Rais Magufuli afanya mambo makubwa ya kihistoria


Rais Magufuli afanya mambo makubwa ya kihistoria

Uthubutu wa Rais Magufuli wa kujenga miradi mikubwa kwa kutumia fedha za ndani, umewashangaza watu wengi. Katika kipindi hiki cha miaka minne Rais Magufuli amefanya mambo makubwa na ya kihistoria.

Novemba 5, 2015 Tanzania iliandika historia mpya kwa kuanza kwa enzi mpya ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya tano chini ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli.

Kiongozi huyo aliyechukua kijiti cha uongozi kutoka kwa mtangulizi wake Dk Jakaya Mrisho Kikwete, mwaka huu anatimiza miaka minne madarakani huku akiwa amejizolea sifa kemkem kitaifa na kimataifa kutokana na uhodari wake wa kufanya uamuzi mgumu na kusimamia miradi mikubwa.

Katika kipindi chote hicho, Rais Magufuli amefanya mambo mengi makubwa ambayo yamempaisha kitaifa na kimataifa kiasi cha baadhi ya nchi kutamani awe rais wao.

Baadhi ya mambo yaliyompaisha Rais Magufuli tangu aingie madarakani ni kutokuwa na kigugumizi kuwafukuza watumishi anaoona hawaendani na kasi yake na wale wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma kama mafisadi na wala rushwa.

Uthubutu wa Rais Magufuli wa kujenga miradi mikubwa kwa kutumia fedha za ndani, umewashangaza watu wengi. Katika kipindi hiki cha miaka minne Rais Magufuli amefanya mambo makubwa na ya kihistoria. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na;

Kufufua ATCL

Ununuzi wa ndege mpya aina ya Bombardier, Boeing 787-8 Dreamliner na Airbus umenogesha zaidi hali ya usafiri wa anga nchini kwani usafiri wa ndege umekuwa wa uhakika zaidi kwenda na kurudi mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi.

Ununuzi wa ndege hizi ulikuwa ni mpango wa Serikali ya Awamu ya Tano kulilifua upya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ambalo lilikuwa halifanyi vizuri.

Akizungumzia kuhusu juhudi hizo za Serikali ya Awamu ya Tano, Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Josephat Kagirwa anasema ni hatua iliyosaidia kuboresha sekta ya usafiri wa anga nchini.

“Ununuzi wa ndege hizi umechangia kwa kiasi kikubwa kuleta mapinduzi katika sekta ya usafiri wa anga nchini kupitia ATCL, jambo hili limechangia katika pato la taifa, kupanua wigo wa shughuli za kitalii, kuongeza idadi ya wawekezaji wanaokuja hapa nchini, kuwawezesha Watanzania kufanya biashara zao nje na ndani ya Tanzania pamoja na kutoa ajira kwa Watanzania,” anasema Kagirwa.

Ujenzi wa barabara za juu (Ubungo & Tazara Flyover)

Ujenzi wa barabara za juu maeneo ya Tazara ni jambo lingine lililompa sifa kubwa Rais Magufuli hasa kutokana na ilivyosaidia kuondoa kabisa foleni kubwa iliyokuwa inaonekana muda wote.

Serikali ya Awamu ya Tano pia inasimamia utekelezaji wa mradi wa barabara za juu makutano ya Ubungo jijini Dar es Salaam ambako nako kumekuwa na foleni kubwa muda wote.

Mradi wa ufungaji wa rada za kisasa

Septemba 16 mwaka huu, Rais Dk Magufuli alizindua Rada mbili za kuongozea Ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa KIA.

Akizungumza kuhusu mradi huo, Makurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Aanga Tanzania (TCAA), Hamza Johari amesema kukamilika kwa mradi huo wa ufungaji wa rada ni muendelezo wa juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuboresha sekta ya usafiri wa anga nchini.

Mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Julius Nyerere

Mafanikio mengine ya Rais Magufuli ni utekelezaji wa mradi mkubwa wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2115) katika eneo la Rufiji maarufu kama Stieglers Gorge.

Elimu Bure

Ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya tano, tumeshuhudia Rais Magufuli akitekeleza kwa vitendo ahadi yake ya kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne.

Mikopo ya elimu ya juu

Mafanikio mengine ni wanufaika wa mikopo elimu ya juu kuongezeka jambo hilo lilitokana na ongezeko la bajeti ya bodi kufuatia maelekezo ya Rais John Magufuli.

Ujenzi Viwanda

Azma ya kufikia uchumi wa viwanda nayo imeonekana dhahiri kwani katika kipindi cha miaka minne ya utawala wake, viwanda vikubwa na vidogo vimezinduliwa na vinafanya kazi.

Safari ya Dodoma

Uamuzi mwingine mgumu wa kujivunia uliofanywa na Rais Magufuli ni kuhamishia Serikali mkoani Dodoma ambapo Wizara mbalimbali, mashirika na taasisi za umma, Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu zikiwa tayari zimehamia Dodoma. Hivi karibuni Rais Magufuli alitangaza rasmi kuhamia katika jiji hilo.

Mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi

Hili ni moja ya eneo ambalo limempa sifa kubwa Rais Magufuli na Serikali yake. Rais amekuwa akichukua maamuzi ya papo kwa papo pindi linapotokea suala la rushwa na ufisadi kwa viongozi wa umma.

Wananchi wanasemaje

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sauti ya Jamii Taifa, Richard Nnako anasema Rais Magufuli ameonyesha mfano mzuri na anapaswa kuungwa mkono kutokana na mambo makubwa anayoyafanya.

“Taasisi ya Sauti ya Jamii ni taasisi isiyo ya kiserikali lakini inafanya shughuli zake kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano. Sisi kama taasisi tunamuunga mkono Rais na Serikali yake kutokana na mambo makubwa anayoyafanya,” anasema Nnako.

Lucas Mazoya mkazi wa Dar es Salaam anasema, “Kumekuwepo na upotoshaji mwingi kutoka kwa baadhi ya viongozi kutokana na mambo anayofanya Rais Magufuli jambo ambalo sio sahihi. Rais anafanya mambo makubwa sana na inahitaji uelewa mdogo tu kuweza kufahamu kwa sababu kila kitu anachofanya kinaonekana,”

“Serikali ya Awamu ya Tano tangu iingie madarakani imefanya kazi kubwa kuleta maendeleo kwa wananchi. Serikali pia imefanya mambo makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu ambapo sasa hivi wanafunzi wanasoma bure, sekta ya afya, ujenzi wa miundombinu na kubwa zaidi kupambana na mafisadi ambao kipindi cha nyuma walichangia nchi yetu kurudi nyuma kiaendeleo,” anasema Brenda George mkazi wa Dar es Salaam.

Mwanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Gerard Mathias anasema miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano imeleta mapinduzi katika nyanja nyingi za kimaendeleo nchini.

“Tukizungumzia upande wa elimu ambao mimi nipo, tumeona mambo makubwa yamefanyika, kama vile elimu bure, pamoja na kuongezwa kwa bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. Serikali ya Awamu ya Tano imefanya juhudi kubwa kuhakikisha kwamba wanafunzi wanaostahili kupata mikopo wanapata bila tabu yoyote.”

 

<