Mambo yanayoweza kukupotezea haki ya kulipwa fidia ya bima


Mambo yanayoweza kukupotezea haki ya kulipwa fidia ya bima

Bima katika dunia ya leo imekuwa ni jambo la msingi sana hususan katika mazingira tunayoishi kwa mashaka na hali ya kutokufahamu nini kitakachotokea kesho.

Bima katika dunia ya leo imekuwa ni jambo la msingi sana hususan katika mazingira tunayoishi kwa mashaka na hali ya kutokufahamu nini kitakachotokea kesho.

Hakuna mwenye uhakika wa usalama dhidi ya majanga yasiyotarajiwa yanayoweza kutokea muda wowote, yawe aidha ya asili au yale yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu.

Tumekuwa mashahidi namna watu binafsi na makampuni mbalimbali yanavyojibiidisha katika kukata bima za mahitaji yao, hii ni ishara nzuri kwani bima inaendelea kuongezeka thamani.

Bima ni bidhaa ya kipekee, inayouzwa tofauti na bidhaa nyingine yoyote. Ikumbukwe bima ni makubaliano ya kisheria yanayoingiwa baina ya pande mbili (kampuni ya bima na mkat-aji bima).

Kile ambacho watu wanashindwa kuelewa ni kwamba haki ya kulipwa fidia baada ya kukumbwa na janga hufanyika pale tu mkataji bima anapotimiza majukumu yake.

Na mbaya zaidi, asilimia kubwa ya wakataji bima (wanunuzi wa bima) hawafahamu sababu ambazo zinaweza kumpotezea haki za kulipwa fidia hata kama alikuwa na bima hapo mwanzoni.

Gazeti la Mwananchi limefanya mazungumzo na baadhi ya wataalam wa masuala ya bima kuhusiana na sababu ambazo zinaweza kukupotezea haki za kulipwa fidia.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Insurance Broker, Arthur Mosha anasema kuwa, “Labda, nikueleze bima ni mkataba wa kisheria, moja ya kipengele cha msingi ni kile kinachoweka wazi kuwa hakutakuwa na malipo ya fidia kwa watu watakaojihusisha na wizi au uhalifu. Endapo ingetokea ajali na watu kuumia au kufariki, hiyo ingehesabika ni tukio halali la kufidiwa na gari lingefidiwa na watu wote waliopata ajali.

“Ajali ya moto Morogoro ni mfano mzuri wa jambo hili, kiten-do cha watu kwenda kuiba mafuta na betri ni kosa na moja kwa moja inapoteza haki ya msingi ya majeruhi na marehemu kufidiwa hata kama walinunua bima hapo mwanzoni.

Hivyo watu waliokuwa wanatakiwa kulipwa fidia ni wale ambao moto uliwafuata katika maeneo yao na hawakuhusika na wizi wa mafuta ingawa ni vigumu si rahisi kuweza kuthibitisha nani alikwenda kuchota mafuta na akaungua, na nani alibaki kwake moto ukamfuata na akaungua?

Kwa upande wa mali, wapo miongoni mwa wale waliojumuika na wenzao kwenda kuiba mafuta kweye lori ambao walikuja na pikipiki zao na kuziacha pembeni au umbali fulani kuto-ka eneo la tukio, na kwa bahati mbaya zimeungua pikipiki zile, kampuni ya bima inaweza kulipa fidia ya pikipiki zile zilizoungua, “ anafafanua Mosha. Mosha anaendelea kutaja mambo mengine,

“Mbali na wizi, ukijiua hauwezi kulipwa fidia. Makampuni mengi ya bima hulipa fidia vitu vitatu vinavyofafanua dhana ya ajali; tukio lisilotarajiwa, tukio halisi (kama ajali ionekane kweli imetokea) na hali ya ughafla. Kujiua mwenyewe ni dhahiri, si miongoni mwa matukio yanayotokea kwa ghafla, kwa hivyo hakuna fidia itakayolipwa.

Hii pia ni pamoja na vitendo vya kukata mikono au miguu, kugonga magari yako kwa makusudi, kuchoma moto nyum-ba na vitendo vingi ambavyo vimeanzishwa kufanywa kwa hiari.”

Kwa upande wa Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu wa Kampuni ya Bima ya Sanlam, Charles Mbaga naye hakuwa mbali na kile alichokisema mzungumzaji aliyepita, “Hii ni moja ya mada nzuri kuwahi kuletwa mbele yangu. Nina uhakika mkubwa sana kutokana na uzoefu wangu, wanunuzi wa bima wengi hawana ufahamu kuhusiana na wajibu na haki zao, katika maana ya mambo yanayoweza kupoteza haki zao za kulipwa fidia.

Yawezekana watu hawafahamu kuwa, wizi ni kosa kubwa na halina fidia.Hata ukirejelea mazingira ya ajali ya kule Msamvu, Morogoro, bima ya maisha ingewafaa sana majeruhi na marehemu kwa sababu bima hii ingeweza kulipa fidia kwa ndugu wa marehemu na kugharamia matibabu kwa maje-ruhi mbalimbali.

Mbaga anasema kuwa, “Pia, walihitaji bima ya vyombo vya moto ambayo ingesaidia kufidia gari lililoungua na baadhi ya pikipiki zilizoteketea na moto ule. Lori lililopinduka kama lingekuwa limekatiwa bima lingefidiwa kutokana na kupata ajali, lakini changamoto ni wale watu ambao waliamua kwenda kuiba mafuta na kusababisha mlipuko, hawawezi kufidiwa hata kama wangekata bima kwa sababu wamevunja sheria kwa kwenda kuiba mali za mmiliki wa lori.”

Kila mmoja wetu ana jukumu kubwa kuhakikisha analinda usalama wake na wa mwenzake kwa kadri anavyoweza. Serikali, nayo kwa kushirikiana na sekta binafsi itengeneze sera, sheria na miongozo mbalimbali itakayoweza kumhakikishia kila Mtanzania anakata bima ambayo ni kinga dhidi ya majanga yasiyotarajiwa.

Kwa upande wa makampuni ya bima, yana jukumu kubwa la kuhakikisha yanawaelimisha wateja wao mara kwa mara kuhu-siana na haki na wajibu mbalimbali wanaotakiwa kuutimiza.

Wito kwa wakataji bima nchini ni kuhakikisha kuwa wanaelewa masharti ya mkataba, kuridhia wakati wanahisi wako tayari, kutimiza wajibu wao ipasavyo ili kujiepusha na matendo yatakay-opoteza haki zao za kulipwa fidia.