DAWASA inavyoishi falsafa za Rais Magufuli kufikisha huduma ya maji kwa wananchi


DAWASA inavyoishi falsafa za Rais Magufuli kufikisha huduma ya maji kwa wananchi

● AGIZO LA RAIS MRADI WA KISARAWE LATEKELEZWA ● KUFIKIA asilimia 95 ya huduma ya Majisafi IFIKAPO 2020 ● Wananchi 43,351 waunganishwa huduma ya Maji ● Miradi 51 yatekelezwa KWA FEDHA ZA NDANI

Ni miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Joseph Pombe Magufuli unaokwenda sambasamba na mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo katika sekta muhimu ya maji.

Ni awamu ya uongozi iliyojikita katika kuleta majibu ya haraka ya changamoto halisi za wananchi zinazogusa maisha yao ya kila siku. Katika hilo, Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) inaadhimisha miaka minne ya utawala wake kwa mafanikio lukuki huku ikijinasua na mafanikio mengi yaliyopatikana katika kipindi hiki kifupi.

Kama ambavyo Rais Magufuli amekuwa akisisitiza wananchi kusogezewa huduma za maji safi karibu na makazi yao ndivyo ambavyo DAWASA imekuwa ikihakikisha inatekeleza adhima hiyo kwa wakazi wa Dar es Salaam na katika miji ya Pwani.

Kwa kuwa na mazingira bora ya kiutumishi yanayochochea ubunifu na kasi ya utekelezaji wa majukumu yake, kipindi cha miaka mine ya Rais Magufuli kimekuwa cha mabadiliko makubwa na ya kasi.

Miradi 68 yatekelezwa

Baada ya DAWASA kukamilisha upanuzi wa miradi mikubwa ya maji katika mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini, kazi kubwa ambavyo imekuwa ikiendelea ni kuboresha mfumo wa usambazaji maji na kupanua mtandao ili kufikisha maji yaliyoongezeka kwa wananchi. Hadi sasa miradi mikubwa na midogo ipatayo 51 imekamilika na kuongezeka wigo wa huduma ikiwa ni pamoja na kufikisha maji katika maeneo mengi ambayo hapo awali hayakuwa na huduma.

Miradi hiyo imetekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Buguruni kwa Madenge, Mafuriko, Kiwalani, Jet Buza, Mtoni Sabasaba, Tandika Undengerekoni, Mbagala Kipati na mashine ya maji na Kibangulile, Kidogo Mwisho, Mburahati NHC, Sinza Kamanyola, Mabibo Jeshini na Magomeni.

Katika Mkoa kazi wa Ubungo ambapo kwa miaka mingi pamekuwa na kero kubwa ya maji, jumla ya miradi midogo midogo 32 ya kuongeza mitandao imetekelezwa. Hii ni pamoja na miradi ya Saranga, Haranga, Mnarani, Bunyokwa Mashariki, Mji Mpya, Makondeko, Kimara B, Mbezi Luis, Temboni, Luguruni, Magari saba na Makabe, Mavuraunza, Msigani, Bunyokwa na mingine mingi ambayo kwa hakika imeleta ahueni kubwa kwa wananchi.

Katika Mkoa kazi wa Tabata ambapo pia kulikuwa na changamoto ya upatikanaji wa maji, huduma imeweza kuboreshwa kwa kufikisha maji mengi zaidi katika mtandao uliokuwepo lakini pia huduma imesogezwa katika maeneo ambayo hayakuwa na maji hapo awali kama vile Kisukuru Migombani, Kisukuru kwa Mkuwa Segerea Liwiti na Misewe.

Katika kipindi hiki miradi zaidi ya 20 ilitekelezwa mkoani Pwani hususan katika miji ya Kibaha na Bagamoyo, miradi hii ni pamoja na Mradi wa Sofu, Galagaza, Kidugalo, Savi, Kiambeni, Kigende Mbwate, Boko Mnamela, Tungutungu, Kihararaka na maeneo mengine. Ili kuweza kufanikisha hayo, DAWASA imeamua kutenga asilimia 40 ya mapato yake yote na kuyaelekeza kwenye utekelezaji wa miradi na hivyo miradi imeweza kutekelezwa kwa wakati na kwa ubora.

Siri ya mafanikio

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa DAWASA, Mkuu wa Majeshi Mstaafu Davis Mwamunyange anabainisha wazi kuwa siri ya mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi hiki kifupi ni uongozi imara uliokuwa na malengo ya kufikisha huduma zaidi kwa wananchi pamoja na utayari wa watumishi wa Mamlaka katika kutoa huduma bora ya Majisafi na Majitaka.

“Katika yote tunajivunia utayari wa Serikali yetu inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli katika kusimamia uboreshaji wa huduma kwa wananchi wake ikiwemo huduma ya majisafi usafi wa watumishi wetu katika kutekeleza kwa vitendo maagizo ya viongozi na mikakati shirikishi iliyowekwa wazi kwa watumishi wote,” anasema Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange.

”Utekelezaji wa miradi mbalimbali ndani ya DAWASA unafanyika kwa weledi, uwazi na kwa kuzingatia vigezo na taratibu za nchi na hii imesaidia sana kuleta umoja katika utekelezaji wake,” anasema na kuongeza kuwa Bodi yake pia imekuwa ikifuatilia na kufanya ziara ili kujionea hali halisi na kutoa maelekezo ili kuboresha utekelezaji.

Jenerali mstaafu Mwamunyange anasema, “Miaka minne ya Rais John Magufuli kwangu mimi kama mwenyekiti wa bodi na wajumbe wengine inatupa faraja ya kuona Mamlaka tunayoisimamia inafanya kazi nzuri inayoonekana na kila umma wa Mtanzania hususani wakazi wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani wanafurahia huduma zake.”

Hali ya upatikanaji maji

Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja anasema awali mwaka 2015 Jiji la Dar es Salaam lilikuwa linapata maji kwa asilimia 68 na jumla ya maunganisho ilikuwa 123,000.

“Kwa wakati huo upotevu wa maji ulikuwa asilimia 53 na makusanyo kwa mwezi yalikuwa ni kiasi cha Tsh Sh3.2 bilioni kwa mwezi. Leo hii hali ya upatikanaji maji jijini Dar es Salaam imepanda hadi asilimia 85 na maunganisho ya maji yameongezeka kutoka 123,000 hadi kufika 326,000,” anasema Mhandisi Luhemeja na kuongeza kuwa lengo ni kufikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2020.

“Zawadi yetu kwa Mheshimiwa Rais Dk John Pombe Magufuli ni kukamilisha mradi wa Maji wa Chalinze-Mboga utakaohudumia wananchi takribani 125,000. Pia, miaka minne hii tutaongeza kasi ya utendaji kazi ili kukidhi matarajio yake kwa wananchi ya kuwasogezea huduma ya maji safi wananchi wanaohudumiwa na DAWASA,” anasema Mhandisi Luhemeja.

Ukusanyaji mapato

Afisa Mtendaji Mkuu anasema upatikanaji wa maji unakwenda sambamba na ukusanyaji wa mapato ambapo yameongezeka na kufikia wastani wa Sh11.2 bilioni kwa mwezi.

Anasema katika Mwaka wa Fedha uliokwisha 2018/2019 DAWASA ilikuwa na lengo la kukusanya Sh144 bilioni ambao ni wastani wa Sh12 bilioni kwa mwezi hivo ni imani yake kuwa lengo litatimia ndani ya mwaka huu wa fedha.

“Naomba kutoa taarifa kwamba kwa mwaka wa fedha uliokwisha hivi karibuni DAWASA imekusanya Sh135 bilioni sawa na asilimia 95 ya lengo, aidha kiwango cha maji yanayopotea kimepungua mwezi Oktoba 2019 DAWASA imeweza kuunguza upotevu na kufikia asilimia ………, ni malengo yetu kufikia Single digit,” anasisitiza Mhandisi Luhemeja.

Mhandisi Luhemeja anabainisha kuwa kwa upande wa huduma kwa wateja imeendelea kuboresha kituo cha mawasiliano na huduma kwa wateja ambacho kinafanya kazi 24 na lengo ni kuwahudumia wananchi.

Bei ya Maji haitapanda

Mhandisi Luhemeja anatabanahisha kuwa kwa kipindi cha miaka minne sasa hivi DAWASA imeendelea kuboresha njia za ulipaji wa Ankara. “Wateja wetu sasa wanalipia kutumia mtandao, hiyo imewarahisishia badala ya kupoteza muda mwingi kulipia kwa fedha katika ofisi za DAWASA ama mabenki.”

“Nichukue fursa hii kutangaza kuwa katika kipindi ambacho Serikali ya awamu ya tano inaingia madarakani DAWASA haijapandisha bili ya maji pia niseme DAWASA haina mpango wa kupandisha bili za maji katika kipindi chote cha uongozi wa serikali ya awamu ya tano,” anasema Mhandisi Luhemeja.

Mhandisi Luhemeja anasema DAWASA inaendelea na mpango wake wa kuunganisha wateja kwa mkopo ambapo wengi sasa wanajitokeza.

“Pia nitumie fursa hii kwa kuwajulisha wananchi kwamba Maji ya DAWASA ni ya mkopo kwa maunganisho ya kwanza kwa hiyo kwa yeyote anayekuja kuchukua fedha kwa ajili ya ada ya kuunganisha huyo atakuwa tapeli, wananchi wamripoti kwenye vyombo vya dola haraka,” anasema Mhandisi Luhemeja.

Miradi mikubwa ya maji

Julai 2019, DAWASA walitia saini utekelezaji wa miradi sita mikubwa ya Usambazaji maji katika miji ya Dar es Salaam na maeneo ya miji ya Pwani.

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa alisema wale wanaopata fursa ya kutekeleza miradi hiyo waifanye kwa weledi huku akiwaonya wakandarasi watakaokuwa wababaishaji wachukuliwe hatua.

Waziri Mbarawa anasema ili kwenda na adhima ya Rais Magufuli ya kuinua viwanda vya ndani, alisema malighafi zitakazotumika zitoke nchini.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Luhemeja alisema kwa mujibu wa miradi hiyo inatarajiwa kwenda kujibu kero za wakazi hao wa Dar es Salaam na mkoani Pwani.

Alisema miradi hiyo ni ishara na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Magufuli, ambaye amekusaidia kuwaondolea wananchi changamoto ya Maji Safi jijini Dar es Salaam na mkoani Pwani.