ZFDA tunahakikisha Wazanzibari wanatumia bidhaa na huduma zenye ubora na usalama


ZFDA tunahakikisha Wazanzibari wanatumia bidhaa na huduma zenye ubora na usalama

Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi (ZFDA) ambao zamani ulitambulika kama Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi (ZFDB) ni Taasisi iliyopo chini ya Wizara ya Afya Zanzibar yenye jukumu la kudhibiti ubora na usalama wa chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi.

Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi (ZFDA) ambao zamani ulitambulika kama Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi (ZFDB) ni Taasisi iliyopo chini ya Wizara ya Afya Zanzibar yenye jukumu la kudhibiti ubora na usalama wa chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi.

Wakala unafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi 2/06 na marekebisho yake ya Sheria nambari 3/17.

Katika kuadhimisha siku ya viwango duniani ambayo huadhimishwa kila Oktoba 14 ya kila mwaka, Mkurugenzi Mtendaji wa ZFDA anaeleza namna wakala huo ulivyojipanga kuadhimisha siku hiyo mwaka huu.

Namna ZFDA ilivyofanikiwa katika kusimamia ubora na usalama wa dawa na chakula

Ukaguzi (Inspection)

ZFDA kupitia wakaguzi wake imekuwa ikifanya ukaguzi katika majengo yote yanayojihusisha na uzalishaji, uuzaji,ufungashaji,usafirishaji wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi,vifaa tiba na vitendanishi kama vile viwanda, maduka ya jumla na rejareja ya chakula na dawa, bekari, bucha.

Kwa kupitia ukaguzi huo bidhaa ambazo zitagundulika kuwa hazina viwango zitakatazwa kutumika kwa matumizi husika.

Usajili (Premises & Products Registration)

ZFDA inasajili majengo yanayoshughulika na bidhaa za Chakula, Dawa, Vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi, aidha ZFDA inasajili bidhaa ambazo inazisimamia ili kuweza kujua Ubora na Usalama wake na kurahisisha ufuatiliaji wake sokoni.

Uchunguzi (Laboratory Services)

ZFDA inayo maabara ya kisasa kwa ajili ya kuchunguzia sampuli za chakula, dawa na vipodozi ili kuweza kujiridhisha na ubora na usalama wake kabla ya matumizi.Pia, ZFDA inazuia bidhaa zote ambazo hazijafikia viwango vilivyowekwa na hivyo basi kuzirudisha nchi zilipotokea au kuziteketeza kwa njia sahihi iliyopendekezwa na idara ya mazingira.

Udhibiti wa Uingizaji na Usafirishaji wa Bidhaa (Controlling Of Importation & Exportation)

Uingizaji na usafirishaji wa bidhaa za Chakula, Dawa na Vipodozi kupitia bandari na viwanja  vya ndege unadhibitiwa na wakaguzi wa ZFDA waliopo sehemu hizo kwa kuhakikisha bidhaa hizo zinachukuliwa na sampuli zake kuchunguzwa ubora na usalama wake kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini.

Ufuatiliaji wa Usalama wa Dawa na Madhara yake (Pharmacovigilance)

ZFDA kupitia kitengo hicho imeanzisha mfumo wa kuzifuatilia dawa ambazo zinasababisha madhara kwa watumiaji wake kwa ajili ya kufahamu ubora na usalama wake, lakini pia kujua kwa kiwango gani dawa hizo zinasababisha madhara.

Ufuatiliaji wa ubora wa dawa sokoni baada ya kusajiliwa Post Market Suvillience (PMS)

ZFDA kupitia kitengo chake cha PMS inafuatilia dawa ambazo zimesajiliwa na tayari zimeruhusiwa kuingizwa na kuuzwa sokoni ili kuhakikisha dawa zinakuwa na viwango vya ubora na salama si tu kabla ya kusajiliwa, lakini hata baada ya kuzisajili na kuingizwa sokoni.

Majaribio ya dawa baada ya uzalishwaji na kabla ya kuanza kutumika (Clinical Trial)

ZFDA kupitia kitengo chake cha Clinical Trial inafanya majaribio ya dawa baada ya kuzalishwa kiwandani. Majaribio hayo hufanywa kabla ya kutumika kwa matumizi ya binadamu ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza ikiwa dawa hiyo itakuwa ina madhara.

Kwa mujibu wa sheria, ZFDA inasimamia ubora na   usalama wa aina za Dawa na Chakula zifuatazo:-

·       Dawa zote za Binadamu

·       Dawa zote za Mifugo

·       Vifaa tiba

·       Vyakula na vinywaji ikiwemo bidhaa za nyama na maziwa, bidhaa za chakula zilizofungashwa.

Kwa mujibu wa sheria 2:2006 na Marekebisho yake nambari 3:2017 ya Wakala wa Chakula, Dawa  na Vipodozi  kifungu nambari 31(1)(2) Mfanyabiashara atakayebainika kufanya biashara ya  chakula kisicho na ubora au kilichoisha muda wake atalazimika kulipia faini isiyozidi miliioni moja za Kitanzania au kifungo kisichozidi miezi sita au vyote viwili kwa pamoja.

Aidha, kwa mujibu wa sheria ya Wakala wa Chakula,Dawa  na Vipodozi Namba 2:2006 na Marekebisho yake nambari 3:2017 kifungu nambari 77(1)(2) Mfanyabiashara atakayebainika kufanya biashara ya  dawa zisizo na ubora na usalama au zilizoisha muda wake atalazimika kulipia faini isiyozidi milioni tano za Kitanzania au kifungo kisichozidi miaka miwili au vyote viwili kwa pamoja.

Taasisi mbalimbali ambazo tunashirikiana nazo ZFDA katika utekelezaji wa majukumu yake ni pamoja na;

Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS)

Katika kuhakikisha ubora wa viwango unapatikana ni lazima tushirikiane na taasisi za viwango ili kupata bidhaa zenye Ubora na Salama katika kulinda Afya za wananchi. Jukumu hili tunalifanikilisha kwa ajili ya kuleta ufanisi wakati wa kufanya kazi zetu ili kuhakikisha bidhaa ambazo zinachunguzwa zinakuwa na kiwango kinachotakiwa.

Mashirikiano na Jumuiya mbalimbali za Kimataifa

Katika kufanikisha kazi za ZFDA ni vyema kuimarisha mahusiano na jumuiya mbalimbali za kikanda, kitaifa na kimataifa. Hivyo basi ZFDA kupitia kitengo chake cha mashirikiano na jumuiya hizo kama vile East African community (EAC), (SADC ) na nyinginezo imeweza kupiga hatua za pamoja, kwa mfano kuanzishwa kwa ukaguzi na usajili wa pamoja wa dawa kwa nchi wanachama wa umoja wa Afrika Mashariki ili kuweza kuwa na mfumo na viwango vya pamoja.

Ushirikiano na vyombo vya Ulinzi na Usalama

Vile vile katika kufanikisha mambo mbalimbali ya ZFDA tunashirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo vyombo vya Ulinzi na Usalama ili kuhakikisha tunapata usalama wakati wa kufanya shughuli zetu kama vile ukaguzi na uteketezaji wa bidhaa zisizofaa.

Wizara ya Afya

Aidha, Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi unashirikiana na Wizara ya Afya katika kupanga mipango na kuelezea majukumu yetu ambayo tunayatekeleza kwa  kudhibiti Ubora na Usalama wa Chakula Dawa na Vipodozi ili kuleta ufanisi na ushindani wa biashara.

Vile vile,Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi unashirikiana na Wizara tofauti ikiwemo Wizara ya Biashara na Viwanda,Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali,Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za Vikosi vya SMZ,na Wizara inayoshughulikia Mambo ya Muungano na Mazingira.

Katika suala la udhibiti wa bidhaa, ZFDA inashirikiana na wafanyabiashara wa nje na ndani ya nchi katika kudhibiti uingizwaji wa bidhaa zisizozingatia Ubora na Usalama kama ifuatavyo;-

ZFDA inashirikiana na wafanyabiashara kwa kuwashirikisha katika chombo cha maamuzi cha ZFDA ambacho kinajulikana kama Bodi ya Ushauri ya ZFDA, ambapo mjumbe mmoja kutoka katika jumuiya ya wafanyabiashara hushiriki kila panapofanyika vikao vya bodi hiyo kwa ajili ya kutoa maamuzi yanayohusiana na ZFDA.

Aidha, ZFDA inawapatia Mafunzo mbalimbali Wafanyabiashara yanayohusiana na udhibiti wa uingizaji wa bidhaa zisizozingatia Ubora na Usalama na madhara yake.

ZFDA pia inawashirikisha wafanyabiashara katika utengezaji wa Sheria, Kanuni na Miongozo hususan inayohusiana na udhibiti wa bidha zisizofaa na madhara yake.

ZFDA inawashirikisha wafanyabishara katika matokeo mbalimbali yanayohusiana na shughuli za ZFDA ambazo mfanyabiashara anahusika mfano, uteketezaji huwashirkisha wafanyabiashara ili kujiridhisha kuwa bidhaa zake kweli zinaangamizwa kwa sababu ya kukosa viwango ambavyo hupelekea kukosa vigezo vya kuwa bora na salama kwa matumizi ya binadamu.

Vile vile ZFDA inashirikiana na wafanyabishara wa nje ya Zanzibar kwa kufanya ukaguzi wa viwanda vya nje ya nchi (GMP INSPECTION).

Ushirikiano huu umeongeza tija mbalimbali katika kulinda afya za Wazanibar kama hivi ifuatavyo:

Kuongezeka kwa uelewa wa wafanyabiashara na wananchi

Katika kuhakisha wananchi na wafanyabiashara wanapata uelewa, ZFDA inatoa elimu kupitia vyombo mbalimbali kama vile Radio, Runinga, Magazeti na kutoa vipeperushi ili kuwezesha shughuli za ZFDA kufikia lengo lililotarajiwa pamoja na kuwapatia fursa wananchi na wafanyabiashara kuuliza maswali pamoja na kutoa mapendekezo.

Aidha, ZFDA imepata tija kubwa ikiwemo wananchi na wafanyabiashara kuwa na utayari wa kutoa taarifa pale inapojitokeza kupatikana kwa bidhaa zisizokuwa na Ubora na Usalama, hali kadhalika kutoa taarifa kwa mtu yeyote anayehisiwa kujihusisha na bidhaa zisizo sahihi.

Vile vile, ZFDA imepata tija ya kuongezeka kwa bidhaa zenye viwango masokoni, hali iliyosaidia kwa hatua kubwa kufanikisha zoezi la kupunguza madhara ya uteketezaji na kuboresha afya za wanachi wa Zanzibar.

ZFDA imepata faida ya kukua kwa uchumi, kupitia wanachi na wafanyabiashara kujisajili kwa wingi hali inayosaidia kuongezeka kwa ulipaji wa ada ya maduka inayotozwa na ZFDA kama maduka ya chakula, mabucha, viwanda na kadhalika.

ZFDA inajivunia mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika usimamizi wa Ubora na Usalama wa Chakula na Dawa ikiwemo;

Mabadiliko ya Sheria

Mabadiliko ya sheria kutoka Bodi ya Chakula na Dawa na kuwa Wakala wa Chakula na Dawa. Mabadilio hayo yalifanyika mnamo mwaka 2017, sheria nambari 3 ya mabadiliko ya sheria namba 2;2006 ya mwanzo ya Bodi ya Chakula na Dawa ilipitishwa kupitia chombo cha kutunga sheria cha Baraza la Wawakilishi na kutiwa saini na Rais wa Zanzibar. Mabadiliko hayo ya sheria yameipa nguvu zaidi ya kisheria taasisi ya ZFDA katika kutekeleza kazi zake za kila siku.

Kuongezeka kwa Wataalamu

Wakala wa Chakula na Dawa umepata jumla ya wataalamu 70 kuanzia 2010-2019. Kuboresha kazi za kitaalamu (Technical Working Groups) (TWG’S) kwa vitengo vyote vya wakala kama vile GMP –Good Manufactring Practice (Ukagzi wa viwanda)

IMS – Information Management System (kitengo cha mifumo ya teknolojia ya habari)

QMS – Quality Management System (mfumo wa uhakiki na utoaji huduma bora)

Ununuzi wa gari na vyombo vya usafiri kwa ajili ya ukaguzi

Jumla ya gari tano zimenunuliwa katika kufanikisha kazi mbalimbali za ZFDA ikiwemo ukaguzi wa chakula, ukaguzi wa dawa na vipodozi, mabucha, viwanda, mabekari na kadhalika. Hivyo ZFDA inajivunia mafanikio iliyopata katika kusiamia ubora na usalama wa Dawa na Vipodozi.

Ujenzi wa jengo jipya la Afisi na maabara ya kisasa ya ZFDA

Wakala wa chakula dawa na vipodozi imepata tija kwa kutarajia kupata jengo jipya la Afisi na maabara ya kisasa kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa kuchunguza bidhaa.

Kupata Ithibati ya Kimataifa ISO 9001:2015

ZFDA imepata ithibati ya kimataifa ya kutoa huduma bora kwa wateja ambayo inaipa ithibati ZFDA kufanya shughuli zake kwa uhakika na kwa kuwajali wateja wake ambao ni wananchi na wafanyabiashara.

Matumizi ya Teknolojia

Teknolojia mbalimbali zinatumika katika kuhakiki Ubora na Usalama wa bidhaa, teknolojia hizo ni vifaa na mashine za uchunguzi ikiwemo HPLC ambapo vifaa vifaa na mashine hizo zinatumika katika kubaini mambo mbalimbali ambayo yanahatarisha Ubora na Usalama wa bidhaa pamoja na afya za watumiaji.

Teknolojia hizo hutumika katika ukaguzi wa kila siku unaofanyika katika sehemu mbalimbali ikiwemo vituo vya forodha, maduka, maghala, viwanda na kadhalika.

Vile vile teknolojia hizo zinatumika katika uchunguzi wa kimaabara kwa sampuli mbalimbali zinazoletwa kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ili kuweza kubainn Ubora na Usalama wa bidhaa hizo katika kiwango kinachokubalika kabla ya matumizi muafaka.

Teknolojia ni sehemu ya muhimu na ya msingi wa maamuzi mbalimbali ya ZFDA ya kila siku.

Maadhimisho ya siku ya viwango duniani

Hii ni siku muhimu na adhimu kuadhimishwa kila mwaka ili kuweza kutoa uelewa kwa wananchi na jamii kwa ujumla juu ya umuhimu wa kuwa na bidhaa zenye viwango.

Siku hii ina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya jamii na wafanyabishara kwa sababu nguvu kazi ya jamii na wafanyabiashara inategemea na afya bora za wananchi wenyewe ambazo hupatikana kwa kutumia  bidhaa zenye Ubora na Usalama na zenye viwango. Hivyo basi jamii yenye afya huzalisha kwa kiwango kikubwa.

Aidha, Serikali hutumia fedha kidogo za matibabu ukilinganisha na jamii isiyo na Afya Bora.

Kukosekana kwa bidhaa zenye Ubora na Usalama na viwango hususan bidhaa za Chakula, Dawa na Vipodozi Vifaa tiba na Vitendanishi Afya za wanchi zitazorota,  uchumi wa nchi utashuka na uchumi wa wafanyabiashara utashuka.

Mambo ambayo ZFDA tunatarajia kuyafanya katika maadhimisho ya siku hii

Kutoa Makala ya siku ya viwango katika gazeti la Mwananchi.

Kufanya vipindi mbalimbali vya televisheni na radio na  

Kushiriki maonyesho mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu.

Mikakati ya ZFDA

·       Kujenga jengo jipya la afisi na maabara ya kisasa

·       Kutafuta ithibati ya kimataifa ya huduma za maabara ISO 17025:2015 ili kuweza kufanya uchunguzi kwa ufanisi zaidi.

·       Kuanzisha kwa mfumo wa kieletroniki ambao husaidia wafanyabiashara kuweza kufanya maombi na miamala kwa njia ya mtandao (online) mubashara bila ya kuwa na ulazima wa kufika ofisini ambao utapunguza muda na gharama.

·       Kuanzisha mfumo wa kulipia kwa njia ya simu (online bank).

·       Kuimarisha ukaguzi wa ndani na wa nje ya Zanzibar

·       Kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuweza kwenda nao sambamba na kujua kwamba Ubora na Usalama wa bidhaa zenye viwango ni ghughuli yetu sote kwa pamoja.

Wito

ZFDA kupitia siku hii ya viwango Duniani inasema “Kwa pamoja tunalinda afya ya jamii.”