TaCRI yatoa aina zinazovumilia ukame kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi


TaCRI yatoa aina zinazovumilia ukame kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Jukumu kubwa la TaCRI ni kuhakikisha inaendeleza na kueneza matokeo ya utafiti ili kuinua tija na ubora wa kahawa nchini.

Jukumu kubwa la TaCRI ni kuhakikisha inaendeleza na kueneza matokeo ya utafiti ili kuinua tija na ubora wa kahawa nchini.

Baada ya kutoa aina 19 za Arabika zenye ukinzani kwa magonjwa sugu ya chulebuni - ugonjwa unaoozesha matunda ya kahawa, na kutu ya majani ambazo ni: N39-1, N39-2, N39-3, N39-4, N39-5, N39-6, N39-7, N39-8, N39-9, N39-10, N39-11, N39-12, KP423-1, KP423-2, KP423-3, TaCRI IF, TaCRI 3F, TaCRI 4F na TaC-RI 6F; pia aina nne za kahawa zenye ukinzani kwa ugonjwa wa mnyauko fuzari: Maruku1, Maruku2, Bukoba1 na Muleba1.

Kutokana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, TaCRI imefanya utafiti kubaini iwapo miongoni mwa aina 19 za Arabika zina uwezo wa kuvumilia athari za ukame.

Jopo la watafiti likiongozwa na Dk Damian Mtenga limefanyia utafiti aina tisa (9) miongoni mwao zikiwemo aina saba (7) ambazo zilishaidhinishwa rasmi na aina mbili mpya katika majaribio yaliyofanyika katika Wilaya za Rombo, Tarime, Buhigwe na Mbozi.

Utafiti katika sehemu hizo ume-fanyika katika kuangalia uwezekano wa upungufu wa mavuno, mwonjo na athari za magonjwa sugu za chulebuni na kutu ya majani. Utafiti huo ulianza mwaka 2013. Kati ya ana hizo saba: N39-3, N39-10 na TaCRI 3F zimeonyesha uwezo mkubwa wa uvumilivu wa ukame.

Katika hali ya kawaida aina hizi huwe-za kutoa mavuno kati ya tani 2 hadi 3 za kahawa safi kwa hektari. Katika hali ya ukame zilionyesha upungufu wa mavuno kati ya asilimia 17 – 22.

Kwa upande wa mwonjo aina hizi zilipata daraja la wastani la alama 5+ ambalo hukubalika na soko la ndani na nje ya nchi. Mkakati uliopo kwa sasa ni kuhakikisha kwamba miche ya kahawa ya aina hizi inazalishwa kwa wingi ili kukidhi mahitaji ya upandaji wa kahawa katika maeneo ya zamani na mapya.

Inakadiriwa kwamba Tanzania ina jumla ya hektari 235,000 zinazostawisha kahawa kwa sasa. Maeneo yanayofaa kwa kilimo cha kahawa yanakadiriwa kuwa zaidi ya hektari 275,000.

Iwapo maeneo haya yote yataoteshwa miche aina bora za kahawa, Tanzania inaweza kuzalisha takriban tani 275,000 (kadirio la tani moja ya kahawa safi kwa hektari kama itatunzwa vizuri) za kahawa safi kwa msimu.

Hii itakuwa ni mara 5.5 ya kahawa inayozalishwa kwa sasa. Mtafiti Suzuna Mbwambo ambaye ni Mkuu wa Programu ya Kanuni Bora za Kahawa anashauri kwamba ili kuweza kuzalisha kahawa zaidi ya tani moja kwa hektari ni muhimu kuzingatia yafuatayo: Ujazo wa mibuni ya kutosha kwa hektari.

kwa mfano kwa mibuni ya Arabika aina fupi inapotumika; nafasi kati ya mstari hadi mstari ya mita 2 inapotumika na mbuni hadi mbuni mita 1.5 ndani ya mstari, husababisha ujazo wa mibuni 3330 kwa hektari sawa na mibuni 1,332 kwa ekari moja.

Aina ndefu za Arabika nafasi ya mita 2.5 kwa mita 2 hupelekea ujazo wa mibuni 2000 kwa hektari, sawa na mibuni 800 kwa ekari. Kwa upande wa kahawa ya Robusta nafasi ya mita 3 kwa mita 2.5 hupelekea ujazo wa mibuni 1333 kwa hektari sawa na mibuni 533 kwa Ekari.

 Pia, mibuni hiyo inapaswa kuwa na matawi yanayozaa (primary branches) kati ya 35-40, na pingili zenye matunda katika tawi zisizopungua 18. Mkulima anapaswa kuhakikisha anatumia samadi wakati wa kupanda miche, na mbolea za viwandani miche inapokua ili kusababisha maua ya kutosha yatakayotoa matunda.

Kwa vile aina hizi za kahawa hazina uwezo wa ukinzani kwa wadudu waharibifu wa kahawa, udhibiti unatakiwa kutumia mbinu shirikishi. Mtafiti uchumi jamii, Leonard Kiwelu anawahakikishia wakulima iwapo watafuata kanuni hizi bei zilizopo za kahawa zinalipa.

Katika usambazaji wa matokeo ya utafiti, TaCRI imeunda mtandao imara wa wakulima viungo 200 hivi wanaosaidia shughuli za ugani.

Mkuu wa Programu ya Usambazaji wa Matokeo ya Utafiti anaongezea mbinu nyingine za matokeo ya utafiti kuwa ni mafunzo kupitia vikundi, mafunzo kwa vitendo kupitia vituo vidogo vya utafiti vilivyoko katika kanda: Tarime (Mara), Maruku (Kagera, Geita na Mwanza), Mwayaya (Kigoma), Mbimba (Songwe, Mbeya, Rukwa na Katavi), Ugano (Ruvuma, Iringa na Njombe), na Lyamungu (Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Morogoro).

Pia, maonyesho ya siku ya wakulima nane nane ni msaada mkubwa sana wa kusambaza matokeo ya utafiti wa kahawa. Programu hii pia hujihusisha na uzalishaji wa miche ya kahawa amba-po katika msimu huu wa 2018/19 ilizalishwa miche 7,284,735 ambapo lengo lilikuwa kuzalisha miche 8,358,074.

Ndani ya miche milioni 7.3 iliyozalishwa zipo pia aina zinazovumilia ukame N39-3, N39-10 na TaCRI 3F. Miche hii ikifuatiliwa na kutunzwa vizuri itaweza kuchangia si chini ya tani 7.3 ya kahawa safi baada ya miaka 3-4 toka sasa.

Ili kukamilisha mchakato wa utafiti wa aina zinzovumilia ukame, TaCRI imeshawasiliana na Taasisi inayohusika na udhibiti wa mbegu, hatua inayofuata itakuwa kutathmini aina mpya kabisa zilizopo katika majaribio, zifanyiwe tathmini ya Ubainishi (Distinct-ness); Ufanani (Uniformity) na Uthabiti (Stability).

Aina hizi zikithibishwa sifa zinazostahili, zitapendekezwa katika Kamati Maalum ya Kuidhinisha Mbegu iliyoko Wizara ya Kilimo.

Mkurgenzi Mkuu Mtend-aji wa Taasisi, Dk Deusdedit Kilambo anatoa wito kwa wadau kutumia matokeo ya utafiti wa kahawa toka TaCRI ndiyo njia pekee ya kuleta mapinduzi ya kilimo cha kahawa nchini Tanzania.

Ofisa Mtendaji Mkuu

Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI)

Lyamungu,

P.O. Box 3004, Moshi,

TANZANIA.

Simu: 0754 377 181Simu: + 255-27-2756868/759

Barua pepe: [email protected]

Tovuti: www.tacri.or.tz