Mikakati ya EWURA katika kuboresha utoaji wa huduma za nishati na maji nchini

Muktasari:

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ni moja ya Mamlaka za Udhibiti nchini ambayo ilianzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ya mwaka 2001 (Sura ya 414 ya Sheria za Tanzania) pamoja na majukumu mengine, kupewa majukumu chini ya Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 (Sura ya 392 ya Sheria za Tanzania) kudhibiti shughuli za mkondo wa kati na wa chini wa petroli (yaani mafuta na gesi asilia) katika Tanzania Bara.

Maendeleo ya kiuchumi kitaifa ni mchakato wa mabadiliko ya kiuchumi, kutoka chini kwenda juu ambao unatokana na ushiriki wa moja kwa moja wa wananchi kwa kushirikiana na Serikali pamoja na taasisi za watu binafsi kwa kufanya kazi kwa bidii, ikiwemo kutumia fursa za kiuchumi zilizopo kwa wakati husika.

Maendeleo ya kiuchumi katika nchi huletwa na mambo mengi, lakini kubwa zaidi ni watu kufanya kazi kwa bidii pamoja na taasisi za kimaendeleo zikiwemo za Serikali na zisizo za Serikali kuwawezesha wananchi kutambua na kuzitumia vizuri fursa za kiuchumi zilizopo kwenye maeneo yao.

Moja ya taasisi za Serikali ambazo zinachangia katika kuleta maendeleo hapa nchini ni Mamlaka za usimamizi ambazo zimepewa jukumu la kusimamia na kuratibu shughuli zote za kiuchumi na kijamii ili kuhakikisha Serikali kupitia mamlaka hizo, huduma zake zinawafikia moja kwa moja wananchi.

Mamlaka hizi zinahusika moja kwa moja katika kuleta maendeleo ya kiuchumi, kutokana na kusimamia na kuratibu shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii ikiwemo kudhibiti, kutoa leseni, kupanga bei, ukusanyaji wa mapato, uratibu wa mawasiliano, afya, utalii, usafiri pamoja na huduma nyingine za kijamii. Hapa nazungumzia Mamlaka kama EWURA, ambazo zimepewa jukumu kama hilo.

EWURA ni nini?

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ni moja ya Mamlaka za Udhibiti nchini ambayo ilianzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ya mwaka 2001 (Sura ya 414 ya Sheria za Tanzania) pamoja na majukumu mengine, kupewa majukumu chini ya Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 (Sura ya 392 ya Sheria za Tanzania) kudhibiti shughuli za mkondo wa kati na wa chini wa petroli (yaani mafuta na gesi asilia) katika Tanzania Bara.

Shughuli hizo ni kusafisha au kuchakata mafuta ghafi au gesi asilia, kusafirisha, kusambaza na kuuza bidhaa ya mafuta na gesi asilia nchini.

Majukumu makubwa ya Mamlaka hii ni kutoa leseni za uendeshaji wa shughuli za nishati na maji hapa nchini, mapitio ya ushuru, utendaji wa ufuatiliaji wa viwango, ubora, usalama, afya na mazingira.

EWURA pia ina wajibu wa kukuza na kuendeleza ushindani wenye tija kiuchumi, kulinda maslahi ya walaji pamoja na kuendeleza upatikanaji wa huduma zilizowekwa kwa watumiaji wote ikiwa ni pamoja na kipato cha chini, watumiaji wa vijijini na wasiostahili katika sekta zilizosimamiwa.

Pia, EWURA inadhibiti shughuli za gesi asilia zinazojumuisha usindikaji, usafirishaji, uhifadhi na usambazaji. Miundombinu ya gesi asilia kama mitambo ya kusindika gesi, mabomba ya upitishaji na usambazaji, pia vinadhibitiwa na mamlaka na mamlaka inaendesha uchunguzi kwenye maeneo husika ambako shughuli hizo zinaendeshwa.

Katika kutekeleza majukumu haya, EWURA inajitahidi kuboresha ustawi wa jamii ya Tanzania kwa:

·       Kukuza ushindani mzuri na ufanisi wa uchumi,

·       Kulinda maslahi ya watumiaji (walaji),

·       Kulinda uwezo wa kifedha wa wasambazaji wenye ufanisi,

·       Kukuza upatikanaji wa huduma zilizodhibitiwa kwa watumiaji wote pamoja na wenye vipato vya chini, watumiaji wa vijijini na wanyonge,

·       Kuzingatia umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira,

·       Kuongeza uelewa kwa umma, uhamasishaji na uelewa wa sekta za usimamizi.

Kabla ya kuanzishwa kwa EWURA, taasisi kama Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira na kampuni zinazojishughulisha na biashara ya mafuta, zilikuwa zikipanga bei ama kwa utashi au kutokana na hali ya bei katika soko la dunia.

Kutokana na kukosekana kwa udhibiti, bei za huduma kwa rejareja kama mafuta, zilipanda kiholela. Hatua hiyo iliwaumiza watumiaji na wakati huo huo wafanyabiashara walikuwa wakitumia mwanya huo kuwakandamiza wateja.

Lakini baada ya kuanzishwa kwa EWURA kupitia sheria ya Bunge, watumiaji wa bidhaa husika walianza kupata unafuu na upangaji holela wa bei za mafuta, gesi, maji na umeme ukaanza kupungua na sasa imekuwa historia.

Kuanzishwa kwa EWURA kuliwezesha taasisi zote kuheshimu sheria, kanuni na taratibu pamoja na kufuata hatua mbalimbali ikiwamo kushirikisha wadau, hususan watumiaji wa bidhaa husika kama vile umeme na maji.

Kwa sasa, ikiwa mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira, Tanesco au kampuni binafsi ya kuzalisha umeme inataka kupandisha bei ni lazima ipitie hatua mbalimbali.

Miongoni mwa hatua hizo ni kuwasilisha maombi EWURA, kufanya mikutano na wadau ili kuwashirikisha juu ya nia ya kurekebisha gharama ya huduma husika na wadau kutoa maoni yao kama ya kupinga au kukubali. Pia taasisi husika ni lazima ieleze sababu za kusudio la kurekebisha bei.

Katika kufuata hatua hizo, Tanesco imeshuhudiwa ikianzisha mchakato wa kutaka kupandisha bei za umeme kwa wateja wake. Shirika hilo lilifuata taratibu zote ikiwamo kufanya mikutano na wadau kupitia Baraza ya Walaji (Watumiaji) wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA-CCC).

Mikutano hiyo iliyofanyika maeneo mbalimbali nchini, ilitoa fursa kwa watumiaji wa huduma hiyo kupinga nia ya kupandisha bei ya umeme. Kwa mantiki hiyo, taasisi inapotaka kupandisha bei ni lazima ihusishe wadau ili nao watoe maoni yao kabla ya hatua zaidi kufuata ili kutimiza lengo lililokusudiwa.     

Hata bei za mafuta, kutokana na udhibiti makini wa EWURA, zimekuwa zikitangazwa kila mwezi huku zikionyesha wakati mwingine kupanda pamoja na kushuka kulingana na sababu mbalimbali kama vile bei katika soko la dunia, kodi mbalimbali na umbali kutoka bandarini ambako mafuta hutolewa hadi kwenye eneo la soko (mikoani au wilayani).

Aidha, kuwapo kwa udhibiti huo wa bei za mafuta, kumesaidia kuwapunguzia mzigo wananchi wanaotumia mafuta kwa shughuli mbalimbali pamoja na kuwabana wafanyabiashara waliokuwa wakifanya njama za kupanga bei kwa utashi wao, hivyo kuwaumiza wateja (watumiaji wa mafuta).

Sambamba na hilo, kuwapo kwa EWURA kumesababisha wafanyabiashara waliokuwa wakigoma kuuza mafuta wakisubiri mafuta yaadimike ndipo wapandishe bei, kutofanya hivyo pamoja na hatua kadhaa kuchukuliwa dhidi ya wenye tabia kama hizo.

EWURA ina nafasi kubwa katika kuleta maendeleo hapa nchini kwa mfano, kwa utoaji wa bei kikomo kwenye mafuta, Watanzania wanapata nafuu kwa bidhaa ukilinganisha na kablaya uwepo wa EWURA. Kwa hiyo fedha iliyobaki inatumika kwenye matumizi mengine ya kimaendeleo.

Ubora wa bidhaa na huduma zinazodhibitiwa na mamlaka hii kama vile maji na nishati, huchangia kwa kiasi kikubwa kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kuwa Watanzania hutumia bidhaa na kupata huduma bora na za uhakika.

EWURA katika mapambano dhidi ya soko holela la mafuta, udhibti wa ubora wa mafuta ya petroli na udhibiti wa gesi asilia

Mapambano dhidi ya soko holela la mafuta

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeendelea na mapambano ya udhibiti wa uuzwaji holela wa bidhaa za mafuta aina ya petroli, kwa wanaofanya biashara hiyo kinyume cha sheria.

Meneja wa Ufundi Kitengo cha Mafuta EWURA, Mhandisi Shabani Suleiman anasema EWURA haitavumilia wanaofanya biashara ya mafuta katika vituo bubu na maeneo mengine yasiyoruhusiwa. “Kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na adhabu yake ni kulipa faini kiasi kisichozidi milioni tano au kifungo cha miaka mitatu jela,” alisema.

Aidha, EWURA imepania kuendelea kudhibiti mkondo wa chini wa sekta ya petroli kwa kuhakikisha inaondoa mianya yote ya wizi, ili watumiaji wa bidhaa hizo wapate huduma iliyobora, kulinda afya pamoja na mazingira kwa maendeleo.

Katika muendelezo wa jitihada hizi za kupambana na soko holela la mafuta, EWURA, imeviadhibu zaidi ya vituo 30 vya mafuta kwa kufanya biashara bila leseni ya EWURA, kujengwa bila vibali na kutokidhi viwango vya ubora vya utoaji huduma ya mafuta.

EWURA imechukua hatua hiyo baada ya kubaini kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa masharti ya uendeshaji wa vituo hivyo, kupitia ukaguzi uliofanywa kati ya mwezi Januari na Februari 2019, katika maeneo mbalimbali nchini.

EWURA hufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika vituo vya mafuta ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi viwango vya ubora, kulinda afya na kuzingatia usalama wa afya na mazingira ya Watanzania.

Katika ukaguzi huo, EWURA ilibaini vituo saba (7) vilivyokuwa vinauza mafuta yasiyo na vinasaba katika maeneo ya Tunduru, Nachingwea, Momba, Rombo, Siha, Ubungo na Kinondoni.

Uuzaji wa mafuta yasiyo na vinasaba ni mwanya wa ukwepaji kodi na ni uhujumu uchumi wa nchi, hivyo EWURA imekuwa ikisimamia suala hili kwa umakini mkubwa.

Udhibiti wa ubora wa mafuta ya petroli

Moja ya majukumu ya msingi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ni kuhakikisha wafanyabiashara ya mafuta wanafuata sheria, kanuni na kukidhi viwango vya ubora katika utoaji huduma za mafuta nchini.

Sheria ya EWURA na Sheria ya Petroli zinaipa EWURA mamlaka ya kudhibiti masuala ya kiufundi, kiuchumi na kiusalama katika sekta ya petroli.

EWURA husimamia wauzaji wa jumla na rejereja wa mafuta ili kuhakikisha wanatoa huduma yenye ubora na viwango vinavyostahili na kwa gharama ambayo watumia huduma hiyo wanaimudu.

EWURA pia ina jukumu la kuhakikisha kuwa mafuta yanayotumika nchini yanakidhi viwango vya ubora kama vilivyoanishwa na Shirika la Viwango (TBS) kabla mafuta yalipokelewa kutoka nje ya nchi hayajaingia katika matumizi.

Wafanyabishara ya mafuta nao wana wajibu wa kuhakikisha kuwa bidhaa zao wakati wote zinazingatia vigezo na masharti yaliyowekwa. EWURA hufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa vituo vya mafuta, maghala ya kuhifadhia mafuta na katika magari ya kusafirishia mafuta ili kujiridhisha endapo uendeshaji wa biashara ya mafuta, unazingatia masuala muhimu ya kiufundi na kiusalama.

Ukaguzi huo pia huhusisha kujiridhisha kuwa taratibu za kisheria na kanuni za uendeshaji biashara zinafuatwa kikamilifu. Mamlaka huchukua sampuli za mafuta ili kujiridhisha endapo bidhaa za mafuta zilizo sokoni zinakidhi viwango vya ubora na ni salama kwa matumizi.

Hii inafanyika kwa kupima wingi wa vinasaba katika mafuta ya soko la ndani ili kujiridhisha kuwa hakuna uchakachuaji, udanganyifu au ukwepaji wa kodi za Serikali. Unapobainika ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za kiufundi na kiusalama katika uendeshaji wa biashara ya mafuta, EWURA huchukua hatua kali dhidi ya mhusika.

Hatua hizo zinaweza kuwa faini, kifungo au vyote. EWURA hufanya ufuatiliaji kwa umakini wa hali ya juu wa uendeshaji wa biashara ya mafuta nchini kwa lengo la kuhakikisha huduma inayotolewa inamlinda mtumia huduma dhidi ya madhara ya kiafya, kiusalama na kimazingira.

Ubunifu wa vituo vya Mafuta kuhudumia vijijini

Ili kupunguza changamoto za upatikanaji wa huduma za mafuta kwa Watanzania walioko maeneo ya vijijini, EWURA imebuni vituo vya mafuta jongefu ili kuondokana na uuzaji wa mafuta ya petroli katika mazingira hatarishi, bila kuzingatia vigezo na ubora wa bidhaa hiyo.

EWURA imekuja na mkakati huu mpya wa vituo jongefu, ambavyo vitakuwa maeneo ya vijijini na vitatumia magari maalumu, zikiwamo pikipiki za miguu mitatu, zitakazotengenezwa kwa kazi hiyo, ili kuhakikisha kuwa mafuta yanapatikana vijijini tena katika hali ya usalama.

Mpango huo unalenga kurahisisha upatikanaji wa mafuta katika maeneo mbalimbali nchini hususani vijijini kwa kuwa kujenga vituo vikubwa ni gharama, hivyo njia hii ya vituo jongefu ni bora na itakuwa rahisi kuwafikia wateja walio wengi.

Nishati ya mafuta inatakiwa kuuzwa kwa utaratibu unaokubalika hivyo, EWURA imeamua kuja na mpango wa kuanzisha vituo vya mafuta tembezi hasa vijijini ili kupunguza gharama za kujenga vituo katika maeneo mbalimbali na kukidhi mahitaji ya mafuta kutokana na kushamiri kwa usafiri wa pikipiki maarufu kama bodaboda.

EWURA inawakaribisha wafanyabiashara wenye nia ya kuwekeza katika biashara ya mafuta lakini wana mitaji midogo, kujitokeza katika mpango huo ili kuimarisha upatikanaji wa nishati ya mafuta vijijini ambao umekuwa mgumu kutokana na changamoto ya miundombinu ya barabara hususani kipindi cha mvua.

Udhibiti wa gesi asilia

EWURA inatambuliwa kuwa mdhibiti huru katika mkondo wa kati na chini (kuchakata, kusafirisha, kusambaza na biashara) ya gesi asilia na mafuta. Katika sekta ya gesi asilia, EWURA inazidhibiti taasisi zinazohusika na kuchakata, kusafirisha, kusambaza na kufanya biashara ya gesi asilia.

Taasisi hizi ni Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Pan African Energy Tanzania (PAET), Songas Tanzania na Maurel et Prom.

Kwa mujibu wa Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano EWURA, Titus Kaguo kampuni hizi huomba na kupatiwa leseni mbalimbali na EWURA, ambayo hufuatilia uendelezaji wa miundombinu (mitambo ya kuchakata, mabomba na maghala ya kuhifadhi) gesi asilia, utendaji na kupitisha maombi ya tozo na bei za gesi asilia kwa wateja wa mwisho.

Ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na shughuli za gesi asilia kwa wananchi wa maeneo husika na kuwaacha maskini, Serikali ilipitisha sera ya Nishati (2015) kuwa gesi ya Tanzania ni mali ya Watanzania wote, na itatumika kwa manufaa ya Watanzania wote.

Hivyo EWURA imejipanga vyema kulinda maslahi ya Watanzania, ili athari zinazoweza kujitokeza kutokana na shughuli za gesi asilia, ikiwamo uchakataji na usambazaji zisisababishe madhara kwa wananchi wanaozunguka.

Katika kufanikisha hilo, elimu ya vyuo vikuu imekuwa ikitolewa bure kwa wazawa wenye sifa ili kuongeza wataalam kwenye kada ya gesi asilia, na taarifa za utekelezaji zinasambazwa kila mara miongoni mwa wadau. Akizungumzia Sheria ya Mafuta (2015), Kaguo alisema inataka wazawa washirikishwe katika masuala yote ya gesi asilia na watayarishwe vizuri ili waajiriwe katika shughuli za gesi asilia, pamoja na uwekezaji katika shughuli saidizi kama huduma za chakula, hoteli, bima na nyinginezo.

Sheria pia inatoa masharti kwa kampuni zote za kigeni zinazojihusisha na shughuli za gesi asilia kununua bidhaa za hapa nchini ambapo TPDC, EWURA na PURA zimepewa jukumu la kufuatilia.

Sekta ya gesi asilia imekuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa hasa katika kipindi hiki cha ujenzi wa uchumi wa viwanda, ambapo kwa kiasi kikubwa huhitaji nishati za gesi na umeme kama mhimili muhimu wa sekta hiyo.

Jinsi ya kuwasilisha maombi ya kuwekwa kwenye kanzidata ya Watanzania wenye uwezo wa kuuza bidhaa au kutoa huduma (LSSP) kwenye shughuli za mafuta na gesi asilia nchini

Kanuni ya 38 ya Kanuni za Petroli (Ushiriki wa Watanzania) za mwaka 2017 huitaka EWURA kukusanya, kutunza na kila mwaka kutangaza kwenye kanzidata (database) ya Watanzania wenye uwezo wa kuuza au kutoa huduma (LSSP) kwenye shughuli za petroli, ambayo huzuia taasisi, asasi, kuuza bidhaa, kujenga au kutoa huduma kwenye shughuli za petroli (petroleum activities) labda atokane na kanzidata inayotunzwa na EWURA au Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA).

Kwa mujibu wa Kanuni za Petroli (Ushiriki wa Watanzania) za mwaka 2017 shughuli za petroli zinazohitaji ushiriki wa Watanzania ni uuzaji wa bidhaa mbalimbali, utoaji wa malazi, uuzaji wa vyakula na vinywaji, utoaji wa huduma za usafiri na usafirishaji, upokeaji na utumaji wa mizigo, utoaji wa huduma za matibabu, za ulinzi, za kisheria, za bima, za benki na ajira.

Sheria inataka wazabuni wote kuwa na ushiriki wa Watanzania usiopungua asilimia 25 ya hisa au vinginevyo. Kanzidata ya LSSP itatayarishwa kutokana na taarifa zitakazopatikana kutoka kwenye maombi ya Watanzania na kuchujwa kwa kutumia Utaratibu wa Kuwianisha Viwango vya Ubora (Common Qualification Systems, (CQS). Hadi sasa Kampuni zilizosajiliwa ni Zaidi ya 400 na EWURA inaendelea na shughuli hiyo angalau kufikia kampuni 1,000.

Miradi iliyopo kwenye Mkondo wa Kati na wa Chini wa Petroli

Kanuni za Petroli (Ushiriki wa Watanzania) za mwaka 2017 zilianza kutumika rasmi tarehe 5 Novermba 2017. Shughuli za Petroli za kwanza ni Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (nchini Uganda) hadi Tanga (nchini Tanzania) utakaotekelezwa na Kampuni ya Bomba la Mafuta Ghafi ya Afrika Mashariki (yaani the East African Crude Oil Pipeline (EACOP).

Shabaha ya Mchakato wa Kanzidata ya LSSP

Shabaha ya mchakato wa ushiriki wa Watanzania ni kuhimiza ongezeko la thamani na ajira hapa nchini kupitia wataalam wa ndani, bidhaa na huduma, biashara, kazi na kuwezesha uwekezaji katika shughuli za petroli ambapo fedha nyingi zaidi zitabaki nchini Tanzania. Uwezo wa ndani wa kutoa huduma kwenye shughuli za petroli kupitia kutoa elimu, kuandaa wataalam, kufanya tafiti kuhusu jinsi ya kupata maarifa mapya.

Ili kuongeza uwezo wa Watanzania na kuruhusu ushindani wa kimataifa katika shughuli za ndani; itabidi kuwezesha kukua kwa shughuli za petrol ili zichangie kukua kwa uchumi, na kuweka taratibu za wazi za kufuatilia na kutoa taarifa husika.

Fomu N-100

Fomu N-100 hutumika kukusanya taarifa mbalimbali kutoka kwa waombaji wa usajili kwenye Kanzidata ya Watanzania wenye uwezo wa kushiriki na kutoa huduma (LSSP) kwenye shughuli za Petroli, ambazo hujazwa, mara nyingi, na Watanzania. Sheria zimeipatia majukumu EWURA, ya kuanzisha na kila mwaka kuuwisha, na kutangaza Kanzidata ya LSSP.

Siku zote, EWURA inazuia mtoa huduma au taasisi yoyote kutokuuza bidhaa au kutoa huduma kwenye shughuli za petroli hadi kwanza asajiliwe kwenye Kanzidata ya LSSP. Maelekezo ya jinsi ya kujaza Form N-100 yanapatikana kwenye tovuti ya EWURA www.ewura.go.tz.

Mahitaji ya Msingi

Mwananchi yeyote mwenye sifa ya kuitwa Mtanzania na kufanya kazi kwenye shughuli za petroli au shughuli zozote zinazosaidia biashara ya petroli anaweza kuomba kusajiliwa kwenye Kanzidata ya Watanzania wenye uwezo wa kutoa huduma kwenye shughuli za petroli (LSSP).

Mahitaji ya msingi ni yafuatayo;

(a) Awe na umri usiopungua miaka kumi na minane (18) siku ya kujaza Fomu N-100,

(b) Awe mkazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi kinachokubalika,

(c) Aishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo awe na makazi kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu (3) kabla ya kujaza Fomu N-100,

(d) Athibitishe kuishi mfululizo kwa kipindi kinachokubalika,

(e) Athibitishe kuwa anayo maadili, sifa na mwenendo mwema,

(f) Athibitishe kuwa ana elimu na ufahamu wa shughuli za petroli au shughuli nyinginezo zinazosaidia biashara ya petroli; na

(g) Ataapishwa kiapo cha uaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ushahidi utakaohitajika

Ikumbukwe, waombaji wa usajili kwenye Kanzidata ya LSSP atatakiwa kuwasilisha EWURA Fomu N-100 na taarifa zifuatazo kwa njia ya kielektroniki;

(a) Uthibitisho kuwa mwombaji wa usajili kwenye Kanzidata ya LSSP ili kuuza bidhaa mbalimbali au kutoa huduma kwenye shughuli za Petroli ni Mtanzania, ikiwa ni pamoja na Hati ya Usajili wa Kampuni nchini Tanzania,

(b) Hati kuwa ni mlipa kodi (Tax Clearance Certificate) inayotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania au mamlaka yenye hadhi sawa kwa makampuni yenye usajili wa nje ya Tanzania,

(c) Hati ya usajili kwenye mabaraza ya taaluma (Certificate of Professional Registration) zinazotolewa na Engineers Registration Board (ERB), Contractors Registration Board (CRB), Tanzania Law Society (TLS), Tanzania Insurance Regulatory Authority (TIRA), Bank of Tanzania (BOT) au asasi nyingine ya usajili wa taaluma,

(d) Hati ya Hifadhi ya Jamii (National Social Security Clearance Certificate) inayotolewa na NSSF au Mifuko ya Hifadhi mingine kwa kampuni zilizosajiliwa Tanzania au Mifuko ya Nje kama NSSF kwa kampuni za nje zinazofanya kazi Tanzania,

(e) Barua ya utambulisho wa benki inayokufahamu na kutoa huduma za fedha kwako,

(f) Uthibitisho wa upeo wa shughuli zako na maelezo ya ubobezi wako katika shughuli za petroli, ukiwemo uwezo wako (wataalam, mashine, na mitambo) au miundombinu mingine inayohusika; na

(g) Kitambulisho cha uraia wako wa Tanzania au maelezo yanayoambatana na ukurasa wa mwisho wa hati ya kusafiria (a valid passport) kwa wasio Watanzania lakini wakiomba kujumuishwa kwenye Kanzidata ya LSSP kama washauri nasaha (Consultants).

Waombaji pekee watakaosajiliwa kwenye Kanzidata ya LSSP ya Watanzania wenye uwezo wa kuuza bidhaa au kutoa huduma kwenye shughuli za petroli ni wale watakaotimiza sifa zilizotajwa hapo juu.

Wapi na lini pa kuwasilisha maombi?

Maelezo yote yametolewa na EWURA kwenye tovuti yake www.ewura.go.tz bonyeza kwenye LOCAL CONTENT LSSP DATABASE kuona mwongozo, maelekezo na hatimaye Kanzidata. Kuna Fomu N-100 ambayo imeambatishwa ili ijazwe na yeyote mwenye sifa lakini kama hajawasilisha maombi yake kwa ajili ya Kazidata ya LSSP kwa mwaka 2018.

Uchakataji wa Taarifa

Fomu N-100 ambayo itawasilishwa EWURA pasipo kutiwa saini haitapokelewa. Maombi yoyote ambayo hayakukamilika kwa mujibu wa maelekezo yaliyotolewa na EWURA, yenye kurasa au nyaraka pungufu, au ambazo hazitakamilishwa kwa ufasaha au zisizothibitishwa kwa nakala halisi, nazo zitakataliwa.

Endapo Fomu N-100 yako itakataliwa, maombi yako yatarejeshwa kwako na maelezo ya mapungufu yaliyoonekana. Unaweza kufanya marekebisho ya mapungufu na kutuma upya Fomu N-100. Maombi hayatakuwa kamili hadi yakubaliwe na EWURA. 14. Mara EWURA itakapopokea maombi yako, itachunguza ukamilifu wake.

Endapo utashindwa kujaza Fomu N-100 na kuwasilisha maombi yako, EWURA itashindwa kujua uhalali wa uraia wako na uwezo ulionao, hivyo hautawekwa kwenye Kanzidata ya LSSP. 15. EWURA yaweza kuomba kuwa uwasilishe taarifa au ushahidi zaidi ili kuboresha maombi yako.

Unaweza kuombwa na EWURA kuwasilisha hati halisi ya nakala uliyowasilisha. Ukiombwa hati halisi, wasilisha hati hiyo EWURA na baada ya kuiona utarejeshewa ili urudi nayo. Unaweza kuombwa kufika Ofisi za EWURA kwa mahojiano kuhusu maombi yako Matokeo ya Fomu N-100 ni kuhakikisha kuwa Mtanzania anapata manufaa zaidi ya unayoyatarajia. EWURA itatoa taarifa kwako kufuatia uamuzi wa mwisho kuhusu maombi yako kwa maandishi.

Faini kwa Mwenendo Mbaya

Endapo kwa kujua au kutokujua, kudhamiria au kutokudhamiria utajaza uongo au taarifa zisizo za kweli kwenye Fomu N-100, EWURA yaweza kukataa kupokea Fomu N-100 na maombi yako hivyo ukapoteza manufaa. Zaidi ya kutokupata manufaa unaweza kushtakiwa kwa makosa ya jinai na kuhukumiwa kwa mujibu wa Sheria zilizopo.

Ukamilifu na Utekelezaji

Kwa kutia saini kwenye Fomu N-100, utakuwa umeruhusu taarifa zako ambazo zitakuwa zimewasilishwa zikiwa kamilifu na za ukweli, kuwa zinaweza kutumiwa na taasisi nyingine za umma. Vile vile, unaruhusu EWURA itumie taarifa zako kupata uhalali wa uraia wako ili uwekwe kwenye Kanzidata ya LSSP, hivyo EWURA itahakiki taarifa zako kabla na baada kufanya maamuzi ya kukuweka kwenye Kanzidata ya LSSP (Tanzania Local Suppliers and Service Providers Database).

Mpango mkakati wa miaka mitano wa EWURA (2018/19 – 2021/23)

Mpango Mkakati wa miaka mitano ulioanza 2018/19 mpaka Juni 2023 ulitengenezwa kupitia michakato ya maingiliano na shirikishi. Kupitia mfululizo wa semina za mipango ya maingiliano ya kimkakati, kazi za EWURA na shughuli zake zilitengenezwa ili kuleta mambo muhimu ambayo yanaathiri utoaji wa huduma za EWURA, ubora na udhaifu wake.

Mchakato huu wa maingiliano ulilenga kutengeneza uelewa wa pamoja juu ya mchakato wa kuandaa mpango mkakati na matokeo yake ya baadaye.

Warsha za kuunda mpango mkakati huu zilijumuisha uchambuzi wa yafuatayo;

·       Chimbuko la EWURA

·       Kazi na majukumu ya EWURA

·       Tathmini ya matokeo ya Mpango Mkakati uliopita ikiwa ni pamoja na kufanya uchambuzi wa mipango ya hivi karibuni, mafanikio na changamoto zake,

·       Uchambuzi wa wadau

·       Mapitio ya Shirika na,

·       Tathimini ya uelekeo wa taasisi

Uchambuzi huu ulitokana na mambo muhimu yafuatayo:

(a) Katika kipindi cha kupanga mkakati huu, EWURA itahitaji kukutana na changamoto mpya kila wakati na maagizo ya serikali, hivyo EWURA itajipambanua kila wakati ili kukabiliana na changamoto hizo,

(b) Muingiliano wa kijinsia (Gender Mainstreaming), utawala bora, VVU / UKIMWI, magonjwa yasiyoambukiza, afya na utimamu wa wafanyakazi, unywaji wa dawa za kulevya na pombe na ulinzi wa mazingira, vitaendelea kushughulikiwa na kuimarishwa katika Mpango Mkakati huu,

(c) Ili EWURA iweze kufikia matarajio ya wadau, Mamlaka itahitaji kupitisha mikakati itakayoongeza uwezo wa Mamlaka wa kupata, kuchambua na kusambaza taarifa kwa ajili ya kufanya maamuzi,

Kwa kuongezea, EWURA itahitaji kuunda mfumo wa kupata habari kutoka kwa sekta za usimamizi ili kusimamia vyema na wakati huo huo, kuwa na huduma zenye uwazi na kuweka viwango vya huduma vinavyotarajiwa na wadau wake (mkataba wa huduma kwa Wateja na kupata mrejesho),

(d) Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuboresha mazingira ya biashara nchini Tanzania. Ili kutekeleza juhudi hiyo, EWURA itaendelea kukuza zana za kisheria zilizopo kwa ajili ya kuvutia uwekezaji katika sekta husika,

(e) Ili kushughulikia uwekezaji duni katika sekta husika, EWURA itaongeza juhudi zake za kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi na Ushirikiano wa Umma na Sekta Binafsi (PPPs),

(f) Masuala ya mtaji wa rasilimali watu ikiwa ni pamoja na ukuzaji wa wafanyakazi, ushiriki wao, kuzingatia utamaduni wa taasisi, kuajiri, kuboresha mazingira ya kufanya kazi, vitaendelea kuwa muhimu ili kuhakikisha kuwa, EWURA inakuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa kasi na ubora unaokubalika,

(g) Ufadhili wa kifedha kwa EWURA ni eneo lingine la kipaumbele kwenye Mpango Mkakati huu, kwa sababu shughuli za EWURA zinapopanuka, ufadhili wa kifedha utakuwa muhimu zaidi. Ni muhimu kwa EWURA kuwa na nguvu za ifedha kama ilivyoainishwa katika Sheria ya EWURA, Sura ya 414.

(h) Umma lazima ujue na kushiriki katika mchakato wa kusimamia sekta za nishati na maji. Elimu kwa umma na uhamasishaji vitaendelea kushughulikiwa katika Mpango Mkakati huu.

Elimu kwa umma na uhamasishaji

EWURA imepania kutoa elimu kuhusu utekelezaji wa majukumu yake na dhana nzima ya udhibiti. Pamoja na kutoa elimu kwa umma kwa ujumla, msukumo wa elimu hii pia unawalenga viongozi serikalini na wadau wengine.

Programu hii imeanzia katika Mikoa yote ya Kanda ya Ziwa kwa mwaka wa Fedha wa 2018/2019. Ofisi ya EWURA ya Kanda ya Ziwa ina hudumia mikoa saba ambayo ni Mwanza, Shinyanga, Mara, Kagera, Geita, Simiyu na Kigoma.

Kama ilivyoaanishwa katika Sheria ya EWURA kipengere cha 6 (e, moja ya majukumu ya EWURA ni kutoa elimu kwa wadau wake kuhusu kazi na majukumu ya Mamlaka kwa sekta inazozidhibiti. Elimu hutolewa kwa kutumia njia mbalimbali za mawasiliano kama luninga, magazeti, redio na mitandao. Hata hivyo, pamoja na kutumia njia hizo zote za mawasiliano.

Elimu kwa Umma kwa sehemu kubwa imekuwa ikitekelezwa vizuri kwa ngazi ya kitaifa kupitia kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Umma Makao Makuu. Hata hivyo, Ofisi za Kanda zinawajibu pia wa kutoa elimu kwa wadau wake kwa ushirikiano na kitengo cha Mwasiliano makao makuu.

Ifahamike kuwa, wadau wa EWURA ni pamoja na watoa huduma zinazodhibitiwa na EWURA, watumiaji wa Huduma za Nishati na Maji, Wizara, Idara za Serikali, Mashirika ya Umma, Serikali za Mitaa, Vyama vya Kiraia, Vyombo vya habari, Wabia wa Maendeleo, Wawekezaji, Wanasiasa na wananchi kwa ujumla.

Mkakati wa elimu kwa umma ulivyowafikia wahariri wa vyombo vya habari

EWURA imekutana na wahariri wa vyombo vya habari nchini katika jitihada zake za kufikisha elimu kwa wadau mbalimbali na umma kwa ujumla juu ya masuala ya udhibiti.

Katika mkutano huo, wahariri wote kutoka vyombo mbalimbali vya habari vikiwemo, Televisheni, redio, magazeti na habari za mtandao walipata wasaa wa kusikiliza wasilisho kutoka kwa Meneja wa Uhusiano na Mawasiliano kutoka EWURA, Titus Kaguo lililohusu, kazi, wajibu na changamoto mbalimbali zilizoikabili taasisi katika kipindi cha mwaka 2018/2019, pamoja na mipango mikakati ya mbeleni ya Mamlaka.

Kaguo alisema EWURA ni mdhibiti wa huduma za nishati na maji, ambazo humgusa moja kwa moja, mtumiaji wa mwisho ambaye ni mwananchi pamoja na watoa huduma hivyo basi kupitia wahariri na vyombo vya habari ni rahisi kufikisha taarifa muhimu kwa wananchi hao.

“Ninyi ni mabalozi wetu muhimu katika kuhakikisha taarifa zinawafikia wananchi katika muda muafaka, hivyo basi, tumeona tukutane nanyi, ili mpate kufahamu masuala muhimu ya kiudhibiti na kuifahamu taasisi yetu vizuri ili mwende kuelimisha umma juu ya kazi na wajibu wetu,” alisema.

EWURA itaendelea kuboresha ushirikiano na wahariri pamoja na waandishi wa habari, ili kuongeza uwazi katika kufanya kazi zake na kuwahabarisha wananchi moja kwa moja kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

Uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji miradi ya umeme

Ili kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi kwenye uwekezaji wa miradi midogo ya kuzalisha umeme (chini ya Megawati 10), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) iliandaa mikataba elekezi ya kuuziana umeme (Model Power Purchase Agreements) kati ya TANESCO na wawekezaji.

Mikataba hii, pamoja na masuala mengine hupunguza muda wa majadiliano kati yao na inawezesha uwekezaji na utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.

EWURA imetayarisha bei elekezi za ufuaji umeme utokanao na maji, gesi asilia, makaa ya mawe, jotoardhi, umeme wa jua, upepo na mafuta ili kuiwezesha Tanzania kuwa na umeme wa uhakika kwa matumizi ya viwanda.

Hatua hizi ni sehemu ya jitihada kubwa zinazofanywa na EWURA katika kuimarisha mazingira ya kuvutia uwekezaji katika miradi ya umeme ili kushajihisha utekelezaji wa sera ya viwanda.

Mamlaka imeendelea kuratibu mabadiliko katika sekta ndogo ya umeme (ESI) ambayo yanalenga kuongeza uwezo wa uzalishaji kufikia Megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.

Aidha, katika kutekeleza majukumu yake ya kiudhibiti, EWURA imeboresha huduma za utoaji leseni za umeme kwa kuimarisha mfumo wa uombaji leseni kwa njia ya mtandao yaani LOIS, upangaji wa bei pamoja na kusimamia ubora wa huduma zinazotolewa.

EWURA kukabiliana na mafundi umeme wasiyo na leseni ya Mamlaka hiyo

EWURA imetoa onyo kwa mafundi umeme wote wanaofanya shughuli za ufungaji wa mifumo ya umeme, bila kuwa na leseni hai iliyotolewa na EWURA.

EWURA inatoa tahadhari kwa mafundi umeme wanaotoa huduma za uwekaji mifumo ya umeme, bila kuwa na leseni halali, kuacha mara moja na kuomba leseni itakayo waruhusu kufanya shughuli hizo EWURA.

Kwa mujibu wa sheria ya umeme, kazi zote za ufungaji umeme, ikiwemo upanuzi, kubadili, kufanya marekebisho na matengenezo kwenye mifumo, zinatakiwa zifanywe na fundi mwenye leseni iliyotolewa na EWURA. ili kuhakikisha shughuli hizo zinaendeshwa na watu wenye utaalamu stahiki kwa usalama wa watu na mali zao.

EWURA inawatahadharisha wateja wa huduma za uwekaji mifumo ya umeme kuepuka kutumia mafundi wasiokuwa na leseni. Kwa utambuzi ni vyema kuomba kitambulisho cha fundi husika au kutumia orodha ya mafundi inayopatikana kwenye tovuti ya EWURA www.ewura.go.tz.

Kwa mantiki hiyo ni kosa la jinai kuendesha shughuli za ufungaji umeme bila kuwa na leseni halali, mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kuendesha shughuli hizo bila leseni atatozwa faini ya shilingi milioni tano au kifungo cha miaka mitano au adhabu zote kwa pamoja.

Mpaka mwishoni mwa mwezi Machi 2019, jumla ya leseni zaidi ya 1,000 zilikuwa zimetolewa kwa mafundi umeme Tanzania bara. Hivyo, ni kosa kisheria kufanya shughuli za ufungaji umeme, bila ya kuwa na leseni ya EWURA. Mtu yeyote akikamatwa na kosa hilo atapata adhabu ya kulipa fine au kifungo cha miaka mitatu jela.

EWURA yazipiga msasa Mamlaka za maji

Katika kuimarisha utoaji huduma za maji na usafi wa mazingira kwa wananchi, EWURA imekuwa ikikutana na Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuhakiki taarifa zao za utekelezaji wa majukumu ili kuiwezesha EWURA kuandaa taarifa ya utendaji kazi wa Mamlaka.

Kikao hicho kiliandaliwa ili kuhakikisha wadau wote wa sekta ya maji wanapata uelewa wa namna EWURA inavyoandaa taarifa za kiutendaji kazi na ushiriki wao pamoja na vigezo vinavyotumika kupima utendaji wa Mamlaka za Maji na Usafi wa Mazingira nchini.

Mpango wa Mamlaka hii ni kupima utendaji kazi ni wa uwazi na umelenga kuhakikisha Mamlaka zinaimarisha ukusanyaji mapato, utoaji huduma na kuzingatia viwango vya ubora. Upimaji wa utendaji wa mwaka 2019 pia utaangalia suala la uwepo wa mkataba wa huduma kwa mteja katika kila mamlaka.

Kikao kazi hicho kilichofanyika Dar es Salaam, kilishirikisha zaidi ya wadau 100 kutoka Wizara ya Maji, Ofisi ya Rais-TAMISEMI na watendaji kutoka Mamlaka za Maji za Wilaya, Miji Midogo, Mikoa na Miradi ya Kitaifa.

EWURA ilivyong’ara tuzo za NBAA 2017

Mwaka 2017, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ilishinda tuzo ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA), kwa kuwa mshindi wa pili katika uandaaji na uwasilishaji bora zaidi wa taarifa ya fedha, kwa mwaka 2017.

Tuzo hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji katika hafla iliyofanyika katika Kituo cha Uhasibu na Ukaguzi cha NBAA, Bunju, Dar es Sar es Salaam na kupokelewa na Mkurugenzi wa Fedha, Rasilimali Watu na Utawala wa EWURA, Stanley Mahembe.

Meneja wa Fedha wa EWURA, Joctan Matogo ambaye alihudhuria hafla hiyo, alisema ushindi wa EWURA umetokana na kufuata miongozo ya kitaifa na kimataifa katika uandaaji wa hesabu pamoja na kutoa maelezo ya ziada yanayofafanua vizuri zaidi na kwa undani hesabu na utendaji kazi wa Mamlaka.

EWURA ni mongoni mwa taasisi tatu bora kuwa na hati safi ya taarifa za fedha kwa upande wa Mamlaka nchini, kwa mujibu wa ukaguzi uliofanywa na NBAA kwa mwaka 2017.

Kwa kuhitimisha, kipengele cha 6(e) cha Sheria ya EWURA, kinasema kwamba ni wajibu wa Mamlaka kuhakikisha inaboresha ustawi wa jamii ya Watanzania kwa kuimarisha elimu kwa umma, ufahamu na uelewa wa sekta zinazodhibitiwa ikiwa ni pamoja na haki na wajibu wa walaji na watoa huduma wa sekta zinazodhibitiwa; Njia za kutatua migogoro na kusikiliza malalamiko, kazi na shughuli za mamlaka kwa ujumla.