Ajenda ya viwanda ni injini ya ukuzaji uchumi wa nchi


Ajenda ya viwanda ni injini ya ukuzaji uchumi wa nchi

Katika awamu yake, Mheshimiwa Rais Magufuli ameweza kufanya ziara katika mikoa kadhaa yenye idadi kubwa ya viwanda hapa nchini. Pwani inatajwa kama mkoa wa kipekee wa viwanda; ilipongezwa na Rais kutokana na mipango yao ambayo imewapa wenyeji fursa nyingi za ajira.

Kiongozi ni mvumbuzi, anayekatisha msituni kutengeneza njia. Yeye kila wakati huweka mwelekeo mpya na kuunda maono yenye kutia moyo kwa ukuaji ujao.

Akiwa anafahamu ukubwa wa kundi la watu anaowaongoza; anapaswa kujua mahali gani anataka kuwaongoza watu wake akitumia ujuzi wake wa masuala ya uongozi; uwe ni wa kuzaliwa nao au kwa kufundishwa kufikia malengo yake maalum.

Ikiwa Rais ndiye kiongozi wa ngazi ya juu katika serikali; analazimika kuanzisha na kutekeleza mikakati ya kuongoza mashua katika njia sahihi kwa maendeleo ya pamoja na utulivu.

Rais wa kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alilazimika kuunda sera, kanuni na sheria ili kutekeleza maono yake ya Tanzania. Alitumia Mfumo wa Ujamaa na Siasa ya Kujitegemea kama nyenzo yake muhimu kwa ukuaji wa kiuchumi na kijamii wa wakati huo; na kufanikiwa kutengeneza umoja wa kitaifa miongoni mwa watu kote nchini na kuwa mfano wa kuigwa linapokuja falsafa zake makini.

Tuliona Tanzania ikipitia awamu tatu za uongozi na ajenda tofauti zenye vipaumbele vya kitaifa kama vichochezi kuelekea maendeleo ya taifa.

Kinyume na tawala zingine zilizopita; Rais Magufuli aliamua kuitekeleza ajenda kubwa ya kitaifa ya kuifanya Tanzania iwe nchi ya uchumi wa kati na viwanda.

Rais Magufuli mwenye ufasaha anapozungumza, muda wote ameweka matumaini yake makubwa katika mpango huo kama msingi wa maendeleo endelevu ya watu na ukuaji wa uchumi. Zaidi, ameruhusu kwa moyo mmoja uanzishwaji wa viwanda vingi nchini ambao utawanufaisha Watanzania wapatao Milioni 55 kwa kupewa ajira.

Katika awamu yake, Mheshimiwa Rais ameweza kufanya ziara katika mikoa kadhaa yenye idadi kubwa ya viwanda hapa nchini. Pwani inatajwa kama mkoa wa kipekee wa viwanda; ilipongezwa na Rais kutokana na mipango yao ambayo imewapa wenyeji fursa nyingi za ajira.

Katika miaka minne ya Rais John Pombe Magufuli madarakani, Profesa wa Masomo ya Masuala ya Maendeleo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benedict Mongula ameshiriki maoni yake juu ya mwelekeo wa nchi chini ya ajenda ya ukuaji wa uchumi.

Mongula anafafanua kuwa, "Kwa maoni yangu, sera maalum ya ukuaji wa uchumi inapaswa kuandikwa na kusema wazi nini kifanyike. Ajenda imekuwa mjadala mpana kwa wanasiasa lakini kamwe haielezi wazi nini kifanyike kuwa na Tanzania bora. Lazima kuwe na mpango maalum ambao unaweza kufafanua majukumu ya kila mmoja kwa wakati; ukielezea jinsi uwekezaji unapaswa kufanywa? Nani wa kuwekeza? Wapi uwekezaji ufanyike? Na kwa aina gani ya viwanda?

Mbali na hiyo, tunahitaji kuanzisha mpango utakaojumuisha sekta nyingi katika kufikia malengo maalum ya nchi yenye uchumi wa kati na viwanda. Ndani ya mchakato; mpango huo unapaswa kuhakikisha kuwa sekta zote zimeunganishwa. Kwa kusema ukweli ni changamoto kupima utendaji kazi wa ajenda bila kuweka vigezo; na hii inasababishwa sana na kutokuwepo kwa vigezo vya ajenda.

Mbali na hayo, yapo matarajio makubwa ya ujaji wa mara kwa mara wa wawekezaji na kuwekeza katika sekta tofauti. Tunataka kuona wadau kama vile Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inashiriki katika uwekezaji kuwashawishi wadau zaidi. Serikali kama mdau muhimu anahitaji kuweka mazingira mazuri na wezeshi kwa ajili ya uwekezaji mkubwa kutoka kwa wawekezaji.

Profesa Mongula anaendelea kueleza faida za nchi inayoingia katika mfumo wa viwanda. Anasema, "Ni nani katika ulimwengu ambaye haelewi faida zinazopatikana kutokana na kuwa viwanda vingi? Viwanda vinawapa watu fursa za ajira; husaidia kukuza uchumi wa nchi; kwa mtazamo wa kimataifa, viwanda hurejelewa kama "injini ya ukuzaji uchumi" kwani inasaidia kupunguza umaskini na kuwa kichocheo cha kukuza mapato.

Anaendelea, "Viwanda vinahakikisha upatikanaji wa masoko kwa mazao yote ya kilimo, misitu, mifugo na uvuvi. Ni ajenda nzuri na haishangazi kuitekeleza kwani tayari imethibitisha kufanikiwa kwa mataifa mengine yaliyoendelea kama India, Uchina, Korea. "

Gaudence Mpangala haendi mbali na maoni ya Professa Mongula. Anasema, "Viwanda sio jambo jipya nchini Tanzania baada ya uhuru wetu mnamo 1961. Kile kinachofanywa sasa chini ya Rais Magufuli ni msisitizo mkubwa tu. Ajenda hii ni kwa hisani ya Mwalimu Nyerere iliyotokana na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Taifa (FYD) kwenye miaka ya 1960 na 1970 ambayo kimsingi ilijikita kuangazia maendeleo ya vijijini na viwanda. Viwanda vingi vilijengwa lakini mambo yaliharibika baada ya mfumo huria na ubinafsishaji, awamu ya pili ya mwaka 1980. Viwanda vya ubanguaji wa korosho na nguo vilikuwa vingi wakati huo. "

Anaendelea kuwa, "Kama viwanda vyote vingekuwa vinafanya kazi hadi leo, Tanzania ingekuwa miongoni nchi yenye viwanda vingi ulimwenguni. Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF) ziliiwekea masharti magumu Tanzania; yaliyolenga kukomesha ukiritimba wa Serikali juu ya viwanda na kutaka wapewe watu binafsi. Mbaya zaidi, watu waliokabidhiwa viwanda vingi walishindwa kuviendeleza na viwanda vilikufa."

Profesa Mpangala ameongeza kuwa, juhudi za Serikali ya sasa ya kufufua viwanda ni mkakati bora kwa kuzingatia ugumu wa kupiga hatua za kimaendeleo ulimwenguni bila ya kuwa na viwanda kwa sasa, na ningependa kumpongeza Rais Magufuli kwa hili.

"Hoja kubwa hapa, Je, tumefanya upembuzi yakinifu kwa viwanda hivi? Mwalimu Nyerere alianzisha viwanda vya uzalishaji vilivyojitegemea, kwa hivyo lazima tuwe wazi kwa aina gani ya viwanda tunahitaji, Je, ni viwanda vya uzalishaji vilivyojitegemea au viwanda mama? ”Profesa alimaliza.

Ni wito kwa wadau wote kushiriki katika ajenda hii, Taasisi za kifedha kama benki na taasisi za mikopo zinapaswa kuangalia njia sahihi ya kutoa masharti nafuu ya mikopo kwa watu binafsi na hata kampuni za kati tukijiandaa kwa ajenda ya viwanda.