutambua umuhimu wa bima katika maisha ya Watanzania, Taasisi ya Bima Tanzania ikijumuisha wanachama wake ambao ni makampuni ya bima, madalali, mawakala, wakadiriaji wa hasara, Mamlaka ya Bima Tanzania pamoja na Kampuni ya Bima Mtawanyo Tanzania, iliamua kuwa kila ifikapo mwezi Septemba kila mwaka kuwepo na maadhimisho ya Bima ili kutoa elimu pamoja na kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu masuala yote yanayohusiana na bima.

Siku ya bima mwaka huu inafanyika kitaifa mkoani Mwanza. Rais wa Taasisi ya Bima Tanzania (IIT), Bosco Bugali ambaye ni mmoja ya waandaaji wa maadhimisho hayo anaeleza historia ya siku ya bima pamoja na lengo la kuanzishwa kwake.

Historia ya maadhimisho ya siku ya bima nchini

Maadhimisho ya siku ya bima hufanyika kila ifikapo mwezi Septemba ya kila mwaka. Maadhimisho haya yalianza kuadhimishwa miaka 21 iliyopita na mwaka huu yanatimiza mwaka wa 22.

Ni yapi malengo makuu ya kuanzishwa kwa maadhimisho haya?

Malengo makuu ya kuanzishwa kwa maadhimisho haya ni kuwakutanisha kwa pamoja wadau wote wa bima ili kufanya tathimini ya mambo waliyofanya kwa mwaka mzima.

Katika maadhimisho haya wataalamu mbambali wa masuala ya bima hualikwa kutoka ndani na nje ya nchi ili kuweza kuwasilisha mada zinazohusu maendeleo ya bima pamoja na maendeleo ya sekta ya bima kitaifa.

Je, kwa kiasi gani malengo haya yamefikiwa?

Kwa kweli malengo ya kuanzishwa kwa maadhimisho haya yameweza kufikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na mwamko uliosababisha kuongezeka kwa utoaji wa huduma za bima hapa nchini.

Tumeweza kutanua wigo wa maadhimisho kwa kuyatoa nje ya Mkoa wa Dar es Salaam na kwenda nje, tualianzia Tanga na sasa tupo Mwanza.

Ni mafanikio gani yamepatikana kutokana na maadhimisho haya toka yalipoanza?

Kumekuwa na mafanikio makubwa, tumeweza kushiriki katika shughuli za afya kwa ajili ya jamii, tumekuwa tukichangia katika shughuli mbalimbali za kijamii kama vile elimu, afya na miundombinu.

Je, mapokeo kwa jamii yako vipi?

Mapokeo kwa jamii ni mazuri. Watu wengi wamekuwa wakijitokeza kushuhudia maonyesho haya. Pia, kampuni mbalimbali za bima, mawakala pamoja na madalali wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kwa lengo la kutoa elimu pamoja na huduma za bima kwa wananchi.

Kwa mwaka huu baadhi ya makampuni ya benki na makampuni mengine ambayo hayafanyi shughuli za bima yameshiriki katika maonyesho ambayo yapo katika viwanja vya Rock City Mall.

Jamii ina uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa maadhimisho haya?

Jamii haina uelewa sana wa maadhimisho haya. Tunachukua hatua za makusudi ili ujumbe tunao utoa uweze kufika kwa walengwa kwa kutumia madalali wa bima pamoja na wakala ambao baada ya kupata hamasa kutoka kwenye maadhimisho haya huenda sehemu mbalimbali za nchi yetu kusamba-za elimu kwa jamii kuhusu bima.

Je, IIT inashirikiana vipi na wadau katika kuboresha maadhimisho haya?

IIT katika kuboresha maadhimisho haya inawashirikisha wadau kwa kuwaalika kuja kushiriki, wadau hawa wanatoka kwenye mashirika na taasisi mbalimbali zinazotoa huduma kwa jamii hapa nchini ili waje kuwaelimisha wadau wa bima shughuli wanazozifanya kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na taifa.

Jitihada gani ambazo mnazifanya ili kuhakikisha sekta ya bima inakua na kukidhi mahitaji ya soko?

Ili kulifanikisha hili, Taasisi ya bima Tanzania tunatoa mafunzo ya bima kwa wadau wetu. Walimu wanaotumika wanatoka ndani ya kampuni za bima, ni wazoefu na wamebobea katika masuala ya bima.

Pia, tunafanya mawasiliano na kampuni za bima za kimataifa ili kuendesha kozi ambazo bado ni ngeni katika soko letu kama vile bima ya gesi na mafuta, bima ya kilimo na nyinginezo. Ili kuweza kukidhi mahitaji ya soko tunahitaji kufanya uchunguzi kuhusu bima zinazokidhi mahitaji ya jamii. Tumeanzisha kitengo cha kushughulikia mafunzo na uchunguzi wa bima.

IIT mnaliona wapi soko la bima hapa nchini katika kipindi cha miaka 10 ijayo?

Katika kipindi cha miaka 10 ijayo tunaliona soko la bima kuwa litakuwa na uwezo wa kufikisha mchango wa pato la taifa (GDP) 5%. Litakuwa ni soko ambalo wananchi watakuwa na uelewa mpana kuhusiana na huduma zake kwa kuwa kutakuwa na bima nyingi ambazo zitakuwa ni kwa mujibu wa sheria kama ilivyo kwa bima za magari. Wakulima wataweza kunufaika zaidi na bima za kilimo na mifugo.

Upatikanaji na ukataji wa bima utakuwa ni rahisi kwa kuwa mitandao itatumika zaidi na hata wateja watashauriwa mambo ya bima na kulipa ada ya bima kwa mtandao. Usambazaji wa bima utaongezewa wigo, bima itauzwa kupitia vituo vya mafuta, supermarket n.k.

Ni changamoto gani zinaikabili sekta ya bima nchini na mnafanya juhudi gani kuzipunguza kama sio kuzimaliza kabisa?

Changamoto zinazoikabili sekta ya bima ni jamii kutoifahamu bima vizuri. Ili kutatua changamoto hii, IIT tunaendelea kutoa elimu ya bima kwa jamii pia makampuni ya bima yanatoa matangazo mbalimbali ya bima.

Changamoto nyingine ni baadhi ya wateja wa bima kupeleka madai ya udanganyifu na baadhi ya makampuni hayalipi madai kwa wakati hivyo wananchi huvunjika moyo wa kukata bima.

Nini malengo mapana ya IIT?

Malengo mapana ya IIT ni kuwa taasisi ambayo itategemewa kwa kuzalisha wataalam wa bima (professionals). Imeaandaa mitaala ambayo itaanza kutumika mwakani kwa kutoa mitihani hapa hapa nchini badala ya sasa ambapo Watazania wamekuwa wakifanya mitihani kupitia taasisi za nje kama vile Uingereza, India, Australia n.k. ambako gharama zipo juu sana. Tutazalisha wataalam wengi kwa gharama nafuu na hawa watashiriki katika kuisaidia Serikali kufanya utafiti wa kupata bima mpya mbalimbali ambazo zitakuza soko la bima.