Kuzimwa kwa vituo vya kuzalisha umeme wa mafuta kunaokoa mabilioni ya fedha za Serikali


Kuzimwa kwa vituo vya kuzalisha umeme wa mafuta kunaokoa mabilioni ya fedha za Serikali

Gharama za Mradi wa Umeme wa Makambako – Songea ni sawa na bilioni 216 za Kitanzania, na umetekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Sweden (Sida).

Aprili 6, 2019, Rais John Magufulia alizindua mradi mkubwa wa njia ya usafirishaji umeme wa Kilovoti 220 kutoka Makambako mkoani Njombe hadi Songea mkoani Ruvuma.

Umeme huo unachakatwa katika kituo cha kupoza na kusambaza umeme kilichopo Unangwa Songea mjini mkoani Ruvuma. Kituo hicho ni miongoni mwa vituo vitatu vya Madaba na Makambako.

Akizungumza katika hafla hiyo Rais Magufuli alisema mojawapo ya faida kubwa za mradi huo ni kusaidia kutatua changamoto ya umeme iliyokuwa ikiikabili mikoa ya Njombe na Ruvuma na kuokoa kiasi cha Sh 9.8 bilioni kwa mwaka, zilizokuwa zikitumika kulipia gharama za uzalishaji umeme wa mafuta.

Alisema; “kwa mujibu wa utafiti uliowahi kufanywa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), watu takribani 600,000 hupoteza maisha kwa sababu ya matatizo yanayohusiana na matumizi ya mafuta ya taa, mkaa au kuni. Hivyo, kuzinduliwa kwa mradi huo wa kusafirisha umeme kunampa faraja kubwa. Kwa mujibu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), umeme huo hivi sasa unavinufaisha vijiji zaidi ya 122.

Rais alisema azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuipatia Tanzania umeme wa kutosha, wenye uhakika na wa gharama nafuu.

Akizungumzia athari za ukosefu wa umeme kwa Tanzania, Rais alisema kila mwaka, nchi yetu hupoteza takribani ekari 400,000 za miti kwa ajili ya mkaa na kuni, hali inayochangia uharibifu mkubwa wa mazingira.

Alisema ni ukweli usiopingika kwamba uharibifu huo hauwezi kuisha endapo serikali isipotafuta suluhisho kwa kuwapa wananchi wanaotegemea nishati ya kuni na mkaa, njia mbadala ili waache kukata miti.

Akizungumza na Mwananchi wiki iliyopita Jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk Tito Mwinuka alisema katika kipindi cha miaka minne ya Rais Magufuli akiwa madarakani, changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara iliyokuwapo Mkoani Ruvuma, imepata suluhisho baada ya kuwapo kwa mradi huo.

Akizungumzia mradi huo, Waziri wa Nishati, Dk Medadi Kalemani yeye anasema changamoto iliyopo sasa ni uwapo wa umeme mwingi unaozidi matumizi ya wananchi hali inayosababisha kuungua kwa baadhi ya vifaa vya wateja.

“Mahitaji ya umeme kwa sasa katika Mkoa wa Ruvuma ni megawati 12.5 na kwa Songea Mjini ni megawati 9.7 tu. Umeme uliokuja sasa ni megawati 48. Matokeo yake umeme umekuwa ukimiminika kwa kasi wakati mahitaji ni madogo,” anasema.

Waziri huyo anasema Serikali inafanya utaratibu wa kutatua changamoto hiyo kwa kufunga kifaa kitakachodhibiti umeme uendane na mahitaji ya wananchi.

Pia, anatoa wito kwa wananchi wa Ruvuma kuutumia umeme kwa wingi ikiwamo kuanzisha viwanda na biashara mbalimbali.

Aidha, Waziri anasema katika maeneo ambako mradi unapita, jumla ya vijiji 122 vimesambaziwa umeme na kuunganisha wateja takribani 22,700.

Anapongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Magufuli kwa namna inavyotekeleza mikakati mbalimbali ya kusambaza nishati hiyo ya umeme kwa wananchi.

Balozi wa Sweden hapa nchini, Anders Sjoberg ambaye alikuwapo siku ya uzinduzi wa mradi wa Makambako Songea, alisema Mkataba kati ya Serikali za Tanzania na Sweden kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, ulisainiwa mwaka 2008 na Sweden ilitoa Krona milioni 700 sawa na Sh 165 bilioni.

“Tunapoona matokeo haya; tunaweza kuhitimisha kwamba, haya ni mafanikio makubwa, ni uwekezaji mkubwa,” alisema Balozi Sjoberg.

Gharama za Mradi wa Umeme wa Makambako – Songea ni sawa na bilioni 216 za Kitanzania, na umetekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na ya Sweden kupitia Shirika la Maendeleo la Sweden (Sida).

Akizungumzia hilo, Dk Kalemani anasema kukamilika kwa mradi huo kumesaidia kuongeza uwezo wa njia za usafirishaji umeme na kuimarisha hali ya upatikanaji umeme kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kupitia Gridi ya Taifa.

Anasema mradi huo umesaidia kupunguza gharama za uendeshaji kwa Tanesco baada ya kuzimwa kwa mitambo yote ya mafuta na kuweza kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 9.8 kwa mwaka.

Usambazaji wa umeme wa gridi ya Taifa

Akizungumzia usambazaji wa umeme wa gridi ya Taifa, Dk Mwinuka anasema Serikali inaokoa wastani wa Sh 23.5 bilioni baada ya kuanza kusambaza umeme huo kwenye mikoa ya Kusini mwa Tanzania.

Anasema ndani ya miaka minne, Tanesco iliendesha programu ya usambazaji wa nishati hiyo nchini na amewashukuru wananchi na viongozi wa mikoa ya Kusini kwa ushirikiano waliotoa kwa wahandisi na wafanyakazi wengine  wa Tanesco ambao wameshiriki kikamilifu kukamilisha kazi hiyo.

“Fedha zilizookolewa zimetumika kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na lengo likiwa kila Mtanzania afikiwe na umeme popote alipo,” anasema Dk Mwinuka.

Vituo vilivyozimwa Genereta

Dk Mwinuka amevitaja vituo ambavyo mashine za genereta za dizeli zimezimwa baada ya kuunganishwa na umeme wa gridi ya Taifa kuwa ni Songea, Mbinga, Namtumbo, Madaba na Liwale.

“Tunayo furaha kulieleza Taifa kwamba katika kutekeleza programu ya miaka minne ya usambazaji wa nishati ya umeme, tumepata mafanikio makubwa sana.  Sasa Serikali inaokoa wastani wa Sh 23.5 bilioni kwa mwaka kwa sababu tumezima mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta katika vituo vyetu vya Songea, Mbinga, Namtumbo, Madaba na Liwale,” amesema Dk Mwinuka.

Anasema, Shirika linajivunia mafanikio hayo yaliyochagizwa kwa kiwango kikubwa na bidii ya wafanyakazi wake ambao hujitolea usiku na mchana kuona kazi zinakamilika kwa wakati.

Usambazaji wa nyaya za umeme wa gridi unahusisha kuweka nguzo za miti na za vyuma hata katika maeneo ya hatari kwa sababu umeme unapita mbugani, juu ya mito, mabonde, misitu na milima.

Usambazaji wa umeme chini ya mpango wa miaka minne uliobuniwa na Tanesco, ni sehemu ya mchango wa  shirika hilo katika kutekeleza mpango wa  kitaifa wa ‘kukazania utoaji huduma katika maeneo sita ya kipaumbele’ yaliyoanishwa katika mwaka wa fedha 2012/13. 

Maeneo hayo ni nishati na gesi asilia, kilimo, maji, elimu, usafiri na ukusanyaji mzuri wa raslimali za taifa. Maeneo hayo yalitamkwa wakati wa kuzindua mpango wa taifa wa ‘Matokeo Makubwa Sasa (BRN) mwaka huo wa fedha.