Miradi ya kimkakati ya umeme itakayofikisha MW 10,000 mwaka 2025


Miradi ya kimkakati ya umeme itakayofikisha MW 10,000 mwaka 2025

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk Tito Mwinuka ameeleza kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo inalenga kutimiza adhima ya Serikali ya kuwa na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk Tito Mwinuka ameeleza kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo inalenga kutimiza adhima ya Serikali ya kuwa na megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.

Taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo aliitoa Oktoba 23, 2019 katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilichofanyika jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliiongoza Wizara ya Nishati katika uwasilishaji wa taarifa hiyo akiwa ameambatana na Katibu Mkuu, Dk Hamisi Mwinyimvua na Menejimenti ya Wizara pamoja na Taasisi zake.

“Wizara ya Nishati kupitia Tanesco inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ya umeme ikiwamo ya kuzalisha umeme, usafirishaji umeme katika msongo mkubwa na usambazaji, lengo likiwa ni kukidhi mahitaji ya umeme yanayoongezeka na miradi hii itakapokamilika itachangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa sekta ya umeme nchini,” alisema Dk Mwinuka.

Dk Mwinuka alitaja miradi mbalimbali ukiwamo mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (MW 2115) ambao Mkandarasi ameanza rasmi utekelezaji wake tarehe 15 Juni, 2019 kwa kuanza ujenzi wa bwawa pamoja na njia ya kuchepusha maji ambapo mpaka sasa uchorongaji wa handaki la mchepuko wa maji unaendelea na matarajio ya kumaliza mradi huo ni Juni 2022.

Alitaja mradi mwingine wa kimkakati kuwa ni mradi wa kuzalisha umeme wa Rusumo (MW 80) ambao kwa sasa umefikia zaidi ya asilimia 55 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2020.

“Mradi mwingine tunaoutekeleza ni mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia wa Kinyerezi I Extension (MW 185) ambao upo katika hatua za mwisho za utekelezaji kwani umefikia asilimia 84 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2020,” alisema Dk Mwinuka.

Mkurugenzi huyo Mtendaji wa Tanesco alitaja miradi mingine ya kuzalisha umeme wa maji ambayo ipo katika hatua za awali za utekelezaji kuwa ni mradi wa Ruhudji (MW 358), Mradi wa Kakono (MW 87), mradi wa Rumakali (MW 222), mradi wa Malagarasi (MW 45) na mradi wa Kikonge (MW 300).

Pia, aliongeza kuwa, mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia ambao upo katika hatua za awali za utekelezaji ni mradi wa Mtwara ambao utazalisha    megawati 300.

Wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge walitoa maoni mbalimbali yatakayosaidia kuboresha sekta ya umeme nchini ambayo Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliahidi kuwa yatafanyiwa kazi.

Hata hivyo, ikiwa imetimia miezi 48 sasa sawa na miaka minne tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alipochukua jukumu rasmi la kuiongoza nchi Novemba 5, 2015.

Kiongozi huyu amefanikiwa kuhakikisha Watanzania wanatoka hatua moja kwenda nyingine kimaendeleo badala ya kubaki kama walivyo miaka nenda miaka rudi. Aina ya uongozi wa rais Magufuli umeonesha uwezo au karama ya kuondoa taratibu zilizo zoeleka katika jamii na kisha kubuni, kuelekeza njia sahihi kwa vitendo ni ushindi wa mafanikio katika uongozi.

Jumanne Mei 28, 2019, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani aliwasilisha kwenye Bunge la Bajeti makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo mwaka 2019/2020 ya Sh2trilioni huku fedha nyingi zikielekezwa katika miradi mikubwa mitatu ya kimkakati ya umeme. Bajeti hiyo ilikuwa Sh1.69 trilioni. Aliliambia Bunge kuwa miradi hiyo inagharimu Sh1.86 trilioni.

Aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na wa kuzalisha umeme katika Mto Rufiji wa Megawati 2,115 unaogharimu Sh1.44 trilioni, mradi wa kusambaza umeme vijijini awamu ya tatu unaogharimu Sh363.11bilioni na mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi I Extension MV185 wa Sh60 bilioni.

Kupitishwa kwa bajeti hiyo kulitoa fursa kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuendelea kutekeleza Miradi yake mikubwa kwa kasi ya ajabu.

Inaelezwa kuwa utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa ya kihistoria, kwa kiasi kikubwa kumechagizwa na chachu inayotolewa na Rais John Magufuli katika sekta ya nishati hapa nchini.

Akizungumza na Mwananchi wiki iliyopita Jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk Tito Mwinuka alisema katika kipindi cha miaka minne ya Rais Magufuli akiwa madarakani, changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara iliyokuwapo mkoani Ruvuma, imepata suluhisho baada ya kuwapo kwa mradi huo.

Akizungumzia mradi huo, Waziri wa Nishati, Dk Medadi Kalemani yeye anasema changamoto iliyopo sasa ni uwepo wa umeme mwingi unaozidi matumizi ya wananchi hali inayosababisha kuungua kwa baadhi ya vifaa vya wateja.

“Mahitaji ya umeme kwa sasa katika Mkoa wa Ruvuma ni megawati 12.5 na kwa Songea Mjini ni megawati 9.7 tu. Umeme uliokuja sasa ni megawati 48. Matokeo yake umeme umekuwa ukimiminika kwa kasi wakati mahitaji ni madogo,” anasema.

Waziri huyo anasema Serikali inafanya utaratibu wa kutatua changamoto hiyo kwa kufunga kifaa kitakachodhibiti umeme uendane na mahitaji ya wananchi.

Pia, anatoa wito kwa wananchi wa Ruvuma kuutumia umeme kwa wingi ikiwamo kuanzisha viwanda na biashara mbalimbali.

Vilevile, Waziri anasema katika maeneo ambako mradi unapita, jumla ya vijiji 122 vimesambaziwa umeme na kuunganisha wateja takribani 22,700.

Anapongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Magufuli kwa namna inavyotekeleza mikakati mbalimbali ya kusambaza nishati hiyo ya umeme kwa wananchi.

Mradi wa njia ya Kusafirisha Umeme wa North – East Grid (Mw 185)

Dk Kalemani aliwahi kuliambia Bunge kuwa kuna miradi mingine inayotekelezwa na Tanesco ukiwamo wa kuzalisha umeme wa Rusumo MW 80, Ruhudji MW 358 na Rumakali MW 222.

Lakini pia alisema kazi nyingine ni ya kuimarisha mifumo ya usafirishaji wa umeme nchini kwa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mradi wa North - West Grid Extension kV 400 yenye umbali wa kilomita 1,384 inayojumuisha Iringa - Mbeya - Sumbawanga - Mpanda - Kigoma hadi Nyakanazi; Singida - Arusha - Namanga kV 400, km 414; Rufiji - Chalinze - Dodoma kV 400, km 512; Rusumo - Nyakanazi kV 220, km 98; Geita - Nyakanazi kV 220, km 133; Tabora - Urambo - Kaliua - Nguruka hadi Kidahwe Mkoani Kigoma kV 132, KM 391 na Tabora - Ipole – Inyonga hadi Nsimbo (Katavi) kV 132, km 381.